Mzozo wa Sudan:Mahasimu wa Sudan wakubaliana 'kimsingi' kusitisha mapigano kwa wiki moja

Ghasia kati ya jeshi na Wanajeshi wa (RSF) sasa ziko katika wiki yake ya tatu - huku kila upande ukishutumu mwingine kwa kukiuka makubaliano ya hapo awali.

Moja kwa moja

Ambia Hirsi

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Hadi kesho kwaheri.

  2. Mlinzi aliyemuua waziri wa Uganda alipewa kazi mwezi mmoja uliopita

    th

    Chanzo cha picha, Alamy

    Mwanajeshi wa Uganda aliyempiga risasi na kumuua Charles Okello Engola, naibu waziri wa jinsia na leba ametambuliwa kwa jina la Wilson Sabiiti.

    Alikuwa ametumwa kutoa ulinzi kwa waziri huyo mwezi mmoja uliopita.

    Wakati wa tukio hilo nyumbani kwa Kanali Engola Jumanne asubuhi, Private Sabiiti pia alimjeruhi msaidizi wa waziri mkuu Lt Ronald Otim.Kwa sasa anapokea matibabu katika Hospitali ya Mulago katika mji mkuu, Kampala.

    Mwanajeshi huyo anaripotiwa kufyatua risasi hewani katika eneo la tukio kabla ya kujiua .

  3. Katika picha: Mabomu ya machozi na matairi kuchomwa nchini Kenya

    Polisi wa kutuliza ghasia katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, wamewarushia vitoa machozi wabunge wa upinzani wakati wa maandamano ya hivi punde dhidi ya serikali kuhusu gharama ya juu ya maisha na uchaguzi wa mwaka jana wenye utata.

    Mabomu ya machozi pia yalipigwa katika mtaa wa mabanda wa Kibera, ngome ya mwanasiasa mkongwe wa upinzani Raila Odinga:

    Maandamano

    Chanzo cha picha, AFP

    Na katika mji wa magharibi wa Kisumu, pia ngome ya Bw Odinga:

    O

    Chanzo cha picha, Reuters

    M

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wabunge hao walikuwa wakitaka kuwasilisha ombi kwa Rais William Ruto kuhusu kile walichokitaja kuwa gharama ya juu isiyokubalika ya chakula, mafuta na umeme.

    Magari kadhaa yalichomwa jijini Nairobi, ambapo maafisa wengi wametumwa baada ya polisi kutaka kupiga marufuku maandamano hayo:

    Polisi Kenya

    Chanzo cha picha, AFP

    Magari yaliyoteketezwa

    Chanzo cha picha, AFP

    Vijana pia walichoma matairi ili kuziba barabara katika vitongoji duni kadhaa:

    R

    Chanzo cha picha, AFP

    Vijana

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mbinu hiyo hiyo ilitumika kuziba barabara za ndani na nje ya Kisumu.

    Bw Odinga na Rais Ruto walikuwa wamekubali kushughulikia mvutano wa kisiasa kupitia mazungumzo baada ya maandamano ya upinzani mwezi Machi kukumbwa na ghasia. Lakini mchakato huo umekwama kutokana na kutoelewana kuhusu nani anafaa kujumuishwa katika mazungumzo hayo.

  4. Mahasimu wa Sudan wakubaliana 'kimsingi' kusitisha mapigano kwa wiki moja

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Majenerali wanaopigana nchini Sudan wamekubaliana "kimsingi" usitishaji vita wa wiki moja kuanzia Alhamisi, wizara ya mambo ya nje katika nchi jirani ya Sudan Kusini, mojawapo ya nchi zinazoongoza juhudi za amani, imesema.

    Wakati hivi sasa kuna makubaliano ya kuzuia vita kwa siku tatu , mapigano yameendelea, huku mzozo mkubwa wa kibinadamu ukikaribia.

    th

    Ghasia kati ya jeshi na Wanajeshi wa (RSF) sasa ziko katika wiki yake ya tatu - huku kila upande ukishutumu mwingine kwa kukiuka makubaliano ya hapo awali.

    Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir alisisitiza umuhimu wa kuwa na usitishaji vita kwa muda mrefu ili kuruhusu kila upande kutaja wawakilishi kwa ajili ya mazungumzo ya amani, shirika la habari la Reuters linaripoti taarifa hiyo.

    Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amezungumza na viongozi kutoka nchi jirani kutafuta njia za kutatua ghasia nchini Sudan huku Umoja wa Afrika ukizitaka pande hizo mbili kusitisha mapigano.

