Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Ukraine inajaribu kuwatisha Warusi-Putin

Rais wa Urusi anasema mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya Moscow yalilenga raia, huku Ukraine ikikanusha kuhusika.

Moja kwa moja

  1. Tunakomea hapo kwa leo. Hadi kesho kwaheri.

  2. Iran yawafungulia mashtaka waandishi wa habari wanawake walioripoti kifo cha Mahsa Amini

    Waandishi wawili wa habari wa kike wa Iran waliosaidia kuchapisha kisa cha kifo cha Mahsa Amini akiwa kizuizini mwezi Septemba wamefikishwa Mahakamani.

    Niloufar Hamedi na Elaheh Mohammadi wameshtakiwa kwa "kushirikiana na serikali ya Marekani yenye uadui" na "propaganda dhidi ya utawala huo".

    Mume wa Bi Hamedi alisema kesi yake ilifunguliwa mjini Tehran siku ya Jumanne, siku moja baada ya Bi Mohammadi kuanza.

    Wanawake hao wanakanusha mashtaka na kusisitiza kwamba walikuwa wakifanya kazi zao tu.

    Mamlaka ya Iran imewatia mbaroni waandishi wa habari 75 tangu maandamano makubwa ya kuipinga serikali yalipoanza kote nchini kufuatia kifo cha Bi Amini,kulingana na Waandishi Wasio na Mipaka (RSF).Kumi na saba, akiwemo Bi Hamedi na Bi Mohammadi, bado wako gerezani.

    Bi Amini alifariki katika hospitali mjini Tehran tarehe 16 Septemba, siku tatu baada ya kuzuiliwa na polisi wa maadili kwa madai ya kuvaa hijabu yake "isivyofaa".

    Mashahidi walisema mwanamke huyo wa Kikurdi mwenye umri wa miaka 22 alipigwa akiwa kizuizini, lakini mamlaka ililaumu "kushindwa mshtuko wa moyo ghafla" kama sababu ya kifo chake.

    Bi Hamedi, mwanahabari mwenye umri wa miaka 30 wa gazeti la Sharq, alipiga picha babake Bi Amini na nyanyake wakikumbatiana.Aliichapisha kwenye Twitter na nukuu: "Nguo nyeusi ya maombolezo imekuwa bendera yetu ya kitaifa."

    Maelezo zaidi:

    • Mahsa Amini: Gharama ya kutangaza habari ya kifo iliyotikisa Iran
    • Jinsi mwanamke alivyokuwa ishara ya uasi nchini Iran
    • Je, kweli maandamano nchini Iran yanaweza kusababisha mabadiliko ya serikali?
  3. Rais anawaambia Wanigeria kuacha kununua mafuta kwa hofu

    Ofisi ya Rais mpya wa Nigeria Bola Tinubu imetoa wito kwa umma kuacha kununua kwa hofu kwani ruzuku ya mafuta haitaondolewa hadi mwisho wa mwezi Juni.

    Taarifa hiyo inalenga kukomesha machafuko yaliyosababishwa na kauli ya wakati wa kuapishwa kwake Jumatatu wakati aliposema ruzuku "itandolewa", lakini hakutoa muda au maelezo mengine.

    Taarifa hiyo inasema matamshi yake "sio mapya wala si hatua ya utawala wake mpya", ikieleza kuwa ruzuku ya miongo mingi ilifadhiliwa hadi mwisho wa Juni.

    "Alikuwa akiwasilisha tu hali ilivyo, ikizingatiwa kuwa bajeti ya utawala uliopita ya ruzuku ya mafuta ilipangwa na kuidhinishwa kudumu kwa nusu ya kwanza ya mwaka," ilisema.

    "Kwa hakika, hii ina maana kwamba kufikia mwisho wa Juni, serikali kuu itakuwa haina fedha za kuendeleza utawala wa ruzuku, ikimaanisha kukomeshwa kwake.

    “Ununuzi wa hofu ambao umetokea kutokana na mawasiliano hauhitajiki; haitafanya kazi mara moja.”

