Kwanini Trump anaipongeza Nigeria?

Rais huyo wa zamani ametoa wito kwa nchi zingine kufuata mkondo na kuzifungia Facebook na Twitter " kwa kudhibiti uhuru wa kujieleza".

Moja kwa moja

Ambia Hirsi and Lizzy Masinga

  1. Tumefika mwisho wa taarifa zetu za moja kwa moja, mpaka kesho panapo majaaliwa

  2. Wanamuziki wawili nusura 'wazichape' hadharani nchini Nigeria

    Seyi Shey na Tiwa Savage ni wanamuziki wakubwa Nigeria

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wanamuziki wanawake wawili wa Nigeria, ambao hawapatani, Sheyi Shey na Tiwa Savage walikuwa na mzozo kwenye saluni huko Lagos.

    Katika video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Sheyi alijaribu kumsalimia Tiwa ambaye aliikataa salamu yake akikumbusha wimbo wa Seyi ambao ulionekana kumkera Tiwa.

    Seyi alikuwa amemwita Tiwa majina mbalimbali kwenye wimbo wake alioshirikiana na mwanamuziki wa Kenya Victoria Kimani.

    Tiwa alimwambia Seyi hakusahau alichosema juu yake miaka miwili iliyopita akisema kuwa salamu yake kwake ni ya kuigiza baada ya kumsema hadharani.

    Seyi alisema kuwa alitaka kuomba radhi lakini Tiwa alisema alipaswa kufanya hivyo kwa kumpigia simu na kuzungumza naye.

    Wawili hao karibu wapigane walipokuwa wakirushiana maneno.

  3. Kiongozi wa waasi wa Rwanda akamatwa kwenye sherehe za ubatizo wa mtoto wake

    Kanali Augustin Nshimiyimana wa waasi wa FDLR amekamatwa jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC wakati alipohudhuria ubatizo wa mtoto wake, msemaji wa kundi hilo ameeleza.

    Kanali Nshimiyimana ambaye amekuwa naibu mkuu wa idara ya intelijensia ya waasi hao wa Rwanda kati ya mwaka 2011 na 2019, alichukuliwa wiki iliyopita na watu wenye silaha waliokuwa wamevalia mavazi ya kiraia.

    ''Walifika mahali alipokuwa kanisani walikokuwa wakisheherekea ubatizo wa mtoto wake na kumkamata'', Msemaji wa FDLR Curé Ngoma’ aliiambia BBC.

    Bwana Ngoma amesema wanaamini operesheni hii ilifanywa na vikosi vya Rwanda vikishirikiana na jeshi la Congo.

    Mamlaka za Rwanda zimekana uwepo wa vikosi vya Rwanda kwenye ardhi ya Congo.

    Majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri kunafanyika doria za kudhibiti vurugu na kudhibiti uasi katika maeneo hayo.

    FDLR nchini DRC limekuwa likishutumiwa kuwasajili watoto kwenye jeshi, vitendo vya ubakaji na uporaji, wakati serikali ya Rwanda ikilishutumu kundi hilo kuhusika kwenye mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

  4. UN yalaani mauaji ya wafanyakazi wa misaada nchini Sudan Kusini,

    Ramani ya Sudani Kusini

    Umoja wa Mataifa umelaani mauaji ya wafanyakazi wawili wa misaada katika jimbo la Central Lake nchini Sudan Kusini.

    Raia wa Sudan Kusini walikuwa wakifanya kazi kwa wakala wa misaada wa Italia.

    Walivamiwa na watu wenye silaha kali waliporudi kutoka kupeleka vifaa vya lishe kwenye vituo vya afya katika eneo la Yirol.

    UN ilisema gari lao lilikuwa linatambulika wazi na umetoa wito kwa mamlaka kuchunguza mara moja mauaji hayo.

    Hatua hiyo inakuja wakati kukiwa na ongezeko kubwa la mauaji na vurugu kote Sudan Kusini ambazo zimegharimu maisha ya watu zaidi ya 200 tangu katikati ya mwezi Mei.

    Wafanyakazi wanne wa misaada wameuawa nchini Sudan Kusini mwaka huu pekee, wote katika mwezi uliopita.

