Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mkutano wa nchi za Ghuba waanza huku kukiwa na wito wa 'kusitisha mapigano mara moja' huko Gaza
Mkutano wa 45 wa wakuu wa nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba umeanza nchini Kuwait siku ya Jumapili, huku kukiwa na hali ya wasiwasi na hali ambayo Mashariki ya Kati imekuwa ikishuhudiwa kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Muhtasari
- Mkutano wa nchi za Ghuba waanza huku kukiwa na wito wa 'kusitisha mapigano mara moja' huko Gaza
- Ngorongoro Tanzania Rais Samia kuunda Tume kuchunguza malalamiko ya jamii ya Wamasai Ngorongoro Tanzania
- Nigeria Zaidi ya watu 50 wapoteza maisha na wengine hawajulikani walipo baada ya boti kuzama Nigeria
- Syria Washirika, wapinzani wa Rais Assad wa Syria wanasema nini?
- Tanzania Mwenyekiti wa Ngome ya vijana ya chama pinzani nchini Tanzania, ACT Wazalendo, Abdul Nondo aripotiwa kutekwa
- GazaMashirika ya misaada yasitisha shughuli Gaza baada ya wafanyakazi kuuawa kwa shambulizi la Israel
- Syria Wanajeshi wa Syria waondoka Aleppo huku waasi wakisonga mbele
- Lebanon Israel yashambulia Lebanon 'baada ya kugundua shughuli za vitisho' licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano
Moja kwa moja
Na Lizzy Masinga
Mkutano wa nchi za Ghuba waanza huku kukiwa na wito wa 'kusitisha mapigano mara moja' huko Gaza
Mkutano wa 45 wa wakuu wa nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba umeanza nchini Kuwait siku ya Jumapili, huku kukiwa na hali ya wasiwasi na hali ambayo Mashariki ya Kati imekuwa ikishuhudiwa kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Amir wa Kuwait, Sheikh Meshal Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah, alitoa wito wa "kusitisha mapigano mara moja" huko Gaza.
Sheikh Meshaal alisema, "Tunarudia kulaani uvamizi wa kikatili wa Israel katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, na mauaji ya kimbari ya mfululizo dhidi ya watuwa Palestina," akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuhakikisha "kusitishwa kwa mapigano mara moja, kutoa ulinzi wa kimataifa kwa raia wasio na hatia." na kuhakikisha kufunguliwa kwa njia salama na kuwasili kwa msaada wa dharura wa kibinadamu."
Sheikh Meshaal alishutumu " kutokuwepo usawa katika kutumia sheria, mikataba na maazimio husika ya kimataifa" ambayo yalisababisha "kuenea kwa uvamizi wa Israel na kuvuruga usalama na uthabiti wa eneo hilo," kama alivyosema.
Mataifa ya Ghuba, ikiwa ni pamoja na Saudi Arabia, UAE na Qatar, yalikaribisha usitishaji vita kati ya Israel na Hezbollah ulioanza kutekelezwa alfajiri ya Jumatano, wiki iliyopita, baada ya mwaka mmoja wa mzozo uliosababisha vifo vya maelfu ya watu nchini Lebanon na kusababisha watu wengi kuyahama makazi yao katika pande zote za mpaka.
Huu sio mkutano wa kwanza wa kilele kufanyika huku kukiwa na mzozo unaoendelea katika eneo hilo.
Mapema Desemba 2023, mkutano wa kilele wa Ghuba ulifanyika Doha, takribani miezi miwili baada ya shambulio la Oktoba 7 lililotekelezwa na Hamas dhidi ya miji na maeneo ya kijeshi ya Israeli katika eneo linalozunguka Ukanda wa Gaza.
Shambulio hilo lilikuwa mahali pa kuanzia kwa vita ambavyo athari zake hazikuishia Gaza pekee.
Unaweza kusoma;
Rais Samia kuunda Tume kuchunguza malalamiko ya jamii ya Wamasai Ngorongoro Tanzania
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema ataunda Tume mbili ambazo moja itachunguza na kutoa mapendakezo kuhusu masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi wa Ngorongoro.
Tume nyingine itaangalia utekelezaji wa zoezi zima la uhamaji kwa hiari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Rais Samia ameyasema hayo leo Ikulu ndogo, jijini Arusha wakati akizungumza na viongozi wa kimila wa jamii ya Kimasai (Malaigwanani) wanaoishi katika eneo la Ngorogoro.
Mkutano huo umefanyika kwa lengo la kuwasikiliza viongozi hao baada ya kuwepo kwa malalamiko kuhusu baadhi ya maamuzi ya serikali yanayohusu eneo la Ngorongoro.
Amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuimarisha utendaji kazi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa lengo la kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na jamii hiyo.
Vilevile, amesisitiza ulazima wa wananchi kushirikishwa ipasavyo katika upangaji na utekelezaji miradi inayopita kwenye maeneo yao.
Rais Samia amesisitiza kuwa Tanzania ni nchi inayojivunia umoja wa kitaifa na yenye serikali inayowahudumia Watanzania wote, hivyo, ameitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI kushughulikia changamoto zinazojitokeza ikiwemo kukosekana kwa baadhi ya huduma za msingi za kijamii katika eneo la Ngorongoro.
Zaidi ya watu 50 wapoteza maisha na wengine hawajulikani walipo baada ya boti kuzama Nigeria
Takriban miili 54 imepatikana kutoka Mto Niger nchini Nigeria baada ya boti, ambayo huenda ilikuwa imebeba zaidi ya abiria 200, kupinduka mapema siku ya Ijumaa, mamlaka zilisema.
24 kati ya waliokuwemo ndani ya chombo hicho waliokolewa, baadhi yao wakiwa bado wamelazwa hospitalini, lakini huenda makumi wengine hawajulikani walipo.
Wapiga mbizi bado wanatafuta lakini matumaini yanafifia kuhusu uwezekano wa kupata manusura zaidi.
Hili ni tukio la karibuni zaidi katika mfululizo wa ajali za boti kwenye njia za maji za ndani ya nchi.
Licha ya mapendekezo ya usalama kufanywa, sheria hazifuatwi na wachache huwajibishwa.
Boti hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka jimbo la Kogi, katikati mwa Nigeria, kuelekea soko la kila wiki katika jimbo jirani la Niger.
Wafanyabiashara wa sokoni na vibarua wa mashambani walidhaniwa kuwa miongoni mwa abiria.
Chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana lakini kuna dalili kuwa wengi wa wasafiri hao huenda hawakuwa wamevaa jaketi la kujiokoa inavyotakiwa.
Kupata maelezo sahihi kuhusu ni nani hasa alikuwa amepanda boti ni vigumu kwa sababu hakukuwa na kumbukumbu, afisa wa eneo aliyehusika aliambia BBC.
"Tatizo ni kwamba hakuna maelezo ya abiria na kwa sababu ya muda ajali ilitokea, kutoa maelezo sahihi ya watu, walionusurika na waliopotea, ni ngumu sana," Justin Uche, ambaye ni mkuu wa ofisi ya Jimbo la Kogi ya Dharura ya Kitaifa. Shirika la Usimamizi lilisema.
Wakati huo huo Gavana wa jimbo la Kogi Usman Ododo aliagiza hospitali zote ambapo manusura wanapokea matibabu kuhakikisha wanapata huduma ya kutosha ikiwemo chakula.
Pia alihimiza utekelezwaji mkali wa kanuni za usalama ili kuhakikisha kuwa matukio kama hayo yanaepukika katika siku zijazo.
Hii ni mara ya tatu kwa boti ya abiria kupinduka nchini Nigeria katika siku 60 zilizopita.