    Unaweza pia kusoma:

    • Mzozo wa Sudan: Jeshi na RSF zalaumiana kwa kutoheshimu makubaliano ya kusistisha vita
    • Mzozo wa Sudan: Mgogoro wa Sudan unaweza kuisha kwa njia hizi tatu
    • Mapigano Sudan: Hakuna mazungumzo mpaka mashambulio ya mabomu yakome, Hemedti aiambia BBC
  5. Ezekiel Odero:Polisi kumzuilia mhubiri mwingine wa Kenya kwa siku saba zaidi

    th

    Chanzo cha picha, SCREEN GRAB

    Mhubiri mwingine aliyekamatwa polisi polisi kufuatia kugunduliwa kwa makaburi ya Pamoja na miili ya watu waliozkwa katika msitu Pwani mwa nchi hiyo atasalia chini ya ulinzi wa polisi kwa siku saba Zaidi .

    Hata hivyo uamuzi huo wa mahakama ni ushindi kwa Ezekiel Odero ambaye mahakama ilimpa afueni kwa kukataa ombi la upande wa mashtaka kumzuilia kwa siku 30. Atarejeshwa tena kortini katika mji wa Pwani wa Mombasa siku ya Alhamisi .

    Mawakili wake wamewashtumu polisi kwa kujaribu ‘kumpaka doa la kashfa’ baada ya mhubiri mwingine Paul Mackenzie kukamatwa kwa vifo vya Zaidi ya watu 100 waliopatikana wamezikwa katika shamba la msitu linalomilikiwa naye.

    Wamesema hakuna uhusiano kati ya Odero na Mackenzie kama wanavyojaribu kuashiria polisi na upande wa mashtaka .

    th

    Unaweza pia kusoma

  6. Afrika Kusini yakatiza mkataba wa G4S kufuatia tukio la mfungwa kutoroka jela

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mamlaka ya magereza nchini Afrika Kusini imetoa notisi ya kusitisha mkataba na kampuni ya kimataifa ya ulinzi ya G4S.

    Kampuni hiyo inahusika na kusimamia Gereza la Mangaung ambapo Thabo Bester aliyepatikana na hatia alitoroka Mei mwaka jana kwa kughushi kifo chake kwa kuweka maiti kwenye seli yake .

    Kutoroka huko kujulikana mwezi uliopita - hadi wakati huo ilifikiriwa kuwa Bester alikufa katika moto wa kushangaza katika seli yake.

    Yeye na mpenzi wake maarufu walikamatwa mwezi uliopita nchini Tanzania.

    G4S imekiri kukiuka kanuni za usalama katika kituo hicho lakini haikutaka kuwajibikia tukio la kutoroka kwa Bester kutoka gerezani.

    Mkataba wake wa kuendesha gereza ulipangwa kumalizika mnamo 2026.

    Hata hivyo, Waziri wa Sheria Ronald Lamola aliwaambia wabunge kuwa anamaliza mkataba huo mapema kwa ushauri wa mawakili.

    Bester sasa anazuiliwa katika gereza jingine lenye ulinzi mkali na atafikishwa mahakamani baadaye mwezi huu kwa mashtaka mapya yanayohusiana na kutoroka, likiwemo la mauaji.

    Bester anayejulikana kama "mbakaji wa Facebook" kwa kutumia mtandao wa kijamii kuwarubuni wahasiriwa wake, mwaka wa 2012 kwa kosa la kumbaka na kumuua mpenzi wake wa wakati huo.

    Mwaka mmoja mapema, alipatikana na hatia ya kubaka na kuwaibia wanawake wengine wawili.

    Unaweza pia kusoma

  7. Fang Bin: Mtoa taarifa kuhusu Covid-19 wa China arudi nyumbani Wuhan baada ya kufungwa jela

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Fang Bin, ambaye alirekodi mlipuko wa Covid-19 katika mji wa Wuhan nchini Uchina, ameachiliwa kutoka jela baada ya miaka mitatu, vyanzo vimeiambia BBC.

    Bw Fang ni mmoja wa wale wanaojiita waandishi wa habari raia ambao walitoweka baada ya kusambaza video za matukio huko Wuhan, kitovu cha janga hilo.

    Baada ya kutoweka mnamo Februari 2020, alihukumiwa miaka mitatu jela katika kesi ya siri huko Wuhan, vyanzo vilisema.

    Aliachiliwa Jumapili na yuko katika afya njema, waliongeza.

    Bw Fang sasa amerejea nyumbani Wuhan.BBC haikuweza kufikia familia yake kwa maoni.

