Burudani au matokeo? Arsenal yatinga nusu fainali kwa tabu

    • Author, Alex Howell
    • Nafasi, Arsenal reporter at Emirates Stadium
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Mikel Arteta alihitaji kuona "moto" kutoka kwa wachezaji wake wa Arsenal, lakini badala yake walionekana kucheza kwa mwendo wa chini huku wakifanya kilichotosha kufuzu hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Bao la Kai Havertz kwenye mechi ya kwanza pamoja na sare ya 0-0 dhidi ya Sporting kwenye Uwanja wa Emirates viliihakikishia Arsenal tiketi ya kuingia nne bora kwa msimu wa pili mfululizo.

"Ninajua juhudi na kujitolea kwao," alisema Arteta.

"Kuna kazi kubwa nyuma ya mafanikio haya. Tumefanya jambo ambalo halijawahi kufanywa katika historia ya klabu kwa miaka 140, linaonyesha namna lilivyo gumu."

Hata hivyo, kiwango cha Arsenal kimekuwa hakiridhishi kwenye nyakati muhimu. Wameshinda mechi moja tu kati ya tano zilizopita kwenye mashindano yote, wakifunga mabao matatu pekee.

Swali linabaki: je, mtindo wa uchezaji ni muhimu au matokeo ndiyo kila kitu?

''Hatujakamilika, lakini tunathamini kile tulicho nacho"

Kwa Arteta, uzuri wa soka si kipaumbele kwa sasa, kilicho muhimu ni kuvuka hatua na hatimaye kushinda taji msimu huu.

Arsenal wamekuwa wakipata matokeo licha ya kukosa nyota kadhaa kutokana na majeraha. Bukayo Saka, Martin Odegaard, Jurrien Timber na Riccardo Calafiori hawakuwepo dhidi ya Sporting.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Declan Rice alicheza licha ya kuwa na changamoto ya afya.

Na sasa kuna wasiwasi mpya kuelekea mchezo mkubwa dhidi ya Manchester City Jumapili, baada ya winga Noni Madueke kuumia goti na kulazimika kutoka nje mechi ikiendelea.

Arteta alipoulizwa kuhusu hali ya uchovu wa wachezaji wake alisema:

"Ndiyo, ipo. Lakini ukiangalia namna wanavyorudi kukaba tunapopoteza mpira na nidhamu yao uwanjani, ni ya kuvutia.

"Kuna sababu sisi ndio timu pekee ya Uingereza iliyobaki kwenye mashindano haya ratiba ni ngumu sana.

"Hatujakamilika, tunahitaji kuboresha, hilo liko wazi. Lakini kuna thamani kubwa katika kile ambacho wachezaji hawa wamekifanya."

Nedum Onuoha, beki wa zamani wa Manchester City na QPR, aliiambia BBC Sport:

"Kufika nusu fainali kwa msimu wa pili mfululizo ni mafanikio makubwa. Hawakuwa bora sana, lakini walifanya kilichohitajika kufuzu na wamefanikiwa.

"Siku nyingine wangeweza kuunda nafasi zaidi na kufunga mabao zaidi. Lakini licha ya kutocheza vizuri sana, bado wako hatua ya nne bora."

Alinukuu kauli ya nahodha Declan Rice kuwa Arsenal wanataka "kusonga hatua moja zaidi".

"Wataangalia mechi hii na kuona walichokosea, lakini ukweli ni kwamba klabu nyingi Ulaya zingetamani kuwa walipo sasa," aliongeza.

"Haikuwa mechi ya kuonyesha ubora mkubwa, lakini Arsenal wameonyesha wana nafasi sawa na wengine.

"Kwa mfano, Real Madrid walifunga mabao manne katika mechi mbili lakini wakaondolewa. Arsenal walihitaji bao moja tu na walifanya kazi yao kwa ulinzi imara."

Manchester City wanafuata - Je, Arsenal wataweza?

Sasa Arsenal wanaelekeza nguvu zao kwenye pambano la kileleni dhidi ya Manchester City katika Uwanja wa Etihad Jumapili.

Wanabunduki wanawania taji lao la kwanza la ligi baada ya miaka 22. Wanaongoza kwa pointi sita, lakini wamecheza mechi moja zaidi ya kikosi cha Pep Guardiola.

Hata hivyo, kuna hofu kwamba ukosefu wa makali mbele unaweza kuwaathiri, na watalazimika kutegemea zaidi uimara wao wa safu ya ulinzi.

Dhidi ya Sporting, Arsenal walipiga shuti moja tu lililolenga lango. Jumla ya xG ya mechi ilikuwa 0.93, kiwango cha chini zaidi msimu huu wa Ligi ya Mabingwa.

Arteta alisema:

"Kwa sasa, muhimu ni namna unavyopambana hasa unapowania mataji. Hilo ndilo linaamua."

Arsenal hawajashindwa katika mechi nane kati ya 12 walizocheza kwenye Ligi ya Mabingwa msimu huu - rekodi bora kuliko timu nyingine zote.

Chris Sutton aliambia 5 live:

"Bila mpira walikuwa bora sana. Lakini mbele hawatengenezi nafasi za kutosha.

"Hata hivyo, jambo muhimu ni kusonga mbele na wamefanikiwa

"Kama hawataboresha safu ya ushambuliaji, hawatashinda Ligi ya Mabingwa wala Ligi Kuu."

Sutton anaamini Arteta anaendelea kuwaza kuhusu tatizo hilo kila wakati.

"Wachezaji wa pembeni wanachelewa kufanya maamuzi sahihi. Wanahitaji kuwa na ukali zaidi.

"Kai Havertz alipoingia, walionekana bora kidogo. Lakini kwa ujumla bado kuna kazi kubwa ya kufanya.

Eberechi Eze alionyesha baadhi ya miondoko mizuri, lakini bado hajarejea kwenye kiwango chake kamili. Kwa sasa, Arsenal wana kazi kubwa mbele yao. Wengi katika Ligi Kuu watakuwa wakiamini kwamba mchezo wa Jumapili uko mikononi mwa Manchester City."

"Kwa sasa, wengi wanaona Manchester City wana nafasi kubwa zaidi kwenye mchezo wa siku ya Jumapili."

"Ningependa tuonyeshe filamu msimu huu"

Mikel Arteta anasherehekea ushindi huo kwa wakati wote.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Arsenal wanaingia fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa msimu wa pili mfululizo kwa mara ya kwanza katika historia yao

Ingawa Arsenal hawajawashawishi wengi kuwa wanaweza kushinda mataji yote mawili, Arteta anaamini mafanikio yao yanastahili kuthaminiwa.

"Ningependa tungerekodi filamu ya Arsenal msimu huu," alisema, akirejea kinakuwa kikiendelea nyuma ya pazia wakati wa msimu wa 2021-22.

"Watu wafurahie tulipofika kama klabu. Tumefanya jambo la kipekee sana katika historia yetu."

Iwapo Arsenal watafanikiwa kunyanyua taji kubwa huenda hata Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza mashabiki hawatajali namna walivyocheza kwenye mechi kama hii.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid