Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Ujerumani kuchangia dozi 100,000 za chanjo ya mpox kudhibiti mlipuko barani Afrika

Ujerumani itatoa dozi 100,000 za chanjo ya mpox kutoka kwa hisa zake za kijeshi kusaidia kudhibiti mlipuko katika bara la Afrika katika kipindi cha muda mfupi na pia kutoa msaada kwa nchi zilizoathiriwa, msemaji wa serikali alisema Jumatatu, Reuters imeripoti.

Muhtasari

  • Mamlaka zateketeza ekari zaidi ya 1000 za bangi Tanzania
  • Walimu kutofundisha bila shahada Uganda
  • Ujerumani kuchangia dozi 100,000 za chanjo ya mpox kudhibiti mlipuko barani Afrika
  • Shambulio la Urusi nchini Ukraine: Tunachojua kufikia sasa
  • Meneja wa zamani wa England Sven-Goran Eriksson aaga dunia
  • Magonjwa yaenea Gaza wakati maji taka yakichafua kambi
  • Shughuli za uokoaji zaendelea Sudan baada ya watu takribani 60 kupoteza maisha baada ya bwawa kupasuka
  • Zaidi ya makombora 100 na droni zilitumika katika mashambulizi - Zelensky
  • Watatu wauawa wakati Urusi ikifanya mashambulizi makubwa ya anga kote Ukraine
  • 22 wauawa baada ya vitambulisho vyao kukaguliwa Pakistan
  • Urusi yafanya shambulizi la ndege zisizo na rubani kwenye mji mkuu wa Ukraine
  • Australia: Sheria ya kutowaadhibu wanaokataa kupokea simu baada ya kazi yaanza kutekelezwa
  • Kenya: Miungano ya kutetea maslahi ya walimu yatofautiana kuhusu mgomo
  • Mwanamume mzee zaidi duniani: 'Sina siri ya kipekee ya kuishi miaka mingi'
  • Mkurugenzi Mtendaji aliyekamatwa hana 'chochote cha kuficha' - Telegram
  • Muingereza auawa katika shambulizi la kombora nchini Ukraine

Moja kwa moja

Asha Juma

  1. Tumefika tamati ya taarifa zetu kwa leo.

  2. Madaktari wagoma nchini Nigeria baada ya mwenzao kutekwa nyara

    Madaktari katika hospitali za umma nchini Nigeria wameanza mgomo wa siku saba nchini kote wakitaka mwenzao, Dk Ganiyat Popoola, ambaye amekuwa akishikiliwa na watekaji nyara kwa muda wa miezi minane.

    Mama huyo wa watoto watano alichukuliwa kutoka nyumbani kwake katikati ya usiku wa Disemba 27 pamoja na mumewe na mpwa wake.

    Mumewe aliachiliwa mnamo Machi baada ya fidia kuripotiwa kulipwa lakini watekaji nyara walimshikilia daktari wa macho na jamaa yake.

    Madaktari hao wanasema hata hawatatoa huduma ya dharura wakati wa mgomo huo.

    Dk.Popoola anafanya kazi katika hospitali ya Kituo cha Kitaifa cha Macho huko Kaduna, kaskazini-magharibi mwa Nigeria, na anaishi katika sehemu rasmi zinazotolewa na hospitali hiyo.

    Hospitali hiyo ni mojawapo ya hospitali kubwa za macho nchini.

    Wataalamu wanasema eneo la hospitali hiyo nje kidogo ya jiji la Kaduna linaifanya kuwa shabaha rahisi kwa watekaji nyara. Mnamo 2021, wanafunzi kadhaa walichukuliwa kutoka chuo cha karibu cha misitu.

    Dk.Taiwo Shittu wa Hospitali ya Kufundisha ya Chuo Kikuu cha Lagos alisema kilichompata Dkt.Popoola kinaweza kumpata mtu yeyote.

    "Tunataka mamlaka kuchukua hatua haraka, hii imeendelea kwa muda mrefu sana," alisema kwenye video kwenye mtandao wa kijamii.

    Madaktari wanahisi vyombo vya usalama havifanyi vya kutosha kuhakikisha aachiliwe. Watekaji nyara wanaomba 40m naira (£19,000; $25,000) kwa ajili ya uhuru wao. Ingawa sheria tata inayoharamisha malipo ya fidia ilianza kutumika mwaka wa 2022, bado mara nyingi hulipwa na watu wa ukoo wanaotamani kuwaachilia wapendwa wao.

    Sheria ina adhabu ya kifungo jela cha takribani miaka 15 kwa yeyote atakayelipa fidia, ingawa hakuna mtu ambaye amehukumiwa.

  3. Mamlaka zateketeza ekari zaidi ya 1000 za bangi Tanzania,

    Mamlaka nchini Tanzania zimeteketeza ekari 1,165 za mashamba ya bangi na kukamata kilogramu 102 za mbegu za bangi mkoani Morogoro, mashariki mwa nchi hiyo.

    Aidha, katika operesheni maalum kwenye mkoa huo, mamlaka iliwakamata watu sita waliokuwa na kilogramu 342 za bangi.

    Akizungumza leo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo amesema mashamba ya bangi yaliyoteketezwa yamelimwa kwenye eneo la akiba la hifadhi ya Taifa Mikumi.

    Kamishna huyo alisema, “Uharibifu mkubwa sana wa mazingira umefanyika katika eneo hili ambapo miti imekatwa ili kupata eneo la kulima bangi na hivyo kuharibu uoto wa asili…

    “Pia uharibifu uliofanyika katika eneo la akiba la Mikumi unaharibu ikolojia ya eneo hilo na kufanya uharibifu mkubwa wa uoto wa asili na ikizingatiwa mito hiyo inatiririsha maji katika bwawa la Mwalimu Nyerere linalotegemewa kwa uzalishaji wa umeme,” alisema Lyimo.

    Lyimo pia amewaomba wananchi wa mkoa wa Morogoro na mikoa mingine kushirikiana na Mamlaka kupiga vita kilimo cha bangi na aina nyingne za dawa za kulevya.

    Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 2022 iliandaliwa na DCEA ilitaja Morogoro, Arusha, Iringa, Ruvuma, Manyara na Mara kuongoza kwa kilimo cha bangi.

  4. Walimu kutofundisha bila shahada Uganda

    Zaidi ya walimu laki moja nchini Uganda wanafundisha shule za chekechea na msingi baada ya kufuzu kwa kiwango cha cheti cha Daraja la tatu.

    Lakini katika miaka michache ijayo, huenda wakapoteza ajira hiyo iwapo hawatahitimu kwa kiwango cha shahada ya ualimu kama inavyopendekezwa katika muswada wa walimu wa mwaka 2024.

    Muswada wa kitaifa wa walimu wa mwaka 2024 nchini Uganda, unawataka walimu wote nchini humo kuwa na shahada ya ualimu ifikapo 2030.

    Waziri wa Elimu ya kiwango cha juu nchini humo, John Chrysestom Muyingo tayari amewasilisha muswada huo bungeni.

    Pia unapendekeza kuundwa kwa Baraza la kitaifa la walimu ambalo litatoa leseni kwa walimu kufundisha darasani.

    Lakini baadhi ya wadau katika sekta ya elimu, wameutilia mashaka muswada huo na kuulaumu “kukandamiza” walimu.

    “Sioni kwamba mwalimu kufundisha chekechea, inahitaji uelewa wa shahada , wanao kusudia kuleta huo muswada si kwa nia ya kuendeleza elimu, bali ni kuendelea kumkandamiza mwalimu amesema Daktari Levy Masereka, mwalimu wa muda mrefu na mwanazuoni kutoka Chuo kikuu cha Makerere, huku akiongeza kwamba, tuangalie mshahara anaopata (mwalimu) ni kiduchu.”

