Kenya: Wanafunzi wahitimisha masomo ya elimu ya msingi katika mfumo wa 8-4-4
Na, Laillah Mohammed
BBC Swahili

Chanzo cha picha, BBC NEWS
Kabla ya kukamilika kwa Alhamisi hii, wanafunzi zaidi ya milioni moja nukta mbili nchini kenya watakuwa wameshapata matokeo yao ya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane unaofahamika kwa kiingereza kama {Kenya Certificate of Primary Education} KCPE.
Waziri wa Elimu nchini Kenya Ezekiel Machogu ametangaza mapema Alhamisi matokeo ya mtihani huo, baada ya kuwasilisha ripoti ya matokeo hayo kwa Rais William Ruto kama ilivyo ada ya shughuli za mitihani nchini humo.
Kwa wanafunzi waliokuwa watahiniwa mwishoni mwa mwezi Oktoba, bila shaka hali ya tumbo joto imejaa miyoni mwao, kila mmoja akiomba kwamba ametimiza angalau alama 250 kati ya mia tano ili kujipatia nafasi katika shule ya upili nzuri.
Waziri Machogu, anatekeleza kibarua cha pili tangu serikali ya Rais Ruto kuchukuwa uongozi nchini Kenya, ila matangazo haya ni muhimu katika historia ya elimu nchini humo kwa kuwa darasa la nane mwaka wa 2023, ndio la mwisho kabisa katika mfumo wa elimu wa 8-4-4 ambao umekuwepo tangu 1984, wengine wetu tulipozaliwa.
Kwa miaka 39, Kenya imetumia mfumo huo wa elimu ambapo wanafunzi wanasoma miaka minane katika shule ya msingi, minne katika shule ya upili na miaka minne kwenye chuo Kikuu, huku wanaojiunga na vyuo anuwai au taasisi za cheti cha stashahada wakisomea kwa muda wa kati ya miaka miwili na mitatu.
Ukitazama historia ya taifa hili ni kwamba Kenya imekuwa na mifumo kadhaa ya elimu tangu nyakati kabla ya ukoloni ambapo Waafrika walitumia mbinu mbali mbali za kufunza vizazi vinavyokua jinsi ya kuishi na kutekeleza majukumu kama vile ya nyumbani, shambani, sokoni, na hata jinsi ya kuishi katika jamii.
Waarabu walipoingia katika pwani ya Kenya, vyuo vya kidini almaarufu Madrassa vilitumika kutoa mafunzo ya kidini kwa jamii, ili kuwapa elimu ya ziada kando na iliyotolewa na jamii zao.
Vitabu vya historia vimenakili, kwamba masomo ya msingi nchini yalianzishwa katika hali hiyo hiyo Pwani ya Kenya wakati wamisheni walipoingia Kenya mnamo 1946.
Dkt Ludwig Kraf, mmishonari kutoka Ujerumani alianzisha shule ya kwanza Kenya huko Rabai, karibu na Mombasa na masomo yaliangazia kusoma, kuhesabu na kuandika.
Safari ya CBC

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Huku mfumo wa 8-4-4 ulioanzishwa na rais wa pili nchini Kenya Daniel Toroitich Arap Moi ukianza kuondolewa, kwa miaka minne ijayo mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne ambayo kwa kiingereza inafahamika kama {Kenya Certificate of Secondary Edication} KCSE itafanyika sawa na ule wa darasa la kwanza la mtaala mpya CBC {COMPETENCY BASED CURRICULLLUM).
Ifikapo 2024 gredi ya tisa ambayo ni darasa la kwanza kusomea chini ya mfumo huu, watakuwa wanafanya mtihani wa kitaifa ili kujiunga na shule za upili, baada ya miaka mitatu katika shule ya sekondari ya chini yaani Junior Secondary.
Rais wanne wa taifa hili Uhuru Kenyatta, alipoingia madarakani, 2013 alibuni jopo maalum la kufanyia mabadiliko mfumo wa elimu nchini Kenya ambao ulihitajika kuambatana na ruwaza ya jumuiya ya Afrika mashariki kuwa na mfumo wa elimu unaoambatana na mahitaji ya soko la ajira katika karne hii na ambao pia unaangazia teknolojia, upanuzi wa sekta ya ajira kutoka kwa kazi za ofisini hadi kazi za mkono, ambazo ndizo zenye kuhitajika sana duniani.
Rais Kenyatta alipopokezwa ripoti ya jopo hilo, aliamua katika awamu yake ya kwanza kuanza safari ya kukumbatia CBC kikamilifu, ila hatua hiyo haikukosa changamoto zake.