    Baadhi ya watu wamechapisha video mtandaoni wakionyesha jinsi vituo vya mafuta zilivyopandisha bei bidhaa hiyo, wakati mwingine kwa zaidi ya asilimia 200.

    Taarifa kutoka kwa rais iliongeza kuwa mpango wa Bw Tinubu ulikuwa kuelekeza pesa zilizotumiwa kwa ruzuku hiyo "katika mipango ya uwekezaji wenye manufaa".

    "Hii inajumuisha sio uwekezaji katika miundombinu ya umma, elimu, huduma za afya na kazi ambazo zitaboresha maisha ya mamilioni ya Wanigeria na kuongeza uwezo wao wa mapato."

  4. Rais wa Eritrea atua nchini Urusi kwa mwaliko wa Putin

    Rais wa Eritrea Isaias Afwerki ametua mjini Moscow kwa ziara rasmi ya siku nne nchini Urusi kwa mwaliko wa rais Vladimir Putin.

    Mawaziri wa mambo ya nje na utamaduni pia wako kwenye ziara hiyo, Waziri wa Habari Yemane Meskel anasema kwenye Twitter.

    Eritrea na Urusi zina uhusiano mzuri - na Eritrea ni mojawapo ya nchi chache ambazo zimepiga kura dhidi ya azimio la Umoja wa Mataifa kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

    Rais Isaias, ambaye hivi majuzi alirejea kutoka ziara rasmi nchini China, ameitawala Eritrea tangu ilipojinyakulia uhuru wake kutoka kwa taifa jirani la Ethiopia mwaka 1993.

    Nchi hiyo, taifa la chama kimoja na jamii inayoongozwa kijeshi, inashikilia eneo muhimu kimkakati katika Pembe ya Afrika - na haijawahi kufanya uchaguzi wa kitaifa.

    Bw Isaias alilakiwa katika uwanja wa ndege alipowasili na naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Bw Yemane alitweet.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov, ambaye kwa sasa yuko katika ziara ya Afrika iliyoanza nchini Kenya Jumatatu, alitembelea Eritrea mwezi Januari.

  5. Tazama: Video inaonekana kuonyesha ndege isiyo na rubani ikiruka katika viunga vya jiji la Moscow

    Kanda za video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonekana kuonyesha ndege isiyo na rubani ikiruka Il'inskii, kusini mashariki mwa Moscow.

    Majengo kadhaa yameharibiwa katika mji mkuu wa Urusi baada ya ulinzi wa anga kuangusha ndege zisizo na rubani. Hilo ni tukio la pili la ndege zisizo na rubani mjini Moscow baada ya shambulio linalodaiwa kufanywa dhidi ya Kremlin mapema mwezi Mei.

    Shambulizi hilo limetokea kufuatia shambulizi la Urusi katika mji mkuu wa Ukraine wa Kyiv, ambapo mtu mmoja aliuawa.

  6. Teknolojia ya akili bandia inaweza kuchangia kuangamia kwa binadamu, wataalamu waonya

    Teknolojia ya Akili Bandia inaweza kusababisha kutoweka kwa binadamu, wataalam wakiwemo wakuu wa OpenAI na Google Deepmind wameonya.

    Makumi ya wataalamu wameunga mkono taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa wavuti wa Kituo cha Usalama wa AI.

    "Kupunguza hatari ya kutoweka kwa binadamu kutokana na teknolojia ya akili bandia kunapaswa kuwa kipaumbele cha ulimwengu pamoja na hatari zingine za kijamii kama vile milipuko na vita vya nyuklia" ilesema sehemu ya ripoti hiyo Lakini wengine wanasema hofu hiyo imetiwa chumvi.

    Sam Altman afisa mkuu mtendaji mkuu wa ChatGPT OpenAI, Demis Hassabis mtendaji mkuu wa Google DeepMind na Dario Amodei wa Anthropic wote wameunga mkono taarifa hiyo.