    Lakini serikali kwa upande wake inasema unalenga kuleta ufanisi pamoja na kuboresha taaluma ya ualimu nchini humo.

    Katika mahojiano na BBC, Daktari Dennis Mugimba ametupilia mbali wasi wasi kuwa huenda muswada huo ukasababisha uhaba wa walimu nchini humo.

  5. Ujerumani kuchangia dozi 100,000 za chanjo ya mpox kudhibiti mlipuko barani Afrika

    Ujerumani itatoa dozi 100,000 za chanjo ya mpox kutoka kwa hisa zake za kijeshi kusaidia kudhibiti mlipuko katika bara la Afrika katika kipindi cha muda mfupi na pia kutoa msaada kwa nchi zilizoathiriwa, msemaji wa serikali alisema Jumatatu, Reuters imeripoti.

    Serikali italipatia Shirika la Afya Duniani rasilimali za kifedha kupitia vyombo mbalimbali vya kupambana na mpox na pia kusaidia washirika wake barani Afrika kupitia muungano wa chanjo ya GAVI, aliongeza msemaji huyo.

    Ujerumani ina dozi takribani 117,000 za Jynneos, ambazo zinahifadhiwa na jeshi la Ujerumani baada ya Berlin kuinunua mnamo 2022.

    Shirika la Afya Duniani limetangaza mpox kuwa dharura ya afya ya umma duniani baada ya mlipuko katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuenea katika nchi jirani na aina mpya ya virusi, clade Ib, ilisababisha wasiwasi kuhusu kasi ya maambukizi.

    Serikali ilikuwa inaangalia njia ya haraka zaidi ya kupata chanjo hizo kwa nchi zilizoathirika, hasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, lakini pia Burundi na nchi jirani za Afrika Mashariki, kulingana na msemaji wa wizara ya mambo ya nje.

    Unaweza pia kusoma;

  6. Habari za hivi punde, Shambulio la Urusi nchini Ukraine: Tunachojua kufikia sasa

    Maelezo bado yanaibuka kuhusu shambulio la anga la usiku la Urusi dhidi ya Ukraine, lakini haya ndiyo tunayojua kufikia sasa:

    • Takriban watu sita wameuawa katika mikoa mingi, viongozi wa eneo hilo wanasemaRais Zelensky anasema kuwa zaidi ya makombora 100 na takriban drones 100 zilitumika
    • Jeshi la Urusi lilithibitisha shambulio hilo lililenga miundombinu ya nishati na "silaha za usahihi wa hali ya juu" zilitumwa
    • Ukosefu wa umeme umeripotiwa katika miji kote Ukraine na kampuni ya nishati inayoendeshwa na serikali imepunguza nguvu ili kuleta utulivu wa gridi ya taifa.
    • Katika mji mkuu wa Kyiv wakazi walilazimishwa kukaa katika vituo vya metro
  7. Meneja wa zamani wa England Sven-Goran Eriksson aaga dunia

    Aliyekuwa wakati mmoja meneja wa timu ya soka ya England Sven-Goran Eriksson amefariki akiwa na umri wa miaka 76.

    Eriksson, meneja wa kwanza ambaye si Mwingereza katika timu ya England, aliiongoza Three Lions hadi robo fainali katika michuano mitatu mikuu katika kipindi chake cha miaka mitano kama kocha kati ya 2001 na 2006.

    Mwezi Januari Eriksson alisema alikuwa na "kama mwaka" wa kuishi baada ya kugunduliwa na saratani.

    Familia yake ilisema Jumatatu: "Sven-Goran Eriksson ameaga dunia. Baada ya kuugua kwa muda mrefu, SGE alikufa asubuhi nyumbani akiwa amezungukwa na familia."

    Raia huyo wa Sweden aliongoza vilabu 12, vikiwemo Manchester City, Leicester, Roma na Lazio, na kushinda mataji 18.