Waziri wa elimu wakati huo Amina Mohammed, alitangaza kuahirishwa kwa mfumo huo kwa mwaka mmoja ili wizara yake ijiandae vyema kwa mabadiliko hayo. Lakini baada ya kufanya kikao na rais, na wadau katika sekta hiyo, wanafunzi milioni 1.4 walijiunga na gredi ya kwanza chini ya mfumo wa CBC Januari 2017.
Nakumbuka wengi wakipinga mfumo huo nchini akiwemo aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha waalimu nchini KNUT Wilson Sossion ambaye nilimhoji kabla ya hapo, akilalamika kwamba waalimu hawakuwa tayari na kuwa vifaa, madarasa na masuala muhimu ya kufanikisha masomo hayo hayakuwa tayari.
Rais Kenyatta naye, akakata kauli na kusisitiza, ‘safari ya CBC imeshaanza bandarini na wala meli haitorudi nyuma,’
Kwa wazazi ambao mimi ni mmoja kati yao, tatizo kubwa limekuwa kazi ya ziada ambazo wanafunzi wanakabiliwa nazo, na mahitaji ambayo waalimu wameyatosa kwa wazazi.
Kwa upande mmoja, imekuwa sio safari rahisi na kunibidi kufuatilia kwa karibu anachokifanya mwanangu. Ila imekuwa nafasi bora ya mimi na yeye kufanya kazi pamoja na kujuwana vyema.
Kisha, shughuli za mitihani wa majaribio yaani assessment zinaanza katika gredi ya nne ambapo mwaka huu nimekuwa mzazi wa mtahiniwa katika mfumo huo mpya unaotolewa na tume ya mtihani nchini KNEC.
Tofauti na jinsi mimi nilivyofanya mtihani wa KCPE, hamna pilka pilka nyingi za maafisa wa usalama kusimamia mitihani wakiwa wameshika bunduki, kana kwamba wanafunzi wako kizimbani.
Hatua hii ilianzishwa na Waziri wa elimu wakati wa Rais Uhuru Kenyatta – Fred Matiang’i ambaye katika kikao cha wanahabari aliwahi kufichuwa kwamba suala la wizi kwenye mitihani lilikuwa limezidi na Kenya ilikuwa inatazamwa kwa macho makali na vyuo vikuu vya ughaibuni kuhusiana na viwango vya elimu vya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu.
Kwa mfano katika mtihani wa KCPE 2022, kuna baadhi ya shule ambazo zilitoa matokeo ya ajabu ambayo wao wenyewe wanasema sio ya kustaajabisha. Katika shule moja, kwa mfano, wanafunzi waliopata alama ya A ilizidi wanafunzi mia moja jambo ambalo halikuwahi kutokea hapo kabla.
Mfumo wa KCPE unaopungiwa mkono

Ukiendelea kutafakari, turejelee mfumo wa KCPE unaopungiwa mkono huku wanafunzi wakitarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza tareha 8 Januari kwa miaka minne ya shule ya upili.
Wakati nilipofanya mtihani wangu 1998, ilikuwa siku tatu ya mtihani mwezi Novemba na matokeo yalitangazwa siku moja baada ya sikukuu ya Krismasi. Wakati huo masomo yaliyofanyiwa utahini yalikuwa saba huku alama za jumla zikiwa 700. Sitokuambia nilipata alama ngapi, ila nilipita na kujiunga na shule ya upili ya mkoa.
Miaka michache baada ya hapo masomo yalipunguzwa hadi matano na alama zikawa 500, wengi walijivunia kutangazwa nambari moja wakiwa na matokeo ya alama 462 ambazo ni za juu zaidi kutangazwa katika miaka ya hivi karibuni.
Mtihani wa kwanza wa KCPE ulifanyika 1985 na dadangu mkubwa alikuwa katika darasa hilo la watahiniwa laki tatu hivi ambao walijiunga na darasa la nane badala ya kufanya mtihani katika darasa la saba, kama ilivyokuwa hapo awali.
Kakangu mkubwa alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa mwisho kusoma chini ya mfumo wa 7-6-4 ambapo mwanafunzi alikuwa anafika darasa la saba na kufanya mtihani wa Certificate of Primary Education, ambapo alijiunga na kidato cha kwanza na baada ya miaka minne alifanya mtihani uliofahamika kama {Ordinary Level Exams} na kujiunga na Senior School ambapo alisoma kidato cha tano na sita na kufanya mtihani wa {Advanced Level} kabla ya kujiunga na chuo kikuu.
Babangu mzazi, alikuwa shule ya msingi hadi darasa la tatu alipofanya mtihani wa kujiunga na darasa la nne, ambao ulifanyika katika miaka ya arobaini, hadi sitini. Alipomaliza darasa la saba alijiunga na shule ya upili, kwa masomo yake ya juu.