    Ingawa wanaharakati wamekaribisha kuachiliwa kwake, wana wasiwasi juu ya hatima ya mtoa taarifa mwingine - Zhang Zhan, wakili wa zamani wa miaka 39, aliyezuiliwa Mei 2020 na kufungwa jela miaka minne mnamo Desemba 2020.

    Kama Bw Fang, yeye pia alipatikana na hatia kwa "kuzua hofu na kuzusha matatizo", kulingana na wanaharakati wanaosema kosa hilo lisiloeleweka mara nyingi limekuwa likitumiwa dhidi ya wakosoaji wa serikali ya China.Waandishi wengine wawili wa uraia Chen Qiushi na Li Zehua pia walitoweka huko Wuhan mnamo Februari 2020, lakini walijitokeza miezi kadhaa baadaye.

  8. Mfungwa wa Palestina afariki katika jela la Israel baada ya kususia kula kwa siku 86

    Khader Adnan alikuwa mwanaharakati maarufu wa Jihad ya Kiislamu

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Khader Adnan alikuwa mwanaharakati maarufu wa kundi la Islamic Jihad

    Mfungwa mashuhuri wa Kipalestina amefariki dunia katika jela ya Israel baada ya kususia kula kwa siku 86.

    Khader Adnan alikuwa mtu wa hadhi ya juu katika kundi la wanamgambo la Islamic Jihad ambaye Israel ilikuwa imemshtaki kwa makosa ya ugaidi.

    Jeshi la Magereza la Israel lilisema kuwa alikataa matibabu kabla ya kupatikana akiwa amepoteza fahamu kwenye seli yake siku ya Jumanne.

    Saa chache baada ya kifo chake, wanamgambo walirusha makombora matatu kutoka Ukanda wa Gaza kuelekea Israel.Hakuna aliyejeruhiwa.

    Waziri Mkuu wa Palestina aliishutumu Israel kwa "kumuua kimakusudi" Adnan, huku Islamic Jihad ikiionya Israel kwamba italipia "gharama kubwa zaidi".

    Adnan, ambaye alikuwa na umri wa miaka 45 na mkazi wa kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, alikuwa akiingia na kutoka kizuizini na Israel katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.

    Alikuwa amegoma kula mara nne hapo awali kama njia ya kusaidia kutambulisha jina lake kwa Wapalestina.

    Imekuwa kawaida kwa wafungwa wa Kipalestina kukataa kula chakula kwa muda mrefu wakiwa katika jela za Israel, lakini katika miaka ya hivi karibuni vifo hivyo vimekuwa nadra kutokana na uingiliaji wa kimatibabu.

    Adnan alianza mgomo wa tano wa kula mara baada ya kuzuiliwa na vikosi vya Israeli nyumbani kwake huko Arraba, karibu na jiji la Jenin, tarehe 5 Februari.

    Mamlaka za Israel zilimshtumu kwa kuunga mkono ugaidi, kujihusisha na kundi la kigaidi na uchochezi, na alitarajiwa kuhukumiwa mwezi huu.

  9. Mgogoro wa Sudan: Raia wanakabiliwa na 'janga' huku 100,000 wakikimbia mapigano - UN

    Mapigano ya hivi punde yamezidisha mzozo wa kibinadamu nchini Sudan

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mapigano ya hivi punde yamezidisha mzozo wa kibinadamu nchini Sudan

    Zaidi ya watu 100,000 wameikimbia Sudan tangu mapigano makali yazuke kati ya vikosi hasimu tarehe 15 Aprili, Umoja wa Mataifa umesema.

    Maafisa walionya kuhusu "janga kubwa" ikiwa mapigano hayataisha. Watu wengine 334,000 wamekimbia makazi yao ndani ya Sudan.

    Mapigano yanaendelea katika mji mkuu, Khartoum, kati ya jeshi na kitengo pinzani cha wanajeshi wa RSF, licha ya kusitishwa kwa mapigano kutokana na kutekelezwa.

    Siku ya Jumatatu, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Volker Perthes, aliliambia shirika la habari la AP kwamba pande hizo mbili zimekubali kushiriki mazungumzo ya kujadili usitishaji wa mapigano na kuleta "ulivu wa kudumu".

    Saudi Arabia ilikuwa mahali pazuri pa mazungumzo, aliongeza. Ikiwa mazungumzo yatafanyika, itakuwa mkutano wa kwanza kati ya pande hizo mbili tangu mzozo huo uanze.

    Zaidi ya watu 500 wameuawa na zaidi ya 4,000 wamejeruhiwa katika mapigano hayo, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Sudan.

