Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Marekani yasema meli za kivita na biashara zimepita Mlango wa Hormuz
Hatua hii ni baada ya Marekani kutangaza operesheni iitwayo “Project Freedom”, ambayo itahusisha meli za kivita, ndege zaidi ya 100, mifumo ya droni pamoja na wanajeshi takriban 15,000 kusaidia kulinda usafirishaji katika eneo hilo nyeti la Bahari ya Ghuba.
Muhtasari
- Matumizi ya kondomu Kenya yapungua, hofu ya kuenea kwa magonjwa ya zinaa ikiibuliwa - ripoti
- Inter wanyakua ubingwa wa ligi kuu ya Italia Serie A
- Nigeria yapanga kuwarejesha raia wake wanaotaka kuondoka Afrika Kusini baada ya mashambulizi
- Iran yatishia kushambulia Marekani ikijaribu kuingia Mlango wa Hormuz
- Chama cha Modi chakabiliwa na mtihani mkubwa katika uchaguzi muhimu India
- WHO yathibitisha mlipuko wa Hantavirus duniani, waua watatu kwenye meli ya kitalii
- Iran yathibitisha kupokea jibu la Marekani kuhusu pendekezo lake jipya la amani
- Marekani kusaidia meli zilizokwama Hormuz - Trump
Moja kwa moja
Na Yusuph Mazimu & Mariam Mjahid
Qatar yalaani shambulio lililoripotiwa dhidi ya meli ya UAE
Taarifa za hivi karibuni kutoka Fujairah nchini Umoja wa Falme za Kiarabu zimekuja baada ya meli ya mafuta inayohusishwa na Adnoc, kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali, kuripotiwa kushambuliwa katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Qatar, jirani wa UAE, imelaani shambulio hilo dhidi ya meli ya mafuta.
Katika taarifa, Wizara yake ya Mambo ya Nje imesema shambulio hilo ni “ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na kanuni ya uhuru wa usafiri wa baharini.”
Qatar imerudia wito wake wa kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz bila masharti.
Wakati huohuo, UAE imeendelea kuripoti mashambulizi ya makombora, huku tahadhari yake ya hivi karibuni ikitolewa saa 19:49 kwa saa za eneo hilo.
Hadi sasa, hakuna afisa wa Iran aliyetoa kauli ya kuthibitisha mashambulizi hayo.
Soma zaidi;
Moto mkubwa wazuka katika bandari ya mafuta ya UAE baada ya shambulio la droni kutoka Iran
Moto mkubwa umezuka katika bandari ya mafuta ya Fujairah nchini Umoja wa Falme za Kiarabu baada ya eneo hilo kushambuliwa kwa droni kutoka Iran, maafisa wa eneo hilo wamesema.
Fujairah ni bandari kubwa zaidi ya UAE pamoja na kituo chake kikuu cha kuhifadhi mafuta. Kabla ya kusitishwa kwa mapigano, eneo hilo pia liliwahi kulengwa katika mashambulizi ya droni.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, Ofisi ya Habari ya Serikali ya Fujairah imesema vikosi vya ulinzi wa kiraia vinaendelea na juhudi za kudhibiti moto huo.
Taarifa ya shambulio hilo imekuja wakati Wizara ya Ulinzi ya UAE ikisema ilifanikiwa kudungua makombora matatu yaliyorushwa kutoka Iran.
Serikali ya Iran haijatoa kauli yoyote kuhusu shambulio hilo.
Guinness yathibitisha watoto tisa waliozaliwa pamoja watimiza miaka mitano
Rekodi ya dunia ya Guinness imetangaza kuwa watoto tisa wa Halima Cisse kutoka Mali leo wanatimiza miaka mitano tangu kuzaliwa kwao, katika tukio lililoweka historia duniani.
Watoto hao, wanaojulikana kama Cisse nonuplets, walizaliwa tarehe 4 Mei 2021 katika kliniki ya Ain Borja mjini Casablanca, Morocco.
Kwa mujibu wa Guinness World Records, hili ndilo tukio la kwanza linalojulikana duniani ambapo watoto tisa wamezaliwa kwa wakati mmoja na wote wakaendelea kuishi baada ya kuzaliwa.
