Tanzania: 77 waliokolewa katika jengo la Kariakoo lililoporomoka huku idadi ya waliofariki ikisalia kuwa watu 5

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga, amethibitisha kuwa bado kuna watu wamekwama chini ya vifusi vya jengo lililoporomoka Kariakoo, mawasiliano na watu hao yanaendelea

Moja kwa moja

Na Yusuf Jumah

  1. Shukran na Kwaheri

    Na hadi hapo tumefika mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja leo hii.

    Kumbuka sasa unaweza kujiunga na Chaneli yetu ya Whatsapp kwa habari na makala ya kuvutia-Bofya hapa ili kujiunga

    Tukutane kesho alfajiri

  2. Viongozi wa Poland na Ujerumani wazungumza baada ya Urusi kutekeleza mashambulio makali dhidi ya Ukraine

    TH

    Chanzo cha picha, EPA

    Diplomasia ya simu haiwezi kuchukua nafasi ya "msaada wa kweli" kwa Ukraine, Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk anasema.

    Akichapisha kwenye mitandao ya kijamii, anasema: "Hakuna mtu atakayemzuia Putin kwa simu. Shambulio la jana usiku, mojawapo ya makubwa zaidi katika vita hivi, limethibitisha kwamba diplomasia ya simu haiwezi kuchukua nafasi ya msaada wa kweli kutoka nchi za Magharibi kwa Ukraine.

    "Wiki zijazo zitakuwa za maamuzi, sio tu kwa vita vyenyewe, lakini pia kwa mustakabali wetu."

    Viongozi wa nchi nyingine katika eneo hilo pia wamejibu shambulio hilo, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Romania, Luminita Odobescu akisema: "Hili ni jaribio la kijinga na la kudharauliwa la kuitupa Ukraine kwenye baridi na giza mwanzoni mwa msimu wa baridi."

    Rais wa Moldova, Maia Sandu, pia alilaani mashambulio ya Urusi, akisema: "Kutumia silaha wakati wa baridi ili kufungia taifa kwenye uoga i ni ukatili na haukubaliki. Moldova inasimama na Ukraine."

    Kansela wa Ujerumani asema Ukraine inaweza 'kututegemea' baada ya simu yake na Putin kukosa kupunguza makali ya vita

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz anasema Ukraine "inaweza kututegemea" na mazungumzo yoyote ya simu na Urusi yatahitaji idhini ya Ukraine.

    Scholz, akizungumza katika uwanja wa ndege wa Berlin kabla ya kuelekea kwenye mkutano wa G20 nchini Brazil, anasema "hakuna uamuzi utakaochukuliwa bila mchango wa Ukraine".

    Kiongozi huyo wa Ujerumani alikabiliwa na shutuma mapema wiki hii baada ya kumpigia simu kiongozi wa Urusi Vladimir Putin, na kumtaka " kumaliza vita vya uvamizi vya Urusi dhidi ya Ukraine na kuwaondoa wanajeshi wake".

    Hatua hiyo ilikosolewa na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ambaye alisema wito huo ulikuwa "sanduku la Pandora" na kusema kuwa ulidhoofisha kutengwa kwa Putin.

  3. 'Pigano la kuvunja rekodi: Familia 60m zilitazama Tyson vs Paul wakipigana, Netflix yasema

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Netflix inasema familia milioni 60 duniani kote zilitazama moja kwa mojapigano la Mike Tyson na Jake Paul, katika pambano la kwanza la mwanamasumbwi huyo kwenye ndondi za moja kwa moja.

    Tukio hilo, ambalo lilikuwa la bure kwa waliojisajili, linapongezwa na kampuni kubwa ya teknolojia kama "usiku wa kuvunja rekodi".

    Walakini, mashabiki waliotarajia kutazama wameonyesha hasira na kukatishwa tamaa baada ya baadhi ya ripoti kuwa Netflix ilipata matatizo ya kiufundi mara kwa mara katika pambano hilo.

    Lakini pia kulikuwa na ukosoaji kutoka kwa wale ambao waliweza kusikiliza, na wengi wakisema kuwa walipata mchezo huo wa ndondi haukuwa mzuri .

    Katika pambano hilo lililofanyika kwenye Uwanja wa AT&T huko Texas, bingwa wa zamani wa uzani wa juu duniani Tyson, 58, alipigwa na mpiganaji wa YouTube Paul, 27 .

    Pambano hilo lilivutia idadi kubwa ya matangazo ya vyombo vya habari. Tyson ni mmoja wa mabondia maarufu kwenye duniani, wakati Paul alivutia watazamaji wachanga.

  4. Kwa nini mbwa wa roboti wanashika doria Mar-A-Lago kwa Trump?

    th

    Chanzo cha picha, reu

    Mbwa wa roboti anayeitwa "Spot" aliyetengenezwa na kampuni ya Boston Dynamics ndiye chombo cha hivi punde zaidi katika zana Huduma ya Usalama Marekani(Secret Service)

    Kifaa hicho kimeonekana kikishika doria katika makaazi ya mapumziko la Rais Mteule Donald Trump ya Mar-a-Lago huko Palm Beach, Florida.

    Mbwa hao hawana silaha - na kila moja inaweza kudhibitiwa kwa mbali au kiotomatiki - mradi tu njia yake imepangwa mapema.

    Wapita njia wanaonywa kwa ishara kwenye kila mguu wa Spot: "DO NOT PET."

    Video ya Spot akizunguka-zunguka eneo hilo imeenea kwa kasi kwenye TikTok - ambapo maoni mbali mbali yametolewa na watu huku wengine wakiingiza mzaha . Lakini dhamira yake si jambo la mzaha.

    "Kumlinda rais mteule ni jambo la kwanza," alisema Anthony Guglielmi, mkuu wa mawasiliano wa Huduma ya Usalama ya Marekani, katika taarifa yake kwa BBC.

    Katika miezi kadhaa kabla ya uchaguzi wa rais wa Marekani, Trump alikuwa mlengwa wa majaribio mawili ya kumuua. Ya kwanza ilifanyika katika mkutano wa Pennsylvania na jingine lilifanyika katika uwanja wa gofu wa Mar-a-Lago mnamo Septemba.

    Boston Dynamics pia ilikataa kujibu maswali mahususi, ingawa ilithibitisha Huduma ya Usalama ilikuwa ikitumia roboti yake ya Spot.

  5. Urusi yafanya mashambulizi 'makubwa' dhidi ya miundombinu ya Ukraine na kuua takribani watu 10

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Shambulio "kubwa" la kombora na ndege zisizo na rubani la Urusi limelenga miundombinu ya umeme kote Ukraine, Rais wa nchi hiyo Volodymyr Zelensky amesema.

    Takriban watu 10 waliuawa katika mashamabulio hayo ambayo yalilenga mji mkuu wa Kyiv, pamoja na maeneo kadhaa katika mikoa mbali mbali ikiwa ni pamoja na Donetsk, Lviv na Odesa.

    Kampuni kubwa ya kibinafsi ya kawi ya Ukraine, DTEK, ilisema mtambo wake wa nishati ya joto ulipata "uharibifu mkubwa", na kusababisha kukatika kwa dharura kwa umeme.

    Ni shambulio kubwa zaidilililofanyika tangu mapema Septemba, kulingana na mamlaka na vyombo vya habari vya ndani.

    Wanawake wengine wawili waliuawa katika eneo la Mykolaiv huku sita wakiwemo watoto wawili wakijeruhiwa.

    Gavana wa eneo la Mykolaiv Vitaliy Kim anasema ndege zisizo na rubani zilishambulia kwa "mawimbi kadhaa" mapema Jumapili.

    Majengo ya makazi, ghorofa ya juu, magari, kituo cha ununuzi, na miundombinu viliharibiwa, na moto ukazuka’.

    Wafanyakazi wawili wa reli waliuawa baada ya mashambulizi ya anga ya Urusi kwenye vituo vya reli na reli katika eneo la kati la Dnipropetrovsk nchini Ukraine, kulingana na shirika la kitaifa la safari za reli.

    Katika chapisho kwenye X, Shirika la Reli la Ukraine linasema wanaume wawili walikufa na wengine watatu walijeruhiwa kutokana na "kushambuliwa kwa makombora kwa njia ya reli".

    Watu wawili wamefariki na mvulana mwenye umri wa miaka 17 amejeruhiwa katika eneo la Odesa, mkuu wa eneo hilo amesema.

    Oleh Kiper pia anasema kazi inaendelea kurejesha nguvu na maji katika eneo la kusini mwa Ukraine.

    Usafishaji unaendelea huko Kyiv baada ya shambulio la usiku

    Picha mpya kutoka Kyiv zinaonyesha mamlaka za eneo hilo zikisafisha uchafu baada ya mashambulizi ya anga ya Urusi kupiga mji mkuu wa Ukraine.

    Mapema leo asubuhi, wafanyikazi walitumia mashine nzito kuondoa sehemu za makombora ya Urusi kutoka kwa jengo la ghorofa.

