Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Tusaidieni kumaliza vita kufikia mwisho wa mwaka, Zelensky awahimiza viongozi wa ulimwengu

Zelensky alisema hali ya vita itaifanya kuwa ngumu zaidi kwa wanajeshi wake wanapokuwa wanapambana, na kuwataka viongozi wa G7 kufanya kila linalowezekana kumaliza vita hadi mwisho wa mwaka, chanzo kiliiambia AFP.

Moja kwa moja

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo, tukutane tena hapo kesho majaaliwa

  2. Sudan yamuita balozi wake Adis Ababa kupinga kuuawa kwa wanajeshi wake Ethiopia

    Sudan yamuita balozi wake mjini Adis Ababa kwa ajili ya mazungumzo katika hatua ya kupinga madai ya kuuawa kwa wanajeshi saba na jeshi la Ethiopia. Khartoum imemuita pia balozi wake nchiniSudan kuelezea hali iliyozingira mauaji ya wanajeshi kwenye mpaka unaozozaniwa baina ya nchi hizo.

    Jumapili jeshi la Sudanlilisema kwamba wanajeshi waliouawa walikuwa mateka lakini waliuawa na miili yao ilionyeshwa mbele ya umma. Imesema kutakuwa na jibu linalofaa kwa mauaji hayo lakini hakuelezea ni hatua gani hasa ambazo serikali ya Khartoum itazichukua. Ethiopia imekanusha mauaji hayo .

    Hali ya wasi wasi imeendelea kutanda baina ya Ethiopia na Sudan juu ya eneo la kilimo lenye rutuba lililopo baina ya mpaka hizo mbili. Makabiliano baina ya vikosi vya Ethiopia na Sudan yamekuwa ya kawaida kwa miongo , lakini yameongezeka katika muda wa mwaka uliopita. Mkataba baina ya nchi hizo katika mwaka 2008 umeshindwa kumaliza mzozo. Ethiopia na Sudan pia zimekwama katika mzozo juu ya ujenzi wa bwawa kubwa la umeme kwenye Mto Nile.

  3. Mwanasiasa wa Kenya awaomba radhi Wasomali

    Mgombea kiti cha Ugavana wa Nairobi kwa tikiti ya chama cha Jubilee, Polycarp Igathe Kamau, amelazimika kuomba msamaha kufuatia kauli yake iliyozua ghadhabu miongoni mwa wakazi wa Nairobi.

    Igathe, ambaye amekuwa akishutumiwa kwa kulenga jamii fulani mahususi, alisema matamshi yake ni tofauti na kuelewa kwamba alikuwa akiwanyooshea vidole watu binafsi.

    Akielezea matamshi yake ya awali, mwanasiasa huyo alisema alikuwa anazungumzia tu kutanguliza nafasi za kazi, uchumi na manufaa ya Nairobi.

    Igathe alisema nini?

    Hatua ya Polycarp Igathe Kamau kuomba msamaha ilifuatia video iliyosambazwa sana mitandaoni kuhusu hotuba yake ya wiki iliyopita.

    Katika kanda hiyo ya video alisema Bunge la Kaunti ya Nairobi, ambalo wanachama wake "wengi ni Wakikuyu, linadhibitiwa na wabunge watatu wa Kisomali, ambao wanazuiliwa mateka"

    Hakuwataja majina Wasomali hao watatu alidai "wanadhibiti" Bunge la Wawakilishi la Nairobi.

    "Kuna wajumbe 45 katika Bunge la Wawakilishi jijini Nairobi,wote wanatokea jamiii ya Wakikuyu,lakini kusema wote wanadhibitiwa na Wasomali watatu. Huo ndio ukweli. Kuzuiliwa mateka ndio neno halisi. Hata jana walikuwa wanafanya jambo ambalo sio halali," Igathe alionekana akisema.

    Lakini sasa ametoa taarifa ya kuomba msamaha kwa kutoa kauli hiyo, akidai kuwa ilieleweka visivyo.

    Matamshi ya awali ya mwanasiasa huyu yamewakasirisha sana Wasomali nchini Kenya.

    Mbunge wa Garissa Aden Duale alikuwa mmoja wa wanasiasa mashuhuri waliokosoa matamshi ya Igathe, akiyataja kama "kuwabagua Wasomali".

  4. Watano wahukumiwa Kifungo cha maisha jela kwa mauaji ya mtu mwenye ualbino Malawi

    Watu watano akiwemo kasisi wa kanisa la katoliki wamehukumiwa kifungo cha maisha jela na kazi ngumu kwa kumuua mwanamume mwenye ualbino nchini Malawi miaka minne iliyopita.