Mwezi uliopita, mtumbwi wa mbao uliokuwa umebeba takribani abiria 300, ulipinduka na kuzama katikati ya Mto Niger na kuua karibu watu 200.
Wiki iliyopita tu, watu watano walikufa wakati boti mbili zilipogongana katika jimbo la Delta kusini mwa Nigeria.
Washirika, wapinzani wa Rais Assad wa Syria wanasema nini?
Katika siku chache tangu majeshi ya waasi yaanze mashambulizi makubwa kaskazini-magharibi mwa Syria, washirika wa kikanda na wapinzani wa Rais Bashar al-Assad wote wamekuwa wakitazama kwa hofu. Hapa kuna muhtasari wa haraka wa kile ambacho wamekuwa wakisema:
- Iran, mmoja wa washirika wakuu wa Assad, inamtuma waziri wake wa mambo ya nje, Abbas Araghchi, mjini Damascus leo kujadili mzozo unaoendelea.
- Waziri wa mambo ya nje wa Iran ataelekea Uturuki, nchi ambayo inaunga mkono baadhi ya makundi ya waasi.
- Jana, Araghchi alizungumza kwa simu na mwenzake wa Urusi, ambapo wawili hao walizungumza juu ya "haja ya uratibu" kati ya Urusi, Iran na Uturuki.
- Marekani, ambayo iliunga mkono vikosi vya waasi wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, inasema haina uhusiano wowote na mashambulizi yanayoendelea.
- Msemaji wa Ikulu ya White House amesema hali hiyo ni matokeo ya utawala wa Assad kukataa kujihusisha na mchakato wa kisiasa, na kutegemea Urusi na Iran.
- Kujibu mashambulizi ya waasi, Urusi imeanzisha "msururu wa mashambulizi ya anga" maeneo ya vijijini kaskazini-magharibi mwa Syria, siku moja baada ya kupiga Aleppo kwa mara ya kwanza tangu 2016, Shirika la kutetea Haki za Kibinadamu la Syria linasema.
Mwenyekiti wa Ngome ya vijana ya chama pinzani nchini Tanzania, ACT Wazalendo, Abdul Nondo aripotiwa kutekwa
Mwenyekiti wa Ngome ya vijana ya chama upinzani nchini Tanzania, ACT Wazalendo, Abdul Nondo ameripotiwa kutekwa asubuhi ya leo na watu wasiojulikana akitokea mkoani Kigoma alikokuwa na viongozi wengine wa kitaifa wa chama hicho, walioongoza kampeni kwenye mikoa ya magharibi mwa Tanzania katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27.
Taarifa za kutekwa kwa Nondo zimetolewa na ACT Wazalendo kupitia taarifa kwa umma iliyosainiwa na Naibu Katibu wa haki za binadamu na vyombo vya uwakilishi wa wananchi, Taarifa hiyo inasema: Nondo aliwasili katika kituo cha basi cha Magufuli eneo la Mbezi kwa usafiri wa basi la Saratonga lenye namba za usajili T221 DKB.
Pia taarifa hiyo imewanukuu mashuhuda wa tukio waliosema kuwa kulikuwa na purukushani katika utekeji wa Nondo uliosababisha mkoba wake wa nguo na pingu iliyobebwa na mmoja wa watekaji kudondoka.
"Katibu Mwenezi wa chama hicho, mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala na Afisa Harakati na Matukio Taifa, Wiston Mogha waliofika mapema kituoni hapo walitambua haraka kuwa aliyetekwa ni Abdul Nondo kwa sababu walizitambua nguo zake kwenye mkoba uliodondoka pamoja na notebook yake", ilifafanua taarifa hiyo.
Imeongeza: ACT inaendelea kufuatilia taarifa zaidi kuhusu tukio hilo na taarifa zaidi itatolewa. Chama hicho kimemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Camillus Wambura, kufuatilia haraka tukio hilo na kuhakikisha Bw. Nondo anaachiwa huru mara moja.