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Unaweza pia kusoma

  6. Trump, Musk na wateule wapya wa baraza la mawaziri washerehekea katika UFC

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Donald Trump alipokelewa vyema aliposherehekea ushindi wake katika uchaguzi kwenye mashindano ya Ultimate Fighting Championship (UFC) mjini New York pamoja na Elon Musk na baadhi ya wateule wake katika baraza la mawaziri.

    Trump aliingia uwanjani kwa muziki mkali na shangwe kutoka kwa umati wa UFC 309 katika Maddison Square Garden.

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Alitumia muda mwingi wa usiku kukaa kati ya Rais wa UFC Dana White na Mkurugenzi Mtendaji wa Tesla Musk.

    Wateule wawili wakuu wa baraza la mawaziri la Trump, Robert F Kennedy Jr na Tulsi Gabbard, pamoja na Vivek Ramaswamy, ambaye ataongoza "Idara ya Ufanisi ya Serikali" ya Trump na Musk, pia walikuwa kwenye umati.

    Trump alimsalimia mtangazaji wa podikasti na mtangazaji wa UFC Joe Rogan kwa uchangamfu.Ni mtangazaji huyo ambaye aliidhinisha rais mteule baada ya kuonekana kwenye kipindi chake kabla ya uchaguzi.

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Trump aliwapungia mkono mashabiki walioimba "Marekani" alipokuwa akitembea hadi jukwaani, kabla ya kushangiliwa na kucheza huku UFC ikicheza picha za kusherehekea ushindi wake dhidi ya Kamala Harris katika uchaguzi.

    Jon Jones, ambaye alihifadhi taji lake la uzito wa juu wa UFC, kisha akasherehekea kwa kuelekea kumsalimia Trump, na kumpa rais mteule taji lake.

    "Nataka kusema asante sana kwa Rais Donald Trump kwa kuwa hapa usiku wa leo," Jones alisema, akipokea kishindo kikubwa cha kushangiliwa na umati.

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Unaweza kusoma zaidi

  7. Tanzania: Saba waokolewa huku mamlaka zikithibitisha kunaswa kwa baadhi ya watu chini ya vifusi

    TH

    Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema watu saba wameokolewa leo na kupelekwa hospitali kwa ajili ya uangalizi huku akisisitiza kuwa, kazi ya uokoaji inaonesha matumaini.

    “Kutoka saa nane hadi saa tisa usiku tumekuwa tukipokea simu kutoka kwa wadau nje na maneeo haya kwamba bado kuna watu na ndugu zao ambao wanawasiliana nao wakiwa hai pale basement (chini) naomba niwape taarifa kuwa, katika watu hawa saba ambao tumewaokoa wanatoka basement hiyohiyo na miongoni mwao ndugu wamekiri kuwa walikuwa wanawasiliana nao, kwa lugha nyepesi ni ushindi ambao unaendelea kupatikana,” amesema Chalamila na kusisitiza kuwa kazi ya uokoaji halijasitishwa.Chalamila amesema hadi sasa idadi ya watu waliookolewa lililoporomoka jana Novemba 16, 2024 eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam, imefikia 77 huku waliopoteza maisha wakiwa watano.

    Huku hayo yakiriafiwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga, amethibitisha kuwa bado kuna watu wamekwama chini ya vifusi vya jengo lililoporomoka Kariakoo, mawasiliano na watu hao yanaendelea na wapo katika hali nzuri huku wakiendelea kupatiwa msaada.

    Kamishna Jenerali, alisema hayo alipokuwa akitoa taarifa ya shughuli za uokoaji zinazoendelea kufuatia jengo hilo kuporomoka Kariakoo, Dar es Salaam, Jumamosi Novemba 16, 2024.

    Kwa mujibu wa Kamishna Jenerali Masunga, mawasiliano bado yanaendelea na watu ambao bado wamekwama kwenye kifusi, na wanaripotiwa hali zao zinaendelea vizuri.

    "Shughuli za uokoaji zimekuwa zikiendelea tangu jana. Kuna watu wamenaswa hapa chini, na tunawasiliana nao. Wako hai, na tumeweza kuwapa maji, glukosi, na msaada wa kihisia,” alisema.

    Aliongeza: Tuliwahakikishia kuwa timu zote za ulinzi na uokoaji ziko hapa, na tumejitolea kuhakikisha wanaokolewa salama. Tumefarijika kwa kufanikiwa kuwasilisha vitu hivi muhimu huku wakiwa wamesalia chini ya vifusi,” alisema.