    Walipatikana na hatia ya kumuua MacDonald Masumbuka ambaye alitoweka Machi 2018 Kusini mwa Malawi.

    Ni kesi iliyoshtua Malawi. Na sasa wauaji wa MacDonald Masumbuka watatumikia maisha yao yote gerezani kwa mauaji ya kijana huyo mwenye umri wa miaka 22 ambaye alikuwa na ualbino.

    Watu wengine sita akiwemo polisi na ndugu wa mwathiriwa walihukumiwa kifungo cha kati ya miaka 30 na 60 jela kwa kosa la kufanya biashara haramu ya viungo vya binadamu.

    Bw Masambuka alitoweka mapema Machi 2018, mwili wake ulipatikana wiki kadhaa baadaye ukizikwa kwenye kaburi lenye kina kifupi. Mauaji yake yalikuja wakati wa mashambulizi kadhaa dhidi ya zaidi ya watu arobaini wenye ualbino katika nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika.

    Zaidi ya kesi nyingine 20 za unyanyasaji dhidi ya watu wenye ualbino zinaendelea katika mahakama za Malawi. Mauaji hayo yanahusishwa na mila zinazohusishwa na uchawi, huku watendaji wakiamini kimakosa kuwa viungo vya waathiriwa vinaleta bahati nzuri.

  5. Nato kupanua kwa kiasi kikubwa nguvu ya kikosi cha ‘makabiliano’ ya haraka

    Nato inaongeza idadi ya wanajeshi wanaopatikana kwa kikosi chake cha kukabiliana na jeshi kutoka 40,000 hadi 300,000, katibu mkuu wa muungano huo wa kijeshi ametangaza.

    "Tutaimarisha ulinzi wetu wa mbele. Tutaimarisha vikundi vyetu vya vita katika sehemu ya mashariki ya muungano, hadi viwango vya brigedi. Tutabadilisha kikosi cha NATO na kuongeza idadi ya vikosi vyetu vilivyo tayari zaidi ya 300,000," Jens Stoltenberg amewaambia waandishi wa habari mjini Madrid kabla ya mkutano wa kilele hapo wiki hii.

    Anaielezea Urusi kama tishio kubwa na la moja kwa moja kwa usalama na maadili ya muungano huo na jibu la Nato kwa uvamizi wa Ukraine kama marekebisho makubwa zaidi ya ulinzi na uzuiaji wa pamoja tangu Vita Baridi.

    Urusi na Ukraine: Mengi zaidi

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  6. AU yataka uchunguzi ufanywe kufuatia mauaji ya wahamiaji katika mpaka wa Morocco na Uhispania.

    Umoja wa Afrika umetoa wito wa kufanyika uchunguzi wa haraka kuhusu vifo vya wahamiaji wasiopungua 23 waliofariki wiki jana Ijumaa.

    Hata hivyo, mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema idadi ya vifo inaweza kuwa ya juu zaidi. Wahamiaji hao walikufa walipojaribu kuvuka hadi katika eneo la Afrika Kaskazini la Melilla, nchini Uhispania.

    Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, alisema ameshtushwa na ana wasiwasi kuhusu jinsi wahamiaji wa Kiafrika wanavyotendewa walipojaribu kuvuka mipaka ya kimataifa.

    Alizitaka nchi zote kuwatendea utu wahamiaji na kuacha kutumia nguvu kupita kiasi. Mashirika kadhaa ya kutetea haki za binadamu, likiwemo Shirika la Kimataifa la Wahamiaji na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, yametaka uchunguzi ufanyike.

    Mamlaka nchini Morocco ilisema baadhi ya waliofariki wameanguka kutoka juu ya ualinalotenganisha nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na Melilla. Zaidi ya watu 130 walifanikiwa kuruka ua hilo

    Waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez alisema anajuta kwamba watu wengi walilazimika kufa walipokuwa wakitafuta maisha bora. Aliongeza kuwa wahalifu wanaofanya kazi kwenye mipaka ndio wa kulaumiwa kwa vifo vya wahamiaji.

    Wahamiaji hao wanatarajiwa kuzikwa leo, lakini Chama cha Haki za Kibinadamu cha Morocco kimeonya dhidi ya kuwazika hadi vifo vyao vitakapochunguzwa.

  7. Jimbo la Zamfara nchini Nigeria lawaambia wakazi kuchukua silaha dhidi ya magenge ya utekaji nyara

    Mamlaka za Nigeria katika jimbo la kaskazini-magharibi la Zamfara zinatoa wito kwa wenyeji kujizatiti dhidi ya magenge ya wahalifu, katika jaribio la kukabiliana na ongezeko la idadi ya utekaji nyara na mashambulizi ya kikatili.

    Wakazi wa huko lazima wajiandikishe kabla ya kupata silaha, na mamlaka ya serikali inasema hatua zinachukuliwa ili kuwaongoza watu kupitia mchakato huu.

    Kuwauliza raia kujizatiti dhidi ya vitisho vya ukatili daima kutakuwa na utata. Lakini serikali ya jimbo hilo inaamini kuwa kuwapa raia silaha kutasaidia kukabiliana na ongezeko la hali ya ukosefu wa usalama katika eneo hilo.

    Katika hatua nyingine, gavana wa Zamfara pia ameagiza kufungwa kwa masoko katika wilaya tatu, kupiga marufuku matumizi ya pikipiki na uuzaji wa mafuta ya petroli.

    Amri ya kuua kwa risasi imetolewa kwa yeyote atakayepatikana akitumia pikipiki katika maeneo haya.

    Nigeria inajitahidi kukabiliana na wimbi kubwa la utekaji nyara unaofanywa na magenge yenye silaha kaskazini mwa nchi hiyo.

    Mara nyingi magenge hayo yanalenga jamii za vijijini ambazo hazina ulinzi, shule na madereva wa magari kwenye barabara kuu.

  8. Tusaidieni kumaliza kufikia mwisho wa mwaka, Zelensky awahimiza viongozi wa ulimwengu

    Rais wa Ukraine Zelensky ameiambia G7 kwamba alitaka vita vya Urusi nchini Ukraine viishe kabla ya msimu wa baridi kuanza, kulingana na Reuters.

    Zelensky alisema hali ya vita itaifanya kuwa ngumu zaidi kwa wanajeshi wake wanapokuwa wanapambana, na kuwataka viongozi wa G7 kufanya kila linalowezekana kumaliza vita hadi mwisho wa mwaka, chanzo kiliiambia AFP.

    Zelensky alihutubia viongozi wa G7 kupitia kiunga cha video kwenye mkutano wa kilele katika Kasri la Elmau huko Kruen, Ujerumani, ambapo aliomba msaada wa ujenzi mpya, mifumo ya ulinzi wa ndege, usaidizi wa usafirishaji wa nafaka na dhamana ya usalama.

    Pia aliwataka viongozi hao "kuongeza vikwazo" dhidi ya Urusi.

    Urusi na Ukraine: Mengi zaidi

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  9. Miaka 65 ya BBC Swahili: Forodhani Garden Zanzibar - ni zaidi ya unavyolijua na kuliskia

    Moja ya maeneo yanayokusanya watu wengi, hasa nyakati za jioni visiwani Zanzibar, ni Forodhani Garden, ukubwa wake si zaidi ya kilomita moja za mraba, lakini hubeba melfu ya wageni wa ndani na wa nje ya Tanzania.

    Upekee wa bustani hii ni uwepo wa vyakula vya aina mbalimbali, vikiwemo vya asili. Hapa ni kama kioo cha uso wa Zanzibar na taswira ya visiwa hivi eneo lililo kando ya bahari na linalotazama majumba ya asili ya mji mkongwe…

    Kutokana na umuhimu wake, haikushangaza kutumika kwa karibu dola milioni 3 mwaka 2009 kuboresha eneo hili kukidhi matakwa ya kitalii bila kuathiri, asili yake.

    Asubuhi na mapema ukifika eneo hili liko kimya kiasi, kwenye viti vya kupumzikia, utakuta watu wachache wamejipumzisha na wengine kusoma vitabu, kusikiliza muziki kwenye simu.

    Ni eneo la maarufu pia kwa watu wanaotaka kutafakari wakihitaji utulivu nyakati za asubuhi, lakini nyakati za alasiri eneo hili linakuwa na shughuli nyingi zaidi za biashara ya chakula cha mtaani, pengine kuliko maeneo yote ya Zanzibar na mengi ya Tanzania.

    Kwa Wazanzibari eneo hili ni mali na linawakilisha utamaduni wao, kwa wageni eneo hili ni burudani na starehe.

  10. Zaidi ya miili 100 ilipatikana katika jengo lililoharibiwa la Mariupol – mamlaka

    Zaidi ya miili 100 imepatikana chini ya vifusi vya jengo la makazi huko Mariupol, mshauri wa meya huyo anasema.