Taarifa ya Jeshi la Polisi limesema kuwa Disemba 1, majira ya saa 11 alfajiri katika stendi ya Magufuli jijini Dar es Salaam, kuna mtu mmoja mwanaume amekamatwa kwa nguvu na kuchukuliwa na watu waliokuwa wakitumia gari lenye usajili T 249 CMV aina ya Landcruiser rangi nyeupe.
Polisi imesema mashuhuda walieleza kuwa vitu vilivyodondoshwa na baadhi ya vitu vilivyokuwemo kwenye mkoba vimetambuliwa ni vya Abdul Omary Nondo.
Polisi imesema kuwa ufuatiliaji wa tukio hilo ulianza mara tu baada ya kupokelewa kwa taarifa ya polisi, sambamba na kufungua jalada
Tukio hili linaweza kuamsha upya hisia na kumbukumbu za matukio ya utekaji wa watu hususan viongozi au wafuasi wa vyama vya upinzani.
Tukio la karibuni zaidi ni la aliyekuwa mjumbe wa sekretarieti ya chama cha upinzani cha Chadema, Ally Kibao aliyetekwa na baadaye kuuawa jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa Septemba mwaka huu.
Mashirika ya misaada yasitisha shughuli Gaza baada ya wafanyakazi kuuawa kwa shambulizi la Israel
Shirika la kutoa misaada la World Central Kitchen (WCK) limesema kuwa linasitisha shughuli zake huko Gaza baada ya gari lililokuwa limebeba wafanykazi wake kupigwa na shambulio la anga la Israel.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema mlengwa wa shambulizi hilo alishiriki katika mashambulizi ya Oktoba 7 dhidi ya Israeli, na kwa sasa ameajiriwa na WCK.
WCK ilisema "imesikitishwa" kwamba gari lililokuwa limebeba wafanyakazi lilipigwa na ilikuwa ikitafuta maelezo zaidi, ingawa iliongeza "haijui" kwamba mtu yeyote kwenye gari alikuwa na uhusiano na shambulio la Oktoba 7.
Shirika la habari la serikali ya Palestina, Wafa liliripoti kuwa watu watano waliuawa katika shambulio hilo huko Khan Younis, kusini mwa Gaza, siku ya Jumamosi, na watatu kati yao wakiwa wafanyakazi wa WCK.
Walijumuisha mkurugenzi wa jikoni za WCK huko Gaza, shirika liliongeza.
Kando na hilo, shirika la misaada la Uingereza Save the Children lilisema mmoja wa wafanyakazi wake pia aliuawa Jumamosi alasiri huko Khan Younis.
Ahmad Faisal Isleem Al-Qadi, 39, alikuwa akirejea nyumbani kwa mkewe na bintiye wa miaka mitatu kutoka msikitini alipouawa, shirika la misaada liliongeza.
"Ahmad, ambaye alikuwa kiziwi, atakumbukwa kwa uamuzi wake wa kusaidia wengine, kwa fahari yake kwa binti yake, na kwa uwezo wake wa kufurahisha wengine,"
Save the Children ilisema katika taarifa. Haijulikani ikiwa aliuawa katika shambulizi kama ilivyokuwa kwa wafanyakazi wa WCK.
Shirika la Save the Children linasema kulikuwa na mashambulizi mawili mjini Khan Younis siku ya Jumamosi, lakini BBC haijaweza kuthibitisha hili.
Unaweza kusoma;
Wanajeshi wa Syria waondoka Aleppo huku waasi wakisonga mbele
Majeshi ya serikali ya Syria yameondoka katika mji wa Aleppo baada ya mashambulizi ya waasi wanaopinga utawala wa rais Bashar al-Assad.
Jeshi lilikiri kwamba waasi walikuwa wameingia "sehemu kubwa" ya mji huo, ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini humo, lakini wakaapa kufanya mashambulizi ya kukabiliana.
