Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mashambulio mapya yakumba Ukraine huku viongozi wa G7 wakikutana
Makombora ya Urusi yamelenga shabaha kote nchini huku viongozi wa dunia wakikutana kwa mkutano wa kilele nchini Ujerumani.
Moja kwa moja
Polisi wa Afrika Kusini wanachunguza vifo katika klabu ya usiku
Mamlaka za Afrika Kusini zinachunguza vifo vya vijana wasiopungua 22 katika klabu ya usiku.
Mili ya waathiriwa ilipatikana imetapakaa kwenye sakafu na meza katika ukumbi wa Enyobeni Tavern katika mji wa pwani wa London Mashariki.
Miili hiyo ilipelekwa kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti, ambapo uchunguzi wa baada ya maiti - ikiwa ni pamoja na vipimo vya sumu - utatafuta kubaini chanzo cha kifo.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alitoa "rambi rambi" zake kwa familia za waathiriwa.
"Janga hili linafanywa kuwa mbaya zaidi kwa kutokea wakati wa Mwezi wa Vijana - wakati ambao sisi ... kutetea na kuendeleza fursa za kuboreshwa kwa hali ya kijamii na kiuchumi kwa vijana wa taifa letu," alisema katika ujumbe wa Tweeter.
Oscar Mabuyane, Waziri Mkuu wa Mkoa wa Cape Mashariki ambapo mkasa huo ulitokea, hakutoa sababu zinazowezekana za vifo hivyo, lakini alilaani "unywaji wa pombe bila kikomo".
Akizungumza katika eneo la tukio, alisema: "Huwezi tu kufanya biashara katikati ya jamii hivi na ukafikiri kwamba vijana hawatafanya majaribio."
Kisa hicho kilitokea alfajiri ya Jumapili. Waliopatikana wamekufa walikuwa na umri wa kati ya 18 na 20.
Zaidi ya nyumba 4,000 zimeharibiwa katika mkoa wa Kharkiv tangu kuanza kwa vita- gavana
Mkoa wa kaskazini-mashariki wa Kharkiv nchini Ukraine hivi majuzi umekuwa chini ya mashambulizi makali ya Urusi, na kusababisha vifo vya watu kadhaa. Mkuu wa mkoa Oleh Syniehubov anasema eneo hilo lilipigwa makombora tena usiku kucha.
Tangu kuanza kwa uvamizi wa Kirusi mnamo 24 Februari, askari wa Kirusi wameharibu nyumba za makazi 4,019, vituo vya matibabu 97 na taasisi za elimu 427, mkuu wa kikanda anakumbusha.
Alichapisha picha za kituo cha michezo kilicholipuliwa katika mji mkuu wa mkoa Kharkiv, akisema kuwa uwanja huo ulikuwa unatumiwa na maelfu ya watoto na wanafunzi kabla ya vita.
"Hakuna hata siku moja iliyopita bila wakazi wa eneo la Kharkiv kushambuliwa! Kwa hivyo, hatuwezi kupumzika, kila wakati unapopuuza ving'ora vya hewa vinaweza kugharimu maisha yako!" Syniehubov anaonya.
Ni nini kinaendelea kwa sasa katika mkutano wa G7?
Kama vile tulivyotangulia kuripoti, vita nchini Ukraine vimekuwa ajenda kuu huku viongozi wa baadhi ya mataifa yenye nguvu zaidi duniani wakikutana nchini Ujerumani.
Mkutano wa G7 unatawaliwa na mijadala kuhusu uvamizi wa Urusi na jinsi Ukraine inavyoweza kuungwa mkono.
Viongozi wanatarajiwa kuahidi msaada zaidi wa kijeshi kwa Kyiv na kuweka vikwazo zaidi dhidi ya Moscow
- Mwenyeji wa mkutano huo, Kansela Olaf Scholz, alisema umoja juu ya Ukraine ni ujumbe wazi wa G7 kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin.
- Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ametoa wito kwa nchi za Magharibi kuendelea kuiunga mkono Ukraine, na kukubali athari ambazo inayoweza kutokana na hatua hiyo kwa mataifa yao yenyewe.