    Wafanyakazi tisa wa misaada waliuawa mwaka 2020. Mashambulio hayo yameleta hofu juu ya uwezekano wa kusimamishwa kwa shughuli za kibinadamu ambazo zinaweza kuathiri mamilioni ya watu wanaohitaji msaada wa chakula.

  5. Tundu Lissu afanyiwa upasuaji kwa mara ya 25

    Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu amefanyiwa upasuaji wa 25, baada ya shambulio dhidi yake mnapo tarehe 7 mwezi Septemba mwaka 2017.

    Tundu Lissu amechapisha katika mtandao wa twitter picha yake akiwa katika kitanda cha hospitalini na kuandika:

    ''Leo nimefanyiwa upasuaji wa 25 baada ya jaribio la mauaji ya Septemba 7 mwaka 2017, ni wakati sasa kwa Rais Samia kuniambia, kuliambia taifa na dunia ni nani alitekeleza shambulio na kwa nini?...

    Ruka X ujumbe
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe

    Polisi walisema nini?

    Mwezi Aprili,msemaji wa jeshi la polisi nchini Tanzania David Misime alisema uchunguzi juu kesi ya Bwana Lissu ulisimamishwa baada ya kukataa kujibu ombi la polisi la ushirikiano katika uchunguzi huo .

    Aidha Bw Misime alisema polisi wana wajibu wa kisheria wa kuwalinda watu na mali zao bila kujali utaifa wao, kutambua, kuzuia na kutekeleza sheria ili kuimarisha Amani, na usalama na mwingiliano.

    Alisema polisi wanahakikisha usalama kwa raia wote bila ubaguzi na upendeleo, akisema changamoto za kiuslama zinapaswa kuripotiwa kulingana na taratibu ili mamlaka husika zichukue hatua.

    Mara baada ya shambulio dhidi yake tarehe 7 Septemba, 2017, Bw Lissu alisafirishwa kwa ndege hadi katika Hospitali ya Nairobi Kenya ambako alipokea matibabu kabla ya kuhamishiwa nchini Ubelgiji kwa matibabu maalumu.

  6. Rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi kufanya ziara ya kikazi kesho nchini Tanzania

    Rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi

    Chanzo cha picha, Botswana Government

    Rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania Alhamisi kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku mbili, baada ya mwaliko wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

    Rais Masisi atawasili kesho majira ya asubuhi.

    Rais Masisi atafanya mazungumzo na Rais Samia Ikulu ya jijini Dar es Salaam.

    Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Liberata Mulamula amesema viongozi hao watakuwa wakizungumzia masuala mbalimbali, lakini zaidi kuhusu ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, ikiwemo kufanyika kwa mikutano ya tume ya pamoja ya ushirikiano (Joint Permanent commission) ambayo ilianzishwa mwaka 2009.

    ''Katika mahusiano yetu na ushirikiano tumekuwa na utamaduni wa kuanzisha tume za pamoja, kupitia tume hizi huwa tunaangalia masuala mbalimbali, sasa katika ziara hii tunatarajia kwamba watazungumzia masuala ya kidiplomasia lakini kubwa zaidi matumizi ya lugha ya kiswahili nchini Botswana''. Alisema Waziri Mulamula.

    Mwaka 2019 kilipofanyika kikao cha wakuu wa nchi wa SADC nchini Tanzania azimio kubwa lililotokana na kikao hicho ni kuanzisha na kuendeleza lugha ya kiswahili katika nchi za jumuia hiyo.

    Lakini pia kutumika kama lugha ya vikao katika mikutano ya SADC.

    ''Botswana walilipokea azimio hilo kwa kuona jinsi gani wataweza kuanzisha mitaala ya kufundisha kiswahili katika vyuo vyao vikuu lakini pia kuiendeleza katika mawasiliano katika wizara ya mambo ya nje na wizara nyingine.'' Alisema Waziri Mulamula.

    Masuala mengine ni mahusiano ya kibiashara na uchumi kati ya nchi hizo na kujadili namna ya kuimarisha zaidi jumuia ya SADC.