Kuzaliwa kwao kulivunja rekodi ya dunia na kuvuta hisia za kimataifa kutokana na upekee wake wa kitabibu.
Soma zaidi:
Rais wa Kenya William Ruto aanza ziara ya siku mbili nchini Tanzania
Rais wa Kenya William Ruto amewasili jijini Dar es Salaam, Tanzania, kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili nchini humo.
Ruto amepokewa katika uwanja wa ndege na ujumbe wa maafisa kutoka Kenya na Tanzania.
Katika ziara hiyo, Ruto atafanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan, kabla ya viongozi hao wawili kuongoza mazungumzo rasmi ya pande mbili yatakayohusisha ujumbe kutoka mataifa yote mawili.
Mazungumzo hayo yanatarajiwa kujikita katika kuimarisha ushirikiano katika sekta muhimu, zikiwemo biashara, uwekezaji, miundombinu na usafiri, maeneo yanayoendelea kuwa nguzo ya muungano wa kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Kenya, mazungumzo hayo yanalenga kuimarisha uhusiano wa kindugu wa muda mrefu kati ya Kenya na Tanzania, huku pande zote mbili zikitarajiwa pia kuchunguza maeneo mapya ya ushirikiano wa pamoja.
Baadaye viongozi hao watazungumza na vyombo vya habari na kueleza matokeo muhimu ya mazungumzo yao.
Jumanne Mei 5, Rais Ruto anatarajiwa kuelekea Dodoma ambako atalihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, heshima adimu ya kidiplomasia inayodhihirisha kuimarika kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Katika taarifa iliyotolewa wiki iliyopita, Mussa Azzan Zungu aliwajulisha wabunge kuhusu hotuba hiyo inayotarajiwa kuanza saa tano asubuhi.
Mei 5, 2021, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alihutubia kikao cha pamoja cha bunge nchini Kenya ambapo alitumia lugha ya Kiswahili.
Rais Samia aliandikisha historia ya kuwa Rais wa kwanza wa kike kuwahi kuhutubia bunge la Kenya, wakati alikuwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili.
Marais wa zamani wa Kenya akiwemo Uhuru Kenyatta waliwahi kufanya ziara za kikazi nchini Tanzania wakiwa madarakani lakini hatua hii ya Rais Ruto kuhutubia bunge ni ya kipekee.
Bei ya mafuta yapanda baada ya Iran kudai kushambulia meli ya Marekani, Centcom yakana
Bei ya mafuta imepanda kwa kasi kufuatia taarifa za vyombo vya habari vya serikali ya Iran zilizodai kuwa makombora mawili yalikumba meli ya kivita ya Marekani ilipokuwa ikijaribu kuingia katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Bei ya mafuta ghafi ya Brent ilipanda zaidi ya dola 4 kwa pipa ndani ya dakika chache baada ya taarifa hizo kusambaa, ikifikia dola 114, ikiwa ongezeko la zaidi ya asilimia 5 kutoka bei ya ufunguzi wa siku.
Hata hivyo, bei hiyo ilishuka kidogo baada ya Marekani kukanusha kuwa shambulio hilo lilitokea.
Usiku wa kuamkia leo, Rais Donald Trump alitangaza mpango wa kusaidia meli zilizokwama katika Ghuba ya Uajemi, akielezea hatua hiyo kama “ishara ya kibinadamu.”
Iwapo jaribio la kupitisha meli kupitia mlango huo litasababisha kuibuka tena kwa mapigano, huenda hilo likapunguza uwezekano wa kurejea kwa usafirishaji wa mafuta na gesi, hali ambayo inaweza kusababisha bei ya mafuta kupanda zaidi.
Soma zaidi:
Centcom yasema meli za Marekani na za biashara zimepita Mlango wa Hormuz
Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (Centcom) imetoa taarifa fupi ikisema kuwa meli mbili za biashara zinazokuwa na bendera ya Marekani zimefanikiwa kupita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Centcom imeongeza kuwa meli za kivita za Marekani aina ya waharibifu wa makombora zinazoongozwa (guided-missile destroyers) zinaendelea na shughuli zake katika Ghuba ya Uajemi baada ya kupita pia katika mlango huo.
Taarifa hiyo imesema: “Vikosi vya Marekani vinaendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za kurejesha usafiri wa meli za kibiashara.”
Centcom haijabainisha majina ya meli hizo zilizofanikiwa kuvuka mlango huo.
Soma zaidi:
Wafanya biashara Meru waanza uchuuzi wa miraa katika msongamano wa magari na kuibua mjadala Kenya
Video iliyosambazwa mtandaoni na Mkenya imeibua mjadala baada ya kuonyesha bidhaa zinazouzwa na wachuuzi katika foleni za magari mjini Meru.
Badala ya maji na biskuti za kawaida, wachuuzi hao wa pembezoni mwa barabara wameonekana wakiwa na vifurushi vya miraa, jambo linaloonesha utamaduni wa kipekee wa biashara katika eneo hilo pamoja na uhusiano wake wa karibu na zao hilo maarufu la kichangamshi.
Kwa nchi jirani, ni haramu kula miraa nchini Tanzania.
Miraa au Mirungi ni mmea wenye uwezo wa kumlewesha mtumiaji ambaye anautafuna.
Nchini Kenya mmea huu wa Miraa unakuzwa na kuuzwa hadharani. Yaani, serikali ya Kenya inawasaidia wakuzaji kupata soko nje ya nchi.
Moja ya mataifa yanayonunua Mirungi ni Ethiopia.
Mji wa Awwaaday ulioko nchini Ethiopia unatambulika kama mji mkuu wa mirungi kwa kutokana na maelfu ya tani za miraa zinazouzwa.
Kati ya dola milioni 1.1 na dola milioni 1.3 za Marekani hutumika katika biashara hiyo ndani ya mji huo kila siku.
Rais wa Taiwan azuru Eswatini baada ya mvutano na China kuhusu safari yake
Rais wa Taiwan, Lai Ching-te, amewasili nchini Eswatini, siku chache baada ya serikali yake kusema safari yake ilivurugwa kutokana na shinikizo la China kwa baadhi ya mataifa ya Afrika kuzuia ndege yake kupita katika anga zao.
Lai amesema ziara hiyo katika Eswatini, taifa pekee barani Afrika lenye uhusiano wa kidiplomasia na Taiwan, ilifanyika baada ya “maandalizi ya siku kadhaa yaliyofanywa na timu za diplomasia na usalama wa taifa,” bila kutoa maelezo ya jinsi alivyofika nchini humo.
China imeitaja ziara hiyo kama “uvamizi wa siri,” ikisisitiza msimamo wake kwamba Taiwan ni sehemu ya eneo lake na haina haki ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia kama taifa huru.
Kwa upande wake, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema ziara ya Lai ni ya kawaida na haipaswi kuingizwa katika siasa.
Picha zimeonyesha Rais Lai akipokelewa na Waziri Mkuu wa Eswatini, Russell Dlamini, katika hafla rasmi ambapo pia alipita mbele ya askari waliokuwa wamepanga kumheshimu.
Ujumbe wa Taiwan unaoambatana naye unajumuisha Waziri wa Mambo ya Nje Lin Chia-lung na Mshauri wa Usalama wa Taifa Alex Huang, kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya rais wa Taiwan.
Soma zaidi:
Polisi apiga mbizi katika mto wenye mamba kutafuta mabaki ya binadamu Afrika Kusini
Polisi wa Afrika Kusini wamefanikiwa kupata mabaki ya binadamu baada ya afisa wa polisi kushushwa kwa helikopta ndani ya mto wenye mamba akiwa katika operesheni ya kumtafuta mfanyabiashara aliyesombwa na maji ya mafuriko zaidi ya wiki moja iliyopita.
Mamba anayeshukiwa kumla mtu huyo alikuwa tayari ameuawa, lakini Kapteni Johan “Pottie” Potgieter amesema hali ya eneo hilo bado ilikuwa ya kutisha.
“Eneo linalokuwa na kichwa cha mamba si mahali salama pa kujikuta,” alinukuliwa akiiambia News24.
