Mlipuko wa gesi Nairobi:Shughuli ya uokoaji yaendelea katika mkasa ulioua watu watatu na kuwajeruhi mamia

Lori lililokuwa limebeba mitungi ya gesi lililipuka katika wilaya ya Embakasi na "kuwasha moto mkubwa", msemaji wa serikali alisema.

Moja kwa moja

Asha Juma

  1. China yawanyonga wanandoa waliowatupa watoto 2 wachanga kutoka ghorofa ya 15

    ..

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Uchina imewaua wanandoa ambao waliwatupa watoto wawili nje ya dirisha la jengo la ghorofa.

    Zhang Bo - baba wa watoto - na Ye Chengchen hapo awali walipatikana na hatia ya kumuua msichana wa miaka miwili na mvulana wa mwaka mmoja mnamo 2020.

    Zhang alikuwa ameanza uchumba na Ye na baadaye akatalikiana na mke wake, na kuanza kupanga njama ya kuwaua watoto wake.

    Mahakama ya Juu ya Uchina ilikuwa imetaja nia za wanandoa hao kuwa "mbaya sana", ikiangazia "mbinu zao za kikatili".Wanandoa hao walinyongwa katika mji wa kusini-magharibi wa Chongqing siku ya Jumatano.

    Haijabainika wazi jinsi mauaji hayo yalivyotekelezwa, ingawa hukumu za kifo nchini China mara nyingi hutekelezwa kwa kudungwa sindano ya kuua au kupigwa risasi.

    Zhang alikuwa ameanza uhusiano "usiofaa" na Ye bila kumjulisha hali yake ya ndoa au ya mzazi, lakini Ye aliendelea kumuona baada ya kujua ukweli, mahakama ilisikiliza.

    Baada ya Zhang kuachana na mkewe mnamo Februari 2020, Ye bado aliwaona watoto hao wawili kama "vizuizi kwake kuolewa na Zhang na mizigo kwa maisha yao ya baadaye pamoja".

    Mara kwa mara walimshinikiza Zhang kutekeleza mauaji, ambayo walipanga njama kama kuanguka kwa bahati mbaya, mahakama ilielezwa Mnamo tarehe 2 Novemba 2020, Zhang aliwatupa watoto wake nje ya dirisha la nyumba yake kutoka ghorofa ya 15.

  2. Segun Aremu: Mfalme wa kitamaduni wa Nigeria auawa kwa kupigwa risasi na mkewe kutekwa nyara

    .

    Chanzo cha picha, OLUKORO OF KORO PALACE

    Maelezo ya picha, Segun Arem

    Watu wenye silaha wamemuua kwa kumpiga risasi mtawala wa kitamaduni, na kumteka nyara mke wake pamoja na mtu mwingine mmoja kusini-magharibi mwa Nigeria, mamlaka zilisema.

    Washambuliaji hao walivamia ikulu ya Segun Aremu - jenerali mstaafu wa jeshi na mfalme ambaye cheo chake rasmi ni Olukoro wa Koro - Alhamisi usiku.

    Haijabainika ni akina nani waliokuwa wamejihami kwa bunduki au kama wanadai fidia.

    Mauaji haya ya hivi punde na utekaji nyara yanakuja siku chache baada ya wanakampeni kudai hali ya hatari kushughulikia suala hilo.

    Baadhi ya mashirika 50 ya kiraia yanamtaka Rais Bola Tinubu kutoa tamko , wakisema zaidi ya watu 1,800 wametekwa nyara tangu aingie madarakani mwezi Mei mwaka jana.

    Akilaani mauaji ya Olukoro wa Koro katika jimbo la Kwara, kama "ya kutojali, ya kushangaza, na ya kuchukiza", Gavana AbdulRahman AbdulRazaq aliapa kwamba mamlaka itawakamata waliohusika.

    Polisi wanasema msako unaendelea.

  3. Mlipuko wa gesi Nairobi: Tazama video ya hasara iliosababishwa na mlipuko huo

    Maelezo ya video, Mlipuko wa gesi Nairobi: Tazama hasara iliosababishwa na mlipuko huo
  4. 'Niliona viungo vimetawanyika kila mahali',

    .

    Mlinzi aliyewaarifu watu katika jengo lake kuhusu mlipuko huo amekuwa akiiambia BBC jinsi mlipuko huo ulivyotokea.

    Obedi Kwamesa anasema kulikuwa na yadi iliyojaa lori na wasafirishaji karibu na gorofa yake.

    Majira ya saa 21:00 kabla hajalala, alisema lori lilikuja na gesi na kuegeshwa ndani ya yadi tayari kwa usambazaji siku ya Ijumaa.

