Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Israel yatoa wito kwa Hamas kujisalimisha huku jeshi likishambulia mji wa Gaza
Vita vinaweza kumalizika mara moja iwapo Hamas itawaachilia mateka waliosalia wanaoshikiliwa Gaza na kuweka chini silaha zake, Israel imesema.
Muhtasari
- Waziri Mkuu wa Japan Shigeru Ishiba ajiuzulu
- Israel yatoa wito kwa Hamas kujisalimisha huku jeshi likishambulia mji wa Gaza
- Sudan Kusini yamrudisha Mmexico aliyefukuzwa Marekani
- Rubani aliyejaribu kuzima injini ya ndege katikati ya safari akiri kuwa na hatia
- Boko Haram waua takriban watu 60 katika shambulio kwenye kijiji cha Nigeria
- Wakatoliki wa LGBTQ+ wafanya hija yao ya kwanza Vatican
- Urusi yashambulia jengo la serikali ya Ukraine kwa mara ya kwanza
- Israel yaharibu jengo la pili kwa urefu Gaza
Moja kwa moja
Na Asha Juma
Waziri Mkuu wa Japan Shigeru Ishiba ajiuzulu baada ya kushindwa katika uchaguzi
Waziri Mkuu wa Japan Shigeru Ishiba ametangaza kujiuzulu baada ya kuhudumu chini ya mwaka mmoja katika nafasi hiyo, kufuatia kushindwa vibaya mara mbili kwenye uchaguzi.
Hatua hiyo inajiri siku moja kabla ya chama chake cha Liberal Democratic Party (LDP) kutarajiwa kupiga kura ya iwapo kingefanya kura ya ndani ya uongozi ambayo ingemlazimu kujiondoa.
LDP imetawala Japan kwa zaidi ya miongo saba iliyopita, lakini chini ya Ishiba kilipoteza wingi wake wa viti katika baraza la mawaziri kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 15 na kisha ikapoteza wingi wake katika baraza la juu mwezi Julai.
Ishiba, 68, alikuwa amepinga madai ya kujiuzulu kutoka kwa wapinzani ndani ya chama chake mwenyewe. Alisema alitaka kuepuka ombwe la kisiasa wakati Japan inakabiliwa na changamoto kuu za ndani na kimataifa, ikiwa ni pamoja na ushuru wa Marekani, kupanda kwa gharama za bidhaa na kuongezeka kwa mvutano katika Asia-Pasifiki.
Ishiba alieleza katika mkutano wa wanahabari Jumapili usiku kwamba alikuwa amekusudia kwa muda fulani kuwajibika kwa kushindwa kwa chama chake kwenye uchaguzi lakini alidhamiria kwanza kuendeleza mazungumzo ya ushuru na Marekani akilitaja kuwa suala la maslahi ya taifa.
"Nani atajadiliana kwa dhati na serikali ambayo kiongozi wake amesema atajiuzulu?" Ishiba alisema.
Alisema wakati umefika na agizo la Rais wa Marekani, Donald Trump mnamo Ijumaa la kupunguza ushuru wa magari ya Japan na bidhaa zingine kutoka 25% hadi 15%.
"Baada ya kufikia hatua muhimu katika mazungumzo ya ushuru wa Marekani, niliamua sasa ni wakati wa kutoa nafasi kwa mrithi," Ishiba alisema.
Japan, nchi ya nne kwa uchumi duniani na mshirika mkuu wa Marekani, sasa inakabiliwa na kipindi cha sintofahamu kisiasa huku mvutano kati yake na China na ukosefu wa usalama wa kikanda ukiongezeka.
Israel yatoa wito kwa Hamas kujisalimisha huku jeshi likishambulia mji wa Gaza
Israel imetoa wito tena kwa Hamas kujisalimisha huku jeshi likiendeleza mashambulizi katika jiji la Gaza ambako mamia kwa maelfu ya Wapalestina wanatafuta hifadhi.
