Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Stoltenberg: Ni wakati wa kuruhusu Ukraine kutumia silaha za NATO kwenye eneo la Urusi

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, katika mahojiano na Economist, ametoa wito kwa nchi wanachama wa muungano unaosambaza silaha za Ukraine kuondoa vikwazo vya matumizi.

Muhtasari

  • Manchester United watwaa ubingwa wa Kombe la FA England
  • Tanzania: Mtibwa Sugar yashuka daraja baada ya miongo mitatu
  • Stoltenberg: Ni wakati wa kuruhusu Ukraine kutumia silaha za NATO kwenye eneo la Urusi
  • Chile yawakamata maafisa zima moto wakishutumiwa kuanzisha moto ulioua watu 137
  • Mbio za kuwaokoa wanakijiji walionaswa baada ya maporomoko ya ardhi
  • Wamishonari wa Marekani wauawa katika ghasia za magenge ya Haiti
  • Ulimwengu unapuuza hatari ya mauaji ya kimbari Sudan - mtaalam wa UN
  • Ten Hag anajiandaa kwa fainali ya Kombe la FA bila kujua mustakabali wake
  • Polisi wa Kenya kuwasili Haiti katika kipindi cha 'wiki tatu'

Moja kwa moja

Lizzy Masinga

  1. Manchester United watwaa ubingwa wa Kombe la FA England

    Manchester United imetwaa ubingwa wa Kombe la FA kwa ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya mahasimu wao Manchester City likiwa ni taji lao la 13 mshindano hayo, taji moja pungufu ya Arsenal.

    Katika pambano la fainali lilipigwa kwenye dimba la Wembley, magoli mawili ya Manchester United yamefungwa na Alejandro Garnacho na Kobbie Mainoo, huku kukiwa na goli pekee la Manchester City lililofungwa na Jeremy Doku.

    Si tu kombe la FA ambalo Manchester United wamenyakua kwa ushindi huu, pia watacheza mashindano ya Ligi ya Uropa msimu ujao.

    Kocha wa Man United, Erik ten Hag amelazimika kujibu maswali mengi na hakika amesikia mengi kuhusu mustakabali wake wikendi hii kwani bado hakuna uhakika iwapo atakuwepo msimu ujao hususan kutokana na kumaliza nafasi ya nane katika Ligi Kuu ya England.

  2. Tanzania: Mtibwa Sugar yashuka daraja baada ya miongo mitatu,

    Mabingwa wa zamani wa soka wa Tanzania Bara, Mtibwa Sugar wameshuka daraja kutoka Ligi Kuu ya nchi hiyo, baada ya miaka 29 tangu walipopanda daraja mwaka 1995.

    Mabingwa hao mara mbili wa 1999 na 2000 wameshuka daraja rasmi baada ya kukubali kichapo cha magoli 3-2 mbele ya timu ya Mashujaa ya Kigoma katika pambano lililofanyika dimba la Lake Tanganyika.

    Kwa kichapo hicho Mtibwa wamebaki na alama 21 huku ukibakia mchezo mmoja kabla ya kukamilisha msimu, hivyo hata wakishinda watakuwa na alama 24 ambazo tayari zimevukwa na timu nyingine 15 za ligi hiyo ya timu 16.

    Timu mbili za mwishoni mwa msimamo zinashuka daraja moja kwa moja wakati timu mbili za nafasi ya 13 na 14 zitacheza mtoano na timu za Championship kupigania kubaki ligi kuu.

    Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakamilika mwisho mwa juma lijalo na tayari mabingwa Yanga walionyakua taji la tatu mfululizo wamekabidhiwa kombe la ubingwa Jumamosi katika uwanja wa Benjamin Mkapa katika jiji kuu la kibiashara la Dar es Salaam.

  3. Stoltenberg: Ni wakati wa kuruhusu Ukraine kutumia silaha za NATO kwenye eneo la Urusi

    Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, katika mahojiano na Economist, ametoa wito kwa nchi wanachama wa muungano unaosambaza silaha za Ukraine kuondoa vikwazo vya matumizi yao kwa mashambulizi ya shabaha za kijeshi nchini Urusi.

    "Ni wakati wa washirika kufikiria kuondoa baadhi ya vikwazo walivyoweka kuhusu matumizi ya silaha zilizopelekwa Ukraine," Stoltenberg alisema katika mahojiano ya Mei 24.