    Geoffrey Hinton, ambaye alitoa onyo la awali kuhusu hatari ya AI, pia ameunga mkono wito huo. Yoshua Bengio, profesa wa sayansi ya kompyuta na chuo kikuu cha Montreal pia alitia saini.

    Dkt Hinton, Prof Bengio na Profesa wa NYU Yann LeCunn wamekuwa wakitajwa kama "godfathers wa AI" kwa kazi yao ya mufti - ambayo kwa pamoja walishinda Tuzo ya Turing ya 2018 - ambayo inatambua mchango bora katika sayansi ya kompyuta. Lakini Prof LeCunn, ambaye pia anafanya kazi na kampuni ya Meta, amesema onyo hilo limezidishwa kupita maelezo.

    Wataalamu wengine pia wanaamini kwamba hofu ya AI kuangamiza binadamu si ya kweli wakiongeza kuwa ni njama ya kusambaratisha teknolojia hiyo kwa kupendelea mifumo ambayo tayari ni tatizo.

  7. Urusi kushiriki katika mkutano wa kilele wa Afrika Kusini 'katika ngazi ifaayo'

    Akihojiwa iwapo kiongozi wa Urusi Vladimir Putin atahudhuria mkutano wa Brics nchini Afrika Kusini mwezi Agosti, msemaji wa Kremlin amesema Urusi itashiriki "katika ngazi ifaayo".

    Rais wa Urusi alialikwa kwenye mkutano huo mapema mwaka huu, lakini waranti iliyotolewa baadaye na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa jinai (ICC) inamaanisha Afrika Kusini ingetarajiwa kumkamata iwapo atahudhuria.

    Muungano wa Brics unawakilisha baadhi ya mataifa yenye uchumi unaokua duniani, ikiwa ni pamoja na Brazil,Urusi, China, India na Afrika Kusini.

    "Urusi inatilia maanani sana maendeleo ya muundo huu wa ushirikiano. Na Urusi itashiriki katika mkutano huu kwa kiwango kinachofaa," msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema katika mkutano huo.

    Kulingana na shirika la habari la Urusi la Tass, Bw Peskov aliahidi kutoa "maelezo yote" baadaye.

    Alipobanwa zaidi kuhusu hati ya kukamatwa, Reuters ilimnukuu akisema: "Bila shaka tunahesabu kama kiwango cha chini kabisa kwa nchi washirika katika muundo muhimu kama huo ambao hauongozwi na maamuzi hayo haramu."

    Afrika Kusini imetoa kinga ya kidiplomasia kwa maafisa wanaohudhuria mkutano huo, lakini msemaji wa maswala ya kigeni aliongeza kuwa kinga hizo ni za kawaida kwa mikusanyiko ya kimataifa na hazikufutilia mbali vibali vilivyotolewa na mahakama za kimataifa.

    Bw Putin ameshutumiwa na ICC kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu uliofanywa wakati wa vita nchini Ukraine.

    Afrika Kusini imekataa kulaani uvamizi wa Urusi, ikisisitiza kuwa inataka kutoegemea upande wowote.

    Maelezo zaidi:

    • https://www.bbc.com/swahili/articles/cj5ezz1n53ro
    • Afrika inaongoza juhudi za amani kati ya Urusi-Ukraine - Ramaphosa
    • Kwa nini jeshi la wanamaji la Afrika Kusini linajiunga na Urusi na China kwa mazoezi?
  8. Putin asema Ukraine inajaribu kuwatia hofu Warusi

    Rais wa Urusi Vladimir Putin amejibu mashambulizi ya Jumanne ya droni kwenye mji mkuu wa Moscow, akiishutumu Ukraine kwa kujaribu kuwatia hofu Warusi.

    Alisema raia walilengwa, lakini ulinzi wa anga ulishughulikia tishio hilo kwa njia ya kuridhisha.

    Wizara ya ulinzi ilisema takriban ndege nane zilisababisha uharibifu mdogo, lakini Kyiv imekana kuhusika.

    Hii ni mara ya kwanza kwa mji huo kulengwa na ndege nyingi zisizo na rubani tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

    Shambulio la droni Moscow: Urusi yaishtuhumu Ukraine kwa shambulio la 'kigaidi'

    Huku hayo yakiarifiwa Urusi imeishutumu Ukraine kwa kufanya shambulizi la ndege zisizo na rubani mjini Moscow mapema asubuhi ya leo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa mji huo kulengwa na ndege nyingi zisizo na rubani tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

    Wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema Kyiv ilifanya "shambulio la kigaidi" kwa kutumia ndege nane zisizo na rubani na kusababisha uharibifu mdogo wa majengo kadhaa.

    Meya wa Moscow Sergei Sobyanin alisema hakuna mtu aliyejeruhiwa vibaya.

    Ukraine imekanusha kuhusika mashambulizi hayo ya ndege zisizo na rubani.

    Mshauri wa rais Mykhailo Podolyak alisema kuwa Kyiv haikuhusika moja kwa moja, lakini Ukraine ilifurahia kufuatilia yaliyojiri na kutabiri ongezeko la matukio hayo.

    Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema ndege zote nane zisizo na rubani zimenaswa.

    "Tatu kati ya ndege hizo zilikabiliwa na vita vya kielektroniki, kupoteza udhibiti na kupoteza mwelekeo wa malengo yaliyokusudiwa. Ndege zingine tano zisizo na rubani zilidunguliwa na mfumo wa makombora wa kutoka ardhini hadi angani wa Pantsir-S katika mkoa wa Moscow," wizara hiyo ilisema.

    Ripoti za awali za vyombo vya habari vya Urusi zilisema kwamba ndege 30 zisizo na rubani zilihusika na shambulio hilo.

    Mamlaka pia imesema baadhi ya ndege hizo zilianguka kwenye majengo baada ya kudunguliwa.

    Bw Sobyanin alisema kuwa baadhi ya wakazi walikuwa wamehamishwa lakini baadaye wakaruhusiwa kurejea nyumbani.

    Mashambulizi hayo ya angani yalikumba baadhi ya vitongoji mashuhuri vya Moscow. Maeneo yaliathiriwa ni pamoja na Leninsky Prospekt, boulevard kuu iliyoundwa chini ya Josef Stalin.

    Sehemu ya magharibi mwa Moscow ambako Rais wa Urusi Vladimir Putin ana makazi, pamoja na watu wengine mashuhuri wa Urusi, pia ilipigwa.

    Baadhi ya wanasiasa wamenukuliwa na shirika la habari la Urusi Tass wakisema kuwa mashambulizi hayo ya ndege zisizo na rubani yalikusudiwa kuzua hofu, lakini jaribio hilo halikufikiwa.

    Putin amefahamishwa kuhusu uvamizi huo na amekuwa akifanya kazi katika Ikulu ya Kremlin, msemaji wake aliripoti.

    Msaidizi wa muda mrefu wa rais, Dmitry Peskov, pia alisema ulinzi wa anga wa Moscow na wizara ya ulinzi zimefanya kazi vizuri.

    Soma zaidi:

  9. Malaysia inashikilia meli ya Uchina inayoshukiwa kupora mabaki ya meli za WW2 za Uingereza

    Malaysia imeizuilia meli iliyosajiliwa na Uchina inayoshukiwa kupora meli mbili za Uingereza katika Vita vya Pili vya Dunia.

    Meli hiyo kubwa ilikamatwa Jumapili kwa kutia nanga kinyume cha sheria katika eneo la Bahari ya Kusini ya China.

    Risasi zinazoaminika kuwa kutoka kwa HMS Prince of Wales na HMS Repulse, ambazo zilizamishwa na vikosi vya Japan zaidi ya miaka 80 iliyopita, zilipatikana kwenye boti.

    Wizara ya Ulinzi ya Uingereza hapo awali ililaani uvamizi huo unaodaiwa kuwa ni"unajisi" wa makaburi ya vita vya baharini.

