Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Waasi wa DR Congo wasalimu amri na kujiondoa kabisa katika maeneo ya mashariki

Kundi la waasi la M23 Movement (M23) linatarajiwa kujiondoa kabisa katika maeneo muhimu katika jimbo la Nord Kivu mashariki mwa DR Congo.

Moja kwa moja

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa leo

  2. Kenya: Wabunge kujadili mapendekezo ya utafutaji haki dhidi ya wanajeshi wa Uingereza nchini humo

    Wabunge wa Kenya wanatazamiwa kujadili ripoti inayopendekeza mashtaka ya mauaji dhidi ya wanajeshi waliozuru Kenya yafunguliwe katika mahakama za nchini humo.

    Pendekezo hilo litakalojadiliwa siku ya Jumanne, limo katika ripoti ya timu ya bunge inayopitia mkataba wa ushirikiano wa ulinzi kati ya Kenya na Uingereza.

    Inafuatia ghadhabu ya umma baada ya madai kwamba wanajeshi wa Uingereza huenda walihusika katika mauaji ya Agnes Wanjiru - mwanamke Mkenya aliyepatikana amekufa mwaka wa 2012 baada ya kutumia tafrija ya jioni na wanajeshi.

    Inafuatia ghadhabu ya umma baada ya madai kwamba wanajeshi wa Uingereza huenda walihusika katika mauaji ya Agnes Wanjiru - mwanamke Mkenya aliyepatikana amekufa mwaka wa 2012 baada ya kuwa katika tafrija ya jioni na wanajeshi.

    Jeshi la Uingereza lilishutumiwa kwa kuficha ukweli, kwa mujibu wa ripoti ya Sunday Times, lakini Wizara ya Ulinzi ya Uingereza baadaye ilisema inashirikiana na uchunguzi wa Kenya kuhusu kifo hicho.

    Wabunge nchini Kenya walio katika kamati ya ulinzi pia wanapendekeza kwamba wanajeshi wanaozuru walazimike kuhudumia jamii kupitia uwajibikaji wa kijamii wa shirika.

    Walikutana na maafisa wa ubalozi wa Uingereza, maafisa kutoka wizara ya ulinzi na mashauri ya kigeni ya Kenya, pamoja na wapelelezi wanaochunguza mauaji ya Bi Wanjiru kabla ya kuandika ripoti hiyo.

    Jeshi la Uingereza lina kitengo cha kudumu cha kufaya mazoezi katika mji wa kati wa Nanyuki chini ya makubaliano na serikali ya Kenya.

  3. Polisi Tanzania: Thabo Bester na mpenzi wake kurejeshwa Afrika Kusini

    Mhalifu maarufu wa Afrika kusini Thabo Bester na mpenzi wake Dr Nandipha Magudumana hawataendelea na kesi yoyote katika mahakama ya Tanzania, watashtakiwa katika mahakama za Afrika Kusini.

    Msemaji wa Polisi wa Tanzania, David Misime ameiambia BBC kuwa Bester na mpenzi wake huyo waliingia nchini kinyume cha sheria, lakini kwa mujibu wa sheria za kimataifa watafata utaratibu wa kuwarudisha Afrika kusini ili waendelee na mashtaka yao.

    “Baada ya polisi wetu kupata taarifa zake na anayedaiwa kuwa mpenzi wake Dk Nandipha. Walikamatwa na bado wapo kizuizini. Tunakamilisha taratibu za kisheria kati ya nchi hizo mbili na tutamkabidhi kwa maafisa wa Afrika Kusini.

    Siku ya Jumamosi Polisi walithibitisha kukamatwa kwa Thabo Bester, mpenzi wake Dk. Nandipha Magudumana, na Zakaria Alberto huko Arusha, Kaskazini mwa Tanzania.

    Bester ambaye anajulikana kama "mbakaji wa Facebook" kwa kutumia mtandao wa kijamii kuwarubuni waathiriwa wake.

    Alipatikana na hatia mwaka wa 2012 kwa kumbaka na kumuua mpenziwe mwanamitindo Nomfundo Tyhulu. Mwaka mmoja mapema, alipatikana na hatia ya kubaka na kuwaibia wanawake wengine wawili.

    Alifanikiwa kutoroka gerezani na kuaminisha mamlaka za Afrika kusini kuwa alijiua kwa moto katika chumba chake cha gereza.