    Petro Andryuschenko anasema katika chapisho kwenye Telegram hakuna mipango ya vikosi vya Urusi kutafuta na kuzika miili baada ya makazi kukumbwa na shambulio la anga.

    Mji wa bandari ulitekwa na Warusi mwezi uliopita, baada ya kuharibiwa kwa makombora kwa wiki kadhaa.

    Namna wanajeshi wa Urusi walivyoteka eneo la Mariupol

  11. Belarus inaendelea kutoa msaada wa kijeshi kwa Urusi

    Belarus inaendelea kutoa msaada wa kijeshi kwa Urusi kulingana na taarifa za mkuu wa idara ya usalama Ukraine iliyotolewa saa 06:00 mnamo Juni 27, 2022.

    Kwa mujibu wa habari zilizopo, uongozi wa Belarus unaendelea kutoa msaada wa kijeshi kwa Urusi, hasa, kundi jingine la silaha zinazojumuisha hadi magari 20 yametumwa katika eneo la Belgorod.

    Huko Donetsk, adui kwa msaada wa silaha, anajaribu kuzuia Lisichansk kutoka kusini.

    Silaha zake zinashambulia miundombinu ya kiraia na kijeshi katika maeneo ya Lisichansk, Vovchoyarovka, Loskutovka na Verkhnekamenka.

    Ndege ya adui ilishambulia karibu na Lisichansk.

    Mapigano yanaendelea katika eneo la Volchoyarovka.

    Karibu na Verkhnekamenka, vikosi vya ulinzi vilisababisha hasara kubwa kwa adui na kumlazimisha kurudi.

    Ripoti hiyo pia inasema, hakukuwa na vita vikali katika masaa ya hivi karibuni, lakini katika maeneo mengi makombora, mizinga na roketi yameshuhudiwa katika makazi ya watu wa Ukraine.

    Soma zaidi:

    Urusi na Ukraine: Mengi zaidi

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  12. Zelensky atoa wito kwa nchi za Magharibi kusambaza mifumo ya ulinzi wa anga kwa Ukraine

    "Tunahitaji ulinzi wa anga ulioimarika - wa kisasa, unaofaa kabisa. Ambao unaweza kutoa ulinzi kamili dhidi ya makombora haya. Tunazungumza juu ya hili kila siku na washirika," Volodymyr Zelenskyy alisema katika hotuba yake ya jioni ya televisheni Jumapili.

    “Tayari kuna baadhi ya mikataba. Na washirika wanahitajika kuchukua hatua haraka iwezekanavyo ikiwa kweli ni washirika wala sio waangalizi. Kucheleweshwa kwa uhamishaji wa silaha katika nchi yetu, vizuizi vyovyote kwa kweli ni mwaliko kwa Urusi kutushambulia tena na tena," Zelensky alisema.

    Hapo awali, Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Oleksiy Reznikov pia alitoa wito kwa nchi za Magharibi kuipatia Ukraine mifumo madhubuti ya ulinzi wa makombora.

    Kulingana na yeye, ukweli kwamba Urusi inaishambulia Ukraine kwa makombora kutoka eneo lake, kutoka eneo la Belarusi na kutoka kwa maji ya Bahari ya Caspian na bahari Nyeusi, inaleta tishio kwa usalama wa Uropa.

    Soma zaidi:

  13. Bloomberg: Urusi imeshindwa kulipa deni la nje ya nchi kwa mara ya kwanza tangu 1918

    Kipindi kilichowekwa cha kulipa deni nje ya nchi kwa Urusi la takriban $100 milioni ambao unadaiwa kumalizika tarehe 27 Mei usiku, ulipita Jumatatu usiku, na tarehe hii ya mwisho inachukuliwa kuwa tukio la kukwepa kulipa deni kulingana na shirika la Bloomberg.

    Shirika hilo linabainisha kuwa kushindwa huko ndiko ‘’kilele cha vikwazo vikali vya Magharibi ambavyo vilikata njia za malipo kwa wakopeshaji wa kigeni na vilitokea kwa mara ya kwanza tangu 1918.

    Kulingana na shirika hilo, ‘’hii ni ishara mbaya inayoenda kwa kasi sana kwa nchi hiyo katika mageuzi ya kiuchumi, kifedha na kisiasa,’’ huku akiba ya fedha za kigeni ya benki kuu ikiwa imesitishwa na benki kubwa zaidi zikiondolewa katika mfumo wa fedha wa kimataifa.

