Mwili wa Mtanzania aliyekufa vitani Ukraine waagwa
Ndugu na jamaa wa Mtanzania, wameuaga mwili wa Nemes Tarimo hii leo jijini Dar es Salaam, miezi mitatu baada ya kukutwa na umauti akiwa vitani nchini Ukraine.
Mapema alfajiri ya leo, mwili wa Nemes uliwasili jijini Dar es Salaam na kukabidhiwa kwa ndugu, ambao wameeleza kuwa ndugu yao atazika kesho Jumamosi katika eneo la Tukuyu, Mbeya katika Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania.
Nemes alijiunga na kikosi cha jeshi binafsi cha Wagner mwezi Oktoba mwaka jana, miezi saba baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani nchini Urusi kwa kosa la jinai.
Kwa mujibu wa taarifa ya Serikali ya Tanzania, akiwa gerezani alipewa nafasi ya kujiunga na kikundi hicho cha Wagner kwa ahadi ya kulipwa fedha lakini kwa ahadi ya kuachiwa huru mara baada ya vita.
Tarimo alikwenda nchini Urusi mwaka 2020 kwa ajili ya masomo ya shahada ya uzamili katika fani ya biashara.
Katika msiba wa Nemes, ndugu na jamaa walimlilia wakisema alikuwa kijana mtulivu, mtaratibu na alipenda watu.