    Wakati huo huo, Askari wa gereza aliyesimamishwa kazi na baba yake mpenzi wa Thabo Bester wanakabiliwa na msururu wa mashtaka yakiwemo mauaji, uchomaji moto na kusaidia kutoroka kwa Thabo Bester.

    Kulingana na stakabadhi za mahakama, watu hao wawili wanadaiwa kumuua kimakusudi mtu asiyejulikana Machi mwaka jana.

    Kesi yao imeahirishwa hadi Aprili 17 kwa uwezekano wa maombi ya dhamana, Wamewekwa rumande ya polisi.

    Kampuni ya ulinzi inayomilikiwa na Uingereza ya G4s ilikuwa ikiendesha gereza alimofungiwa Bester. Tangu wakati huo imechukuliwa na maafisa wa magereza ya Afrika Kusini kufuatia kashfa yake ya kutoroka.

    Soma zaidi:

  4. Misri yakanusha madai ya mpango wa kutoa makombora kwa Ukraine

    Afisa wa Misri ameeleza kuwa madai "yasio na msingi kabisa" katika nyaraka za Pentagon zilizovuja kwamba Cairo ilipanga kuzalisha kwa siri na kuipatia Urusi makombora 40,000.

    Ukanaji huo, na chanzo ambacho hakikutajwa jina, umetajwa na vituo kadhaa vya habari vinavyounga mkono serikali.

    Nyaraka hizo zilipatikana na gazeti la Washington Post kutoka kwa karatasi zilizovuja za idara ya ulinzi ya Marekani.

    Kama sehemu ya kukanusha, afisa huyo alinukuliwa akisema Cairo haikuunga mkono upande wowote katika vita vya Ukraine.

    Kremlin ilielezea madai hayo kama "tu kashfa nyingine".

    Soma zaidi:

  5. Somali ni waathirika wa mabadiliko ya hali ya hewa - mkuu wa Umoja wa Mataifa

    Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema watu wa Somalia ndio wahanga wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi licha ya kutochangia mabadiliko hayo.

    Ujumbe wa Nukuu: Ingawa Somalia haitoi mchango wowote katika mabadiliko ya hali ya hewa, Wasomali ni miongoni mwa waathirika wakubwa"

    Bw Guterres alitoa wito wa kuungwa mkono kwa wingi kimataifa mwanzoni mwa Ziara ya nchi hiyo katika hali ya ukame mkubwa.

    Umoja wa Mataifa umezindua ombi la mabilioni ya dola kwa Somalia ambako mamilioni wanakabiliwa na njaa.

    Ujumbe wa Nukuu: Takriban watu milioni tano wanakabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula, na bila shaka kupanda kwa bei kunafanya mambo kuwa mabaya zaidi.

    Takriban watu milioni tano wanakabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula, na bila shaka kupanda kwa bei za bidhaa kunafanya mambo kuwa mabaya zaidi.

    Ujumbe wa Nukuu: Kwa hivyo, natoa wito kwa wafadhili, na ninatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza uungaji mkono wao ili kufadhili haraka mpango wa kukabiliana na misaada ya kibinadamu wa 2023, ambao kwa sasa unafadhiliwa kwa asilimia 15 tu."

    Kwa hivyo, ninatoa wito kwa wafadhili, na nitoe wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza uungwaji mkono wao kufadhili haraka mpango wa kukabiliana na misaada ya kibinadamu wa 2023, ambao kwa sasa unafadhiliwa kwa asilimia 15 tu."

    Awali, Antonio Guterres aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter kwamba ziara yake nchini Somalia inaendana na desturi yake ya kila mwaka ya kutembelea nchi za Kiislamu wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa "kufunga kwa mshikamano na kushiriki Iftari."

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia ilisema umuhimu wa ziara hiyo ni 'kufanya mazungumzo ya kisiasa, usalama, maendeleo na kibinadamu'.

    Bwana Guterres amekutana na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud.

    Kuhusu uasi wa Kiislamu, serikali ya Somalia imepata mafanikio katika vita vyake na Al-Shabaab, hasa katikati mwa Somalia.