    Eriksson pia aliwahi kuinoa Mexico, Ivory Coast na Ufilipino.

    Baada ya kustaafu kama mchezaji akiwa na umri wa miaka 27, Eriksson alianza kazi yake ya ukocha na Degerfors mwaka 1977 kabla ya kujiunga na timu ya Uswidi ya Gothenburg, ambapo alishinda taji la Uswidi, vikombe viwili vya Uswidi na Kombe la Uefa la 1982.

    Kisha aliendelea kufurahia vipindi viwili akiwa na wababe wa Ureno Benfica pamoja na kusimamia vilabu vya Italia Roma, Fiorentina, Sampdoria na Lazio - ambapo alishinda mataji saba likiwemo taji la Serie A, Vikombe viwili vya Italia na Kombe la Washindi wa Kombe la Ulaya.

    Baada ya kugunduliwa na maradhi hayo Eriksson alitumia mwaka mzima kutembelea baadhi ya vilabu vyake vya zamani, ikiwa ni pamoja na Lazio na Sampdoria.

    Mnamo mwezi Machi Msweden huyo, shabiki wa muda mrefu wa Liverpool, alisaidia kuongoza timu ya Liverpool Legends ambayo iliishinda timu ya Ajax Legends 4-2 katika uwanja wa Anfield.

    Alitoa ujumbe mzito mwishoni mwa filamu yake mpya ya hali halisi 'Sven', ambayo ilitolewa mapema mwezi huu.

    Alisema: "Natumai utanikumbuka kama mtu mzuri anayejaribu kufanya kila kitu anachoweza kufanya.

    "Usisikitike, tabasamu. Asante kwa kila kitu, makocha, wachezaji, umati wa watu, imekuwa ya ajabu. Jitunze na uangalie maisha yako. Na uishi."

  8. Magonjwa yaenea Gaza wakati maji taka yakichafua kambi

    Maji kwenye sehemu za ufuo wa Mediterania wa Gaza yameanza kubadilika rangi na kuwa ya hudhurungi huku wataalamu wa afya wakionya kuhusu kuenea kwa maji taka na magonjwa katika eneo hilo.

    Picha za satelaiti, zilizochambuliwa na BBC idhaa ya Kiarabu, zinaonesha kile kinachoonekana kuwa ni utiririshaji mkubwa wa maji taka kwenye pwani ya Deir al-Balah.

    Afisa mmoja wa eneo hilo aliiambia BBC kwamba watu waliokimbia makazi yao katika kambi za karibu wanapeleka maji taka yao moja kwa moja baharini.

    "Ni kwa sababu ya ongezeko la idadi ya watu waliokimbia makazi yao na wengi wanaunganisha mabomba yao wenyewe kwenye mfumo wa mifereji ya maji ya mvua," alisema Abu Yazan Ismael Sarsour, mkuu wa kamati ya dharura ya Deir al-Balah.

    Wim Zwijnenburg, mtaalamu wa mazingira kutoka shirika la Pax for Peace, alithibitisha kuwa maji machafu yalionekana kuelekea baharini kutoka kwenye kambi za karibu zilizojaa watu, baada ya kuchunguza picha za satelaiti.

    Haijabainika ikiwa uchafuzi wa mazingira wa pwani bado unaongezeka kwani picha za hivi karibuni zaidi za satelaiti hazipatikani.

    Mashambulizi makali ya Israel yamesababisha kuporomoka kwa miundombinu ya usimamizi wa maji taka Gaza, ripoti ya mazingira ya Umoja wa Mataifa ilihitimishwa mwezi Juni.

    Chombo cha wizara ya ulinzi ya Israel kinachosimamia sera za maeneo ya Palestina, Cogat, kiliiambia BBC Kiarabu kwamba kikosi kazi kilichojitolea cha kibinadamu kimechukua hatua kuboresha mfumo wa maji taka huko Gaza.