    Msururu wa usitishaji mapigano kwa muda haujafanikiwa, huku jeshi likiendelea kuishambulia Khartoum kwa mashambulizi ya anga kwa nia ya kuidhoofisha RSF.

    Mapigano makali pia yameshuhudiwa huko Darfur magharibi mwa Sudan.

  10. Paul Mackenzie- Kiongozi wa dhehebu tata nchini Kenya aachiliwa na kukamatwa tena

    Paul Mackenzie(katikati), akiwa mahakamani akiwa mahakamani mjini Malindi

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Paul Mackenzie(katikati) akiwa mahakamani akiwa mahakamani mjini Malindi

    Kiongozi wa dhehebu tata la Kenya na wengine sita wamekamatwa tena dakika chache baada ya mahakama ya Malindi kuwaachilia huru.

    Hakimu Ivy Wasike aliwaachilia huru Paul Nthenge Mackenzie na washirika wake baada ya maombi ya upande wa mashtaka kufunga faili hiyo.

    Mwendesha mashtaka wa serikali Vivian Kambaga alisema alitaka wahukumiwe katika mahakama nyingine - kwa mashtaka ambayo yatajumuisha ugaidi.

    Wamekamatwa nakusafirishwa hadi kaunti jirani ya Mombasa.

    Hapo awali walishtakiwa kwa mdhehebu hilo la kidini kupatikana kwenye makaburi ya pamoja mwezi uliopita.

    Bw Mackenzie, kiongozi wa dhehebu hilo, alishtakiwa kwa kuwahimiza wajiue kwa njaa. Amepinga kuhusika na kosa lolote.

    Ripoti ya uchunguzi wa maiti ilionyesha kuwa baadhi ya wahasiriwa pia waliuawa kwa kukosa hewa na kunyongwa.

    Maelezo

    Soma:

    • Paul Makenzi:Mhubiri huyu alianzaje safari tata ya kuwashawishi watu kufunga hadi kufa?
    • Kufunga mpaka kufa: 'Mke wangu na watoto sita walimfuata Mchungaji Mackenzie'
  11. Magari yamechomwa katika maandamano ya upinzani Kenya

    Protests by the opposition resumed in the capital on Tuesday

    Chanzo cha picha, AFP

    Basi na lori zimeripotiwa kuteketezwa katika matukio tofauti katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, kufuatia maandamano yaliyoandaliwa na upinzani.

    Polisi wamekabiliana na waandamanaji katika baadhi ya maeneo ya jiji, lakini maeneo mengi yamesalia tulivu.

    Hapo awali wabunge kadhaa wa Muungano wa Upinzani nchini Kenya leo walirushiwa vitoa machozi jijini Nairobi walipokuwa wakijaribu kuwasilisha ombi katika Ofisi ya Rais.

    Ombi hilo lilijumuisha masuala manne yaliyoibuliwa na muungano wa upinzani ikiwa ni pamoja na kushughulikia gharama ya juu ya maisha, ukaguzi wa kitaalamu wa seva za Tume ya Uchaguzu (IEBC), kurejeshwa kazini kwa maafisa wanne wa tume hiyo waliotimuliwa na kuundwa upya kwa tume ya uchaguzi.

    Polisi wanashika doria kuzunguka jiji ili kudumisha usalama.

    Katika miji ya Kisumu na Homa Bay magharibi mwa nchi, waandamanaji walifunga baadhi ya barabara kwa kuwasha moto.

    Maduka mengi mjini Kisumu yalifungwa huku wafanyabiashara wakihofia uporaji na uharibifu ulioshuhudiwa wakati wa maandamano ya awali.

    Pia unaweza kusoma:

    • Maandamano ya kila mara baada ya uchaguzi Kenya: Faida au hasara?
    • Kwanini maandamano ya Kenya yanaweza kuleta msiba Tanzania na Uganda?
  12. Vita vya Ukraine: Zaidi ya wanajeshi 20,000 wa Urusi wameuawa tangu Desemba- Marekani

    Mwanajeshi wa Ukraine alifyatua risasi kuelekea maeneo ya Urusi nje ya Bakhmut mwezi Novemba

    Chanzo cha picha, AFP VIA GETTY IMAGES

    Maelezo ya picha, Mwanajeshi wa Ukraine akifyatua risasi kuelekea maeneo ya Urusi nje ya Bakhmut mwezi Novemba

    Zaidi ya wanajeshi 20,000 wa Urusi wameuawa katika mapigano nchini Ukraine tangu mwezi Desemba, kulingana na Marekani.