    Bw Obedi anasema kulikuwa na kelele baadaye kwa watu kutoka nje ya nyumba zao kwa sababu lori la gesi lilikuwa limelipuka.

    "Sote tulitawanyika. Kulikuwa na mkanyagano huku moto ukienea. Baada ya muda kikosi cha zima moto kilikuja na kuanza kusaidia majeruhi," alisema.

    "Moto ulizidi kuwa mbaya zaidi kwa sababu baadhi ya nyumba pia zilikuwa na matangi ya gesi. Niliona viungo vimetawanyika. “Jamaa yangu aliungua na yuko hospitalini,” akasema Bw Obedi.

    .
  5. Video: Ndege zisizo na rubani za Ukraine zikiizamisha meli ya kivita ya Urusi kwa makombora

    Maelezo ya video, Bahari Nyeusi: Video inaonesha ndege zisizo na rubani za Ukraine zikiizamisha meli ya kivita ya Urusi
  6. Mlipuko Embakasi: Zaidi ya waathiriwa 20 waliojeruhiwa vibaya wapatiwa matibabu

    Waathiriwa 24 waliojeruhiwa vibaya ambao walipata majeraha ya moto zaidi ya 60% "wamehamishiwa katika hospitali kubwa zaidi kwa huduma maalum," mamlaka imesema.

    Kumi na saba wamepelekwa katika Hospitali ya Kufunza ya Chuo Kikuu cha Kenyatta huku wengine saba wakihamishiwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, serikali ya kaunti ya Nairobi ilisema.

    Zaidi ya manusura 160 kufikia sasa wameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kupokea matibabu katika hospitali za jiji hilo na kuzingatiwa kuwa hali zao zinaendelea vizuri.

    Kaunti hiyo ilisema kuwa manusura 143 waliruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Mama Lucy Kibaki na wengine 20 kutoka Hospitali ya Mbagathi.

  7. Habari za hivi punde, Tunachojua kufikia sasa kuhusu mlipuko wa Embakasi

    .

    Haya ndio tunayoyajua hadi sasa kuhusu mlipuko huo na matokeo yake:

    • Lori ambalo bado halijatambuliwa ambalo lilikuwa limesheheni gesi lililipuka mwendo wa saa 23:30 (20:30 GMT)
    • Silinda ya gesi inayoruka iligonga ghala la karibu ambalo huhifadhi nguo.
    • Moto huo ulizidi kuenea katika nyumba za makazi zilizo karibu na kuharibu magari kadhaa na mali za biashara
    • Watu kadhaa walinaswa kwenye nyumba zao kwani ilikuwa ni usiku sana
    • Polisi wamethibitisha vifo vitatu
    • Zaidi ya watu 250 walijeruhiwa
    • Takriban watu wengine 220 wamelazwa katika hospitali mbalimbali
    • Eneo la tukio sasa limezingirwa na dawati la ufuatiliaji limeanzishwa
  8. 'Msimamizi aligonga milango ya kila mtu kwa hasira'

    .

    Wakaazi wa eneo la makazi la Mradi huko Embakasi, Kusini Mashariki mwa Nairobi wameelezea kushuhudia matukio ya kutisha ya vitu vya chuma vilivyoruka ikiwa ni pamoja na sehemu za gari, mitungi ya gesi na kontena la usafirishaji kufuatia mlipuko mkubwa.

    Jackline Karimi mwenye umri wa miaka thelathini na tano aliambia BBC alikimbia nje ya nyumba na kulala kwenye lami, hatua ambayo huenda ilimuokoa.

    Alipata majeraha ya moto kwenye mkono wa kulia hadi begani na mguu wa kulia.

    "Nilimwona mwanamke akiwaka moto lakini hatukuweza kumsaidia. Kila mtu alikuwa akikimbia."

    Jackline alisema amesikia kuwa mwanamke huyo alifariki kutokana na majeraha yake.

    Mlipuko wa kwanza ulipotokea Jackline alisema kwamba mlinzi wa jengo hilo aligonga milango kwa hasira na kuwaamuru wakaazi watoke nje.

    "Watu walikuwa wakipiga kelele na wengine wakipiga kelele 'moto!'," Jackline alisema."Gesi ilikuwa inawaka katika sehemu tofauti ikichoma chochote ilichopata njiani."

  9. Habari za hivi punde, Serikali kuwalipia kodi ya nyumba watu ambao makao yao yaliharibiwa na mlipuko

    .

    Serikali inapanga kutoa kodi ya miezi miwili kwa manusura ambao nyumba zao zilibomolewa katika mlipuko huo, msemaji wa serikali Isaac Mwaura ameambia vyombo vya habari vya ndani.

