Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Bei ya mafuta Kenya yaongezeka na kutishia kuzidisha zaidi gharama za bidhaa muhimu

Bei hizo ni pamoja na asilimia 8 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Moja kwa moja

  1. Na kufikia hapo tunatamatisha habari zetu hii leo.

  2. Rais wa Zambia amsimamisha kazi mwendesha mashtaka mkuu

    Rais wa Zambia Hakainde Hichilema amemsimamisha kazi mwendesha mashtaka mkuu wa nchi hiyo mara moja - siku mbili tu baada ya kuiambia BBC kwamba maisha yake yalikuwa hatarini.

    Lillian Siyunyi, ambaye aliteuliwa na serikali iliyopita, alitofautiana na utawala mpya na anashtumiwa kwa mwenendo wake wa kitaaluma katika Tume ya Malalamishi ya Mahakama (JCC).

    Katika tangazo lilitolewa siku ya Jumatano jioni, msemaji wa rais Anthony Bwalya amesema uamuzi huo ulitokana na mapendekezo ya mahakama ya JCC kwa rais.

    Katongo Waluzimba ameteuliwa kama mwendesha mashtaka mkuu kwa muda, haya ni kulingana na msemaji wa rais.

    Akizungumzia usimamishaji huo, Bi Siyunyi ameiambia BBC kwamba alikuwa na ‘’mengi ya kusema’’ endapo msamaha wa rais ungetolewa kwa kiapo cha usiri.

    ‘‘Msamaha huo unanuia kunipatia mimi nafasi ya kujitetea bila uoga wa kulipiziwa kisasi kutoka kwa mtu yeyote,’’ alisema.

    Alisema kufika mbele ya JCC kabla ya msamaha huo kutolewa itakuwa kinyume cha sheria.

    Kabla ya kusimamishwa kazi, Bi Siyunyi alikuwa amepokonywa walinzi wake na serikali.

  3. Kagame atoa salamu za rambirambi kwa Mfalme Charles kupitia simu

    Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema amepigiwa simu ya kibinafsi na Mfalme Charles III ambapo alitoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mamake, Malkia Elizabeth II.

    "Rwanda inatarajia kufanya kazi pamoja na Mfalme Charles III ili kuendeleza ajenda ya Jumuiya ya Madola katika kuwatumikia raia wetu wote," Rais Kagame alisema kwenye Twitter.

    Rais Kagame alikuwa mwenyeji wa Mwanamfalme Charles mnamo mwezi Juni wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola, ambapo mfalme alionyesha "huzuni yake ya kibinafsi" na mateso yaliyosababishwa na biashara ya utumwa lakini aliacha kuomba msamaha.

    Mfalme wa Uingereza aliongeza kuwa ni majimbo binafsi kuamua iwapo yanataka kusalia wanachama wa shirika hilo.

  4. Ghadhabu baada ya Zimbabwe kuwakamata wanafunzi wanaopinga karo ya juu

    Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetoa wito kwa mamlaka ya Zimbabwe kufuta mashtaka dhidi ya wanafunzi wa vyuo vikuu ambao wamekuwa wakiandamana kupinga ongezeko kubwa la ada za masomo.

    Wanafunzi kumi na wanne walikamatwa siku ya Jumatatu na kushtakiwa kwa utovu wa nidhamu.

    Waliachiliwa baada ya kulipa faini au dhamana. Wengine watano walikamatwa siku ya Jumatano.

    Wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Zimbabwe wanakabiliwa na ongezeko la hadi mara 10 la ada.

    Amnesty ilisema ni unyanyasaji wa haki kwamba watu walikuwa wakilazimika kutumia wakati kizuizini na vyumba vya mahakama kwa kuomba tu elimu ya bei nafuu.

  5. Vifaa vilivyoachwa na Urusi vinaashiria jeshi lisilo na mpangilio - Uingereza

    Ripoti ya kila siku ya ujasusi wa Uingereza leo umechambua kutoroka kwa jeshi la Urusi katika jimbo la Kharkiv.

    Vikosi vya Ukraine vinaendelea kuimarisha udhibiti wao katika maeneo mapya yaliyokombolewa ya Kharkiv.

    Vikosi vya Urusi vimeondoka katika eneo la magharibi mwa Mto Oskol;

    Kutorika kwa wanajeshi wa Urusi wiki iliopita kulikuwa tofauti.