    Katika miezi ya hivi karibuni, Cogat iliratibu urejeshaji wa visima vya maji na vifaa vya kuondoa chumvi, pamoja na upanuzi wa mabomba ya maji huko Gaza, kulingana na taarifa yake.

    Unaweza kusoma;

  9. Shughuli za uokoaji zaendelea Sudan baada ya watu takribani 60 kupoteza maisha baada ya bwawa kupasuka

    Shughuli za uokoaji zinaendelea mashariki mwa Sudan baada ya kuporomoka kwa bwawa na kuua takribani watu sitini.

    Maji ya mafuriko yalisomba karibu mashamba na vijiji kumi na vitano chini ya mto na mamlaka inahofia idadi ya wathiriwa inaweza kuongezeka.

    Bwawa hilo katika jimbo la Bahari ya Shamu lilisambaza maji kwa Bandari ya Sudan, ambako ni makazi ya serikali ya kijeshi.

    Kuna hofu kuwa jiji hilo linaweza kukumbwa na uhaba wa maji.

    Vyombo vya habari vya ndani pia vinaripoti kuwa mvua hiyo kubwa imeharibu kebo ya fibre optic, na hivyo kuzuia mawasiliano kote Sudan.

    Zaidi ya raia 100 wa Sudan wamefariki katika mafuriko ya hivi karibuni.

  10. Zaidi ya makombora 100 na droni zilitumika katika mashambulizi - Zelensky

    Rais wa Ukraine Volodymr Zelensky amesema hivi punde kuwa zaidi ya makombora 100 na takribani ndege 100 za mashambulizi zilirushwa na Urusi usiku kucha.

    Anasema kuwa lengo kuu lilikuwa "miundombinu muhimu ya kiraia" katika mikoa mingi ya Ukraine, akitoa mfano wa mashambulizi dhidi ya Kharkiv, Kyiv, Odesa na maeneo ya magharibi.

    Katika chapisho kwenye Telegram, Zelensky anaongeza kuwa kumekuwa na uharibifu mkubwa wa vifaa vya nishati, lakini anasema kazi ya ukarabati inaendelea na wafanyakazi "watafanya kazi ya ukarabati saa nzima".

    Anaendelea kutoa wito kwa washirika wa Magharibi kuiruhusu Ukraine kutumia silaha za masafa marefu na kuwaruhusu kupiga maeneo nchini Urusi ambayo mashambulizi yanaanzishwa.

    Unaweza kusoma;

  11. Watatu wauawa wakati Urusi ikifanya mashambulizi makubwa ya anga kote Ukraine

    Tunaweza kukuletea habari za hivi punde asubuhi ya leo wakati Urusi ikifanya mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya Ukraine.

    Msururu wa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora yalianza kote nchini usiku wa Jumatatu.

    Milipuko ilitanda katika miji kadhaa katika mikoa 15 kulingana na Waziri Mkuu wa Ukraine Maafisa wa mkoa wanasema takribani watu watatu wameuawa nchi nzima iko chini ya tahadhari ya uvamizi wa anga.

    Tumeshuhudia kukatika kwa umeme huku mashambulizi ya Urusi yakilenga miundombinu ya nishati na maji.

    Wakazi wa Kyiv wanatafuta makazi katika vituo vya treni .

    Jirani wa Ukraine, Poland, anasema kuwa jeshi lake la anga limeanzishwa kwa sababu mashambulizi yamekaribia anga ya Poland.

    Tunasikia kwamba Ukraine imekabiliana na mashambulizi ya ndege yake isiyo na rubani lakini kwa kiwango kidogo zaidi.

  12. 22 wauawa baada ya vitambulisho vyao kukaguliwa Pakistan

    Watu wenye silaha wamewaua takriban watu 22 kusini-magharibi mwa Pakistan baada ya kuwatoa kwenye magari yao kwa nguvu na kuangalia utambulisho wao, maafisa wanasema.