    Bw Mwaura aliongeza kuwa akina mama tisa wasio na waume na watoto wao 21 wanahifadhiwa kwa muda katika shule ya mafunzo ya urubani iliyo karibu.

    .
  10. Lori lilikuwa likivuja kwa saa moja – Waathiriwa

    .

    Chanzo cha picha, bbc

    Waathiriwa wanasema lori lililohusika katika mlipuko huo lilikuwa likivuja kwa muda wa saa moja.

    Mmiliki kisha akajaribu kulianzisha, na ndio likasababisha mlipuko huo, wamenukuliwa wakisema.

    Ni miongoni mwa magari ambayo yaliharibiwa kabisa.

    Wachunguzi sasa wako kwenye eneo la tukio

  11. Mlipuko wa gesi Nairobi:Mwanamume ajeruhiwa wakati akitahadharisha wengine juu ya mlipuko,

    .

    Ben Malasi amezungumza na BBC kuhusu kile kilichompata usiku kucha.

    Anaishi karibu na mahali mlipuko ulitokea na alinaswa na moto alipokuwa akijaribu kutahadharisha umati wa watu wasisongee karibu na eneo la tukio.

    Anakumbuka alivyorushwa chini kwa mshindo mkubwa

    Ameungua vibaya kichwani na mikononi.

    Watu watatu wamethibitishwa kufariki na wengine wengi wamelazwa hospitalini wakiendelea kupata matibabu.

  12. Mlipuko wa gesi Nairobi: Polisi wamkamata mshukiwa wa kwanza - ripoti

    Polisi nchini Kenya wamemkamata mlinzi aliyekuwa akilinda kituo cha kushughulikia gesi wakati mlipuko huo ulipotokea, ripoti za ndani zinasema.

    Bado haijafahamika ni mashtaka gani huenda akakabiliwa nayo.

    Vyombo vya habari vya eneo hilo pia vinaripoti kuwa mamlaka inawatafuta makanika wawili ambao walionekana wakirekebisha gari karibu na eneo la mlipuko.

    Mafundi hao wanadaiwa kusababisha moto baada ya kuwasha gari walilokuwa wakitengeneza, kulingana na ripoti za tovuti ya Kenyans news, ikitaja wakazi waliokuwa wanatoa ushuhuda.

    .
  13. Mlipuko wa gesi Nairobi:Mamlaka ya kuthibiti Kawi Kenya (EPRA) ilikataa kutoa kibali cha ujenzi wa kiwanda cha gesi

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mamlaka ya kuthibiti kawi nchini Kenya (EPRA) imesema ilikataa kutoa kibali cha ujenzi wa kiwanda cha kujaza na kuhifadhi mitungi ya gesi ya kupikia katika eneo ambako mlipuko mkubwa umetokea jana usiku na kuua watu watatu huku wengine takriban 300 wakijeruhiwa.

    Kupitia taarifa, EPRA imesema ilipokea ombi la ujenzi wa kiwanda hicho tarehe 19 Machi 2023, Juni 20, 2023 na tarehe 31 Julai 2023 lakini maombi hayo yote yalikataliwa baada ya muombaji wa leseni kushindwa kuthibitisha mikakata ya kuwahakikishia usalama wakaazi wengi wanaoishi katika eneo hilo na pia kushindwa kutoa tathmini ya hatari ya kiwanda hicho kuwepo katika eneo la makazi.

    EPRA imesema uchunguzi wao kuhusu kilichotokea utasaidia kuvumbuachanzo cha mlipuko huo.

    .

    Soma zaidi:

  14. Tazama: Watu wanakimbia moto na moshi baada ya mlipuko mkubwa kutokea

    Maelezo ya video, Tazama: Watu wanakimbia moto na moshi baada ya mlipuko mkubwa

    Video inaonyesha moto mkubwa baada ya lori lililokuwa limebeba gesi kulipuka katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

    Watu watatu wameuawa huku wengine karibu 300 wakijeruhiwa katika mlipuko huo.

    Chanzo cha mlipuko huo bado kinachunguzwa.

    Moto huo unaripotiwa kuenea kupitia majengo kadhaa ya ghorofa.

    .
  15. Katika Picha: Uharibifu katika eneo la mlipuko wa gesi ulioua watu watatu na kuwajeruhi mamia

    .

    Lori lililokuwa limebeba mitungi ya gesi lililipuka katika wilaya ya Embakasi mwendo wa 23:30 (20:30 GMT), "na kuwasha moto mkubwa", msemaji wa serikali alisema.

