Mzozo wa Ngorongoro: Kaya 86 kutoka jamii za wafugaji kuhamishiwa katika mkoa jirani wa Tanga.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amefichua Alhamisi kuwa amepokea orodha ya wakazi 453 walio tayari kuhamishwa kutoka Hifadhi ya Ngorongoro baada ya serikali kuanza zoezi la hiari la kusajili wanaotaka kuhama.
Serikali inawaruhusu Wamasai kuishi katika eneo la hifadhi pamoja na wanyamapori, lakini hivi karibuni ilizua wasiwasi juu ya ongezeko la watu, idadi ya makazi, mifugo na shughuli za kibinadamu zinazotishia uendelevu wa eneo lililoorodheshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni (UNESCO) kuwa moja ya Urithi wa Dunia.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, ilisema kuwa kaya 86 kutoka katika jamii za wafugaji ambazo zimeeleza nia ya kuhama zitahamishiwa Kaskazini Mashariki mwa Tanzania, katika mkoa jirani wa Tanga.
Akihutubia wazee wa Kimasai zaidi ya 350 wanaofahamika kwa jina la Laigwanan, Waziri Mkuu alisema Mkuu wa Nchi, Samia Suluhu ameeleza masikitiko yake juu ya hatma ya eneo hilo kutokana na kuongezeka kwa mifugo na binadamu wanaoishi kwa Pamoja na wanyamapori.
Waziri Mkuu Majaliwa alieleza kuwa miaka ya 1960 na 1970 hakukuwa na wasiwasi wowote katika makazi ya Ngorongoro kwa sababu mwaka 1959 kulikuwa na wakazi 8,000 tu katika eneo hilo huku wengi wao wakimiliki mifugo kati ya 20 na 30.
Alisema hivi sasa idadi ya watu wanaoishi katika makazi hayo inafikia zaidi ya 110,000 huku idadi ya mifugo ikiwa zaidi ya 813,000.
Soma zaidi:
