    Soma pia

  8. Urusi yalenga miundo mbinu ya nishati ya Ukraine kwa shambulio kubwa la makombora

    TH

    Chanzo cha picha, Reuters

    Shambulio "kubwa" la kombora na ndege zisizo na rubani la Urusi limelenga miundombinu ya nishati kote Ukraine, waziri wa nishati wa nchi hiyo Galushchenko amesema.

    Ni shambulio kubwa zaidi kama hilo tangu mapema Septemba, na kuna ripoti za milipuko kadhaa kote Ukraine, kulingana na mamlaka na vyombo vya habari vya ndani.

    Poland, jirani ya Ukraine upande wa magharibi, ilituma ndege za kivita ili kushika doria katika anga yake kama tahadhari ya usalama, Kamandi wa jeshi la Poland ilisema.

    Katika taarifa yake kwenye mitandao ya kijamii, Bw Galushchenko alisema kuwa "shambulio kubwa dhidi ya mfumo wetu wa nishati linaendelea" na kwamba vikosi vya Urusi "vinashambulia vituo vya kuzalisha na kusambaza umeme".

    Kusini mwa Ukraine, mji wa Mykolaiv ulikuwa miongoni mwa miji iliyoathiriwa zaidi, na takriban watu wawili waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa, wakati bandari ya Bahari Nyeusi ya Odesa ilikumbwa na kukatwa kwa umeme katika jiji zima.

    Katika mji mkuu, Kyiv, vipande vya makombora na ndege zisizo na rubani vilianguka katika maeneo kadhaa, lakini hakukuwa na ripoti za majeruhi.

    Katika taarifa yake, Poland ilithibitisha kuwa operesheni za ndege za Poland na washirika zinaendelea.

    "Kutokana na mashambulizi makubwa ya Urusi, ambayo inafanya mashambulizi kwa kutumia makomboraya kawaida , makombora ya balestiki na ndege zisizo na rubani dhidi ya maeneo yaliyoko, miongoni mwa maeneo mengine, magharibi mwa Ukraine, operesheni za ndege za Poland na washirika zimeanza," ilisema.

    Unaweza pia kusoma

  9. Kiongozi wa China Xi asema atafanya kazi na Trump katika mkutano wa mwisho na Biden

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kiongozi wa China Xi Jinping ameahidi kufanya kazi na rais anayekuja wa Marekani Donald Trump katika mkutano wake wa mwisho na kiongozi wa sasa wa Marekani Joe Biden.

    Wawili hao walikutana Jumamosi kando ya mkutano wa kila mwaka wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia-Pasifiki (Apec) nchini Peru ambapo walikubali kuwepo kwa "panda shuka" katika uhusiano wa nchi zao katika kipindi cha miaka minne ya Biden.

    Lakini nchi zote mbili zilionyesha maendeleo katika kupunguza mvutano katika masuala kama vile biashara na Taiwan.

    Wachambuzi wanasema uhusiano kati ya Marekani na China unaweza kudorora zaidi Trump atakaporejea madarakani baada ya miezi miwili, kutokana na sababu zikiwemo ahadi ya kuongeza ushuru wa forodha kwa bidhaa za China.

    Rais mteule ameahidi kutoza ushuru wa asilimia 60 kwa bidhaa zote kutoka China. Pia amewateua wakosoaji mashuhuri wa China kushika nyadhifa za juu za wizara za kigeni na ulinzi.

    Katika muhula wake wa kwanza, Trump aliitaja China "mshindani wa kimkakati". Mahusiano yalizidi kuwa mabaya wakati rais wa zamani alipoita Covid "virusi vya Wachina" wakati wa janga hilo.

    Akizungumza siku ya Jumamosi kwenye mkutano huo uliofanyika katika hoteli yake mjini Lima, rais wa China alisema lengo la Beijing la kuwa na uhusiano thabiti na Washington halitabadilika.

    "China iko tayari kufanya kazi na utawala mpya wa Marekani ili kudumisha mawasiliano, kupanua ushirikiano na kudhibiti tofauti," Xi alisema.

    Biden alisema ushindani wa kimkakati kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu duniani haupaswi kuzidi kuwa vita.

    "Nchi zetu mbili haziwezi kuruhusu mashindano yoyote kati ya haya yaingie kwenye migogoro. Hilo ni jukumu letu na kwa miaka minne iliyopita nadhani tumethibitisha kuwa inawezekana kuwa na uhusiano huu," alisema.

    Unaweza pia kusoma

  10. Hujambo na karibu

    Hujambo na karibu Jumapili hii kwa matangazo yetu ya moja kwa moja.Mimi ni Yusuf Jumah nikiwa Nairobi,Kenya