    Shambulio hilo lilitokea usiku wa kuamkia leo kwenye barabara kuu ya mkoa wa Balochistan, ambapo vikosi vya usalama vinapambana na ghasia za kidini, kikabila na wanaotaka kujitenga.

    Watu hao waliokuwa na silaha walikagua hati za utambulisho, wakiripotiwa kuwatenga wale kutoka Punjab ili wapigwe risasi, kabla ya kuwasha moto magari, maafisa walidai.

    Kundi la wapiganaji wa Baloch Liberation Army (BLA) limedai kuhusika na mashambulizi hayo katika wilaya ya Musa Khel.

    "Idadi ya wanamgambo hao ilikuwa kati ya 30 hadi 40. Walisimamisha magari 22," alisema Najibullah Kakar, afisa mkuu wa eneo hilo, ameliambia shirika la habari la AFP.

    "Magari yaliyokuwa yakisafiri kwenda na kurudi Punjab yalikaguliwa, na watu kutoka Punjab walitambuliwa na kupigwa risasi."

    BLA imesema ilikuwa inalenga wanajeshi wanaosafiri wakiwa wamevalia kiraia, kulingana na shirika la habari la Reuters.

    Waziri Mkuu Shehbaz Sharif "alihuzunishwa sana" na tukio hilo na "kulaani shambulio hilo la kigaidi" katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake.

    Balochistan ni jimbo kubwa zaidi la Pakistani lakini, ingawa lina rasilimali nyingi kuliko majimbo mengine, ndilo lenye maendeleo duni.

  13. Urusi yafanya shambulizi la ndege zisizo na rubani kwenye mji mkuu wa Ukraine

    Ukraine na Urusi zilikabiliana kwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani Jumatatu asubuhi.

    Serhiy Popko, mkuu wa utawala wa kijeshi huko Kyiv, alisema kwenye jukwa la Telegram kwamba hadi ndege zisizo na rubani 10 ziliharibiwa zilipokaribia mji, katika eneo karibu na Kyiv.

    Utawala wa kijeshi katika eneo la mji mkuu ulieleza kuwa mifumo ya ulinzi wa anga ya Ukraine katika eneo hilo ilishiriki katika kuzima shambulio hilo, baada ya "kugundua mienendo ya ndege zisizo na rubani za adui."

    Walioshuhudia waliripoti kusikia milipuko karibu na Kyiv siku ya Jumatatu wakati mifumo ya ulinzi ya anga ya Ukraine ikionekana kuzima shambulio la angani, Reuters iliripoti.

    Kwa upande wa Urusi, Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema Jumatatu kwamba mifumo ya ulinzi wa anga ya Urusi iliharibu ndege 20 zisizo na rubani zilizorushwa na Ukraine dhidi ya nchi hiyo usiku kucha.

    Ndege tisa zisizo na rubani ziliharibiwa katika eneo la Saratov, tatu katika eneo la Kursk, na mbili katika maeneo ya Belgorod, Bryansk na Tula, wizara hiyo ilisema kwenye mtandao wa Telegram.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Australia: Sheria ya kutowaadhibu wanaokataa kupokea simu baada ya kazi yaanza kutekelezwa

    Nchini Australia, sheria ya kutowaadhibu wafanyakazi wanaokataa kupokea simu baada ya saa za kazi kumalizika imeanza kutekelezwa.

    Hatua hii imetoa fursa kwa watu wanaohisi kulazimishwa kupokea simu au kusoma ujumbe kutoka kwa waajiri wao baada ya kumaliza kazi ya siku.

    Sheria hiyo mpya inaruhusu wafanyikazi kupuuza mawasiliano baada ya saa za kazi ikiwa wataamua kufanya hivyo, bila kuogopa kuadhibiwa na wakubwa wao.

    Zaidi ya nchi 20, haswa za Ulaya na Amerika Kusini, zina sheria sawa na hiyo.