    "Hasa sasa, kutokana na mapigano makali yanayoendelea Kharkov, karibu na mpaka, kuinyima Ukraine uwezo wa kutumia silaha hizi dhidi ya shabaha halali za kijeshi kwenye eneo la Urusi inafanya iwe vigumu zaidi kwake kulinda eneo lake."

    Mtangulizi wa Stoltenberg , Anders Fogh Rasmussen, mnamo Mei 14 alitoa wito wa kuruhusu nchi za NATO za Ulaya Mashariki kutumia ulinzi wa anga wa ardhini kuharibu makombora ya Urusi na ndege zisizo na rubani zinazolenga Ukraine.

    Stoltenberg hakuunga mkono pendekezo hili. "Hatutakuwa sehemu ya mzozo," alisema. Kwa maoni yake, kazi ya Magharibi ni kinyume chake , "kuzuia vita hivi kugeuka kuwa vita kamili kati ya Urusi na NATO huko Ulaya."

    Rais wa Ukraine Vladimir Zelensky mara kwa mara anatoa wito kwa washirika wa Magharibi "kuonesha dhamira" na kuruhusu zitumike kwa mashambulizi kwenye eneo la Urusi.

    Unaweza kusoma;

  4. Chile yawakamata maafisa zima moto wakishutumiwa kuanzisha moto ulioua watu 137

    Mamlaka ya Chile imemkamata mfanyakazi wa zima moto na mfanyakazi wa shirika la misitu kwa tuhuma za kuanzisha moto ambao uliua takribani watu 137 mnamo Februari.

    Mmoja wa watu hao aliajiriwa na Shirika la Kitaifa la Misitu ambalo linahusika na kupambana na moto msituni, mkurugenzi wa polisi Eduardo Cerna alisema.

    Washukiwa hao wamerudishwa rumande, wakikabiliwa na shtaka la kuchoma moto na kusababisha kifo. Moto huo ulikuwa mbaya zaidi nchini, uliharibu eneo la Valparaíso, ambalo ni zaidi ya kilomita 122 (maili 75) kutoka mji mkuu wa Chile, Santiago.

    Maafisa wanadai kuwa moto ulianzishwa kwa wakati mmoja, ambapo upepo ulisababisha moto huo kuenea.

    Zaidi ya watu 16,000 waliathiriwa na moto huo ambao uliharibu nyumba na kuharibu eneo hilo, ambalo ni makazi ya Vina del Mar, sehemu maarufu ya mapumziko nyakati za likizo.

    Akizungumzia kukamatwa afisa wa zima moto, Vicente Maggiolo, kamanda wa Kampuni ya 13 ya Zimamoto huko Valparaiso, aliviambia vyombo vya habari vya eneo hilo: "Tumesikitishwa sana na kilichotokea, ni tukio la pekee kabisa.

    "Tumeitumikia Valparaiso kwa zaidi ya miaka 170 na hatuwezi kuruhusu mambo kama hayo." Mwendesha mashtaka Osvaldo Ossandón alisema: "Kulikuwa na takribani milipuko minne, sawa kutoka kwa kila mmoja."

    Alisema vifaa vilivyotumika kuwasha moto vilipatikana katika nyumba ya mmoja wa washukiwa hao, na kuongeza kuwa wachunguzi wanachunguza uwezekano wa uhusiano na mashambulio mengine ya uchomaji moto.

  5. Yatima waozwa Nigeria licha ya mpango wa harusi ya pamoja kupingwa

    Takriban wasichana 100 miongoni mwao yatima kadhaa wameolewa katika sherehe tofauti nchini Nigeria licha ya mpango huo kuzua gumzo kali nchini humo.

    Tukio la Ijumaa lilikusudiwa kuwa harusi ya pamoja lakini Waziri wa Masuala ya Wanawake Uju Kennedy-Ohanenye aliwasilisha agizo la mahakama kuikomesha, akihofia kuwa baadhi ya wasichana walikuwa na umri mdogo.

    Alirejea uamuzi huo baada ya kufikia makubaliano na Spika wa Bunge la Jimbo la Niger, Abdulmalik Sarkin-Daji, ambaye aliunga mkono harusi hiyo ya halaiki, kwa wasichana hao kuwa na sherehe za kibinafsi.