    Moto huo umejeruhi mamia ya watu.

    .

    Nyumba, biashara na magari vimeharibiwa wakati moto mkubwa ukiwaka karibu na majengo ya ghorofa.

    .
    .
    Maelezo ya picha, Raia wakitazama maafa yaliyosababishwa na moto huo.
    .
    .

    Mashahidi waliambia vyombo vya habari kuwa walihisi tetemeko mara baada ya mlipuko huo.

    Soma zaidi:

  16. Mateka waachiliwa baada ya kuzuiliwa kwa saa tisa Uturuki

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wafanyakazi saba walioshikwa mateka katika kiwanda cha Proctor & Gamble (P&G) nje ya jiji la Uturuki la Istanbul waliokolewa baada ya saa tisa, maafisa wanasema.

    Polisi huko Gebza waliingia ndani baada ya mshukiwa ambaye inaonekana alikuwa akiandamana kwasababu ya vita huko Gaza kwenda chooni.

    Gavana wa eneo hilo Seddar Yavuz alisema kuwa mateka hao hawakupata majeraha yoyote.

    Picha mtandaoni zilionyesha mshukiwa, uso wake umefichwa na skafu ya Wapalestina, akiwa amevalia kile kinachoonekana kama fulana ya vilipuzi na akiwa amebeba bunduki.

    Alizuiliwa bila kujeruhiwa baada ya oparesheni iliyofanyika kwa "umakini mkubwa" ya uokoaji, Bw Yavuz aliongeza.

    Mtekaji nyara aliingia kwenye kiwanda karibu 15:00 saa za eneo (12:00 GMT), shirika la habari la DHA linaripoti. Mateka hao waliachiliwa muda mfupi kabla ya saa sita usiku.

    Maafisa wanasema mshukiwa huyo alitaka kuangazia hali inayoendelea Gaza.

    Imeripotiwa kuwa bendera ya Palestina ilichorwa na kupakwa rangi kwenye mlango wa jengo hilo ikiwa na maandishi yanayosema "milango itakuwa wazi kwa Gaza".

    Maafisa wa polisi walizingira njia ya kufikia kiwanda hicho na wafanyikazi wa matibabu walitumwa kwenye eneo la tukio.

    Maafisa wanasema uchunguzi mkubwa kuhusu tukio hilo unaendelea.

  17. Lewis Hamilton: Dereva wa Mercedes kujiunga na Ferrari mnamo 2025 kwa mkataba wa miaka mingi

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Lewis Hamilton ataondoka Mercedes mwishoni mwa msimu wa 2024 na kujiunga na wapinzani wa Formula One Ferrari kwa mkataba wa miaka mingi mnamo 2025.

    Dereva huyo wa magari yaendayo kasi mwenye umri wa miaka 39 alisaini mkataba mpya wa miaka miwili na Mercedes majira ya joto yaliyopita.

    Hata hivyo, inafahamika kuwa mkataba wake ulikuwa na kipengele cha mapumziko baada ya mwaka mmoja.

    Hamilton alisema "anajivunia" mafanikio aliyoyapata kwa miaka 11 akiwa na Mercedes.

    Bingwa huyo wa dunia mara saba aliongeza: "Mercedes imekuwa sehemu ya maisha yangu tangu nilipokuwa na umri wa miaka 13.

    “Ni sehemu ambayo nimekulia, hivyo kufanya uamuzi wa kuondoka ni moja ya maamuzi magumu ambayo nimewahi kufanya.

    "Lakini wakati umefika kwangu kuchukua hatua hii na ninafuraha kukabiliana na changamoto mpya."

    Kuondoka kwa Hamilton hadi timu ya Italia ni mojawapo ya uhamisho mkubwa wa madereva ambao Formula 1 haujawahi kuona - ikiwa sio mkubwa zaidi.

    Anatazamiwa kushirikiana na Charles Leclerc mnamo 2025, na kumwacha Mhispania Carlos Sainz akiwa kwenye mwaka wake wa mwisho kama dereva wa Ferrari.

    Hamilton alijiunga na Mercedes kutoka McLaren kwa msimu wa 2013 na kupata ubingwa wake mara sita kati ya saba akiwa na timu hiyo.

    Pia alishinda mara 82 ya rekodi yake ya mbio 103 akiwa na Silver Arrows.

    Pia unaweza kusoma:

  18. Mdukuzi wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Marekani ahukumiwa kifungo cha miaka 40 jela

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Afisa wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) amehukumiwa kifungo cha miaka 40 jela kwa kuvujisha hazina yenye thamani ya udukuzi kwenye jukwaa lisilo la kiserikali linalochapisha habari za siri zinazofichuliwa na watu wasiojitambulisha Wikileaks.