    Bloomberg, hata hivyo, inasisitiza kwamba hadi sasa kukwepa huko kulipa deni hakuna maanishi jambo kubwa kwa Warusi.

    Waziri wa Fedha wa Urusi, shirika hilo linaandika, aliita matumizi ya neno ‘’kukwepa kulipa deni’’ kuwa kichekesho katika hali hii.

    Urusi inasema ina pesa za kulipia bili zozote zile zake.

    Ilitangaza wiki iliyopita kwamba itabadilisha na kuanza kulipa deni lake kuu lililobaki (dola bilioni 40) kwa sarafu ya nhi yake ya 'ruble', kwani nchi za Magharibi ndizo zilizotengeneza hali ya sasa katika ubadilishaji wa fedha za kigeni.

    Wizara ya Fedha ya Urusi ilisema kwamba majukumu yake yalitimizwa kwa ukamilifu, kwani wakala wa kulipa kwa Eurobonds alipokea 'ruble' bilioni 12.51.

    Wizara ya Fedha inabadilisha utaratibu mpya wa malipo ya Eurobond, ulioanzishwa na amri ya Rais wa Urusi ya tarehe 22 Juni.

    Soma zaidi:

  14. Ethiopia yatuhumiwa kuwanyonga wanajeshi wa Sudan

    Jeshi la Sudan limeshutumu jeshi la Ethiopia kwa kuwanyonga wanajeshi saba wa Sudan na raia mmoja waliokuwa mateka.

    Taarifa iliyochapishwa kwenye vyombo vya habari vya serikali ya Sudan haikutoa maelezo zaidi.

    Lakini iliyaita mauaji hayo yanayodaiwa kuwa ya kisaliti, na ikasema itazungumza..

    Hakujawa na maoni hadi sasa kutoka kwa upande wa Ethiopia.

    Mzozo wa muda mrefu wa mpaka umepamba moto katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, na mapigano ya hapa na pale katika eneo la al-Fashaga yameshuhudiwa.

    Sudan pia imekasirishwa na ujenzi wa Ethiopia wa bwawa kubwa kwenye Mto Nile.

    Soma zaidi:

  15. Vita vya Ukraine: Zelensky kuhutubia G7 huku makombora ya Urusi yakiendelea kupiga miji

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anatarajiwa kuhimiza kuwasilishwa kwa silaha nzito zaidi atakapohutubia kundi la mataifa tajiri ya G7 baadaye hii leo.

    Inafuatia msururu wa mashambulizi ya makombora ya Urusi katika mji wa Kyiv na maeneo mengine mwishoni mwa juma, ambayo yaliua takriban mtu mmoja.

    Mashariki mwa Ukraine, Urusi imechukua udhibiti kamili wa Severodonetsk na inalenga Lysychansk iliyo karibu.

    Siku ya Jumapili Bw. Zelensky alisema kuchelewesha uwasilishaji wa silaha ‘’ni mwaliko kwa Urusi kushambulia tena na tena.’’

    Akizungumza kupitia hotuba yake ya kila siku kwa njia ya video. pia alitoa wito wa mifumo ya ulinzi wa anga na vikwazo vipya kwa Urusi.

    ‘’Washirika wanahitaji kuchukua hatua haraka ikiwa kweli ni washirika, wala sio waangalizi,’’ alisema.

    Vita nchini Ukraine ni ajenda kuu ya G7 na mataifa yanatarajiwa kuahidi msaada zaidi wa kijeshi kwa Kyiv na vikwazo zaidi dhidi ya Moscow.

    Viongozi wa nchi za Magharibi wanajaribu kuwasilisha msimamo mmoja, huku Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akisema mashambulio ya makombora ya Urusi yalionyesha ‘’ni haki ya kusimama pamoja na kuunga mkono Waukraine.’’

    Hapo awali, Rais wa Marekani Joe Biden alisema Rais wa Urusi Vladimir Putin anategemea Nato na G7 ‘’kugawanyika... lakini hatujafanya hivyo na hatutafanya hivyo.’’

    Hata hivyo, mwandishi wa BBC wa masuala ya kidiplomasia James Landale, ambaye yuko kwenye mkutano huo, anasema umoja wa nchi za Magharibi kuhusu vita hivyo umedorora katika wiki za hivi karibuni, huku baadhi ya viongozi wakijadili uhusiano wa muda mrefu na Urusi na wengine wakisisitiza uungwaji mkono mkubwa na wa kudumu kwa Ukraine.

    Soma zaidi:

    Urusi na Ukraine: Mengi zaidi

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  16. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja