Tunachojua kufikia sasa kuhusu shambulio la Marekani katika harusi huko Sirik Iran?
Saa moja baada ya kuanza kwa mashambulio ya anga ya Marekani dhidi ya maeneo ya kusini mwa Iran ambayo kwa mujibu wa CENTCOM yalilenga vituo na silaha za Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi, vyombo vya habari nchini Iran viliripoti kuwa sherehe ya harusi katika bandari ya Koh-e-Sirak ililengwa, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua watano, akiwemo mtoto mmoja, na majeraha kwa watu wengine wasiopungua 68.
Vyombo vya habari ndani ya Iran, ikiwemo Shirika la Utangazaji la Iran, vilichapisha picha zilizodaiwa kuwa za eneo la shambulio hilo.
Kuhusiana na hayo, chanzo cha habari cha eneo hilo kililiambia BBC Persian kuwa kinaamini lengo la shambulio hilo la anga lilikuwa "mnara wa mawasiliano" uliopo "mita chache kutoka nyumba iliyofanyika harusi hiyo."
Chanzo hicho cha eneo hilo kililiambia BBC Persian kuwa kwa sasa kuna "uhitaji mkubwa wa michango ya damu" na kwamba barabara zinazoelekea eneo lililoshambuliwa zimefungwa.
Wakati huo huo, Kapteni Tim Hawkins, msemaji wa CENTCOM, alijibu swali kutoka BBC Persian kwa kusema kuwa Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) "inafahamu" ripoti zinazohusu tukio hili na kusisitiza kuwa "vikosi vya Marekani havilengi kamwe raia katika mashambulio yao."