    Wengine 80,000 wamejeruhiwa, msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa John Kirby alisema, akinukuu taarifa mpya za kijasusi zilizofichwa.

    Nusu ya waliofariki ni kutoka kundi la Wagner, ambao wamekuwa wakishambulia mji wa Bakhmut mashariki mwa nchi hiyo.

    Urusi imekuwa ikijaribu kuuteka mji huo mdogo tangu mwaka jana katika vita vikali.

    Kwa sasa Moscow inashikilia sehemu kubwa ya Bakhmut, lakini wanajeshi wa Ukraine bado wanadhibiti sehemu ndogo ya mji huo upande wa magharibi.

    Maafisa wa Ukraine pia wamesema wanatumia vita hivyo kukabiliana vikali na wanajeshi Urusi na kudhoofisha hifadhi zake.

    "Jaribio la Urusi kushambulia Donbas [eneo] kwa kiasi kikubwa kupitia Bakhmut limeshindwa," Bw Kirby aliwaambia waandishi wa habari.

    "Urusi haijafanikiwa kunyakua eneo lolote muhimu la kimkakati. "Tunakadiria kuwa Urusi imekumbwa na zaidi ya majeruhi 100,000, ikiwa ni pamoja na zaidi ya 20,000 waliouawa wakiwa katika harakati hizo," aliongeza.

    Maelezo zaidi:

  13. Waziri wa Uganda auawa kwa kupigwa risasi na mlinzi wake

    g

    Chanzo cha picha, Ugandan Parliament

    Maelezo ya picha, Kanali mstaafu Charles Okello Engola alipigwa risasi nyumbani kwake

    Mwanajeshi wa jeshi la taifa la Uganda amempiga risasi na kumuua waziri wa serikali aliyekuwa akimlinda.

    Kanali Mstaafu Charles Okello Engola, ambaye alikuwa naibu waziri wa jinsia na leba, alipigwa risasi nyumbani kwake Jumanne asubuhi.

    Bado haijabainika iwapo kulikuwa na mabishano kati ya mwanajeshi huyo na Kanali Engola.

    Askari huyo ambaye bado hajatambulika rasmi, kisha alijiua kwa kujipiga risasi dakika chache baadaye.

    Baadhi ya walioshuhudia walisema askari huyo alizunguka eneo jirani na sehemu hiyo akifyatua risasi hewani.

    Ripoti za awali zinaonyesha kuwa watu kadhaa huenda wamejeruhiwa na video kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha wenyeji wakiwa wamekusanyika katika eneo la tukio kwa mshtuko.

    Kanali Engola alikuwa afisa mkuu wa serikali, na hapo awali aliwahi kuwa naibu waziri wa ulinzi.

    Spika wa bunge la Uganda alithibitisha kifo cha Kanali Engola katika taarifa fupi alipokuwa akiongoza kikao cha asubuhi bungeni.

    "Leo asubuhi nilipokea habari za kusikitisha kwamba Mhe Engola amepigwa risasi na mlinzi wake aliyejiua pia. Roho yake ipumzike kwa amani. Huo ulikuwa mpango wa Mungu. Hatuwezi kubadilisha chochote," Anita Among aliwaambia wabunge Jumanne.

  14. Kufunga hadi kufa: Mke wa kiongozi wa dhehebu tata akamatwa

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Uchunguzi wa maiti kwa baadhi ya wahanga 110 wa dehebu tata la kikristo ulionyesha kuwa walikufa kwa kunyongwa

    Mke wa mchungaji wa Kenya ambaye anatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumanne kuhusiana na vifo vya waumini wake amekamatwa.

    Mke wa Paul Mackenzie, Rhoda Maweu, amekamatwa katika mji wa pwani ya Kenya wa Mtwapa Jumatatu baada ya kujificha kwa wiki kadhaa, vimeripoti vyombo vya habari nchini humo.

    Alikamatwa pamoja na shangazi yake Everlyne Nduku Muema.

    Polisi inasema Bi Maweu ni mtu muhimu katika kesi ambapo dhehebu tata lilisababisha vifo vya watu zaidi ya 100.

    Anatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumanne pamoja na mume wake mchungani Mackenzie.

    Baadhi ya wahanga wa shughuli za dhehebu tata linaloendesha shughuli zake katika msitu wa Kilifi wa Shakahola waliuawa kwa kunyongwa, ulibaini uchunguzi wa sampuli za vipimo vya baadhi ya miili 110 iliyofukuliwa.

