Uingereza yaunga mkono mpango wa haki za binadamu unaolenga kuondolewa kwa wahamiaji haramu
Uingereza pamoja na mataifa mengine ya Ulaya yamesaini tamko muhimu linalotaka mahakama kutathmini upya namna zinavyotoa maamuzi kuhusu kesi za uhamiaji, katika juhudi za kurahisisha kuwafukuza wahamiaji haramu.
Makubaliano hayo, yaliyotangazwa katika mkutano uliofanyika Moldova siku ya Ijumaa, yanaonya kuwa demokrasia ya Ulaya inaweza kudhoofishwa ikiwa nchi hazitaweza kukabiliana kwa ufanisi zaidi na usafirishaji haramu wa watu pamoja na shinikizo la kisasa la uhamiaji.
Tamko hilo linataka nchi wanachama kuachiwa mamlaka makubwa zaidi katika kushughulikia kesi za uhamiaji.
Akizungumza kabla ya mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Yvette Cooper, alieleza makubaliano hayo kuwa ni “mbinu ya busara” na kusema anataka kuhakikisha mifumo hiyo “haitumiwi vibaya kwa njia isiyo ya haki.”
Tamko hilo jipya si mabadiliko rasmi ya sheria za haki za binadamu, jambo ambalo linaweza kuchukua miaka mingi, bali ni ishara ya kisiasa kutoka kwa nchi zote wanachama kwenda kwa majaji wa haki za binadamu kwamba wanapaswa kuzingatia zaidi maslahi ya umma na demokrasia wanapotoa maamuzi kuhusu kesi za uhamiaji.
Tamko hilo limesainiwa na wanachama wote 46 wa chombo cha kisiasa kinachosimamia mahakama ya haki za binadamu na ambacho ni tofauti kabisa na Umoja wa Ulaya.
Waraka huo unasema kuwa changamoto zinazozikabili nchi za Ulaya zimebadilika kwa kiwango kikubwa au hazikutarajiwa wakati mkataba wa haki za binadamu ulipoandaliwa.