Potgieter alitumia kamba kumvuta mamba huyo kabla yeye na mnyama huyo kuinuliwa kutoka Mto Komati ulioko kaskazini mashariki mwa nchi.
Sampuli za DNA sasa zinafanyiwa uchunguzi kuthibitisha kama mabaki hayo ni ya mtu aliyepotea.
Gari la aliyesombwa na maji lilizama alipokuwa akijaribu kuvuka daraja katika mto uliokuwa umefurika kwa zaidi ya wiki moja.
Polisi walipofika eneo la tukio walikuta gari hilo likiwa tupu, hatua iliyowafanya kuamini kuwa lilisombwa na maji, amesema msemaji wa polisi wa mkoa wa Mpumalanga, Kanali Mavela Masondo, akizungumza na shirika la utangazaji la taifa SABC.
Mamlaka zilitumia ndege ndogo zisizo na rubani pamoja na ndege za usafiri katika operesheni ya utafutaji, ambapo waligundua kisiwa kidogo ambacho mamba kadhaa walikuwa wakijipumzisha, amesema Potgieter ambaye aliongoza timu ya wapiga mbizi wa polisi.
Amesema kutokana na uzoefu wake wa miaka mingi, yeye na wenzake waliweza kugundua kuwa mmoja wa mamba hao alikuwa amekula hivi karibuni.
Soma zaidi:
UAE yasema meli yake ya mafuta imeshambuliwa katika Mlango wa Hormuz
Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umesema meli ya mafuta inayohusiana na Adnoc, kampuni yake ya mafuta inayomilikiwa na serikali, imeshambuliwa katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo imesema katika taarifa yake kuwa hakuna mtu aliyejeruhiwa, na kuongeza kuwa:
“Shambulio hili ni ukiukaji wa wazi wa azimio kipengee chake 2817 cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo lilisisitiza umuhimu wa uhuru wa usafiri wa baharini na kupinga kulengwa kwa meli za kibiashara au kuzuiwa kwa njia za kimataifa za baharini.”
Taarifa hiyo imeongeza kuwa kulenga meli za kibiashara na kutumia Mlango wa Hormuz kama chombo cha shinikizo la kiuchumi au utesaji wa kiuchumi kunawakilisha vitendo vya uharamia vinavyohusishwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, na ni tishio la moja kwa moja kwa uthabiti wa eneo hilo, watu wake na usalama wa nishati duniani.
UAE imeitaka Iran kusitisha mashambulizi hayo na kuhakikisha inatekeleza kikamilifu kusitishwa mara moja kwa uhasama wote, pamoja na kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz bila masharti.
Soma zaidi:
Watu wanne wakamatwa wakijaribu kuiba mafuta ya ndege nchini Kenya
Watu wanne wamekamatwa wakishukiwa kujaribu kuiba mafuta ya ndege katika Uwanja wa Ndege wa Wilson, ulioko katika mji mkuu wa Kenya.
Washukiwa hao walikamatwa wakiwa katika jaribio la kutoa lita 800 za mafuta ya ndege kutoka kwenye ndege iliyokuwa imeegeshwa katika uwanja huo.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kenya (DCI) amesema kukamatwa kwao kulifanywa na maafisa wa Kitengo cha Polisi wa Viwanja vya Ndege (KAPU), baada ya polisi kubaini shughuli za kushuku katika gari walilokuwa wakitumia.
Wanaume watatu na mwanamke mmoja waliokuwa ndani ya gari aina ya Mitsubishi Canter walijaribu kujifanya kuwa wanafanya kazi za kawaida za uwanja wa ndege, lakini walizuiwa kabla ya kufika langoni pa kutokea.
Matumizi ya kondomu Kenya yapungua, hofu ya kuenea kwa magonjwa ya zinaa ikiibuliwa - ripoti
Ripoti mpya ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu Kenya (KNBS) inaonyesha matumizi ya kondomu nchini Kenya yaliendelea kupungua mwaka 2025, hali inayozua wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa ngono isiyo salama huku watumiaji wengi wakionekana kuelekea zaidi katika njia za muda mrefu za uzazi wa mpango.
