Daktari Mtanzania aliyekuwa akisoma nchini Uganda amefariki
kutokana na virusi vya Ebola, waziri wa afya wa Uganda Dkt Jane Ruth Aceng
amethibitisha.
Raia huyo huyo mwenye umri wa miaka 37 alikuwa akisomea
Shahada ya Uzamili ya Udaktari katika Upasuaji, akiwa mwanafunzi wa kimataifa.
Chama cha madaktari wa upasuaji nchini Uganda kimetoa risala
za rambirambi kwenye akaunti zao za Twitter.
Haijabainika jinsi Dkt Mohammed Ali aliambukizwa lakini kifo chake kinajiri saa
chache baada ya Wizara ya Afya siku ya Ijumaa kutangaza kwamba idadi ya
waliofariki kutokana na mlipuko wa Ebola nchini imeongezeka hadi saba.
“Ni kwa masikitiko makubwa tumepokea taarifa za kufariki kwa
Dk Mohammed Ali, raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 37 ambaye alikuwa
akisomea Shahada ya Uzamili ya Upasuaji katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha
Kampala. Dk. Ali alishindwa katika vita dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Ebola,”
Chama cha Madaktari wa Upasuaji Uganda kiliandika kwenye Twitter Jumamosi.
Waziri wa Afya, Dk Jane Ruth Aceng alisema Dk Ali alipimwa
na kuwa na Ebola Septemba 26, 2022 na alifariki dunia alipokuwa akipatiwa
matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Fort Portal. Alikufa saa 3
asubuhi siku ya Jumamosi.
“Dk Ali ndiye Daktari wa kwanza, na mhudumu wa afya wa pili
kuugua Ebola. Wa kwanza alikuwa mkunga kutoka Kliniki ya St Florence, kisa
kinachowezekana, kwa sababu alifariki kabla ya kupimwa,” Dkt Aceng alituma ujumbe wa Twitter Jumamosi.
Lakini mapema wiki hii, wizara ya afya ilisema kuwa wahudumu
sita wa afya walipimwa na kukutwa na virusi vya Ebola. Inasemekana wengine
waligusana na muathiriwa wa kwanza wa ebola
Wahudumu wengi wa afya walioshughulikia kesi ya kwanza
walikuwa wanafunzi. Baadaye walitangaza kuwa walikuwa kwenye mgomo, wakitaja
ukosefu wa vifaa vya kujikinga na marupurupu yakujiweka hatarini..
Siku ya Ijumaa, wizara ilitangaza kuwa mlipuko wa Ebola
ulikuwa umeenea hadi wilaya ya nne.
Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa jumla ya kesi
zilizothibitishwa zimefikia thelathini na tano, na vifo vinane.
Watu wawili hadi sasa wamepona ugonjwa huo wa virusi,
kulingana na mamlaka ya afya.