- Rais wa Marekani Joe Biden ametoa wito wa kuwepo kwa umoja - katika G7 na Nato - katika kukabiliana na uvamizi wa Urusi, akisema Putin amekuwa akiweka benki katika nchi za Magharibi - lakini haijafanya hivyo.
- Johnson na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wanakubaliana kwamba mzozo wa Ukraine uko katika wakati mgumu, na "fursa ya kubadilisha hali ya vita", Downing Street inasema.
- Mataifa ya G7 "yana malengo sawa - kukata oksijeni kutoka kwa mashine ya vita ya Urusi, wakati wa kutunza uchumi wetu", anasema Charles Michel, rais wa Baraza la Ulaya.
- Uingereza, Marekani, Canada na Japan zitapiga marufuku uagizaji wa dhahabu ya Urusi katika jitihada za kudhibiti uwezo wa Moscow wa kufadhili vita hivyo, na Biden alipendekeza wanachama wengine wa G7 - Ufaransa, Ujerumani na Italia - kuiga mfano huo.
Mlipuko dhdi ya jengo la Kyiv ni mojawapo ya mashambulio kadhaa nchini Ukraine leo
Mashambulizi ya asubuhi ya leo kwenye jengo la makazi huko Kyiv ni mojawapo ya mashambulio kadhaa yaliyofanywa na Urusi nchini Ukraine leo.
Moscow inasema vikosi vyake vimefanya mashambulizi dhidi ya vituo vitatu vya mafunzo ya kijeshi kaskazini na magharibi mwa Ukraine, kikiwemo kimoja karibu na mpaka wa Poland.
"Silaha zenye usahihi wa hali ya juu za vikosi vya anga vya Urusi na makombora ya Kalibr" zilitumiwa, wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema katika taarifa.
Miongoni mwa malengo hayo ni kituo cha mafunzo ya kijeshi kwa vikosi vya Ukraine katika wilaya ya Starychi katika eneo la Lviv, takriban kilomita 30 kutoka mpaka na mwanachama wa Nato Poland - siku chache kabla ya mkutano wa kilele wa Nato mjini Madrid.
Pia kumeshuhudiwa milipuko zaidi huko Kyiv - afisa wa eneo hilo alisema hapo awali kumekuwa na milipuko sita katika mji wa Kyiv - na katikati mwa jiji la Cherkasy, na mashambuluio ya makombora katika mkoa wa Kharkiv.
Shirika la habari la Reuters linaripoti kuwa kuna shimo kubwa la mlipuko karibu na uwanja wa michezo katika shule ya chekechea mita 400 kutoka kwa jengo la ghorofa lililoshambulia katika mji mkuu wa Ukraine.
Ukraine pia imetoa maoni yake kuhusu mashambulizi hayo.
"Zaidi ya makombora 50 ya aina mbalimbali yalirushwa - angani, baharini na ardhini,"Usimamizi wa jeshi la anga la Ukraine unasema, na kuongeza kuwa ni vigumu kuzuia makombora ya Urusi kama vile Iskander.
Vita vya Ukraine: Uingereza, Marekani, Canada na Japan kupiga marufuku uagizaji wa dhahabu ya Urusi
Uingereza, Marekani, Canada na Japan zitapiga marufuku uagizaji wa dhahabu ya Urusi katika juhudi za kuathiri uwezo wa Moscow kufadhili vita nchini Ukraine.
Waziri Mkuu wa Uingereza alisema hatua hiyo "itagusa moyo wa mashine ya vita ya Putin".
Usafirishaji wa dhahabu ulikuwa wa thamani ya £12.6bn ($15.4bn) kwa Urusi mwaka 2021, na Uingereza inasema umuhimu wao umeongezeka tangu uvamizi huo huku oligarchs wakikimbilia kununua bullion ili kuepuka vikwazo.
Inakuja huku mataifa tajiri zaidi duniani maaarufu G7 yakikutana nchini Ujerumani.
Rais wa Marekani Biden alipendekeza mataifa mengine ya G7 - Ujerumani, Ufaransa na Italia - pia yajiunge na marufuku hiyo.
"Kwa pamoja, G7 itatangaza kwamba tutapiga marufuku uagizaji wa dhahabu ya Urusi, mauzo makubwa ya nje ambayo yanaingiza mabilioni ya dola kwa Urusi," alisema katika ujumbe wa Tweeter.
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson aliongeza: "Tunahitaji kuutia njaa utawala wa Putin kutokana na ufadhili wake. Uingereza na washirika wetu wanafanya hivyo."
G7 na Nato lazima zisimame pamoja dhidi ya vita vya Urusi - Biden
Rais wa Marekani Joe Biden amesema nchi za Magharibi lazima ziungane na kuwa kitu kimoja dhidi ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
"Lazima tukae pamoja," Biden alimwambia Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani katika mkutano wa awali, kabla ya mkutano wa G7 kuanza.
"Putin amekuwa akitegemea hilo tangu mwanzo, kwamba kwa njia fulani Nato na G7 itagawanyika ... lakini hatujafanya hivyo, na hatutafanya hivyo.
"Kwa hivyo, hatuwezi kuruhusu uchokozi huu kuchukua muelekeo wake na kuacha nayo."
Urusi na Ukraine: Mengi zaidi
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
Prince Charles "alikubali mkoba uliokuwa na euro 1m", ripoti yadai
Mwanamfalme wa Wales Charles alikubali mkoba uliokuwa na euro milioni moja pesa taslimu kutoka kwa Waziri Mkuu wa zamani wa Qatar, gazeti la Sunday Times limeripoti.
Gazeti hilo linasema hii ilikuwa moja ya michango mitatu ya fedha kutoka kwa Sheikh Hamad bin Jassim yenye jumla ya euro milioni tatu.
Clarence House ilisema michango kutoka kwa sheikh huyo ilipitishwa moja kwa moja hadi moja ya mashirika ya uhisani ya watoto ya mwanamfalme huyo na taratibu zote sahihi zilifuatwa.
Hakuna pendekezo kwamba malipo yalikuwa kinyume cha sheria.
Kulingana na gazeti la Sunday Times, Prince Charles alipokea michango hiyo mitatu ya pesa ana kwa ana kutoka kwa waziri mkuu wa zamani kati ya 2011 na 2015.
Inadaiwa kuwa wakati mmoja pesa hizo zilikabidhiwa wakati wa mkutano katika Clarence House. Kwa upande mwingine, gazeti hilo liliripoti kuwa pesa hizo zilikuwa kwenye mifuko ya bidhaa kutoka duka kuu la Fortnum na Mason
Katika taarifa yake, Clarence House ilisema: "Misaada ya uhisani iliyopokelewa kutoka kwa Sheikh Hamad bin Jassim ilipitishwa mara moja kwa moja hadi moja ya mashirika ya watoto ya mwanamfalme huyo na taratibu zote za kiutawala zilifuatwa.
Fedha hizo zilipokelewa na Mfuko wa Hisani wa Prince of Wales, ambao lengo lake lilikuwa "kubadilisha maisha na kujenga jamii endelevu", kwa kutoa ruzuku kwa mambo mazuri katika nyanja kama vile uhifadhi, elimu, afya na ushirikishwaji wa kijamii.
Hazina hiyo ililiambia gazeti la Sunday Times kwamba wadhamini wake walihitimisha kuwa mfadhili huyo alikuwa halali na kwamba wakaguzi wake walitia saini juu ya mchango huo.
Michango kwa mashirika ya misaada ya Prince Charles imekuwa ikichunguzwa katika miezi ya hivi karibuni kufuatia madai kwamba mmoja wao alitoa msaada wa wafadhili wa Saudi ili kupata heshima na uraia wa Uingereza.
Polisi wa Metropolitan walisema mapema mwaka huu kwamba wanachunguza madai kuhusu Wakfu wa Prince Charles chini ya Sheria ya Heshima (Kuzuia Unyanyasaji) ya 1925.
Takriban watu 20 wapatikana wamefariki katika klabu ya usiku nchini Afrika Kusini
Takriban watu 20 wamepatikana wamekufa katika klabu ya usiku katika jiji la London Mashariki nchini Afrika Kusini, vyombo vya habari vya nchini humo vimeripoti.
Miili ilipatikana katika ukumbi wa Enyobeni Tavern mapema Jumapili na wengine kadhaa wanasemekana kujeruhiwa.
"Hali inayozingira tukio hilo inachunguzwa tunapozungumza," msemaji wa polisi aliambia kituo cha televisheni cha Newzroom Africa.