    Meli za Uingereza, zilizo kwenye bahari ya kilomita 100 (maili 60) kutoka pwani ya mashariki ya Malaysia, zilikuwa zikilengwa kwa miongo kadhaa.

    Meli za kivita za Royal Navy zilitumwa Singapore wakati wa vita ili kuimarisha ulinzi wa Malaysia.Zilizamishwa na makombora ya Kijapani mnamo 10 Desemba 1941.

  10. Afrika Kusini yatia saini kinga ya kidiplomasia kabla ya mkutano wa BRICS

    Afrika Kusini imetia saini kinga ya kidiplomasia kwa maafisa wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi tano zenye uchumi unaokua kwa haraka - BRICS na mkutano wa kilele utakaofanyika mwezi Agosti.

    Hii inafungua milango kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin kuhudhuria, baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), kutoa hati ya kukamatwa kwake inayohusiana na uhalifu dhidi ya binadamu kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

    Ziara iliyopangwa kufanywa na Rais wa Urusi Vladimir Putin nchini Afrika Kusini kwa mara nyingine tena imeiweka nchi hiyo katikati ya utata kuhusu wajibu wa kumkamata rais ambaye bado yuko madarakani.

    Idara ya uhusiano wa kimataifa ya Afrika Kusini ilichapisha katika gazeti rasmi la serikali siku ya Jumatatu ikitambua mikutano miwili ambayo itakuwa na kinga ya kidiplomasia.

    Hii ni pamoja na mkutano wa 15 wa kilele wa BRICS utakaofanyika Johannesburg mwezi Agosti.

  11. Bernice Kariuki ajiuzulu kama mpishi wa timu ya Arsenal

    Mpishi mashuhuri nchini Kenya Bernice Kariuki ametangaza kuacha kazi Arsenal, timu ya soka ya Ligi Kuu ya Uingereza baada ya miaka miwili.

    Chini ya uongozi wa mpishi mkuu wa Arsenal, Kariuki amekuwa mpishi wa wachezaji wa kikosi cha kwanza, uongozi na benchi wataalamu wa ufundi la klabu hiyo.

    Akitangaza kuondoka kwake kupitia mtandao wa kijamii Jumapili, alisema kampeni ya Arsenal 2022/2023 ndio ilikuwa mwaka wao mzuri zaidi,akibainisha kuwa ilikuwa jambo la kufurahisha kufanya kazi kwa klabu hiyo.

    "Siku ya mwisho inashamiri. Ilimaliza msimu kwa kishindo! Bora zaidi!!! Arsenal… Arsenal… Arsenal.. 2020/2023 msimu bora zaidi kuwahi kutokea ninapoondoka kama mpishi wa kujivunia, imekuwa heshima kufanyia kazi klabu bora zaidi duniani… kwa unyenyekevu!” aliandika.

    Mpishi huyo pia aliwashukuru Wakenya kwa kumuunga mkono, na kuongeza: "Baraka zaidi katika kazi yangu ijayo ni kama ndoto ya kifalme... Asanteni sana hasa nchi yangu."

    Kariuki alijiunga na Arsenal katikati ya 2021, baada ya Mikel Arteta kuteuliwa kama meneja wa Arsenal, kama mpishi wa kibinafsi wa kikosi cha kwanza.

    Pia alisimamia ustawi wa kila siku na lishe ya timu kabla na baada ya mechi, na pia menyu za timu inayosafiri.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Mwanaume anusurika kifo kwa kujinasua kutoka kinywa cha mamba Australia

    Mwanamume mmoja raia wa Australia amenusurika kifo baada ya kushambuliwa na mamba wa maji ya chumvi alipokuwa mapumzikoni katika hoteli moja huko Queensland.

    Marcus McGowan, mwenye umri wa miaka 51, ameeleza kwa kina jinsi alivyoweza kukinasua kichwa chake kutoka kinywa cha mamba huyo lakini alipata majeraha.

    Alisafirishwa kwa ndege hadi hospitali ya kisiwa kilicho karibu, na baadaye akasafirishwa hadi Cairns kwa matibabu zaidi.

    Mashambulizi ya mamba si ya kawaida nchini Australia, lakini kumekuwa na ongezeko la visa kama hivyo katika miezi ya hivi karibuni.

    Bw McGowan alisema alikuwa majini na kundi la watu yapata kilomita 28 (maili 17.3) kutoka Kisiwa cha Haggerstone karibu na Cape York alipoumwa kwa nyuma.

    "Nilidhani ni papa lakini nilipofika juu, niligundua kuwa ni mamba. Niliweza kufungua taya zake kwa umbali wa kutosha kunitoa kichwa," alisema katika taarifa.

    Mamba - anayeshukiwa kuwa mchanga - alirudi kwa safari nyingine, alisema, lakini aliweza kumsukuma, akiuma mkono wake.

    Idara ya mazingira ya Queensland inasema itachunguza tukio hilo, lakini "mamba katika bahari ya wazi wanaweza kuwa wagumu kuwapata kwani wanyama hao mara nyingi husafiri makumi ya kilomita kwa siku".

  13. Habari za hivi punde, Urusi yadai Ukraine imehusika na shambulizi la ndege zisizo na rubani Moscow

    Shambulio la ndege zisizo na rubani katika mji mkuu wa Urusi Moscow limeanzishwa na Ukraine, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema.

    Shirika la habari la Reuters limeripoti wizara ya ulinzi ya Urusi likisema: "Leo asubuhi, utawala wa Kyiv ulianzisha shambulio la ndege za kigaidi zisizo na rubani kwenye maeneo yaliyolengwa katika jiji la Moscow.

    "Ndege tatu kati yao zilikabiliwa na shambulizi la vifaa vya kielektroniki, zikapoteza udhibiti na kugeuza muelekeo kutoka maeneo yaliyokuwa yamekusudiwa.

    "Droni nyingine tano zilidunguliwa na mfumo wa makombora wa kutoka ardhini hadi angani wa Pantsir-S katika mkoa wa Moscow."

    Hakuna taarifa zozote za vifo zilizoripotiwa.

    Hata hivyo, Ukraine haijakiri hadharani kuanzisha mashambulizi dhidi ya maeneo lengwa ndani ya Urusi.

    Soma zaidi:

  14. Sheria ya Uganda dhidi ya wapenzi wa jinsia moja yapingwa mahakamani

    Ombi la mahakama la kupinga sheria mpya iliyotiwa saini dhidi ya wapenzi wa jinsia moja nchini Uganda limewasilishwa.

    Bunge la Uganda lilitangaza kuwa rais Yoweri Museveni ametia saini mswada huo kuwa sheria siku ya Jumatatu.

    Ilipitishwa kwa mara ya kwanza mnamo Machi lakini ulirudishwa bungeni kufanyiwa marekebisho.

    Ombi hilo linasema kuwa sheria hiyo ni kinyume na inapinga haki ya kutobaguliwa, kwa kuharamisha mahusiano ya watu wa jinsia moja.

    Sheria hiyo mpya inataja kifungo cha maisha kwa wale wanaopatikana na hatia ya kufanya mapenzi ya jinsia moja.

    Walalamishi hao kutoka Jukwaa la Uhamasishaji na Ukuzaji wa Haki za Binadamu wanaongeza kuwa sheria hiyo ilipitishwa bila kuwapa nafasi walio wachache kutoa maoni yao wakati ilipokuwa ikipitiwa na kamati ya sheria ya bunge.

    Sheria hiyo imeshtumiwa pakubwa, na taarifa kutoka kwa wafadhili wakuu wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na UN AIDS, ikisema kuwa kuna uwezekano wa kufanya iwe vigumu kwa watu walio katika na mahusiano ya jinsia moja kupata huduma za afya zinazookoa maisha.

    Awali, mswada huo ulikuwa umeharamisha kuwatambua walio wachache kijinsia, lakini hii ilirekebishwa baada ya Rais Museveni kudai kuwa ingesababisha kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa watu kutokana na muonekano wao.

    Sheria sawa na hiyo dhidi ya wapenzi wa jinsia moja ilitupiliwa mbali na mahakama ya kikatiba ya Uganda mwaka 2014, kwa kupitishwa bila akidi inayotakiwa bungeni.

    Soma zaidi:

  15. Mzozo wa Sudan: Marekani, Saudi Arabia zaafiki muda wa kusitisha mapigano Sudan

    Marekani na Saudi Arabia zimeafiki kurefushwa kwa makubaliano ya muda wa kusitisha mapigano kati ya pande zinazozohasimiana nchini Sudan kwa siku nyingine tano.

    Serikali za Washington na Riyadh zilitangaza makubaliano ya hivi punde zaidi, na vile vile kuafikiana kuhusu makubaliano ya wiki moja iliyopita.

    Katika taarifa yao ya pamoja, wamekiri kwamba usitishaji mapigano haujazingatiwa kikamilifu, lakini wakasema umeruhusu kufikishwa kwa misaada kwa watu milioni mbili nchini Sudan.

    Shirika la Mpango wa Chakula Duniani lilisema kuwa hali ya utulivu katika mapigano iliiruhusu kutuma vifaa kwa wakazi waliokwama katika mji mkuu, Khartoum, kwa mara ya kwanza tangu mapigano yalipozuka wiki sita zilizopita.

    Jeshi la Sudan na wapinzani wake kutoka kikosi cha dharura wameshutumiana kwa ukiukaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya usitishaji mapigano, hasa katika eneo la Darfur.

    Unaweza pia kusoma:

    • Mapigano Sudan: Hakuna mazungumzo mpaka mashambulio ya mabomu yakome, Hemedti aiambia BBC
    • Omar al-Bashir: Hivi ndivyo Sudan inavyolipa gharama za mateso ya miaka 30 ya utawala wake
    • Mzozo wa Sudan: Mgogoro wa Sudan unaweza kuisha kwa njia hizi tatu
  16. Kosovo: Mapigano mapya yaibuka huku wanajeshi wa Nato wakiitwa kuingilia kati katika miji ya kaskazini

    Nato imelaani mashambulio ambayo inasema "hayakubaliki kabisa" ya waandamanaji huko Kosovo yaliyowajeruhi walinda amani wake 25.

    Polisi na wanajeshi wa Nato walikabiliana na waandamanaji wa Serbia kaskazini ambapo kumekuwa na ghasia kuhusu uteuzi wa mameya wa kabila la Albania.

    Mabomu ya kutoa machozi na maguruneti vilitumiwa kuwazuia waandamanaji wa Zvecan, baada ya kujaribu kuvamia jengo la serikali.

    Wanajeshi wa Nato pia walitengeneza uzio wa usalama kuzunguka kumbi nyingine mbili mjini humo.

    Mgogoro huo ulianza Aprili wakati Waserbia wa Kosovo waliposusia uchaguzi wa mitaa, na hivyo kuwaruhusu jamii ya Waalbania kuchukua udhibiti wa mabaraza ya mitaa ambapo

    Muungano wa Ulaya na Marekani zimeishutumu mamlaka ya Kosova kwa kuyumbisha hali ya mambo huko Kosovo kaskazini, na kuonya dhidi ya vitendo vyovyote vinavyoweza kuchochea mivutano ya kikabila huko.

    Kosovo ilitangaza uhuru wake kutoka kwa Serbia mnamo mwezi wa Februari 2008, baada ya miaka mingi ya uhusiano mbaya kati ya Waserbia wake na wenyeji walio wengi wa jamii ya Waalbania.

    Imetambuliwa na Marekani na nchi kuu za Umoja wa Ulaya, lakini Serbia, ikiungwa mkono na mshirika wake mwenye nguvu Urusi, inakataa kufanya hivyo, kama wafanyavyo wale wa kabla la Waserbia walio wengi ndani ya Kosovo.

  17. Foxconn: Wafanyakazi wa iPhone kuongezewa malipo kabla ya uzinduzi wa muundo mpya

    Msambazaji wa Apple Foxconn anaongeza juhudi za kuwaajiri wafanyakazi zaidi kwa ajili ya kiwanda kikubwa zaidi cha iPhone, kabla ya uzinduzi wa toleo la muundo wake mpya wa simu.

    Faxconn inasema wafanyakazi wapya katika kiwanda chake kilichopo Zhengzhou, Uchina watapokea marupurupu ya hadi yuan 3,000 (sawa na $424; £343) kwa angalau siku 90 za kazi.

    IPhone 15 inatarajiwa kuzinduliwa mnamo mwezi wa Septemba.

    Inaashiria hatua ya hivi punde zaidi ya mtengenezaji wa Taiwan kuboresha maslahi kwa wafanyakazi wake katika kiwanda kikubwa - kinachojulikana kama iPhone City.

    Wafanyakazi wa Foxconn wanaowaelekeza kazi waajiriwa wapya sasa watapokea yuan 500 ikiwa mtu huyo atakaa katika kampuni hiyo kwa mwezi mmoja, taarifa iliyoshuhudiwa na BBC kwenye programu maarufu ya ujumbe wa China WeChat lilisema.

    Kampuni hiyo haikujibu mara moja ombi la BBC la kutoa maoni kuhusu taarifa hizi.

    Mwaka jana, mamia ya wafanyakazi waliandamana katika kiwanda cha iPhone cha Zhengzhou kutokana na vizuizi vya Covid na madai ya malipo kuchelewa.

  18. Kwa picha: Jinsi wakazi wa Kiev walivyojificha wakati wa shambulio la roketi la Urusi

    Zaidi ya wakaazi 40,000 wa mji wa Kiev walikimbilia alasiri hii katika leri ya chini ya ardhi kujificha kutokana na makombora ya jeshi la Urusi. Hii zi ni baadhi ya picha za baadhi yao:

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi:

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  19. Vita vya Ukraine: Mashambulizi ya anga ya Urusi yanalenga Kyiv kwa usiku wa tatu mfululizo

    Milipuko ilisikika mjini Kyiv na majengo kadhaa kuteketezwa kwa moto baada ya Urusi kuulenga mji mkuu huo wa Ukraine kwa usiku wa tatu mfululizo kwa mashambuzi.

    Maafisa wanasema vifusi vya majengo vinavyoanguka vilisababisha moto huo, huku ulinzi wa anga wa Ukraine ukiyalenga makombora yanayokuja. Takriban mtu mmoja anaripotiwa kuuawa.

    Ukraine inasema ilidungua makombora na ndege zisizo na rubani zilizotumika katika mashambulio mawili ya awali ya usiku ya Urusi.

    Rais Volodymyr Zelensky amepongeza ulinzi wa anga wa Patriot unaofanywa na Marekani.

    Alisema walihakikisha makombora yote ya Urusi yanaangushwa kwa "100% ".

    "Urusi inataka kufuata njia ya uovu hadi mwisho, yaani, kushindwa kwake, kwa sababu uovu hauwezi kuwa na mwisho mwingine isipokuwa kushindwa," alisema katika hotuba ya video siku ya Jumatatu.

    "Ulimwengu lazima uone kwamba ugaidi unapotea."

    Wakati huo huo, mkuu wa ujasusi wa kijeshi wa Ukraine, Jenerali Kyrolo Budanov, alionya juu ya jibu la haraka kwa mashambulio ya Urusi.

    Jeshi la Urusi limesema kuwa maeneo yote yaliyokusudiwa kupigwa yalipigwa wakati wa mashambulizi yake ya hivi majuzi dhidi ya Kyiv na miji mingine ya Ukraine.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi:

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  20. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya mubashara ya leo tarehe 30.05.2023