    Baadhi ya wanajeshi wake waliondoka kwa utaratibu mzuri, huku wanajeshi wengine kukimbia kwa hofu.

    Silaha za thamani zilizoachwa na vikosi vya Urusi vinavyotoroka ni pamoja na vifaa vinavyohitajika sana kwa "vita vya kiufundi" .

    Jeshi la Urusi liliacha nyuma angalau rada moja ya kukabiliana na betri na angalau gari moja la amri na udhibiti;

    Magari yaliyoachwa yanaonesha hali isiyo na mpangilio ya baadhi ya vitengo vya jeshi la Urusi

  6. Matokeo ya Uchaguzi Kenya: Abdulswamad Nassir aapishwa kuwa Gavana mpya wa Kaunti ya Mombasa

    Abdulswamad Shariff Nassir ameapishwa kama Gavana mpya wa kaunti ya Mombasa.

    Gavana Nassir ambaye awali alihudumu kama mbunge wa jimbo la Mvita, anachukua nafasi ya Hassan Joho ambaye alihudumu kwa mihula miwili mamlakani.

    Gavana Nassir amekula kiapo cha kazi hiyo katika sherehe iliyofanyika eneo la Mama Ngina Waterfront, Mombasa Alhamisi.

    Sherehe za uapisho wa Gavana wa jimbo la Kakamega magharibi mwa Kenya pia zinaendelea, ambapo mshindi wa ugavana Fernandes Barasa OGW anatarajiwa kuapishwa rasmi kama Gavana mpya wa Kakamega. Bw Barasa anachukua mamlaka hayo baada ya aliyekuwa gavana wa jimbo hilo Wycliffe Oparanya kuhudumu kwa kwa mihula miwili, kulingana na katiba ya Kenya.

  7. Zelensky: Njia pekee ya kusalimika kwa wanajeshi wa Urusi ni kujisalimisha

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema katika hotuba yake ya jioni kwamba shambulio la kombora kwenye bwawa la Krivoy Rog halitaokoa ari ya wanajeshi wa Urusi.

    "Waligundua kuwa amri ya Urusi ni ya wastani, na kwamba wanatarajiwa kushindwa nchini Ukraine katika pande zote. Urusi haitarekebisha hili kwa ugaidi wowote, kwa sababu ugaidi unathibitisha tu udhaifu wa yule anayetekeleza," Zelensky alisema. .

    Kulingana na yeye, njia pekee ya askari wa Urusi ni kujisalimisha kwa wanajeshi wa Ukraine, kwani Urusi hatimaye itashindwa vita.

    ‘’Atapoteza sio tu vita hivi , lakini historia yenyewe pia. Historia huandikwa na binadamu -sio wasio wanadamu – hapana. Utasalia nani katika historia? Wale wote waliotushambulia kwa makombora. Wale waliovamia ardhi yetu, waoga. Ninyi ni watu wwalio na udhoofu ambao baada ya kutoroka katika mstari wam bele wa vita munajaribu kufanya uhalifu kutoka mbali’’, alisema rais huyo wa Ukraine.

  8. Kiongozi wa Kenya afuta ujumbe wa Twitter unaobatilisha mahusiano na Sahara Magharibi

    Rais wa Kenya William Ruto alifuta ujumbe wa Twitter unaobatilisha msimamo wake wa muda mrefu wa nchi hiyo kuitambua Jamuhuri ya Kiarabu ya Sahrawi -Sahrawi Arab Democratic Republic (SADR) kufuatiia mkutano na Waziri wa mambo yan je wa Morocco Nasser Bourita.

    “Kenya inabatilisha utambuzi wake wa SADR na inaanza hatua za kuondoa uwepo wake nchini ,” Bw Ruto alisema katika Twitter siku moja baada ya kuapishwa kama rais wa tano wa Kenya.

    Alielezea kuunga mkono mfumo wa Umoja wa Mataifa unaosimamia mzozo unaohusu Sahara Magharibi (Western Sahara), ambayo kihistoria imekuwa ikidaiwa na Morocco na vuguvugu la Sahrawi, Polisario Front.

    Rais wa SADR Brahim Ghali alikuwa miongoni mwa viongozi waliohudhuria sherehe za kuapishwa kwa Bw Ruto tarehe 13 Septemba.