    Joshua Schulte pia alipatikana na hatia ya kuwa na picha za unyanyasaji wa watoto.

    Waendesha mashtaka wamemshutumu kwa kuvujisha zana za ujasusi "Vault 7", ambazo zinawaruhusu maafisa wa ujasusi kudukua simu mahiri na kuzitumia kama vifaa vya kusikiliza.

    Schulte, 35, alishirikisha nyaraka 8,761 kwa Wikileaks mwaka 2017, ambazo ni uvunjaji mkubwa zaidi wa data katika historia ya CIA, idara ya haki ya Marekani ilisema.

    Alikanusha madai hayo, lakini alihukumiwa kwa makosa mbalimbali katika kesi tatu tofauti huko New York mnamo 2020, 2022, na 2023.

    Siku ya Alhamisi, alihukumiwa kwa makosa ya ujasusi, udukuzi wa kompyuta, kudharau mahakama, kutoa taarifa za uongo kwa FBI na kupatikana na picha za unyanyasaji wa watoto.

    "Joshua Schulte alisaliti nchi yake kwa kufanya baadhi ya uhalifu wa kikatili na wa kutisha wa ujasusi katika historia ya Marekani," alisema Mwanasheria wa Marekani Damian Williams.

    Kulingana na ushahidi uliotolewa katika kesi hiyo, Schulte aliajiriwa kama msanidi programu katika Kituo cha Ujasusi cha Mtandao, ambacho kinafanya ujasusi wa mtandao dhidi ya mashirika ya kigaidi na serikali za kigeni.

    Waendesha mashtaka walisema kuwa mnamo 2016 alisambaza habari zilizoibiwa kwa Wikileaks na kisha kuwadanganya maafisa wa FBI kuhusu jukumu lake katika uvujaji huo.

    Walisema kuwa anaonekana kuchochewa na hasira juu ya mzozo wa mahali pa kazi.

    Schulte alikuwa na changamoto kufikia muda uliowekwa na Msaidizi wa Mwanasheria wa Marekani Michael Lockard alisema moja ya miradi yake ilikuwa nyuma sana ya muda huo na akapewa jina la utani la "Drifting Deadline".

    Waendesha mashtaka walisema alitaka kuwaadhibu wale aliowaona kuwa wamemdhulumu na wakasema katika "kulipiza kisasi hicho, alisababisha uharibifu mkubwa kwa usalama wa taifa hili".

    Wikileaks ilianza kuchapisha data iliyoainishwa kutoka kwa faili mnamo mwaka 2017.

    Soma zaidi:

  19. Marekani yawawekea vikwazo walowezi wa Israel juu ya ghasia za Ukingo wa Magharibi

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Joe Biden ameidhinisha vikwazo kwa walowezi wanne wa Israel wanaotuhumiwa kuwashambulia Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

    Bw Biden alitia saini amri pana ya utendaji, akisema ghasia katika Ukingo wa Magharibi zimefikia "viwango visivyovumilika".

    Vikwazo hivyo vinazuia watu binafsi kufikia mali yote ya Marekani, mali na mfumo wa kifedha wa Marekani.

    Ghasia katika Ukingo wa Magharibi zimeongezeka tangu Hamas ilipofanya mashambulizi dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba.

    Takriban Wapalestina 370 wameuawa katika Ukingo wa Magharibi tangu wakati huo, kulingana na UN. Wengi wao wameuawa na vikosi vya Israel lakini angalau wanane kati yao wameuawa na walowezi wa Israel, Umoja wa Mataifa ulisema.

    Amri hiyo mpya ya utendaji ina maana kuwa serikali ya Marekani ina uwezo wa kuwawekea vikwazo raia wowote wa kigeni wanaoshambulia, kuwatisha au kunyakua mali ya Wapalestina.

    Vikwazo hivyo ni vya kwanza kwa utawala wa Marekani - hatua adimu inayowalenga Waisraeli - na inakuja wakati Bw Biden anasafiri hadi jimbo la Michigan, ambalo lina wakazi wengi wa Kiarabu na Wamarekani ambao wamekuwa wakikosoa uungaji mkono wake kwa Israeli.

    Taasisi ya Kiarabu ya Marekani, ambayo ni kikundi cha utetezi, awali kilisema tangu kuanza kwa mzozo huo, uungwaji mkono wa Wamarekani wa Kiarabu kwa Chama cha Democratic umeshuka kutoka 59% mwaka 2020 hadi 17% tu.

    Soma zaidi:

  20. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 02/02/2024.