Donald Trump
amefahamishwa na idara ya kijasusi ya Marekani kuhusu vitisho kutoka kwa Iran
vya kutaka kumuua, kambi yake ya kampeni ilisema.
Mgombea
urais wa chama cha Republican alifahamishwa "kuhusu vitisho vya kweli na
mahususi kutoka kwa Iran vya kutaka kumuua katika juhudi za kuyumbisha na
kuzusha machafuko nchini Marekani", kambi yake ya kampeni ilisema katika
taarifa.
Haikufafanua madai hayo, na haikufahamika mara moja iwapo
vitisho iliyokuwa inarejelea ni vipya au viliripotiwa awali.
Serikali ya Iran haikujibu mara moja ombi la maoni yake,
lakini Tehran hapo awali ilikanusha madai ya Marekani ya kuingilia masuala ya
Marekani.
"Maafisa wa ujasusi wamegundua kuwa mashambulizi
haya yanayoendelea na yaliyoratibiwa yameongezeka katika miezi michache
iliyopita," mkurugenzi wa mawasiliano wa kambi ya kampeni ya Trump, Steven
Cheung alisema katika taarifa hiyo.
"Maafisa wa utekelezaji wa sheria katika mashirika
yote wanafanya kazi kuhakikisha Rais Trump analindwa na uchaguzi hauingiliwi,"
aliongeza.
BBC imeenda kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Ujasusi wa Kitaifa
nchini Marekani kwa maoni.
Haya yanawadia baada ya Bw Trump kunusurika katika
jaribio la mauaji mnamo Julai 13, alipojeruhiwa na mtu mwingine kuuawa kwa
kupigwa risasi kwenye mkutano huko Pennsylvania.
Nia ya tukio hilo bado haijabainika na bado linachunguzwa.
Siku chache baadaye, vyombo vya habari vya Marekani
viliripoti kwamba maafisa walipokea taarifa za kijasusi kuhusu njama
zinazodaiwa kuwa za Iran dhidi ya rais huyo wa zamani.
Maafisa wa Iran wakati huo walikanusha madai hayo na
kusema ni ya "uovu", iliripoti mshirika wa BBC wa Marekani CBS habari.
"Iwapo 'watamuua Rais Trump,' jambo ambalo linawezekana,
ninatumai kuwa Marekani itaiangamiza Iran, kuifuta kabisa kwenye uso wa Dunia -
Ikiwa hilo halitafanyika, Viongozi wa Marekani watachukuliwa kuwa waoga 'wasio
na ujasiri'!" Bw
Trump aliandika kwenye jukwaa lake la Truth Social platform wakati huo.
Kisha tarehe
15 Septemba, Shirika Maalum la Usalama liliona bunduki ikipenya kwenye uzio
katika Klabu ya Gofu ya Kimataifa ya Trump huko West Palm Beach.
Ofisa wa
shirika hilo alifyatua risasi Bw Trump alipokuwa akicheza gofu.