Trump: Sijaribu kuileta Iran kwenye meza ya mazungumzo

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Rais wa Marekani Donald Trump, katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social usiku wa Jumanne, alikanusha ripoti ya ABC News kwamba utawala wake ulikuwa ukijaribu kuilazimisha Iran kufanya mazungumzo, akisema hajali kuhusu kufikia makubaliano na Tehran.
"Kinyume na kile ambacho ABC ambayo (yeye huiita) Habari za Uongo imeiripoti, sijaribu kuileta Iran kwenye meza ya mazungumzo. Sijali hata kidogo kama watatia saini makubaliano ambayo hayana thamani kwao," Bw. Trump aliandika.
"Napendelea zaidi hali ya sasa, ambapo tuna udhibiti karibu kamili wa Mlango-Bahari wa Hormuz na uchumi wa Iran unaporomoka kabisa. Wanachelewesha tu mchakato ambao hauepukiki," aliongeza.
Rais wa Marekani aliandika mwishoni mwa ujumbe huu: "Ni lini watu wa Iran watainuka na kupambana?"
Kauli hizi zilitolewa saa chache baada ya Trump kuelezea mashambulizi mapya ya Marekani dhidi ya maeneo karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz kuwa ya "haki" na kuonya kwamba Washington ingefanya mashambulizi makali zaidi iwapo Iran ingechukua hatua yoyote ya kulipiza kisasi.
Iran inasema mashambulizi hayo yalilenga raia katika sherehe ya harusi katika kijiji cha Kohstak Sirik, na kuua angalau watu watano, akiwemo mtoto mmoja. Vyombo vya habari vya Iran vinaripoti kuwa zaidi ya watu 60 walijeruhiwa katika tukio hilo.