    Bw Mackenzie alikanusha kufanya kosa lolote, lakini amenyimwa dhamana.

    Mchungaji mwingine anayefahamika kama pastor Ezekiel Odero ambaye alikamatwa kuhusiana na vifo katika kanisa lake ambaye pia ni mkazi wa kaunti ya Kilifi amefikishwa mahakamani Jumanne kujibu mashitaka dhidi yake.

    Unaweza pia kusoma:

    • Paul Makenzie: '' Alisema yeye na familia yake watakua wa mwisho kuaga Dunia na kwenda mbinguni''
    • Paul Mackenzie: Ni kipi kinachojulikana kuhusu kiongozi wa dhehebu la kufa njaa nchini Kenya?
    • Kufunga mpaka kufa: 'Mke wangu na watoto sita walimfuata Mchungaji Mackenzie'
  15. Maandamano Kenya: Ulinzi mkali wa polisi washuhudiwa jijini Nairobi kabla ya maandamano ya upinzani

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Polisi wameoneka wakishika doria katika maeneo mbali mbali ya mji mkuu wa Kenya Nairobi

    Idadi kubwa ya polisi wamesambazwa katika maeneo mbali mbali ya

    mji mkuu wa Kenya Nairobi kabla ya kurejelewa tena kwa maandamano ya Muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja dhidi ya serikali .

    Polisi wamewekwa kwenye maeneo makuu ya barabara muhimu za kuingia katika jiji la Nairobi.

    Vizuizi pia vimewekwa katika barabara inayoelekea katika ofisi za Ikulu, huku maafisa wa polisi wakionekana katika barabara zinazoelekea kwenye Ikulu hiyo.

    Katika baadhi ya meneo ya mji wa Kisumu ambao ni ngome ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga, tayari maandamano yamekwishaanza huku waandamanaji wakiripotiwa kufunga barabara kwa mawe na kuwasha moto barabarani.

    Katika taarifa aliyoitoa kuhusu maandamano ya Muungano wa Azimio la Umoja, Kamanda mkuu wa polisi kanda ya Nairobi Adamson Bungei alidai kuwa Azimio hawakuonyesha kuwa na malengo mazuri katika maandamano yao yaliyopita, akasema hawafai kuongoza maandamano.

    Kwa upande wake, Rais William Ruto aliapa kutumia mamlaka yote aliyonayo kuhakikisha kuwa maandamano yaliyopangwa hayageuki kuwa vurugu na ghasia.

    Hata hivyo kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga ameapa kuwa maandamano lazima yaendelee kwani anasema serikali ya Rais Ruto haiku tayari kushughulikia masuala, mkiwemo kushugulikia gharama za maisha, kufunga seva za matokeo ya uchaguzi, kufanyika kwa mageuzi katika utendaji wa Tume ya uchaguzi.

    unaweza pia kusoma:

    • Kwanini maandamano ya Kenya yanaweza kuleta msiba Tanzania na Uganda?
    • Odinga asema maandamano yataendelea huku mabalozi wakitaka utulivu Kenya
    • Je, Raila Odinga anataka nini haswa?
  16. Kufunga mpaka kufa: Baadhi ya wafuasi wa Dhehebu ‘tata’ la Shakahola Kenya 'walinyongwa'.

    w

    Chanzo cha picha, EPA

    Baadhi ya wahanga wa dhehebu tata linaloendesha shughuli zake katika msitu wa Shakahola katika Kaunti ya Kilifi waliuawa kwa kunyongwa, yameonyesha matokeo ya vipimo vya miili ya baadhi ya watu 110 iliyofukuliwa.

    Zoezi la uchunguzi huo lililoongozwa na mchunguzi mkuu wa miili wa serikali Johansen Odour jana katika Hospitali ya Malindi ulionyesha kuwa watoto wawili walikufa baada ya kuzibwa pua na mdomo.

    Maafisa wa uchunguzi wa miili jana waliweza kuchunguza miili ya watoto tisa na mwanamke mmoja. Watoto walikuwa na umri wa kuanzia mwaka mmoja na nusu hadi miaka kumi, kulingana Dkt Odour.

    “Kwa ujumla walikuwa na muonekano wa njaa kali…Lakini miili miwili ya watoto ilikuwa na rangi ya bluu kwenye kucha za vidole vyao vya mikono… hali iliyosababishwa inayofahamika kama asphyxiation. Hii inamaanisha kuwa walinyimwa hewa ya oksijeni wakati walipokufa na hii inaweza kuashiria kuwa huenda walinyongwa ,” Dkt Odour alisema wakati alipokuwa akitoa taarifa ya uchunguzi.

