Wezi walivyopora benki fedha za kujenga mji mzima kwa saa 4 tu

Wezi walichimba shimo wakaingia ndani ya benki.

Chanzo cha picha, Gelsenkirchen Police

Maelezo ya picha, Wezi walichimba shimo wakaingia ndani ya benki
Muda wa kusoma: Dakika 3

Tukio hili limeelezewa kuwa moja ya wizi wa benki "wa ajabu" zaidi kuwahi kutokea nchini Ujerumani katika miaka ya hivi karibuni.

Ilikuwa mwishoni mwa wiki iliyotulia, muda mfupi baada ya sikuuu ya Krismasi, kundi la wezi liliingia katika benki iliyoko katika mtaa maarufu wa jiji la Gelsenkirchen magharibi mwa Ujerumani. Walitoboa ukuta wa benki hiyo kwa kutumia mashine za kuchimba zinazotumika viwandani.

Walifanikiwa kufungua zaidi ya masanduku 3,000 ya kuhifadhia mali (safe deposit boxes) na kuondoka na mamilioni ya euro.

Zaidi ya mwezi mmoja baadaye, polisi bado hawakuweza kumkamata hata mtu mmoja kuhusiana na tukio hilo.

Kwa wateja wa benki baadhi yao wakisema wamepoteza akiba zao zote za maisha, vito na mali za kifamilia, tukio hilo limeacha hasira, sintofahamu na mshtuko mkubwa.

Kuna hisia zilizoenea kwamba imani kwa taasisi za kibenki imeporomoka.

Tukio hili imeibua maswali magumu, baadhi yake yakiulizwa hadharani na waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la North Rhine-Westphalia, Herbert Reul.

Iliwezekanaje hakuna aliyegundua kilichokuwa kinaendelea? Je, kulikuwa na ushirikiano wa mtu wa ndani?

Vipi mashine za kuchimba hazikusikika? Na wezi walijuaje eneo halisi lenye hazina hiyo?

Ifoto yerekana uaho abajura binjiroye mu bubiko bwa banki

Chanzo cha picha, Gelsenkirchen Police

Je, mifumo ya ulinzi ya benki ilikuwa dhaifu?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Polisi wa jiji la Gelsenkirchen wamewataka yeyote mwenye taarifa kujitokeza kusaidia kupatikana kwa wezi hao.

Wachunguzi wanaamini kuwa wezi waliingia kupitia maegesho ya magari yaliyo karibu na benki hiyo.

Inaaminika pia walivunja ukuta karibu na maegesho hayo, yaliyo juu ya jengo la ghorofa kadhaa, kisha wakaingia kupitia mlango ulioko karibu na maegesho.

Kwa kawaida, mlango huo hauwezi kufunguliwa kutoka nje. Hata hivyo, wezi walifanikiwa kuingia.

Baada ya kupita mlango wa mbele, inaripotiwa walichimba ukuta wa karibu kati ya maegesho na benki.

Kutoka hapo, polisi wanaamini walikwepa mifumo kadhaa ya usalama, kisha wakaelekea kwenye chumba cha kumbukumbu kilichopo ghorofa ya chini karibu na chumba cha hazina (kinachohifadhi fedha na mali zingine).

Hapo waliweka mashine za kuchimba na kutoboa tundu la sentimita 40 kwenye ukuta unaoelekea kwenye chumba cha hazina ambako masanduku ya wateja yalihifadhiwa.

Kwa mujibu wa mamlaka, tukio hilo linaaminika kutokea kati ya Jumamosi, Desemba 27 na Jumatatu, Desemba 29. Pia inaaminika kuwa walikaribia kukamatwa muda mfupi kabla hawajafika kwenye hazina.

Muda mfupi baada ya saa 12:00 asubuhi Desemba 27, idara ya zimamoto ya Gelsenkirchen pamoja na kampuni binafsi ya ulinzi walipokea kengele ya moto kutoka benki hiyo, huenda ikiwa iliwashwa kwa bahati mbaya na wezi.

Polisi na zima moto 20 walifika saa 12:15 asubuhi, lakini hawakuona dalili zozote za uharibifu.

Herbert Reul alieleza kuwa kengele hiyo ilitoka ndani ya chumba cha hazina. Zima moto hawakuweza kuingia kwenye chumba hicho kwa sababu mlango ulikuwa umefungwa kwa mlango wa chuma.

Wakati walipofika hawakuona moshi wala harufu ya moto, hivyo wakadhani ilikuwa tahadhari ama ya uongo au bahati mbaya.

Aliongeza kuwa polisi hawakuwa na kibali cha kisheria (warrant) kufanya upekuzi benki kwa wakati huo, kwani jukumu lilikuwa la zimamoto na walihitaji amri ya mahakama.

Baadaye, walipoingia kwenye chumba cha hazina, iligundulika kuwa karibu masanduku yote 3,250 yalikuwa yamefunguliwa na pesa taslimu, dhahabu na vitu vingine vya thamani vilikuwa vimechukuliwa.

Rekodi za kompyuta zilionyesha kuwa kati ya muda wa sanduku la kwanza kuvunjwa na la mwisho ilikuwa saa 4. Haijulikani kama kazi ilikamilika ndani ya saa 4 au kama mfumo wa kurekodi ulisimama.

Mashahidi kadhaa waliripoti kuwaona wanaume wakibeba mifuko mikubwa usiku wa Desemba 28.

Vyombo vya habari vya Ujerumani vinakadiria kuwa walichukua takriban euro milioni 100.

Pesa hizi zilizoporwa zingetosha kujenga zaidi ya nyumba 5,000 za vyumba vitatu katika maeneo mengi ya Afrika Mashariki, zikigawiwa kwa thamani ya takriban dola 20,000 kila moja. Hii ni sawa na kujenga mji mzima wa makazi. Vinginevyo, kwa bei ya gari moja la Toyota IST takriban dola 6,000, pesa hizo zingetosha kununua zaidi ya magari 15,000 ya aina hiyo.

Kengele nyingine ya moto ilipopigwa Desemba 29, zima moto walikuta uharibifu mkubwa, na vitu vingi vikiwa vimetapakaa chini.

Baadhi ya wateja, wakiwemo walioporwa kiasi kikubwa cha dhahabu na fedha, wamefungua kesi dhidi ya benki wakidai uzembe.

Kila sanduku la kuhifadhia mali kwa kawaida huwa limekatiwa bima au fidia ya euro 10,300 tu.