"Hatutaki kufanya uvumi wowote katika hatua hii," Brigedia Tembinkosi Kinana alisema.
Jamaa za wahasiriwa wameshindwa kuona miili yao, ripoti zinasema, na wenyeji wametaka ukumbi huo kufungwa.
Idadi kubwa ya wafanyakazi wa huduma ya dharura wako kwenye eneo la tukio katika jimbo la Eastern Cape.
Kamishna wa Polisi wa Eastern Cape Nomthetheleli Lilian Mene yuko kwenye eneo la tukio, na aliambia SABC News kwamba "kulikuwa na madai ya mkanyagano ndani ya eneo hilo la burudani".
Brigedia Kinana aliwaambia waandishi wa habari wengi wa waliokutwa wamekufa ni vijana wenye umri kati ya miaka 18 na 20.
Walioshuhudia waliambia gazeti la Daily Dispatch kwamba miili ilikuwa ndani ya ukumbi huo kana kwamba imeanguka sakafuni.
BBC imeshindwa kuthibitisha hili na maelezo bado yanajitokeza.
Urusi yaahidi Belarus makombora yenye uwezo wa nyuklia
Urusi itatuma mifumo ya makombora ya masafa mafupi yenye uwezo wa nyuklia kwa mshirika wake Belarus miezi michache ijayo, Rais Vladimir Putin amesema.
Alisema mifumo ya Iskander-M "inaweza kurusha makombora ya balestiki na ya kusafiri, ya kawaida na ya nyuklia".
Mifumo hiyo inauwezo wa kurusha makombora umbali wa hadi kilo mita 500 sawa na (maili 310).
Mvutano kati ya Urusi na nchi za Magharibi umeongezeka, kufuatia uamuzi wa Rais Putin kuivamia Ukraine tarehe 24 Februari.
Bw Putin amekuwa akirejelea mara kadhaa kutaja silaha za nyuklia tangu wakati huo, jambo ambalo wengine wametafsiri kuwa onyo kwa nchi za Magharibi kutoingilia kati mzozo wa Ukraine.
Akizungumza mjini St Petersburg, Bw Putin alisema Urusi itasaidia kurekebisha ndege za kivita za Belarus SU-25 ili ziweze kubeba silaha za nyuklia, kujibu swali la Bw Lukashenko.
Wakati huo huo milipuko kadhaa iliripotiwa huko Kyiv Jumapili asubuhi, Meya wa jiji hilo Vitali Klitschko alisema."Ambulensi na waokoaji wako kwenye tovuti.
Katika majengo mawili, uokoaji na uokoaji wa wakazi unaendelea," aliongeza.Shirika la habari la AFP liliripoti kuwa makazi ya watu katika jiji hilo yameshambuliwa.
Siku ya Jumamosi Ukraine ilisema vikosi vya Urusi "vimeuteka kikamilifu" mji muhimu wa mashariki wa Severodonetsk, kufuatia wiki za mapigano makali.
Kutekwa kwa mji huo kunamaanisha kuwa Urusi sasa inadhibiti karibu jimbo lote la Luhansk na sehemu kubwa ya jimbo jirani la Donetsk - maeneo mawili ambayo yanaunda Donbas kubwa ya viwanda.Katika hotuba yake ya video mwishoni mwa Jumamosi, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliahidi kurudisha "miji yetu yote" iliyokuwa inakaliwa na Urusi.
Siku ya Ijumaa usiku Urusi ilirusha msururu wa makombora katika maeneo inayolenga kaskazini na magharibi mwa Ukraine.
Watu watatu waliuawa na wengine huenda wamezikwa chini ya vifusi katika mji wa Sarny magharibi mwa Kyiv, afisa wa eneo hilo alisema.
Baadhi ya roketi zilirushwa kutoka Belarus, Ukraine ilisema. Belarus imetoa msaada wa vifaa kwa Urusi lakini jeshi lake halishiriki rasmi katika mzozo huo.Idara ya kijasusi ya Ukraine imesema mashambulizi hayo ya makombora yalikuwa sehemu ya juhudi za Kremlin kuivuta Belarus katika vita.
Urusi naUkraine: Mengi zaidi
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
Hujambo na karibu.