    "Sikuwa na nia ya kusitisha ndoa hiyo lakini kuhakikisha wasichana wamefikia umri wa kuolewa na hawakulazimishwa," Bi Kennedy-Ohanenye alisema katika taarifa.

    BBC inaelewa kuwa sharti la sherehe hizo kuendelea ni kwamba wanawake wote waliohusika walipaswa kuwa na umri wa kisheria, ambao ni 18 nchini Nigeria.

    Waziri Kennedy-Ohanenye alisema angewatunuku biharusi wote ufadhili wa masomo na malipo ya kila mwezi kwa miezi sita ya kwanza ya ndoa zao.

    Mmoja wa wazazi wa maharusi hao, Mallama Amina Mariga, aliiambia BBC kuwa harusi hiyo ya pamojai ilipangwa ili "kuwasherehekea wasichana hao kwa usawa na kuwapa hisia ya umoja".

    Bi Mariga, kama familia nyingi, alipewa vitu kwa ajili ya harusi ya bintiye na malipo ya mahari, ikiwa ni pamoja na kitanda na cherehani kutoka kwa wanasiasa.

    Wengi wa wanawake vijana wamepoteza jamaa zao kutokana na mashambulizi ya majambazi wenye silaha, ambao mara kwa mara huwalenga raia katika jimbo la kaskazini-magharibi la Niger.

  6. Mbio za kuwaokoa wanakijiji walionaswa baada ya maporomoko ya ardhi

    Huduma za dharura ziko mbioni kufikia vijiji vilivyokumbwa na maporomoko makubwa ya udongo katika jimbo la Enga la Papua New Guinea, ambako mamia ya watu wanahofiwa kufariki.

    Timu ya uokozi inayojumuisha matabibu na wanajeshi imefanikiwa kufikia eneo lililotengwa na maporomoko ya ardhi, shirika la kibinadamu la Care Australia lilisema.

    Lakini mazingira magumu na uharibifu wa barabara kuu unafanya juhudi za uokoaji kuwa ngumu, iliongeza, huku njia kuu zikiwa zimefungwa na eneo hilo kufikiwa tu kupitia helikopta.

    Maporomoko ya ardhi yalizika mamia ya nyumba katika nyanda za juu za Enga, kaskazini mwa taifa la kisiwa kusini-magharibi mwa Pasifiki, mwendo wa saa 03:00 kwa saa za huko siku ya Ijumaa (17:00 GMT siku ya Alhamisi).

    Bado haijabainika ni watu wangapi wamenaswa chini ya vifusi.

    "Ingawa eneo hilo halina watu wengi, wasiwasi wetu ni kwamba idadi ya vifo inaweza kuwa kubwa," Care Australia ilisema katika taarifa ya awali.

    Amos Akem, mbunge wa jimbo la Enga, aliliambia gazeti la Guardian kwamba kulingana na ripoti kutoka eneo la tukio, "maporomoko ya ardhi yalizika zaidi ya watu 300 na nyumba 1,182".

    Akinukuliwa na gazeti la Guardian, Bw Akem alieleza kuwa juhudi za uokoaji zimetatizwa na kukatizwa kwa barabara inayounganisha kijiji kilichoathiriwa cha Yambali na mji mkuu.

    Yambali iko umbali wa kilomita 50 kutoka Wabag, mji mkuu wa jimbo hilo.

    Akizungumza na shirika la habari la AP, afisa wa Umoja wa Mataifa Serhan Aktoprak amesema eneo lililoathiriwa na maporomoko hayo lina ukubwa wa viwanja vitatu hadi vinne vya soka.

    Kijiji cha Yambali, aliongeza, ni nyumbani kwa watu 3,895.

    Baadhi ya nyumba katika kijiji hicho ziliokolewa na maporomoko hayo, Bw Actoprak alisema, lakini "kwa kuzingatia ukubwa wa janga hilo" idadi ya waliofariki inaweza kuwa zaidi ya 100.

  7. Wamishonari wa Marekani wauawa katika ghasia za magenge ya Haiti

    Wanandoa wamishonari wa Marekani walikuwa miongoni mwa watu watatu waliouawa nchini Haiti huku ghasia za magenge zikiendelea kukumba nchi hiyo.

    Natalie Lloyd, 21, mume wake David mwenye umri wa miaka 23, na Jude Montis, raia wa Haiti mwenye umri wa miaka 20, walishambuliwa na watu wenye silaha walipokuwa wakitoka kanisani.