    Kulingana na Crisis Group, maendeleo mengi yametokana na kutoridhika kwa wenyeji na kundi hilo, ambako kumesababisha kuundwa kwa wanamgambo wa koo ambao tangu wakati huo wameunda muungano kurudisha nyuma Al-Shabab.

  6. Tazama: Jengo lote laporomoka kwenye barabara nchini Mexico

    Mamlaka mjini Tijuana inasema jengo hilo ni la pili kuporomoka katika eneo hilo kufuatia maporomoko ya ardhi.

    Wafanyakazi wa dharura waliwasli kwenye eneo la tukio, na bado haijabainika iwapo kulikuwa na majeruhi wakati wa tukio

  7. Chama cha Afrika Kusini ‘EFF’ kinaitaka India kumfungulia mashtaka Dalai Lama

    Chama cha upinzani nchini Afrika Kusini cha Economic Freedom Fighters (EFF) kimewataka polisi wa India kumkamata na kumfungulia mashtaka Dalai Lama kwa unyanyasaji wa watoto baada ya video ya maongezi yake yasiofaa na mvulana mdogo kusambaa.

    Katika video hiyo, kiongozi huyo wa kiroho wa Tibet mwenye umri wa miaka 87 anaonekana akimbusu mvulana mdogo kwenye midomo na kumtaka "kunyonya ulimi wake" kwenye hafla ya umma.

    Tukio hilo linaonekana kutokea katika hekalu la Dalai Lama huko Dharamshala mwezi Februari.

    Kufuatia kilio cha kimataifa kuhusu suala hilo, Dalai Lama ameomba radhi na kusema kuwa anajutia tukio hilo.

    Kutoa ulimi nje kunaweza kuwa aina ya salamu huko Tibet.

    Chama cha EFF kilisema "msamaha wa vivi hivi tu" unapaswa kukataliwa kwani ulitolewa mwezi mmoja baada ya tukio hilo.

    Taarifa yake ilisema mamlaka ya India ilihitaji kutuma onyo kali "kwa wale wote wanaothubutu kuwadhuru watoto kwamba watachukuliwa hatua kali bila kujali hadhi zao".

    Dalai Lama amekuwa akiishi uhamishoni nchini India tangu kutoroka Tibet mwaka 1959, kufuatia maasi dhidi ya utawala wa China huko.

    Soma zaidi:

  8. Rais William Ruto asema nchi haitakopa kulipa mshahara wa wafanyakazi wa umma

    Rais wa Kenya William Ruto amesema nchi hiyo haitakopa ili kuwalipa wafanyakazi wa umma hata kama vyama vya wafanyakazi vilitishia kugoma kutokana na kutolipwa mishahara ya Machi.

    Ruto alilaumu ucheleweshaji wa deni kubwa la umma nchini, kutokana na baadhi ya mikopo kufikia hatua ya kulipwa mwezi huu.

    Alisema mishahara hiyo italipwa kutokana na ushuru unaokusanywa na mamlaka ya mapato.

    Angalau mashirika mawili ya wafanyikazi yametoa notisi ya kugoma wiki hii ikiwa hawatalipwa pesa zao.

    Akizungumza na vyombo vya habari siku ya Jumatatu, mshauri mkuu wa marais wa masuala ya kiuchumi alisema mishahara hiyo italipwa hadi mwisho wa mwezi lakini akashauri serikali kupunguza ufujaji wa fedha za umma.

    Deni la umma la Kenya sasa linafikia asilimia sitini na tano ya mapato.

    Nchi inahitaji zaidi ya $420M kila mwezi kulipa mishahara na pensheni kwa watumishi wa umma.

    Haya yanajiri wiki chache tu baada ya Benki ya Dunia na IMF kutoa onyo tofauti kwamba Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara inazama katika mgogoro mpya wa madeni, huku nchi nyingi zikiwa katika hatari kubwa ya kukumbwa na deni.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Marekani yavujisha taarifa inayoonyesha vifaa vya uchaguzi vya Nigeria vilifeli kabla ya upigaji kura

    Faili za Marekani zilizovuja zimeonyesha kuwa baadhi ya vifaa vya kutambua wapiga kura vya Nigeria vilikuwa na hitilafu kabla ya uchaguzi wa Februari 25, tovuti ya kibinafsi ya HumaAngle iliripoti Aprili 10.