    Sheria hiyo haikatazi waajiri kuwasiliana na wafanyikazi baada ya saa za kazi, badala yake, inawapa wafanyikazi haki ya kutojibu isipokuwa kukataa kwao kuwe kutazingatiwa kuwa hakuna sababu ya kufanya hivyo.

  15. Kenya: Miungano ya kutetea maslahi ya walimu yatofautiana kuhusu mgomo

    Shule zimefunguliwa nchini Kenya kwa muhula wa tatu huku kukiwa na mkanganyiko kati ya Muungano wa walimu wa Shule za Msingi KNUT na Muungano wa walimu wa Shule za Sekondari KUPPET.

    Miungano hiyo ya kutetea maslahi ya walimu, awali ilikuwa imetangaza kuanza rasmi kwa mgomo hii leo wakati shule za zinafunguliwa.

    Lakini jana jioni, muungano wa KNUT ulitangaza kusitisha mgomo wa waalimu ukionyesha nia ya kutoa fursa kwa Tume ya Walimu nchini Kenya – TSC kutimiza ahadi zake.

    Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu wa KNUT, Collins Oyuu alitangaza kuwa malalamishi ya walimu yanashughulikiwa kiutawala.

    Hata hivyo, Muungano wa Walimu wa Shule za Sekondari KUPPET, ulitangaza kuendelea na mgomo wao na kusema kwamba hakuna aliyewasiliana nao kusikiliza matakwa yao.

    Tume ya chama cha walimu TSC, ilijitetea kwa kusema kuwa tayari imeanza kushughulikiwa baadhi ya matakwa ya walimu na kuwasihi kufika shuleni kama ilivyopangwa.

    Baadhi ya wanayotaka yaangaziwe ni pamoja na kuchelewesha waalimu kupandishwa vyeo, walimu tarajali kupewa kazi za kudumu, mazingira mabaya ya kufanyia kazi na mengineo.

  16. Mwanamume mzee zaidi duniani: 'Sina siri ya kipekee ya kuishi miaka mingi'

    Mwanamume mwenye umri mkubwa zaidi duniani ametangaza kuwa hana "siri ya kipekee" kueleza kuhusu kuishi kwake miaka mingi alipokuwa akisherehekea kutimiza miaka 112.

    John Tinniswood, ambaye alizaliwa Liverpool tarehe 26 Agosti 1912, aliiambia Guinness World Records "hakujua kabisa" kwa nini ameishi miaka mingi namna hiyo.

    Mwanamume huyo ambaye anaishi katika nyumba ya kutunza wazee huko Southport, alikua mwanamume mzee zaidi duniani mnamo mwezi Aprili wakati Juan Vicente Pérez Mora wa miaka 114 alipofariki dunia.

    Alisema alikuwa "mchangamfu sana wakati wa ujana wake" na "alitembea kweli kweli", lakini aliamini "hakuwa tofauti" na mtu mwingine yeyote, akiongeza kuwa: "Kuishi miaka mingi au michache, ni kitu ambacho huna uwezo nacho."

    Bw Tinniswood, ambaye alizaliwa mwaka ambapo meli ya Titanic ilizama, alisema anatimiza miaka 112 "akiwa na matumaini ya kipekee".

    "Kwa nini nimeishi miaka mingi hivyo, sijui hata kidogo," alisema. "Siwezi kufikiria siri yoyote ya kipekee niliyo nayo.

    "Nilikuwa na shughuli nyingi kama kijana, nilitembea sana ... Ikiwa hilo lilikuwa na uhusiano wowote na umri mrefu, sijui.

    "Lakini kwangu, sio tofauti. Hakuna cha upekee hata kidogo."

    Bw Tinniswood alizaliwa miaka 20 baada ya klabu yake ya kandanda anayoipenda zaidi ya Liverpool kuanzishwa.