Ripoti hiyo inaonyesha matumizi ya kondomu za kiume na za kike yamekuwa yakishuka mfululizo tangu mwaka 2023, wakati vipandikizi vikiendelea kuwa miongoni mwa njia zinazopendelewa zaidi katika vituo vya afya.
Takwimu zinaonyesha matumizi ya kondomu za kiume yalishuka hadi watumiaji 510,173 mwaka 2025 kutoka 638,043 mwaka 2024 na 721,857 mwaka 2023.
Matumizi ya kondomu za kike nayo yaliendelea kupungua, yakishuka hadi 16,760 mwaka 2025 kutoka 25,673 mwaka 2024 na 68,403 mwaka 2023.
Takwimu hizo zinaashiria kuwa Wakenya wachache wanatumia njia za kinga, ambazo ndizo pekee zinazosaidia kuzuia mimba na pia maambukizi ya magonjwa ya zinaa.
KNBS imesema njia nyingi za uzazi wa mpango zilirekodi kupungua katika kipindi cha tathmini.
Kupungua kwa matumizi ya kondomu kunakwenda sambamba na kushuka kwa matumizi ya njia nyingine za uzazi wa mpango. Matumizi ya sindano za uzazi wa mpango, ambazo ni miongoni mwa njia zinazotumiwa zaidi Kenya, yalipungua kwa asilimia 10.9 kwa wateja wapya na asilimia 8.6 kwa wanaorejea.
Vidonge vya uzazi wa mpango vya kumeza pia vilipungua kwa kiasi kikubwa, huku matumizi kwa wateja wapya yakishuka kwa asilimia 29.9 na kwa wanaorejea kwa asilimia 22.7.
Licha ya kupungua kwa njia nyingi, vipandikizi viliendelea kuwa miongoni mwa njia maarufu zaidi kwa wanawake wanaotafuta uzazi wa mpango wa muda mrefu.
Idadi ya watumiaji wapya wa vipandikizi ilisimama katika 692,212 mwaka 2025, ikiwa chini kidogo ya 713,784 ya mwaka 2024, lakini bado juu kuliko 686,954 ya mwaka 2023 na 566,769 ya mwaka 2022.
Upasuaji wa kufunga uzazi kwa wanaume ndio njia pekee iliyoonyesha ongezeko, ukipanda kwa asilimia 9.2 mwaka 2025, ingawa matumizi yake yalisalia kuwa ya chini kwa wateja 415 pekee.
Wataalamu wa afya wameonya kwa muda mrefu kuwa kupungua kwa matumizi ya kondomu kunaweza kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na uelewa wa afya ya uzazi, hasa miongoni mwa vijana na watu wenye mahusiano ya kimapenzi.
Matokeo ya KNBS sasa yanaibua maswali mapya kuhusu iwapo mabadiliko ya mapendeleo ya uzazi wa mpango, changamoto za upatikanaji au kupungua kwa kampeni za uhamasishaji wa umma vinachangia kuporomoka kwa matumizi ya kondomu.
Ripoti hiyo imesisitiza haja ya kuendeleza juhudi za kuongeza matumizi na kuhakikisha huduma za uzazi wa mpango zinapatikana kwa urahisi.
Pia unaweza kusoma:
Inter wanyakua ubingwa wa ligi kuu ya Italia Serie A
Inter Milan imetwaa taji lake la tatu la Serie A katika misimu sita baada ya kuichapa Parma mabao 2 kwa 0 mbele ya mashabiki waliokuwa na shamrashamra katika uwanja wa San Siro.
Bao la Marcus Thuram muda mfupi kabla ya mapumziko liliiweka Inter mbele, kabla Henrikh Mkhitaryan hajafunga bao la pili kipindi cha pili na kuthibitisha ubingwa huo.
Zikiwa zimesalia mechi tatu, Inter inaongoza ligi kwa pointi 12 dhidi ya mabingwa watetezi Napoli na pointi 15 zaidi ya AC Milan iliyo nafasi ya tatu.
Hili ni taji la 21 la ligi ya Italia kwa Inter, ambayo imefanikiwa kurejea kileleni chini ya kocha Cristian Chivu baada ya kumaliza vibaya msimu uliopita.
Chini ya mwaka mmoja tangu ipoteze ubingwa wa 2025 kwa tofauti ya pointi moja na kufungwa mabao 5 kwa 0 na Paris Saint Germain katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Inter sasa imerejea kileleni mwa soka la Italia.
Inter inadaiwa mafanikio haya kwa Chivu, mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, ambaye aliteuliwa kwa mshangao mwezi Juni kuchukua nafasi ya Simone Inzaghi aliyeondoka kuelekea Saudi Arabia.
Inter bado ina nafasi ya kukamilisha makombe mawili ya ligi na kombe la ndani kwa mara ya tatu katika historia yake iwapo itaifunga Lazio katika fainali ya Coppa Italia Mei 13 kwenye Uwanja wa Olimpiki mjini Rome.
Soma zaidi:
Nigeria yapanga kuwarejesha raia wake wanaotaka kuondoka Afrika Kusini baada ya mashambulizi
Nigeria inapanga kuwarejesha nyumbani raia wake walioko Afrika Kusini watakaokubali kurejea kwa hiari, huku hofu ikiongezeka kwamba mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya raia wa kigeni nchini humo yanaweza kuongezeka.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria, Bianca Odumegwu Ojukwu, amesema watu 130 tayari wamejiandikisha kwa mchakato huo, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka.
Amesema Rais Bola Tinubu ana wasiwasi mkubwa kuhusu mashambulizi hayo nchini Afrika Kusini, na amelaani vurugu dhidi ya raia wa kigeni pamoja na maandamano yaliyoambatana na kile alichokiita kauli za chuki dhidi ya wageni, hotuba za chuki na matamshi ya uchochezi dhidi ya wahamiaji.
Nigeria imemuita kaimu Balozi Mkuu wa Afrika Kusini kujieleza kuhusu suala hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria, nchi hiyo itawasilisha rasmi wasiwasi wake mkubwa katika mkutano utakaofanyika baadaye Jumatatu, ikisema matukio hayo yanaweza kuathiri uhusiano uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Taarifa hiyo imesema mkutano huo utajikita katika maandamano ya hivi karibuni yaliyoandaliwa na makundi yanayopinga wahamiaji, pamoja na matukio yaliyoripotiwa ya raia wa Nigeria kunyanyaswa na biashara zao kushambuliwa.
Siku ya Jumapili, waziri wa mambo ya nje wa Nigeria alisema: "Maisha ya Wanigeria na biashara nchini Afrika Kusini lazima zisiendelee kuwekwa hatarini, na tunasalia kujitolea kufanya kazi kutafuta na suluhisho la kumaliza hali hiyo.''
Ametaja pia kuuawa kwa raia wawili wa Nigeria katika matukio tofauti yaliyowahusisha maafisa wa usalama wa eneo hilo, akisema serikali ya Nigeria inadai haki itendeke.
Mwezi uliopita, Ghana pia ilimuita balozi mkuu wa Afrika Kusini baada ya kusambaa kwa video iliyomuonyesha raia wa Ghana akihojiwa kuthibitisha uhalali wa nyaraka zake za uhamiaji.
Hisia za kupinga wahamiaji ziliongezeka mapema mwaka huu baada ya taarifa kwamba kiongozi wa jamii ya Wanigeria katika mji wa bandari wa KuGompo, zamani East London, alitawazwa katika nafasi ya jadi inayoweza kufasiriwa kama mfalme, jambo lililotafsiriwa na baadhi ya raia wa Afrika Kusini kama jaribio la kujipatia ushawishi wa kisiasa.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi, Afrika Kusini ina wahamiaji wapatao milioni 2.4, sawa na chini kidogo ya asilimia nne ya idadi ya watu wake, ingawa inaaminika kuwa wengine wengi wanaishi nchini humo bila vibali rasmi.
Wengi wao hutoka mataifa jirani kama Lesotho, Zimbabwe na Msumbiji, huku idadi ndogo ikitoka Nigeria.