    Vifo vya wanandoa hao vilithibitishwa kwenye mtandao wa Facebook na babake Natalie, Seneta wa Jimbo la Missouri Ben Baker.

    "Walishambuliwa na magenge jioni hii na wote wawili waliuawa," aliandika. "Walikwenda mbinguni pamoja."

    Wenzi hao walifunga ndoa mnamo 2022. Shirika lao, Misheni nchini Haiti, lilithibitisha kwa vyombo vya habari vya Marekani kwamba Bw Montis alikuwa mwathirika wa tatu.

    Katika chapisho la awali la Facebook, shirika hilo lilisema kuwa watatu hao walishambuliwa na makundi mawili tofauti vilivyojihami, wakianza na shambulio la watu wenye silaha kwenye magari matatu.

    Baada ya kundi lingine kufika na mwanachama wa genge kuuawa kwa kupigwa risasi, wamisionari hao watatu walinaswa ndani ya nyumba huku genge likienda "katika hali ya mashambulizi kamili", chapisho hilo liliongeza.

    "Wamejifungia huko, magenge yamepiga madirisha yote nje ya nyumba na kuendelea kupiga risasi," chapisho hilo lilisema. Misheni nchini Haiti ilithibitisha kuwa wote watatu walikufa saa tatu baadaye.

    Idara ya serikali inafahamu kuhusu vifo hivyo, msemaji aliambia mshirika wa BBC wa Marekani CBS.

    "Tunatoa rambirambi zetu za dhati kwa familia kwa msiba wao," msemaji huyo alisema.

    "Tuko tayari kutoa usaidizi wote unaofaa wa kibalozi." Kwenye X/Twitter, Gavana wa Missouri Mike Parson alitaja vifo hivyo kuwa "habari za kuvunja moyo kabisa".

    Maelezo saidi:

  8. Ulimwengu unapuuza hatari ya mauaji ya kimbari Sudan - mtaalam wa UN

    Jimbo la Darfur nchini Sudan linakabiliwa na hatari kubwa ya mauaji ya halaiki huku ulimwengu ukitilia mkazo mizozo ya Ukraine na Gaza, ameonya mtaalamu wa Umoja wa Mataifa.

    "Tuna mazingira ambayo mauaji ya halaiki yanaweza kutokea au yametokea," Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Kuzuia Mauaji ya Kimbari, Alice Wairimu Nderitu, amekiambia kipindi cha Newsday cha BBC.

    Amesema raia wengi walilengwa kulingana na kabila lao katika mji unaozingirwa nchini Sudan wa El Fasher, ambapo mapigano makali yameongezeka katika siku za hivi karibuni. Zaidi ya vifo 700 vimeripotiwa katika siku 10 na shirika la matibabu katika jiji hilo.

    El Fasher ni kituo kikuu cha mwisho cha mijini katika eneo la Darfur ambacho kimesalia mikononi mwa jeshi la Sudan.

    Wanajeshi wamekuwa wakipigana na Jeshi la Wanajeshi la Rapid Support Forces (RSF) kwa zaidi ya mwaka mmoja, katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwalazimisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao.

    Mkazi wa eneo hilo Ibrahim al-Tayeb al-Faki aliiambia BBC dada yake aliuawa katika shambulio la anga la kijeshi ambalo pia liliharibu nyumba yake.

    Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 47 aliiambia BBC kuwa alikuwa amewapeleka watoto wake watatu kuishi na babu yao lakini nyumba yake pia ilipigwa.

    Familia sasa inajificha katika magofu yake. "Hakuna mahali salama katika El Fasher hivi sasa," alisema.

    Unaweza kusoma;

  9. Ten Hag anajiandaa kwa fainali ya Kombe la FA bila kujua mustakabali wake

    Kocha wa Manchester United Erik ten Hag anajiandaa kwa fainali ya Kombe la FA bila kujua hatama yake katika klabu hiyo.

    Uvumi kuhusu mustakabali wa Ten Hag ulizidi Ijumaa asubuhi kabla ya gazeti la The Guardian kuripoti kuwa Mholanzi huyo angepoteza kazi yake baada ya mechi dhidi ya Manchester City leo Jumamosi katika uwanja wa Wembely.

    United wamekataa kuzungumzia taarifa hiyo.