    Alikuwa na miaka miwili wakati Vita vya Kwanza vya Dunia vinaanza na alikuwa ametoka tu kusherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 27 Vita vya Pili vya Dunia vilipoanza.

    Pia unaweza kusoma:

  17. Mkurugenzi Mtendaji aliyekamatwa hana 'chochote cha kuficha' - Telegram

    Programu ya kutuma ujumbe Telegram imesema Mkurugenzi Mtendaji wake Pavel Durov, ambaye alikamatwa nchini Ufaransa siku ya Jumamosi, "hana cha kuficha".

    Bw Durov alikamatwa katika uwanja wa ndege kaskazini mwa Paris chini ya kibali cha makosa yanayohusiana na programu hiyo, kulingana na maafisa.

    Uchunguzi huo unaripotiwa kuhusu ukosefu wa kuzuia misimamo mikali zaidi, huku Bw Durov akishutumiwa kwa kukosa kuchukua hatua za kuzuia uhalifu kwenye programu hiyo.

    Programu hiyo inashutumiwa kwa kushindwa kushirikiana na vyombo vya sheria kuhusu ulanguzi wa dawa za kulevya, maudhui ya ngono ya watoto na ulaghai.

    Telegram ilisema katika taarifa kwamba "usimamizi wake uko ndani ya viwango vya tasnia na uboreshaji kila wakati".

    "Ni upuuzi kudai kwamba jukwaa au mmiliki wake anawajibika kwa matumizi mabaya ya jukwaa hilo," programu hiyo ilisema.

    Telegram iliongeza kuwa Bw Durov husafiri Ulaya mara kwa mara na kuongeza kuwa anafuata sheria za Umoja wa Ulaya, ikiwa ni pamoja na Sheria ya Huduma za Kidijitali, ambayo inalenga kuhakikisha mazingira salama na ya kuwajibika mtandaoni.

    "Takriban watumiaji bilioni moja duniani kote hutumia Telegramu kama njia ya mawasiliano na kama chanzo cha habari muhimu," taarifa ya programu hiyo iliandika.

    "Tunasubiri utatuzi wa haraka wa hali hii. Telegram iko pamoja nanyi nyote."

    Pia unaweza kusoma:

  18. Muingereza auawa katika shambulizi la kombora nchini Ukraine

    Raia wa Uingereza ambaye alikuwa akifanya kazi mashariki mwa Ukraine kama sehemu ya timu ya habari ya Reuters aliuawa katika shambulio la kombora kwenye hoteli siku ya Jumamosi, shirika hilo limethibitisha.

    Mshauri wa masuala ya usalama Ryan Evans alikuwa mmoja wa wafanyakazi sita wa Reuters waliokuwa wakiishi katika Hoteli ya Sapphire katika jiji la Kramatorsk - ambayo iko chini ya udhibiti wa Ukraine lakini karibu na vita – wakati iliposhambuliwa.

    Mamlaka ya Ukraine ilisema hoteli hiyo ilishambuliwa na kombora la Urusi. Hata hivyo, Urusi haijatoa maoni.

    Katika taarifa, msemaji wa Reuters alisema shirika hilo linakabiliana na "mfadhaika" baada ya kufahamu kuhusu kifo cha Bw Evans.

    "Tunatafuta taarifa zaidi kuhusu shambulio hilo, ikiwa ni pamoja na kushirikiana na mamlaka huko Kramatorsk, na tunasaidia wenzetu na familia zao," lilisema.

    "Tunatuma rambirambi zetu kwa familia na wapendwa wa Ryan. Ryan amesaidia waandishi wetu wengi kuandika matukio kote ulimwenguni; tutakosa uwepo wako."

    Liliongeza kuwa wengine wawili wa timu hiyo wamelazwa hospitalini kutokana na shambulizi hilo na kwamba mmoja wao amelazwa kwa majeraha mabaya.

    Soma zaidi:

  19. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya kila siku ikiwa ni tarehe 26/08/2024