Waziri wa mambo ya nje Gideon Saar aliwaambia waandishi wa habari mjini Jerusalem kuwa vita hivyo vinaweza kumalizika mara moja iwapo Hamas itawaachilia mateka waliosalia wanaoshikiliwa Gaza na kuweka chini silaha zake.
"Tutafurahi zaidi kufikia lengo hili kwa njia za kisiasa," alisema.
Katika kujibu, afisa mkuu wa Hamas Basem Naim aliambia Reuters kwamba haitaweka silaha zake chini lakini itawaachilia mateka wote ikiwa Israeli itakubali kumaliza vita na kuondoa vikosi vyake kutoka Gaza, msimamo ambao kwa muda mrefu umekuwa wa kundi hilo la wapiganaji wa Palestina.
Israeli mwezi uliopita ilianzisha mashambulizi katika mji wa Gaza, na vikosi vyake sasa viko kilomita chache tu kutoka katikati mwa jiji.
Usiku kucha, mashambulizi yaliwauwa watu 14 kote jijini, maafisa wa afya wa eneo hilo walisema, ikiwa ni pamoja na shambulizi kwenye shule iliyo kusini mwa mji wa Gaza ambayo imewahifadhi Wapalestina waliokimbia makazi yao.
Soma zaidi:
Sudan Kusini ya mrudisha Mexico aliyefukuzwa Marekani
Sudan Kusini imemrudisha raia wa Mexico nyumbani ambaye alikuwa amefukuzwa Marekani na kuletwa Juba mnamo mwezi Julai, wizara ya mambo ya nje ilisema.
Sudan Kusini ilisema Mexico imetoa hakikisho kwamba raia huyo hatakabiliwa na mateso, kutendewa unyama au kufunguliwa mashitaka yasiyo ya haki atakapowasili.
Jesus Munõz Gutierrez alikabidhiwa kwa balozi wa Mexico, Alejandro Ives Estivill, ambaye aliwasili Juba siku ya Ijumaa, taarifa hiyo ilisema.
Haikuwezekana mara moja kumpata Gutierrez kwa ajili ya kutoa maoni.
Juba ilisema imesalia kujitolea kufanya kazi na washirika wa kimataifa ili kuhakikisha wanarejea salama na kiutu raia wengine sita wa nchi zingine walioko Sudan Kusini kwa sasa baada ya kufukuzwa kutoka Marekani.
Soma zaidi:
Rubani aliyejaribu kuzima injini ya ndege katikati ya safari akiri kuwa na hatia
Rubani wa zamani anayeshtakiwa kwa kujaribu kuzima injini ya ndege ya abiria katikati ya safari amekiri mashtaka katika mahakama ya shirikisho.
Joseph David Emerson hakuwa kazini siku hiyo lakini alikuwa kwenye chumba cha marubani cha ndege ya Alaska Airlines alipowaambia marubani wenzake "siko sawa" kabla ya kujaribu kuzima injini angani, nyaraka za mahakama zilionyesha.
Emerson pia aliwaambia polisi kwamba alikuwa amekula uyoga aina ya ‘psychedelic’ na amekuwa akipambana na msongo wa mawazo.
Chini ya Makubaliano ya Kukiri Kosa, waendesha mashtaka wanaweza kupendekeza kifungo cha mwaka mmoja gerezani, huku mawakili wake wakitarajiwa kutetea asiongezewe muda wa ziada jela.
Soma zaidi:
Boko Haram waua takriban watu 60 katika shambulio kwenye kijiji cha Nigeria
Kundi la wanajihadi la Boko Haram limewaua zaidi ya watu 60 katika shambulio la Ijumma usiku katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria, maafisa wa eneo hilo wamesema.
Wanamgambo walishambulia kijiji cha Darul Jamal, makazi ya kambi ya kijeshi kwenye mpaka wa Nigeria na Cameroon, na kuua takriban wanajeshi watano.
Jeshi la Wanahewa la Nigeria limesema limewaua wanamgambo 30 katika shambulizi baada ya kupokea ripoti za uvamizi wa kijiji hicho, ambapo wakaazi walirejea hivi karibuni kufuatia miaka kadhaa ya kuhama makazi yao.
Shambulizi hilo linakuja huku kukiwa na kuzuka upya kwa shughuli za wanajihadi kaskazini-mashariki mwa Nigeria, huku mapigano ya Boko Haram na wapinzani, tawi la Afrika Magharibi la kundi la Islamic State, wakiimarisha mashambulizi.
Soma zaidi:
Wakatoliki wa LGBTQ+ wafanya hija yao ya kwanza Vatican
Baadhi ya Wakatoliki 1,400 waliovalia mavazi ya upinde wa mvua na kubeba misalaba wameshiriki hija ya kwanza iliyotambuliwa rasmi ya wakatoliki wa LGBTQ+ huko Roma kama sehemu ya Mwaka wa Jubilei wa Vatican.
Wakitoka nchi 20, mahujaji wanahudhuria mikesha ya maombi, misa na shughuli nyinginezo wikendi hii - ingawa hawatakuwa na hadhira ya faragha na Papa Leo XIV.
Mtangulizi wake Papa Francis, ambaye alifariki mwezi Aprili, hakubadilisha mafundisho ya Kanisa Katoliki la Roma kuhusu jumuiya ya LGBTQ+ - lakini alibadilisha mapendekezo katika amri mwaka wa 2023.
Mabadiliko hayo ni pamoja na kuruhusu makasisi kuwabariki wapenzi wa jinsia moja - hatua ambayo iliwakasirisha wahafidhina Wakatoliki, hasa barani Afrika.
Soma zaidi:
Urusi yashambulia jengo la serikali ya Ukraine kwa mara ya kwanza
Moja ya jengo kuu la serikali ya Ukraine limeharibiwa kutokana na mashambulizi ya usiku kucha ya Urusi.
Katika mtandao wa Facebook, Waziri Mkuu wa Ukraine Yulia Svyrydenko ameandika kwamba "kwa mara ya kwanza, jengo la serikali, paa na orofa za juu zimeharibiwa kutokana na mashambulizi ya adui. Waokoaji wanazima moto."
Meya wa Kyiv, Vitaliy Klitschko, amesema jengo la serikali liliwaka moto kutokana na "shambulizi linalodaiwa kuwa la ndege zisizo na rubani".
Jengo hilo lilikuwa katikati mwa wilaya ya Pecherskyi, Klitschko ameandika kwenye chapisho kwenye Telegraph na kuongeza kuwa wazima moto bado wanafanya kazi katika eneo la tukio.
Kwengineko, ghala, jengo la makazi la ghorofa 16, na jengo la ghorofa nne zilishambuliwa.
Soma zaidi:
Israel yaharibu jengo la pili kwa urefu huku mashambulizi ya mji wa Gaza yakiongezeka
Jeshi la Israel limeharibu jengo la pili kwa urefu katika mji wa Gaza, kama lililokuwa imelilenga.
Waziri wa Ulinzi Israel Katz aliweka video ya jengo hilo likiporomoka kwenye mtandao wa X, na nukuu: "Tunaendelea".
Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF), ambalo limekuwa likipanua operesheni zake huko Gaza, lilisema jengo la Sussi lilikuwa linatumiwa na Hamas - madai ambayo yamekanushwa na kundi hilo la wanamgambo.
Haikuweza kufahamika mara moja iwapo kulikuwa na majeruhi. Kabla ya shambulizi la Jumamosi, Israel ilidondosha vipeperushi vinavyorudia wito wa Wapalestina kuhama katika kile inachokiita eneo la kibinadamu kusini.
Soma zaidi:
Hujambo Msomaji wetu, karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja mimi ni Asha Juma.