    ''Kupitia makubaliano ya tume ya pamoja, Tanzania na Botswana zitaimarisha uhusiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji ambapo Tanzania itaweza kuuza mazao ya chakula kama Soya, Mchele,ufuta, alizeti na viungo mbalimbali vya chakula nchini Botswana''.

    Pia mazao ya bahari kama samaki ambao hakuna nchini kwao.

    Nchi hizi mbili zinajivunia kuwa na uhusiano mzuri wa kidugu wa muda mrefu, msingi wa uhusiano uliopo umechangiwa na harakati za kupigania uhuru chini ya mwamvuli wa nchi hizo kuwa mstari wa mbele, ambapo zilichangia sana harakati za uhuru wa nchi mbalimbali za Afrika zikiwemo Afrika Kusini, Angola, Msumbiji, Namibia na Zimbabwe.

  7. Waridi wa BBC: Mahari yangu ilirejeshwa kutokana na utasa

    Roseline Orwa

    Chanzo cha picha, ROSELINE ORWA

    Roseline Orwa ni mama wa miaka 46, yeye ni mwanamke mjane ambaye hakufanikiwa kushika mimba wakati wa ndoa zake mbili , ila hilo halijamkosesha usingizi kwa kukubali hali yake. Kilichomsikitisha ni hatua ya mahari yake kurejeshwa ilimshangaza.Soma zaidi

  8. Trump aunga mkono hatua ya Nigeria kuifungia Twitter

    Bw. Trump alifungiwa na Twitter na Facebook mwezi Januari

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Bw. Trump alifungiwa na Twitter na Facebook mwezi Januari

    Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amepingeza hatu ya Nigeria kuipiga marufuku Twitter - na kutoa wito nchi zingine zifuate mkondo huo.

    "Pongezi kwa nchi ya Nigeria, kwa kuifungia Twitter kwasababu ya kumpiga marufuki Rais wao," alisema katika taarifa.

    Rais huyo wa zamani ametoa wito kwa nchi zingine kufuata mkondo na kuzifungia Facebook na Twitter " kwa kudhibiti uhuru wa kujieleza".

    Bw. Trump alipigwa marufuku na katika mitandao ya kijamii ya Twitter na Facebook mwezi Januari kwa tuhuma za kuchapisha ujumbe wa kuchochea uvamizi wa bunge la Marekani. Watu watano walifariki kutokana na kisa hicho.

    Twitter

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, alijita kwanini hakuzifungia Facebook na Twitter wakati wa Urais wake.

    "Wao ni nani kuamua kizuri na kibaya ikiwa wao wenyewe ni wabaya? Nadhani ningeliwapiga marufuku nilipokuwa Rais. Lakini [Mwanzilishi wa Facebook Mark] Zuckerberg aliendelea kunipigia simu na kuja Ikulu ya White House kwa chakula cha jioni akiniambia jinsi nilivyokua mzuri," alisema.

    Wiki iliyopita Nigeria ilifunga akaunti za Twitter nchini humo kwa madai kwamba "shughuli za mtandao huo zinahujumu uwepo wa Nigeria kama taifa lililoundwa shirikisho".

    Hatua hiyo ilichukuliwa siku kadhaa baada ya ujumbe wa Rais Muhammadu Buhari kuondolewa kwa kukiuka kanuni za mtandao wa huo wa kijamii.

    Ilizua ghadhabu miongoni mwa Wanaigeria na mataifa ya magharibi ambayo yalisema hatua hiyo inaminya uhuru wa kidemokrasi.

    Pande zote mbili zimesema zinajadiliana kuhusu namna ya kusuluhishi

    Soma zaidi:

    • Twitter: Fahamu watu maarufu waliofungiwa na twitter kwa kukiuka sheria zake
  9. Makumi ya watoto 'wametekwa na wanamgambo wa kijihadi' Msumbiji

    Zaidi ya watu 700,000 , nusu yao watito wamefurushwa makwao kutokana na ghasia

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Zaidi ya watu 700,000 , nusu yao watito wamefurushwa makwao kutokana na ghasia

    Makumi ya watoto, wengi wao wasichana, wametekwa na makundi yakijihadi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Shirika la Uingereza la kuwahudumia watoto, Save the Children linasema.