    Western Sahara inatambuliwa na Muungano wa Afrika

  9. Vita vya Ukraine: Nyumba zafurika maji baada ya makombora kupiga- bwawa kuu

    Makombora ya Urusi yamepiga bwawa la akiba ya maji lililopo katika mji wa kusini mwa Ukraine wa Kryvyi Rih, maafisa wamesema.

    Wakazi katika baadhi ya maeneo waliambiwa kuondoka, mkuu wa mji huo Oleksandr Vilkul alisema, lakini akaongeza kuwa hali ilikuwa imedhibitiwa.

    Ukraine ilisema kuwa shambulio hilo lilikuwa ni kisasi cha Urusi kwa mashambulizi yake ya hivi karibuni ya kukabiliana nao.

    Rais Volodymyr Zelensky – ambaye alizaliwa katika mji huo – aliielezea Urusi kama"taifa gaidi " baada ya shambulio katika bwawa la Karachunivske.

    "Ninyi ni wanyonge mnaopigana na raia," Bw Zelensky salisema katika hotuba yake ya Jumamosi usiku "Walaghai, baada ya kutoroka kutoka uwanja wa mapigano, wanajaribu kuleta madhara mahala pengine mbali."

    Katika hotuba yake, Bw Zelensky alisema bwawa lilikuwa "halina thamani ya kijeshi kabisa".

    Bw Vilkul alisema usiku milipuko miwili ililipuliwa kuongeza mtiririko wa maji kutoka kwenye bwawa kuelekea kwenye mto Inhulets.

    Usambazaji wa maji katika mji huo uliathiriwa na shambulio, ambalo lilitumiwa na watu zaidi ya 600,000 kabla ya vita.

    Unaweza pia kusoma:

    • Mzozo wa Ukraine: Jinsi wanajeshi wa Ukraine walivyowazidi nguvu wale wa Urusi katika mashambulizi
    • Vita vya Ukraine: Hasara waliopata wanajeshi wa Urusi inamaanisha nini kwa Putin?
    • Mzozo wa Ukraine: Fahamu uhusiano wa kihistoria kati ya Ukraine na Urusi
  10. Mfalme Charles na Wanamfalme William na Harry walivyosindikiza jeneza la Malkia kwa ajili ya kutazamwa na umma

    Mfalme Charles III na wanawe, Wanamfalme William na Harry, wametembea nyuma ya jeneza la Malkia Elizabeth II kuelekea katika Westminster Hall, ambako Malkia atatazamwa na umma kwa siku nne, kabla ya kuzikwa.

    Ndugu zake Mfalme, Binti mfalme Anne, Mwanamfalme Andrew na Mwanamfalme Edward pia walitembea katika maandamano ya huzuni kupitia katikati mwa London.

    Unaweza pia kusoma:

    • Wageni wa mazishi ya Malkia: Ni nani amealikwa na nani hakualikwa?
    • Malkia Elizabeth II: Maisha ndani ya Land Rovers
    • Malkia Elizabeth II: Ni lini na ni wapi mazishi yatafanyika ?
  11. Miili ya New Zealand katika sanduku: Mwanamke akamatwa Korea Kusini kuhusu vifo vya watoto

    Polisi ya New Zealand inasema mwanamke katika Korea Kusini ameshitakiwa kwa mauaji ya watoto wawili ambao miili yao ilipatikana katika masanduku mwezi uliopita.

    Katika kisa ambacho kiliishutua nchi, masalia ya miili yaligunduliwa na watu ambao walinunua masanduku katika duka moja lililopo katika mji wa Auckland.

    Miili hiyo ilikuwa imehifadhiwa kwa miaka kadhaa. Polisi inasema wahanga hao walikuwa na umri wa kati ya miaka mitano na 10.

    New Zealand imetuma maombi ya kutaka mwanamke huyo asafirishwe kutoka Korea Kusini kukabiliana mashitaka ya uhalifu nchini humo.

    Polisi ilisema wameshirikiana kwa karibu na mamlaka za Korea Kusini kwa kipindi cha wiki tatu zilizopita katika kumsaka mwanamke huyo, baada ya kusema mwezi uliopita kwamba wanaamini alikuwa nchini Korea Kusini.

    Walimzingira baada ya kufanikiwa kuwatambua watoto hao wadogo, ambao majina yao hayajafichuliwa.