Soma zaidi:
Iran yatishia kuishambulia Marekani ikijaribu kuingia Mlango wa Hormuz
Iran imetangaza kuwa jeshi lake litashambulia majeshi ya Marekani endapo yatajaribu kuingia katika Mlango wa Hormuz, kufuatia tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu operesheni ya kusaidia meli kupita katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la Iran kupitia kituo cha utangazaji cha taifa IRIB, mkuu wa kamandi ya kijeshi amesema kuwa Iran itashambulia “kikosi chochote cha kijeshi cha kigeni” kitakachokaribia au kuingia katika mlango huo, hasa majeshi ya Marekani ambayo ameyaita ya “uchokozi”.
Meja Jenerali Ali Abdollahi amesema Iran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa Mlango wa Hormuz uko chini ya udhibiti wa majeshi yake, na kwamba usafiri salama katika eneo hilo lazima uratibiwe na Tehran chini ya masharti yote.
Tishio hilo linakuja baada ya Marekani kutangaza operesheni iitwayo “Project Freedom”, ambayo itahusisha meli za kivita, ndege zaidi ya 100, mifumo ya droni pamoja na wanajeshi takriban 15,000 kusaidia kulinda usafirishaji katika eneo hilo nyeti la Bahari ya Ghuba.
Mvutano kati ya mataifa hayo mawili umeendelea kuongezeka, huku Mlango wa Hormuz ukiwa njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani, na hivyo kufanya hali hiyo kuwa na athari kubwa kimataifa endapo itazidi kushadidi.
Chama cha Modi chakabiliwa na mtihani mkubwa katika uchaguzi muhimu India
Kura za uchaguzi wa majimbo nchini India unaendelea kuhesabiwa katika majimbo manne ya West Bengal, Tamil Nadu, Kerala na Assam, pamoja na eneo la shirikisho la Puducherry.
Matokeo ya uchaguzi huu yanaonekana kama kipimo cha awali cha nguvu ya Waziri Mkuu Narendra Modi na chama chake cha Bharatiya Janata Party (BJP) kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2029.
Chama cha BJP kinalenga kuendelea kushikilia madaraka katika jimbo la Assam, huku kikijaribu kuongeza ushawishi wake kusini mwa India, hususan katika majimbo ya Tamil Nadu na Kerala ambako bado kina changamoto kubwa kisiasa.
Macho yote sasa yako katika jimbo la West Bengal, ambapo BJP inajaribu kukiondoa madarakani chama cha TMC katika kinyang’anyiro chenye ushindani mkali.
Kampeni ya West Bengal iligubikwa na utata kufuatia marekebisho ya orodha ya wapiga kura, ambapo mamilioni ya majina yaliondolewa katika daftari la wapiga kura, hali iliyozua mjadala mkali.
Upigaji kura na hesabu unaendelea kutarajiwa kuchukua muda zaidi, huku matokeo ya awali yakitarajiwa kuanza kutangazwa ndani ya saa chache zijazo.
WHO yathibitisha mlipuko wa Hantavirus duniani, waua watatu kwenye meli ya kitalii
Watu watatu wamefariki dunia kufuatia mlipuko unaoshukiwa kuwa wa virusi vya Hantavirus kwenye meli ya kitalii iliyokuwa safarini kutoka Argentina kuelekea Cape Verde, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 70 alianza kuugua akiwa ndani ya meli ya MV Hondius na kufariki alipowasili katika Kisiwa cha St Helena, huku mwili wake ukisubiri kurejeshwa nchini Uholanzi. Mke wake, mwenye umri wa miaka 69, pia aliugua na kufariki hospitalini mjini Johannesburg, Afrika Kusini. Wawili hao walikuwa raia wa Uholanzi.
Kisa pekee kilichothibitishwa kuwa ni cha virusi hivyo ni ya raia wa Uingereza mwenye umri wa miaka 69 ambaye kwa sasa yuko hoi katika uangalizi maalum (ICU) jijini Johannesburg. Aidha, wahudumu wawili wa meli hiyo wanahitaji msaada wa haraka wa matibabu.
Maafisa wa Uholanzi wanapanga kurejesha nchini mwao watu wawili wenye dalili pamoja na mwili wa mtu wa tatu aliyefariki ambao bado uko ndani ya meli hiyo.