    Shirika hilo limeongeza kuwa karibu watoto 51 wametekwa licha ya ghasia ba ukosefu wa usalama kuwasambaratisha maelfu ya watu.

    Linasema idadi ya waliotekwa huenda ikawa "juu zaidi" - kwani ripoti yake inaangazia visa vilivyoripotiwa pekee.

    Shirika hilo limeelezea wasi wasi wake kuwa visa vya utekeji "ni mbinu mpya inayotumiwa na mara kwa mara na makundi hayo vitani ".

    "Kutekwa, kushuhudia utekaji na kulazimishwa kutoroka mashambulio kutoka kwa makundi ya wanamgambo - ni hali inayowaathiri watoto wadogo kwa wakubwa," mkurugenzi wa shirika hilo nchini Msumbiji Chance Briggs alisema.

  10. Kenya kufunga maelfu ya nambari ya siri ya walipa kodi wasiowajibika

    Mamlaka ya mapato nchini Kenya (KRA) inatarajiwa kuzifungia jumla ya nambari za siri 66,269 za kulipa kodi ambazo hazitumiki kufikia Alhamisi wiki hii, ripoti za vyombo vya habari nchi humo zinasema .

    Wamiliki wa nambari hizo za siri za kulipa kodi ambao ni pamoja na watu binafsi na mashirika ya biashara huenda wakafutiwa usajili malipo ya ushuru wa bidhaa.

    Walipa kodi watakaoathiriwa watazuiwa kutoza ada ya ushuru wa bidhaa katika biashara zao na huenda wakakabiliwa na vikwazo vingine vya utozaji ushuru.

    Hatua kama hiyo pia itachukuliwa dhidi ya watu ambao hawajakuwa wakijaza fomu ya kuthibitisha wanalipa kodi kwa mujibu wa sheria.

    “Kufutiwa kwa jukumu la kulipa ushuru wa bidhaa ni mpango unaoendelea, utawaathiri walipa kodi ambao hawatajaza fomu ya kila mwezi ya kuthibitisha wamelipa ushuru wa bidhaa au wale ambao hawaoneshi jinsi walivyolipa ushuru huo kila mwezi miongoni mwa mambo mengine,” KRA ilisema katika taarifa yake kwa umma.

  11. Rais Museveni ateua baraza jipya la mawaziri

    Yoweri Museveni

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Rais Museveni awateua wanawake 10 katika baraza lake jipya la mawaziri.

    Rais wa Uganda Yoweri Museveni amefanya uteuzi wa baraza jipya la mawaziri 31 na manaibu waziri 50.

    Baraza hilo linajumuisha wanawake 10.

    Jessica Alupo, ambaye ni meja mstaafu wa jeshi, ameteuliwa kuwa Makamu wa Rais. Ni mwanamke wa pili katika historia ya nchi hiyo kuteuliwa katika wadhifa huo. Alupo aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Elimu.

    Robinah Nabbanja, afisa wa ngazi ya juu wa chama tawala, ameteuliwa kuwa Waziri Mkuu na kiongozi wa shughuli za serikali bungeni. Alikuwa naibu waziri wa afya.

    Rebecca Kadaga, wakili na mwanasiasa wa zamani ambaye hadi uteuzi wake katika baraza la mawaziri alikuwa spika wa bunge amepewa wadhifa wa naibu waziri mkuu wa kwanza. Pia amepewa jukumu kusimamia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

    Baraza hilo la mawaziri pia linajumuisha maafisa wapya kutoka jeshini. Kamanda Mkuu wa sasa wa Majeshi, Jenerali David Muhoozi, ndiye naibu waziri wa mambo ya ndani. Jenerali eneral Muhoozi pia anawakilisha jeshi bungeni .

    Mmoja wa mawakili wa kibinafsi wa rais, Kiryowa Kiwanuka, ameteuliwa kuwa Mawanasheria Mkuu.

    Sam Kuteesa, ambaye amekuwa Waziri wa Uganda wa Mambo ya nje kwa muda mrefu, ameondolewa katika baraza la mawaziri.

  12. Karibu katika matangazo mubashara leo Jumatano 09.06.2021