Zambia yafichua kundi 'la kisasa' la uhalifu wa mtandaoni la China
Shirika la kisasa la utapeli kwenye mtandao limefichuliwa nchini Zambia, na kusababisha watu 77 kukamatwa, wakiwemo raia 22 wa China.
Yalikuwa "mafanikio makubwa katika vita dhidi ya uhalifu wa mtandao", mamlaka ilisema baada ya uvamizi dhidi ya shirika linalomilikiwa na Wachina.
Kampuni hiyo iliwaajiri Wazambia ambao waliamini wangekuwa mawakala wa kituo cha simu. Miongoni mwa vifaa vilivyokamatwa ni vifaa vinavyowaruhusu wapigaji kuficha mahali walipo na maelfu ya Sim kadi.
Kampuni ya Golden Top Support Services, iliyohushwa na uvamizi huo, haijatoa maoni yoyote kuhusu madai hayo.
Uvamizi huo katika majengo yake, yaliyoko Roma, kitongoji cha mji mkuu, Lusaka, uliongozwa na Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya (DEC) na pia ulihusisha polisi, idara ya uhamiaji na kitengo cha kupambana na ugaidi.
Hatua hiyo Ilikuja baada ya miezi kadhaa ya kukusanya taarifa za kijasusi na mashirika kufuatia ongezeko la kutisha la visa vya ulaghai kwenye mtandao nchini Zambia, mkurugenzi mkuu wa DEC Nason Banda alisema baada ya uvamizi huo wa Jumanne.