    "Kuwa na mtu fulani mahabusu katika nchi ya ng’ambo katika kipindi kifupi namna hiyo ni jambo lililowezekana kutokana na usaidizi wa mamlaka za Korea Kusini na uratibu uliofanywa na wafanyakazi wa Interpol wa polisi ya New Zealand," alisema Inspekta wa Upelelezi Tofilau Fa'amanuia Vaaelua.

    Alisema kuwa mwanamke huyo alikamatwa na polisi wa Korea Kusini Alhamisi asubuhi, na mamlaka za New Zealand zitatuma maombi ya kutaka anyimwe dhamana kabla ya kuletwa New Zealand.

  12. Abiria afariki alipokuwa akipanda ndege ya KQ kuelekea Mombasa,Kenya

    Shirika la ndege la Kenya Airways limethibitisha kuwa abiria aliyepata matatizo ya kupumua alipokuwa akipanda moja ya ndege zake amefariki.

    Katika taarifa Jumatano, KQ ilisema abiria huyo alitangazwa kuwa amefariki katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) huku ndege hiyo iliyokuwa ikielekea Mombasa ikiwa bado ardhini.

    “Kenya Airways PLC inasikitika kutangaza kwamba abiria alipata matatizo ya kupumua jioni hii alipokuwa akipanda KQ612 ambayo iliratibiwa kuondoka hadi Mombasa saa 1900.

    "Abiria huyo alitangazwa kuwa amefariki na wafanyikazi wa matibabu katika JKIA wakati ndege ilikuwa ingali chini," KQ ilisema katika taarifa.

    Hiki ni kisa cha tatu katika kipindi cha wiki nne zilizopita.

    Shirika hilo mapema mwezi huu lilithibitisha kwamba abiria aliyekuwa kwenye mojawapo ya safari zake za ndege kuelekea New York kutoka Nairobi alikuwa ameaga dunia, ikiwa ni tukio la pili kama hilo kuripotiwa katika muda wa siku tisa.

    Mwezi uliopita, iliripoti tukio lingine ambapo abiria alifariki kwenye mojawapo ya ndege zake kutoka New York kuelekea Nairobi.

    Kulingana na shirika hilo la ndege, abiria huyo alipata matatizo ya kupumua saa saba baada ya ndege hiyo kupaa kutoka New York kabla ya kufariki. Msemaji wa familia alisema alikuwa na historia ya ugonjwa wa kisukari.

  13. Patagonia: Bilionea wa kampuni ya mavazi ya mitindo aikabidhi kampuni yake kwa uhisani

    Bilionea mwanzilishi kampuni ya mavazi Patagonia anasema ametoa kampuni yake kwa wakfu wa uhisani .

    Yvon Chouinard alisema kuwa chini ya muundo mpya wa umiliki, faida yoyote ambayo haijawekezwa tena katika kuendesha biashara itaenda kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.

    Hii itafikia karibu $100bn ($86bn) kwa mwaka, alidai, kulingana na hali ya kampuni.

    Patagonia inauza mavazi ya kupanda mlima na mavazi mengine ya shughuli za nje katika zaidi ya nchi 10.

    Ilianzishwa mwaka 1973, mapato yake yalikuwa $1.5bn mwaka huu, huku thamani ya Bw Chouinard inadhaniwa kuwa $1,2bn.

    "Licha ya ukubwa wake, rasilimali za Dunia sio nyingi, na ni wazi kuwa tumevuka mipaka yake," mjasiriamali huyo alisema juu ya uamuzi wake wa kuacha umiliki.

    "Badala ya kutoa thamani kutoka kwa asili na kuibadilisha kuwa utajiri, tunatumia utajiri ambao Patagonia inaunda kulinda chanzo."

    Kampuni hiyo ya California ilikuwa tayari ikitoa 1% ya faida yake ya kila mwaka kwa wanaharakati wa ngazi ya chini na kujitolea kwa shughuli endelevu. Lakini katika barua ya wazi kwa wateja, mfanyabiashara huyo anayeonekana kusitasita alisema alitaka kufanya zaidi.

    Alisema awali alikuwa amefikiria kuuza Patagonia na kutoa pesa kwa mashirika ya hisani, au kuipeleka kampuni hiyo kwa umma.

    Lakini alisema chaguzi zote mbili zingemaanisha kuacha udhibiti wa biashara. "Hata makampuni ya umma yenye nia njema yana shinikizo kubwa la kutengeneza faida ya muda mfupi kwa gharama ya uhai na uwajibikaji wa muda mrefu," alisema.