Virusi vya hantavirus huenezwa na panya, hasa kupitia hewa yenye chembechembe kutoka kinyesi au mkojo wa panya. Kwa kawaida, maambukizi kutoka mtu kwenda mtu ni nadra sana.
Mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza, Profesa Paul Griffin, amesema hali hii ni ya kushangaza kwa sababu meli za kitalii zina mazingira yanayoweza kurahisisha maambukizi kutokana na msongamano wa watu, ingawa ni nadra sana kuona hantavirus ikisambaa katika mazingira kama hayo, hasa baada ya kuboreshwa kwa viwango vya usafi tangu janga la COVID-19.
Iran yathibitisha kupokea jibu la Marekani kuhusu pendekezo lake jipya la amani
Iran imetangaza kuwa imepokea majibu kutoka Marekani kufuatia pendekezo lake jipya la amani, huku msemaji wa wizara ya mambo ya nje akisema ujumbe huo uliwasilishwa kupitia Pakistan na sasa unafanyiwa tathmini.
Hata hivyo, Marekani haijathibitisha rasmi kupokea au kujibu pendekezo hilo. Rais Donald Trump amenukuliwa akisema kuwa pendekezo au mpango huo wa iran haukubaliki kwake, akieleza kuwa haukidhi matarajio ya Washington.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iran, mpango huo wa vipengele 14 pamoja na mengine, unaitaka Marekani kuondoa majeshi karibu na mipaka ya Iran, kusitisha vikwazo kwenye bandari zake na kumaliza mashambulizi yote, ikiwemo yanayohusishwa na Israel nchini Lebanon.
Pendekezo hilo pia linapendekeza makubaliano yafikiwe ndani ya siku 30, likihimiza pande zote kuzingatia kumaliza vita badala ya kuendeleza usitishaji mapigano wa sasa.
Wakati huo huo, Trump amesema Marekani itaendelea kulinda usafirishaji wa meli katika Mlango wa Hormuz na kuonya kuwa kuna uwezekano wa kurejea kwa mashambulizi iwapo Iran “itafanya makosa”.
Mvutano kati ya mataifa hayo unaendelea huku Iran ikikanusha madai ya kutengeneza silaha za nyuklia, wakati Marekani ikisisitiza kuwa haitaruhusu taifa hilo kuwa na silaha hizo.
Marekani kusaidia meli zilizokwama Hormuz - Trump
Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuwa nchi yake itaanza operesheni maalum ya kusaidia meli zilizokwama katika Mlango bahari wa Hormuz, akieleza hatua hiyo ni kama “msaada wa kibinadamu” kwa mataifa yasiyohusika moja kwa moja na vita kati ya Marekani, Israel na Iran.
Trump amesema operesheni hiyo itaanza rasmi leo Jumatatu, ikilenga kusaidia meli na wafanyakazi wake ambao wamekwama kwa zaidi ya miezi miwili kutokana na vizuizi vya Iran katika njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.
Katika ujumbe wake, Trump alisema Marekani itaziongoza meli hizo kupita salama ili ziweze kuendelea na shughuli zao, huku akionya kuwa jaribio lolote la kuingilia operesheni hiyo litakabiliwa na nguvu.
Hatua hiyo inakuja wakati mvutano ukiendelea kuongezeka, ambapo Iran imezuia usafirishaji mafuta na bidhaa zingine kutoka Ghuba ya Uajemi, huku Marekani nayo ikiweka vikwazo kwa meli zinazotoka bandari za Iran.
Wakati huo huo, Iran imethibitisha kuwa imepokea majibu kutoka Marekani kuhusu pendekezo lake la amani lenye masuala 14, likijumuisha madai ya kuondolewa kwa vikwazo na kusitishwa kwa mapigano, huku Tehran ikisema bado inalichambua jibu hilo.
Hata hivyo, Trump ameashiria kutoridhishwa na pendekezo hilo la Iran, akisema huenda lisikubalike, wakati Iran ikisisitiza kuwa kwa sasa hakuna mazungumzo ya nyuklia hadi vita vitakapomalizika.