    Marekani inaripotiwa kukusanya taarifa hizi wakati ikifuatilia mazungumzo ya ngazi ya juu kati ya Idara ya Huduma za Jimbo la Nigeria (DSS) na afisa wa wakala wa uchaguzi.

    Mhandisi Mkuu wa Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (INEC) Victor Igboh alifahamisha DSS kwamba vifaa vingi vya Mfumo wa Ithibati ya Wapigakura wa Bimodal (BVAS) katika jimbo la kusini la Rivers viliharibika kwa sababu ya kuvimba kwa betri.

    Hati hiyo pia iliripoti "changamoto ambazo hazijabainishwa na BVAS" na mashine za kusoma kadi kaskazini-mashariki.

    Upinzani unaweza kutumia uvujaji huo kutaka matokeo ya kura ya maoni yafutiliwe mbali.

    Hitilafu na madai ya kuvuruga teknolojia ya uchaguzi ni baadhi ya masuala muhimu yaliyoibuliwa na vyama vya upinzani katika kupinga ushindi wa Bola Tinubu.

    Soma zaidi:

  10. Waasi wa DR Congo wasalimu amri na kujiondoa kabisa katika maeneo ya mashariki

    Kundi la waasi la M23 Movement (M23) linatarajiwa kujiondoa kabisa katika maeneo muhimu katika jimbo la Nord Kivu mashariki mwa DR Congo.

    Wanajeshi wa Kikosi cha Kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) watachukua maeneo ambayo waasi hao walisalimu amri, ambao kuibuka kwao tena mwishoni mwa 2021 kumesababisha vifo vya mamia na maelfu ya wengine kuyahama makazi yao.

    Mpatanishi maalum wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Uhuru Kenyatta, alisema tarehe 4 Aprili kwamba M23 watajiondoa katika maeneo zaidi ya Nord Kivu kufikia leo.

    Hapo awali EAC iliweka makataa ya Machi 30 kama siku ya mwisho ya kujiondoa.

    Wakati huo huo, duru ya nne ya mazungumzo yenye lengo la kuleta utulivu eneo la mashariki mwa Congo yanatarajiwa kurejelewa tena hivi karibuni huko Goma, Beni, Uvira, Bukavu na Bunia.

    Duru tatu za awali zilifanyika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

    Soma zaidi:

  11. Kiongozi wa Kenya ataja timu ya kufanya mazungumzo na upinzani

    Wabunge wa muungano unaotawala nchini Kenya wamekutana leo na kuchagua timu ya kujadiliana na upinzani kuhusu gharama ya maisha na masuala mengine yaliyosababisha maandamano ya wiki kadhaa mwishoni mwa mwezi Machi.

    Muungano huo wa Kenya Kwanza umechagua ujumbe wake wa watu saba kwenye mazungumzo ya wabunge wa pande mbili na upinzani.

    Wakati wa mkutano na wanahabari katika Ikulu Jumanne, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung'wa alisema kuwa wabunge hao walichaguliwa kufuatia majadiliano wakati wa mkutano wa awali wa Kikundi cha Wabunge wa Kenya Kwanza.

    Kiongozi wa upinzani Raila Odinga mnamo tarehe 4 Aprili alitishia kuitisha maandamano mapya iwapo serikali itashindwa kuyachukulia kwa uzito mazungumzo hayo.

    Upinzani ulikuwa umesitisha maandamano tarehe 2 Aprili baada ya Ruto kuitisha mazungumzo.

    Muungano wa Azimio la Umoja wa Odinga- One Kenya umetaja timu ya watu saba kwa ajili ya majadiliano hayo.

    Inaitaka serikali kuchukua hatua za kupunguza gharama ya maisha, kufanya mageuzi ya uchaguzi, kufungua seva za tume ya uchaguzi na kuacha kuajiri maafisa wa wakala wa kura.

  12. Louisville, Kentucky: Mwanaume awapiga risasi watu watano kwenye benki

    Watu watano wamefariki dunia wakati mfanyakazi mmoja wa benki mjini Louisville, Kentucky, na kurekodi moja kwa moja shambuliohilo kwenye Instagram, polisi inasema.

    Wahanga walikuwa na umri wa kati ya miaka 40 na 64. Miongoni mwa watu tisa waliojeruhiwa alikuwa ni afisa wa polisi ambaye alikuwa amemaliza mafunzo wiki mbili tu.

    Afisa huyo alipigwa risasi kichwani na bado anafanyiwa upasuaji wa ubongo.

    Polisi ilifika katika eneo la tukio katika muda wa dakika tatu, na kumpiga risasi mshambuliaji ambaye alifariki katika makabiliano ya risasi.

    Shambulio hilo lilifanyika katika benki ya zamani katikati mwa jiji.

    Caleb Goodlet aliviambia vyombo vya habari kwamba mke wake, mfanyakazi wa benki, alijifungia ndani ya jengo wakati shambulio lilipoanza.

    Watu wengine walioshuhudia walielezea ufyatulianaji huo wa risasi baina ya maafisa wa polisi na mshambuliaji.

  13. Hali mbaya ya hewa yachelewesha kuzinduliwa kwa satelaiti ya Kenya,

    Kampuni ya SpaceX ya Elon Musk imechelewesha kurusha satelaiti ya kwanza ya Kenya ya uchunguzi wa dunia kwa saa 24 ikitaja hali mbaya ya hewa katika kituo cha kurushia ndege huko California.

    Satelaiti hiyo iliyopewa jina la Taifa -1 ililipaswa kutumwa kwenye roketi ya Falcon 9 pamoja na satelaiti nyingine kutoka nchi nyingine.

    Taarifa kutoka Shirika la Anga la Kenya ilisema kuchelewa huko kulitokana na "hali mbaya ya upepo wa hali ya juu" ambayo "itaathiri njia ya kuruka ya roketi".

    Uzinduzi huo sasa unatarajiwa kufanyika Jumatano tarehe 12 Aprili katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Vandenberg.

    Dhamira kuu ya satelaiti hiyo itakuwa kutoa data kwa matumizi katika kilimo, usalama wa chakula, usimamizi wa ardhi na ufuatiliaji wa mazingira.

    Taifa-1 iliundwa kikamilifu na kuendelezwa na timu ya wahandisi wa Kenya kutumia sehemu za satelaiti kwa ushirikiano na mtengenezaji wa vifaa vya vyombo vya angani kutoka Bulgaria.

    Kenya ilituma satelaiti yake ya kwanza ndogo ya majaribio kutoka Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu mwaka wa 2018 kwa ushirikiano na Japan.Ilijengwa na wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.

  14. Kenya yakiri kukumbwa na uhaba wa pesa huku wafanyikazi wakitishia mgomo

    Serikali ya Kenya imekiri kwamba inakabiliwa na uhaba wa pesa ambao umechelewesha malipo ya mishahara ya maelfu ya wafanyikazi wa umma.

    Inasema ilibidi kufanya maamuzi magumu iwapo italipa mishahara au kulipa mamilioni ya dola katika deni la nje, linalodaiwa mwezi huu.

    Hazina ya kitaifa pia imeshindwa kutuma pesa kwa serikali za kaunti - vitengo vilivyogatuliwa ambavyo vinasimamia huduma za umma kama vile afya na elimu.

    Wafanyikazi katika wizara, mashirika na serikali za kaunti ndio wameathiriwa zaidi na ucheleweshaji wa mishahara ya Machi.

    Waziri wa Fedha Njuguna Ndung'u alisema serikali inakabiliwa na matatizo ya kifedha yanayosababishwa na mapato adimu na na mzigo wa madeni.

    Vyama viwili vinavyowakilisha wafanyikazi wa serikali ya kitaifa na kaunti vimetoa notisi za nia yao ya kususia kazi.

    Naibu Rais Rigathi Gachagua amelaumu mzozo huo kwa serikali ya zamani ambayo anaituhumu kwa kukopa pesa nyingi ikiwa mamlakani na kuvamia hazina kabla ya kuondoka mamlakani mwaka jana.Lakini hakutoa ushahidi wowote wa madai hayo.

    Mshauri wa rais wa masuala ya uchumi David Ndii alisema mishahara iliyocheleweshwa sio shida na akataja hali kama "Changamoto ya upatikanaji wa hela".

    Katika mahojiano ya runinga, Bw Ndii alisema kuwa serikali ilikuwa inatarajia $500m (£460m) kutoka kwa mkopo ulioidhinishwa na mishahara ya watumishi wa umma italipwa mwishoni mwa wiki ijayo.

    Deni la umma la Kenya sasa linafikia 65% ya mapato.

    Nchi hiyo inahitaji zaidi ya $420m kila mwezi kulipa mishahara na pensheni kwa watumishi wa umma

  15. Waziri wa zamani wa Malawi aliyefungwa kutokana na kashfa ya hati ya kusafiria asamehewa

    Rais wa Malawi Lazarus Chakwera amemsamehe waziri ambaye alikuwa akitumikia kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya kutumia vibaya mamlaka yake.

    Uladi Mussa alihukumia mwaka 2020 kifungo cha miaka sita jela kwa ufisadi unaohusiana na utoaji wa paspoti kinyume cha sheria.

    Kuachiliwa kwake ni kitendo cha huruma katika msimu wa Pasaka, alisema Waziri wa usalama wa ndani ya nchi Ken Zikhale Ng’oma.

    Bw Mussa amesalia kuwa na ushawishi katika siasa za nchi baada ya kuhudumu kama waziri chini ya marais wanne kati ya mwaka 1994 na 2019.

    Alihusika katika sakata ya paspoti wakati wa muhula wa uongozi wa rais wa zamani Joyce Banda.

    Katika mwaka 2019,serikali ya Marekani ilimuwekea vikwazo vya kusafiri binafsi pamoja na mke wake kutokana na nafasi yake katika sakata hiyo.

    Bw Mussa aliachiliwa huru pamoja na wafungwa wengine199 walio “fanya makosa madogo na kuonyesha tabia nzuri wakati walipokuwa wakiishi gerezani ”.

    Watu hao ni pamoja na dereva ambaye alikamatwa baada ya kukataa kuupisha msafara wa magari ya Rais Chakwera.

  16. Marekani na Ufilipino zaanza mazoezi makubwa zaidi baada ya China kufanya mazoezi ya kijeshi

    Beijing ilifanya mazoezi ya siku tatu na kufunga njia za kuelekea Taiwan ili kujibu hatua ya kiongozi wa kisiwa hicho ya kukutana na Spika wa bunge la Marekani wiki iliyopita.

    Marekani iliitolea wito Beijing kuacha hasira. Wakati huo huo, rais wa Taiwan Tsai Ing-wen Jumatatu alisema kuwa hatua za China zilikuwa ni za"kukosa uwajibikaji".

    Mazoezi ya marekani yalikuwa yamepangwa awali mapema.

    Marekani na Ufilipino kwa pamoja zilitoa taarifa mwezi uliopita kwamba mazoezi yake ya kijeshi yatakuwa makubwa kuwahi kushuhudiwa, baada ya Marekani mapema mwaka huu kupata kufanya mkataba mpya wa ulinzi na taifa hilo la Kusini -Mashariki mwa Asia.

    Mwezi Februari, serikali ya Washington ilifanikiwa kusaini makubaliano ambapo ngome zake nne za vikosi vyake vya majini vitaanzishwa katika visiwa vya Ufilipino.

    Njia za maji za Ufilipino na karibu na Kusini - Mashariki mwa Asia ni miongoni mwa maeneo yenye shughuli nyingi katika biashara, n ani maeneo ambayo yamekuwa na madai ya mipaka ya Uchina.

    • China yafanya mazoezi ya kushambulia 'maeneo muhimu' Taiwan
    • Mvutano wa Marekani - China: Fahamu nguvu za kijeshi kati ya mataifa haya mawili
  17. Mzozo wa wahamiaji: Italia yaingilia kati kuwaokoa watu 1,200 waliokuwa ndani ya boti

    Watu takriban 800 wanasafiri katika moja ya maboti ya uvuvi, huku wengine wakisafiri katika boti jingine.

    Walinzi wa Italia wa mwambao tayari walikwisha waokoa watu wapatao 2,000 katika operesheni nyingine zilizofanyika kuanzia Ijumaa wiki iliyopita.

    Takriban watu wawili wamekufa wakati boti hizo zilipokuwa zikivuka kuingia Italia, imesema taasisi ResQship.

    Idadi ya wahamiaji wanaowasili nchini Italia ni ya juu zaidi ikilinganishwa na idadi ya wale waliofika katika kipindi saw ana hiki mwaka jana, licha ya juhudi za serikali ya muungano ya mrengo wa kulia na kushoto ya Italia kudhibiti wahamiaji wasio halali.

    Boti iliyowabeba watu 400, ambayo inaaminiwa kuwa iling’oa nanga kutoka mjiniTobruk nchini Libya, ilikuwa haijapata msaada hadi kufikia Jumatatu jioni, kulingana na taasisi isiyo rasmi inayopokea simu za dharura za wahamiaji walio mashakani, Alarm Phone.

    Ilisema kuwa ilipiga king’ora cha tahadhari kwa mamlaka za Italia, ugiriki na Malta siku ya Jumapili.

    Unaweza pia kusoma:

    • Italia kuzuia kuingia kwa wahamiaji katika pwani
    • Wahamiaji haramu watumia muziki kusahau shida zao Italia
  18. Mama wa mtoto mwenye umri wa miaka 6 aliyempiga risasi mwalimu ashitakiwa

    Mama wa mtoto mwenye umri wa miaka sita ambaye alimpiga risasi mwalimu wake ameshitakiwa kwa kosa la uhalifu.

    Deja Taylor, mwenye umri wa miaka 25, ameshitakiwa na jopo la mahakama kwa kosa la mauaji ya uzembe na tabia mbaya.

    Awali polisi walikuwa wamesema kuwa bunduki iliyotumiwa kufyatua risasi ilikuwa ni mali ya Bi Taylor.

    Mtoto huyo aliileta shuleni ndani ya begi lake tarehe 6 Januari.

    Baadaye akampiga risasi mwalimu wake Abigail Zwerner, aliyekuwa na umri wa miaka 25- kwenye mkono na kifuani wakati alipokuwa akimfundisha. Bi Zwerner alijeruhiwa vibaya lakini alinusurika kifo.

    Jumatatu, waendesha mashitaka walisema katika taarifa yao kwamba, Bi Taylor alishitakiwa kwa shitaka la mauaji ya mtoto ya uzembe na kosa moja la tabia mbaya au kwa "uzembe wa kuacha bunduki iliyojaa risasi kwa ajili ya kumhatarisha mtoto."

  19. Nyaraka za Pentagon zilizovuja ni hatari kwa usalama wa taifa la Marekani, wasema maafisa

    Kuvuja kwa nyaraka za siri za wizara ya ulinzi ya Marekani ni"hatari kubwa " kwa usalama wa taifa, yamasema kamao makuu ya wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon.

    Nyaraka zilizoonekana ni pamoja na taarifa za siri kuhusu vita vya Ukraine, pamoja na zile zinazoihusu China na washirika wa Marekani.

    Maafisa wanasema faili hizo ziko katika mfumo sawa na ule wanyaraka zinazotolewa kwa viongozi wa ngazi ya juu.

    Uchunguzi umeanzishwa kubaini chanzo cha kuvuja kwa nyaraka hizo.

    Nyaraka hizo- ambazo baadhi ya maafisa wanasema huenda maudhui yake ya awali yalibadilishwa – kwa mara ya kwanza zilionekana katika majukwaa ya mitandao kama vile Twitter, 4chan na Telegram, pamoja na seva ya Discord inayotumiwa kwa ajili ya video za michezo Minecraft.

    Zaidi ya maelezo ya kina kuhusu vita vya Ukraine, baadhi ya taarifa zilizovuja zinasemekana kutoa mwangaza kuhusu taarifa za siri kuhusiana na washirika wa Marekani.

    Chanzo cha karibu kabisa cha rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kiliiambia CNN kwamba Ukraine tayari imebadilisha baadhi ya mipango yake ya kijeshi kwasababu ya kuvuja kwa nyaraka hizo.

    Nyaraka nyingine zinaripotiwa kuangazia kuhusu masuala ya ulinzi na usalama katika Mashariki ya Kati pamoja na kanda ya Indonesia na Pasific.

    Unaweza pia kusoma:

    • Kati ya Urusi na Ukraine nani ana jeshi lenye nguvu zaidi?
    • Rais wa Urusi, Vladimir Putin humsikiliza nani?
    • Mkate,mafuta na wanafunzi:Jinsi vita vya Ukraine vinaiathiri Afrika
  20. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya mubashara leo ikiwa ni Jumanne tarehe 11.04.2023