    Dkt Odour alisema kuwa kazi ya uchunguzi wa miili ilikuwa na changangamoto mwanzoni kwani ilibidi waweke machine za X-ray kwa ajili ya kukadiria umri wa marehemu.

    Matokeo hayo sasa yanaonyesha mauaji, hususan kwa watoto wengi ambao ndio wengi wa waathiriwa wa shughuli za dhehebu tata lililoongozwa na Mchungaji Mackenzie.

    Bw Mackenzie anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo mjini Malindi pwani ya Kenya.

    Unaweza pia kusoma:

    • Paul Makenzie: '' Alisema yeye na familia yake watakua wa mwisho kuaga Dunia na kwenda mbinguni''
    • Paul Mackenzie: Ni kipi kinachojulikana kuhusu kiongozi wa dhehebu la kufa njaa nchini Kenya?
    • Kufunga mpaka kufa: 'Mke wangu na watoto sita walimfuata Mchungaji Mackenzie'
  17. ‘Baba’ wa Akili Bandia Geoffrey Hinton aonya kuhusu hatari zake, huku akijiuzulu kazi Google

    d

    Mwanaume ambaye alionekana na wengi kama ndiye baba wa Akili Bandia (AI) ameacha kazi yake, akionya kuhusu kuongezeka kwa hatari katika katika sekta ya kazi hiyo.

    Geoffrey Hinton, mwenye umri wa miaka 75, alitangaza kujiuzulu kutoka kampuni ya Google katika taarifa aliyoitoa katika gazeti la New York Times, akisema sasa anajutia kazi yake

    Aliiambia BBC baadhi ya hatari za programu ya akili bandia inayofahamika kama -AI chatbots kuwa ni za "kutisha sana".

    "Sasa hivi, programu hizo hazina akili kuliko sisi binadamu, kadri ninavyoweza kujua. Lakini ninafikiria kwa zitakuwa na akili zaidi kuliko sisi hivi karibuni."

    Utafiti wa Dr Hinton ndio ulioanzisha tafiti za kina zaidi kuhusu jinsi ya kujifunza na mitandao isiyoegamia upande wowote na hivyo kutoa msingi wa maendeleo ya mifumo ya sasa ya Akili Bandia kama vile ChatGPT.

    Hinton ambaye ni Muingereza mwenye asili ya Canada mwenye taaluma ya utambuzi wa kisaikolojia na sayansi ya kompyuta, aliiambia BBC kwamba mfumo wa Akili Bandia wa chatbot unaweza hivi karibuni kupita kiwango cha taarifa ambazo ubongo wa binadamu unaweza kuzitunza.

    Katika Makala yake kwenye gazeti la New York Times Dr Hinton alielezea "watu wabaya" ambao wanaweza kujaribu kutumia Akili Bandia kwa ajili ya kufanya "vitu vibaya".

    Alipoulizwa na BBC kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu hilo, alijibu : "Hii ni hali tum baya zaidi, mambo mabaya tu zaidi’’

    "Unaweza kufikiria, kwa mfano, watu wabaya kama[Rais wa Urusi Vladimir] Putin akiambua kupatia roboti mbaya uwezo wa kubuni malengo yake ."

    Mwanasayansi huyo alionya kuwa hii hatimaye linaweza"kubuni malengo yake kama vile ya kupatamamlaka zaidi'".

    Aliongeza kuwa : "Nimefikia uamuzi kwamba aina hii ya akili tunayotengeneza ni tofauti sana na akili tuliyonayo.

    "Sisi ni mifumo ya kibaiolojia nah ii ni mifumo ya kidigitali. Na tofauti kubwa ni kwamba kwa mifumo ya kidigitali, unaweza kuwa na nakala nyingi zenye uzito sawa, za aina moja duniani’’.

    "Na nakala zote hizi zinaweza kujifunza tofauti lakini zikaweza kushirikishana ujuzi wake moja kwa moja. Kwahiyo kama ulikuwa na watu10,000 na wakati mtu mmoja kati yao anapojifunza kitu fulani, kila mmoja wao anakuwa amekielewa moja kwa moja. Na hivyo ndivyo mfumo wa chatbots unavyoweza kujua mengi zaidi kuliko mtu yeyote mmoja ."

    Dr Hinton pia anasema kuwa kuna sababu nyingine kadhaa zilizomfanya ajiuzulu kazi yake.