Mashambulizi hayo yanaashiria mapigano makubwa zaidi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria katika miaka ya hivi karibuni.
Zaidi ya watu 300, wakiwemo takribani raia 20, wameuawa tangu ilipoanza siku ya Jumatano, kwa mujibu wa Shirika la Kuchunguza Haki za Kibinadamu la Syria (SOHR) lenye makao yake nchini Uingereza.
Akizungumza siku ya Jumamosi, Rais Assad aliapa "kulinda uthabiti [wa Syria] na uadilifu wa eneo lake mbele ya magaidi wote na wanaowaunga mkono".
"[Nchi] ina uwezo, kwa usaidizi wa washirika na marafiki zake, kuwashinda na kuwaondoa, bila kujali mashambulizi yao ya kigaidi ni makali kiasi gani," ofisi yake ilimnukuu akisema.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vimesababisha vifo vya takribani watu nusu milioni, vilianza mwaka 2011 baada ya serikali ya Assad kujibu maandamano ya kuunga mkono demokrasia.
Mzozo huo umesimama kwa kiasi kikubwa tangu makubaliano ya kusitisha mapigano mwaka 2020, lakini vikosi vya upinzani vimedumisha udhibiti wa mji wa kaskazini-magharibi wa Idlib na sehemu kubwa ya mkoa unaozunguka.
Idlib iko kilomita 55 tu kutoka Aleppo, ambayo yenyewe ilikuwa ngome ya waasi hadi ilipodhibitiwa na vikosi vya serikali mwaka 2016.
Unaweza kusoma;
Israel yashambulia Lebanon 'baada ya kugundua shughuli za vitisho' licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano
Jeshi la Israel lilitangaza siku ya Jumamosi kuwa limefanya mashambulizi kadhaa nchini Lebanon "yakilenga Hezbollah", baada ya kugundua kile ilichokitaja kuwa "shughuli zinazoleta tishio", katika siku ya nne ya utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya pande hizo mbili.
Jeshi lilisema katika taarifa yake kwamba matukio manne tofauti yalihusisha "kuhamisha vifaa vya kivita," vinavyofanya kazi kwenye "eneo lenye kurusha makombora ya Hezbollah," na kufanya kazi "ndani ya miundombinu ya uzalishaji wa makombora," na kubainisha kuwa baadhi ya mashambulizi yalifanywa jeshi la anga.
Mapema siku ya Jumamosi, jeshi la Israel lilitangaza, kwa mujibu wa Agence France-Presse, kwamba lililenga "miundombinu ya kijeshi" karibu na mpaka wa Syria na Lebanon, likisema kwamba Hezbollah inaitumia kusafirisha silaha, katika hatua ambayo ilielezea kama ukiukaji wa sheria na makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya pande hizo mbili.
Jeshi liliripoti kuwa jeshi la anga lilifanya "shambulizi kwenye maeneo ya miundombinu ya kijeshi karibu na vivuko vya mpaka kati ya Syria na Lebanon ambayo Hezbollah ilikuwa ikitumia kikamilifu kusafirisha silaha kutoka Syria hadi Lebanon."
Aliongeza kuwa operesheni hiyo ya magendo ilifanyika “baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kuanza kutekelezwa.Jeshi pia lilitangaza kuwa limekuwa likifanya operesheni za msako kusini mwa Lebanon tangu jana, ambapo wanajeshi waliweza "kunyakua silaha ambazo Hezbollah ilikuwa imezificha ndani ya msikiti."
Usitishaji huo wa mapigano ulianza kutekelezwa Jumatano asubuhi, makubaliano ambayo yanahitimisha zaidi ya mwaka mmoja wa operesheni za kijeshi za kuvuka mpaka na miezi miwili ya vita vya wazi kati ya Israel na Hezbollah.
Unaweza kusoma;
Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu leo