Mwanafunzi afukuzwa shuleni kwa kujichora tattoo

Mzazi amejipata akiwa katika njia panda baada ya kijana wake wa kidato cha tatu kufukuzwa shuleni kwasababu ya Uchoraji wa chale au tattoo iliyochorwa kwenye mkono wake.
Akizungumza na gazeti la The Star nchini Kenya, Rosemary amesema ameshutuka utawala wa shule ya kaunti ya Kakamega ulipomrejesha kijana wake nyumbani na kudai kuwa ataruhusiwa tu kurejea shuleni tattoo hiyo itakapoondolewa.
"Nilipowasili shuleni, niliarifiwa na mkuu wa shule kwamba nitarejea nyumbani na mtoto wangu kwasababu ana tattoo na shule haiwezi kumruhusu mtoto wangu kuendelea na masomo," amesema Rosemaryalipozungumza na gazeti la The Star nchini Kenya.
Mzazi wa mtoto huyo amesema hakujua kuwa mtoto wake ameweka tattoo hadi siku chache kabla ya shule kufunguliwa.
Mama huyo amesema kuwa alimuona mtoto wake akificha mkono wake na baada ya kumdadisi akagundua kuwa alichora tattoo ya nyayo yenye jina la mama yake.
Mama huyo amesema alijaribu kuzungumza na shule lakini hakuna aliyetaka kusikiliza maombi yake na amekuwa akijitahidi kutafuta msaada ila bado hajafanikiwa kwasababu mchakato wa kuondoa tattoo hiyo ni gharama kubwa mno na pia kuna hatari ya mkono wa mtoto wake kupooza na kufura.
Rosemary amesema sasa alichosalia nacho ni imani tu kuwa shule hiyo itampa mtoto wake adhabu ya kufanya kumuwezesha kuendelea na masomo kwasababu tayari ameshalipa ada.
Tatoo hutolewa namna gani?

Kulingana na mtaalamu Munira wa suala la tattoo nchini Tanzania, tattoo hutolewa kwa mfumo wa laser ambao hutumia miale ya moto na Munira anasema wakati mwingine mtu analazimika kutumia laser mbili tofauti hasa inapotokea kuwa tattoo imechorwakwa wino mweusi na mwekundu na tattoo zenye rangi ya bluu, njano, kijani na nyekundi huhitaji laser tofauti na yenye miale yenye moto mwingi zaidi kuliko tattoo iliyochorwa na wino mweusi.
Mtaalamu Munira anasema, iwapo mtu ana mzio wa aina yoyote au mtu anatumia vidonge vya uzio kwa takriban miezi sita huwa hawaruhusiwi kupata matibabu ya laser.
Munira pia ameongeza kuwa mtu mwenye kisukari au virusi vya HIV pia hastahili kutolewa tattoo kwa mfumo huo wa laser.

Mfumo huo wa Laser huvunja vunja wino kwa vipande vidogo na baada ya muda hufanya wino huo kuanza kupotea.
Mtaalam Munira kuna wakati alitumia matone madogo madogo na miale ya rangi ya kijani na ngozi ya mteja ikaanza kuvimba.
Utoaji wa tattoo hutolewa kwa hatua tofauti kulingana na jinsi tattoo hiyo ilivyochorwa. Na mtu akitolewa tattoo mara ya kwanza haitoki kabisa bali wino hupungua tu.
Pia utolewaji wa tattoo kwa kweli si jambo rahisi. Anayetolewa anahitaji kuhimili maumivu.