Nakumbuka akitueleza kwamba shule ya upili ya Ingotse iliyopo katika kaunti ya Kakamega, ilikuwa maarufu kwa viwango vya wanafunzi waliofuzu na akanitajia maafisa wakuu serikalini wakati wake ambao alisoma nao shuleni – Hata yeye aliwahi kuhudumu katika wizara ya fedha nchini Kenya……
Nikitizama kizazi kijacho, mabadiliko yanafanyika tena sio tu Kenya, bali nafahamu kwamba Tanzania na Uganda wanaangazia suala hili la mfumo mpya wa elimu.
Na ikiwa watafuata safari iliyochukuwa Kenya, sitowaficha, haitokosa vizingiti, milima na mabonde. Ila Kenya imetoa nafasi bora ya kipi cha kufanya kabla ya kuanza kutekeleza mfumo wa elimu ambao utaathiri maisha ya usoni ya kizazi kijacho.
Wataalamu wa elimu wametofautiana kuhusu ikiwa turejelee mfumo wa 8-4-4 ama tuendelee mbele, alipokuwa katibu wa elimu ya msingi Dkt. Julias Jwan liwahi kuniambia katika mahojiano kwamba dunia ya sasa inabadilika haraka na Kenya haitowachwa nyuma na kwamba tofauti na 8-4-4 ambayo ni mfumo tu, Kenya haijawahi kuwa na mtaala wa elimu ya vitendo yaani CBC.
Dr. Jwan alikuwa katika taasisi ya elimu wakati huo KIE ambayo kwa sasa inafahamika kama {KENYA INSTITUTE OF CURRICULUM DEVELOPMENT} ambayo ilifanya kazi kwa karibu na jopo la kurekebisha mfumo wa elimu nchini uliioongozwa na Prof. Fatuma Chege ambaye aliwahi kuhudumu kama katibu wa elimu anayesimamia mitaala wakati wa uongozi wa Rais kenyatta.
Kinara wao alikuwa marehemu Profesa George Magoha, aliyeshikilia usukani baada ya Waziri Matiangi’ kuhamia wizara ya usalama wa ndani.
Magoha hakuwahi kusimamia tathmini ya KPSEA ambao alisimamamia maandalizi yake, ila alirejesha mfumo wa kutoorodhesha wanafunzi bora na shule bora nchini ambao aliutumia Profesa Jacob Kaimenyi na kusema ulichangia shule za kibinafsi kushiriki ulaghai wa kuwaweka wanafunzi wenye uwezo wa chini kwenye vituo vingine vya mitihani ili kuhakikisha kwamba alama ya shule ya wastani inasalia bora.
Tofauti na 8-4-4 ambayo wengi wameilaumu kwa kulazimisha wanafunzi kukariri bila kuelewa, CBC imepigiwa upatu kama mtaala unaomuangazia mwanafunzi na kushirikisha masomo ya kutenda jambo kama kwa mfano kujifunza kushona, teknolojia, na mengine mengi.
Mtihani wa KCPE unaondolewa huku wanafunzi wa gredi ya sita waliofanya tathmini yao ya KPSEA {Kenya Primary School Education Assessment} pia wakipokea matokeo yao na kujiandaa kujiunga na shule ya sekondari ya chini yaani junior secondary ambazo zinatoa mafunzo yao katika shule za msingi zilizoidhinishwa.
Kukamilika kwa kitengo kimoja cha 8-4-4 kinaibua maoni tofauti miongoni mwa Wakenya, wengine wakifurahia na baadhi wakisema kwamba 8-4-4 ilihitaji ukarabati mdogo tu na mambo yangekuwa sawa.
Dkt Emmanuel Manyasa ambaye ni mtaalamu wa elimu anayeongoza taasisi ya Usawa Agenda, amewahi pia kiniambia kwamba japo wengi walihisi kuwa mtaala mpya umeshang’oa nanga, kuna haja ya serikali kuketi chini mara kwa mara na waalimu na wataalamu kuhakikisha kwamba suala la ubora wa elimu na wala sio bora elimu linaangaziwa kwa kina.
Kwa kila mmoja anayepokea matokeo yake, hongera! Mfumo wa sasa unafahamika sana kwa ‘100 transition’. Ikiwa na maana kwamba haijalishi ulipata alama ngapi, utapata shule na ukikosa kujiunga na shule, chifu atakutafuta hadi kwenu na maafisa wa polisi. Mambo yamebadilika, sio kama kitambo ambapo wengi walikwepa masomo.
Imehaririwa na Asha Juma