    Vyanzo vya klabu vinasisitiza kwamba lengo lao ni kuangazia fainali ya pili mfululizo ya kombe hilo kukutana na kikosi cha Pep Guardiola na kujaribu kumaliza msimu uliokuwa na hisia mateso kwa kasi.

    Inasisitizwa kuwa United wanaendelea na tathmini ya mwisho wa msimu, na kisha uamuzi juu ya mustakabali wa Ten Hag utafanywa.

    BBC Michezo imebaini hakujawa na mawasiliano na Ten Hag au wawakilishi wake na United.

    Yote haya yanaibua kumbukumbu ya wa miaka minane iliyopita, wakati Mholanzi mwenzake Ten Hag Louis van Gaal alipopata habari kwamba alikuwa karibu kufukuzwa kazi wakati ushindi wa fainali wa 2016 ulipomalizika dhidi ya Crystal Palace.

    Van Gaal alifahamishwa kuhusu uamuzi huo na uongozi wa United saa 24 baadaye.

    Soma pia:

  10. Polisi wa Kenya kuwasili Haiti katika kipindi cha 'wiki tatu'

    Rais wa Kenya William Ruto anasema jeshi lake la polisi wa kulinda amani linatarajiwa kuwasili Haiti kusaidia kuzima ghasia za magenge zinazoongezeka katika kipindi cha takribani wiki tatu.

    Katika mahojiano ya kipekee na BBC, Bw. Ruto alithibitisha timu ilikuwa tayari Haiti na alikuwa amekutana na polisi wa eneo hilo ili kupata mipango kabla ya wanajeshi wa Kenya kutumwa.

    Maoni ya Bw Ruto yalitolewa alipohitimisha safari ya siku tatu Washington DC, ikiwa ni ziara ya kwanza rasmi ya kiserikali nchini Marekani katika zaidi ya miaka 15.

    Wakati wa safari yake, Ikulu ya Marekani ilitoa wito wa kutumwa haraka kwa kikosi cha kimataifa kinachoongozwa na Kenya, baada ya wanandoa wa Marekani kutajwa miongoni mwa wamishonari watatu waliouawa nchini Haiti siku ya Ijumaa.

    "Nina timu tayari Haiti ninapozungumza nawe," Bw Ruto aliiambia BBC Ijumaa.

    "Hiyo itatupa sura ya jinsi mambo yanavyoonekana ardhini, uwezo unaopatikana, miundombinu ambayo imewekwa."

    Aliongeza: "Tunapopata tathmini hiyo tuliyokubaliana na polisi wa Haiti na uongozi wa Haiti, tunaangalia upeo wa kati ya wiki tatu na pale kuhusu sisi kuwa tayari kupeleka, mara kila kitu kitakapowekwa. "

    Mwaka jana, Kenya ilijitolea kuongoza kikosi cha usalama cha kimataifa kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kurejesha utulivu katika kisiwa cha Caribbean.

    Magenge yamechukua sehemu kubwa ya Haiti, na kuleta vurugu na uharibifu katika jiji lake kuu lililozingirwa, Port-au-Prince kufuatia mauaji ya Rais Jovenel Moïse mnamo Julai 2021.

    Siku ya Ijumaa, wamishonari wawili wa Marekani waliuawa huko Haiti na magenge.

    Bw Ruto aliambia BBC kwamba matukio ya aina hii ndiyo "hasa" sababu nchi yake ilikuwa inajiandaa kutuma jeshi lake la polisi.

    "Hatupaswi kupoteza watu. Hatupaswi kuwa tunapoteza wamisionari," alisema.

    "Tunafanya hivi ili kuzuia watu zaidi kupoteza maisha kwa magenge."

    Marekani pia ni sehemu ya muungano wa mataifa mbalimbali unaofanya kazi na Kenya.

    "Hali ya usalama nchini Haiti haiwezi kusubiri," alisema msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa siku ya Ijumaa.

    Walisema Rais Joe Biden aliahidi kuunga mkono "haraka ya kutumwa kwa jeshi" katika mazungumzo yake na Rais Ruto.

    Bw Ruto alisema kuwa kambi ambapo wanajeshi na vifaa vitahifadhiwa, inayojengwa kwa ushirikiano na Marekani, inakaribia kwa "70% kukamilika".

  11. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu hii leo