  18. Misri yamuachilia huru mwandishi wa habari wa Al Jazeera Hisham Abdel Aziz baada ya miaka minne

    k

    Chanzo cha picha, @SAMIRA_ELTAHER

    Maelezo ya picha, Hisham Abdel Aziz alikamatwa alipokuwa akielekea Misri kuitembelea familia yake mwaka 2019

    Mwandishi wa habari wa Shirika la Al Jazeera ameachiliwa huru kutoka gerezani nchini Misri, miaka minne baada ya kukamatwa, limesema shirika hilo lenye makao yake Qatar.

    Hisham Abdel Aziz alikamatwa maka 2019, kwa akishukiwa kuwa mfuasi wa kikundi cha ugaidi . Alikuwa akiachiliwa huru mara kwa mara na kukamatwa tena.

    Al Jazeera iliinukuu familia ya Bw Aziz, ikisema kuwa amerejea nyumbani mjiniCairo.

    Ni mmoja wa wafanyakazi kadhaa wa Al Jazeera waliokamatwa nchini Misri tangu utawala wa sasa ulipoingia mamlakani mwaka 2013.

    Mwezi Julai mwaka ule, aliyekuwa rais wakati huo, Mohammed Morsi, walipinduliwa kufuatia maandamano makubwa ya kupinga utawala wake.

    Makundi ya kutetea haki za binadamu yanasema tangu wakati huo maelfu ya watu wamekuwa wakikamatwa.

    Wengi wamekuwa wakishutumiwa kuwa na uhusiano na vuguvugu lililopigwa marufuku nchini Misri la Undugu wa Kiislamu - Islamist Muslim Brotherhood, ambalo Misri imeishutumu Al Jazeera kuliunga mkono.

    Kulingana na Al Jazeera, Bw Abdel Aziz alikamatwa katika uwanja wa ndege wa Cairo alipowasili kutoka Qatar, ambako alikuwa akiishi. Alikuwa njiani kuitembelea familia yake, ilisema.

  19. Mapigano Sudan: ' Ndege za mapigano zinaunguruma juu ya nyumba yangu',

    Maelezo ya video, Tazama tawi la Benki kuu ya Sudan likiungua moto

    Huku vipimo vya joto vikiendelea kupanda na kufikia zaidi ya 40C wakati huu wa mwaka, kwa kawaida huwa ninalala nje katika bustani yangu, lakini ninaogopa sana kufanya hilo kwa sasa, wakati ndege aina ya jeti za mapigano zikiunguruma juu ya nyumba yangu katika mji wa Sudan Omdurman - licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano ya hivi karibuni.

    Ninaishi na mama yangu na ndugu zangu katikati ya mji wa Omdurman, juu kidogo ya Mto Nile ukitokea katika mji mkuu Khartoum.

    Hivi karibuni mapigano yalikuja upande wetu, nafikiri kombora lilipiga , lakini hatukuwa na uhakika. Tulijificha ndani ya nyumba zetu, kwani ilikuwa ni hatari sana hata kuangalia nje ya madirisha yetu.

    Mapigano kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya dharura- Rapid Support Forces (RSF) yametuzingira – kaskazini , kusini, mashariki na magharibi.

    Yalikuja karibu na nyumba yetu Jumatatu mchana, wakati risasi zilipopaa juu ya paa la nyumba ya Jirani yangu, na kumgonga mguu wake wakati alipokuwa amelala, hakuumia sana.

    Tulisikia kelele kubwa - boom, boom, boom - muda mfupi kabla. Tulidhani ni mlio wa mlipuko wa kombora, lakini hatukuwa na uhakika. Tulijificha ndani ya nyumba zetu, kwani ilikuwa ni hatari hata kuangalia kupitia kwenye madirisha ya nyumba zetu.

    Kuanzia asubuhi hadi jioni, kuwe na usitishaji mapigano, au usiwepo, ndege za kivita zijapaa juu ya anga, zikitoka katika uwanja huo huo wa ndege wa kijeshi, mahala ambapo raia wa kigeni wamekuwa wakiokolewa, na kuelekea Khartoum kushambulia maeneo ya RSF.

    Unaweza pia kusoma:

    • Mzozo wa Sudan: Jeshi na RSF zalaumiana kwa kutoheshimu makubaliano ya kusistisha vita
    • Mzozo wa Sudan: Mgogoro wa Sudan unaweza kuisha kwa njia hizi tatu
    • Mapigano Sudan: Hakuna mazungumzo mpaka mashambulio ya mabomu yakome, Hemedti aiambia BBC
  20. Hujambo na karibu tena kwa matangazo yetu ya mobashara leo ikiwa ni tarehe 02.05.2023