Moja kwa moja, Trump aitaka Iran ijisalimishe bila masharti, Putin azungumza na rais wa Iran

Trump ametoa wito huo wakati vita kati ya Marekani ikishirikiana na Israel dhidi Iran vinaingia wiki ya pili huku mashambulizi ya kijeshi yakiripotiwa kote Mashariki ya Kati.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Martha Saranga

  1. Qatar yafungua anga kuruhusu safari chache za ndege

    xcv

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Shirika la ndege la Qatar Airways linatoa huduma chache za ndege za kuwarejesha nyumbani kwenda London, Rome, Paris, Madrid na Frankfurt

    Qatar imetangaza kuanza tena kwa safari chache za ndege kwa mara ya kwanza tangu vita vilipoanza wiki moja iliyopita.

    Mamlaka ya usafiri wa anga ya nchi hiyo ilisema kuwa anga ya Qatar itafunguliwa kwa sehemu ili kuruhusu tu safari za uokoaji na ndege muhimu za mizigo.

    Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Hamad umefafanua kuwa safari nyingine katika siku zijazo zitategemea tathmini inayoendelea ya hali ya usalama.

    Maafisa wa Qatar walisema mapema wiki hii kuwa jeshi lilifanikiwa kuzuia jaribio la mashambulizi ya Iran dhidi ya uwanja huo wa ndege.

    Wizara ya ulinzi iliripoti kuwa Qatar ilidungua ndege tisa zisizo na rubani siku ya Ijumaa.

    Moja ya hizo ilianguka katika eneo lisilo na watu bila kusababisha majeruhi.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Mashuhuda waripoti milipuko katika uwanja mkubwa wa ndege Tehran

    XCV

    Chanzo cha picha, AFP

    Kumeshuhudiwa shambulio kubwa katika moja ya viwanja vikuu vya ndege vya kibiashara mjini Tehran.

    Ndege inayowaka moto pamoja na moshi mkubwa unaonekana katika uwanja wa ndege wa Mehrabad, ambao ni uwanja wa ndege wenye shughuli nyingi zaidi nchini Iran na kitovu kikuu cha safari za ndani.

    Hali hiyo inaonekana katika video zilizochapishwa na mashuhuda kwenye mitandao ya kijamii.

    Picha za satelaiti zilizopigwa Ijumaa zinaonyesha kuwa kulikuwa na ndege kadhaa katika uwanja huo.

    Vyombo vya habari vya serikali ya Iran pia vinaripoti kuwa baadhi ya sehemu za uwanja wa ndege zimelengwa katika shambulio hilo.

    Tukio hili linakuja baada ya jeshi la Israel kusema kuwa linaanzisha “wimbi jipya la mashambulizi makubwa” nchini Iran.

    Hapo awali lililenga uwanja huo tarehe 4 Machi, likisema mashambulizi yake yalibomoa mifumo ya ulinzi na ilikuwa tishio kwa Jeshi la anga la Israel, ikiwemo sehemu ya kutengeneza helikopta katika uwanja huo.

    Bado haijafahamika ni sehemu gani hasa za uwanja wa ndege zimepigwa katika shambulio jipya, lakini mashuhuda wanasema mashambulizi ya usiku huu yamekuwa makali zaidi.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Trump aitaka Iran ijisalimishe bila masharti, Putin azungumza na rais wa Iran

    a

    Chanzo cha picha, Getty Images/BBC

    Rais wa Marekani Donald Trump ameitaka Iran kujisalimisha bila masharti huku mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na Israel yakiendelea. Trump amesema baada ya Iran kuchagua uongozi mpya unaokubalika na Washington, Marekani na washirika wake wataisaidia nchi hiyo kuimarisha uchumi wake.

    Kauli hiyo imekuja wakati vita vinaingia wiki ya pili tangu kuuawa kwa kiongozi mkuu wa Iran Ali Khamenei katika mashambulizi ya hivi karibuni. Hata hivyo bado haijulikani nani ataIongoza Iran baada ya tukio hilo.

    Ikulu ya Marekani imesema operesheni za kijeshi zinaweza kudumu kati ya wiki nne hadi sita, huku lengo likiwa kudhoofisha uwezo wa kijeshi wa Iran.

    Wakati huo huo, rais wa Urusi Vladimir Putin amezungumza kwa simu na rais wa Iran Masoud Pezeshkian, akitoa pole kwa vifo vilivyotokea katika mashambulizi hayo.

    Urusi imesisitiza kuwa mapigano yanapaswa kusitishwa mara moja na kutafutwa suluhisho la kidiplomasia. Iran nayo imeishukuru Urusi kwa kuendelea kuiunga mkono.

    Wakati huo huo, mapigano yameongezeka katika eneo la Mashariki ya Kati baada ya kundi la Hezbollah kushambulia Israel, huku mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora yakiripotiwa katika nchi kadhaa zenye kambi za kijeshi za Marekani.