    Badala yake, familia ya Chouinard, ambayo imekuwa inamiliki kampunim hiyo imeihamisha kwa vyombo viwili vipya. Patagonia Purpose Trust, inayoongozwa na familia, inasalia kuwa mbia mkuu wa kampuni lakini itamiliki tu 2% ya hisa zake zote, Bw Chouinard alisema.

  14. R.Kelly: Nyota wa R&B apatikana na hatia ya unyanyasaji wa watoto

    R. Kelly, katika picha iliyopigwa 2019, akiwa mahakamani ya shirikisho ya Chicago

    Nyota wa R&B mwenye umri wa miaka 55, R. Kelly amepatikana na hatia ya unyanyasaji wa kingono wa watoto katika kesi ya pili iliyoendeshwa namahakama ya shirikisho.

    Jopo la mahakama lilimpata Bw Kelly na hatia ya makosa sita kati ya 13 katika kesi ya wiki nne iliyoendeshwa katika mji wa anaomishi wa Chicago.

    Mahakama ilimuondolea kesi ya jimbo ambayo ilipaswa kubaini iwapo kuna ushahidi kuhusu mashitaka ya ponografia ya watoto katika mwaka 2008.

    Mwaka jana muimbaji huyo wa Bump n' Grind alipatikana na hatia ya usafirishaji haramu wa watu kwa ajili ya ngono nakuhusika na njama za wizi na ulaghai mjiniNew York. Baadaye alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

    R.Kelly ambaye jina lake halisi ni Robert Sylvester Kelly, alipatikana Jumatano na hatia tatu za kuwalaghai watoto kwa ajili ya ngono na makosa matatu ya kutengeneza picha za ngono za watoto.

    Unaweza pia kusoma:

    • R. Kelly: Fahamu historia ya shutuma dhidi ya nyota huyu
    • R. Kelly ahukumiwa miaka 30 jela katika kesi ya unyanyasaji wa kingono
    • Robert Kelly: Nyota wa muziki wa R&B nchini Marekani maarufu R. Kelly apatikana na hatia ya unyanyasaji wa kingono
  15. Bei ya mafuta Kenya yaongezeka na kutishia kuzidisha zaidi gharama za bidhaa muhimu

    Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli nchini Kenya imetangaza bei mpya za mafuta.

    Katika mabadiliko hayo, lita moja ya mafuta ya petroli itauzwa kwa Sh179.30, bila ruzuku ikiwakilisha ongezeko la Sh20.18.

    Kwa upande mwingine, bei ya dizeli imeongezeka kwa Sh25 na sasa itauzwa kwa Sh165 jijini Nairobi.

    Bei ya Mafuta ya Taa imeongezeka kwa Sh20 kumaanisha kuwa itauzwa Sh147.94 jijini Nairobi.

    Bei hizo ni pamoja na asilimia 8 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

    Kupanda kwa bei ya mafuta kunafuatia kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta kwa bidhaa za petroli na serikali ya Rais William Ruto .

    Ingawa ruzuku ya petroli imeondolewa, ruzuku ya Sh20.82 kwa lita na Sh26.25 kwa lita ilihifadhiwa kwa dizeli na mafuta ya taa mtawalia.

    Mabadiliko ya bei ya mafuta yanaanza kutekelezwa mara moja.

    Ongezeko hilo linamaanisha kuwa gharama ya ya maisha inatarajiwa kupanda wakati bei za bidhaa za viwandani zinapoanza kuongezeka, kwa sababu ya ongezeko linalofuatia la gharama ya umeme.

    Vile vile, gharama ya usafiri na umeme itapanda kwa sababu Kenya inaongeza malipo ya ya mafuta kwenye bili za umeme.

    Ni gharama ya juu zaidi ya nishatinchini Kenya.

    Serikali ya Kenya inasema imetumia takriban dola bilioni 1.2 katika mwaka uliopita kuweka bei ya mafuta chini kupitia ruzuku huku bei ya bidhaa hiyo ikipanda katika soko la kimataifa.

    Kumekuwa na mseto wa maoni mitandaoni nchini humo kuhusu ongezeko hilo Serikali mpya ya rais Ruto imesema ruzuku imeondolewa kwa sababu haijawasaidia Wakenya.

    Unaweza pia kusoma

  16. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja