Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Vikosi vya Uingereza huenda vikatumwa Gaza kusaidia kutoa misaada

Wanajeshi wa Uingereza wanaweza kutumwa huko Gaza kusaidia kutoa msaada kupitia njia mpya ya baharini, BBC imefahamishwa.

Moja kwa moja

  1. Urusi yawakamata waandishi wengine wawili - Ripoti

    Urusi imeripotiwa kuwakamata wanahabari wawili ambao wamekuwa wakifanya kazi na vyombo vya habari vya kimataifa.

    Sergei Karelin, raia wa Urusi na Israel, alizuiliwa siku ya Ijumaa, shirika la habari la Associated Press liliripoti.

    Hapo awali amefanya kazi na shirika hilo la habari. Anashutumiwa kwa vitendo vya "itikadi kali" kuhusiana na madai ya kazi katika wakfu wa kiongozi wa upinzani marehemu Alexei Navalny, mashtaka anayokanusha.

    Siku moja mapema, Konstantin Gabov aliwekwa kizuizini kwa mashtaka kama hayo.

    Bw.Gabov amefanya kazi na vyombo vya habari vya kigeni ikiwa ni pamoja na Reuters.

    Wanaume wote wawili wanakabiliwa na kifungo cha chini cha miaka miwili jela iwapo watapatikana na hatia ya "kushiriki katika shirika lenye itikadi kali".

    Hao ndio waandishi wa habari wa hivi karibuni kukabiliwa na mashtaka huku kukiwa na ukandamizaji uliokithiri nchini Urusi, ambao umeshuhudia uhuru wa vyombo vya habari kuwa mdogo. "Shirika la habari la Associated Press linasikitishwa sana na kuzuiliwa kwa mwandishi wa habari wa video wa Urusi Sergey Karelin," shirika la habari la Marekani lilisema katika taarifa yake. "Tunatafuta maelezo ya ziada."

    Bw Karelin na Bw Gabov wanatuhumiwa kusaidia kuandaa video za chaneli ya YouTube ya Bw Navalny, ambaye kwa miaka mingi alikuwa mkosoaji mkubwa wa Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa miaka mingi.

    Bw Navalny alikufa mnamo Februari katika gereza la Arctic ambapo alikuwa amefungwa.

    Mnamo 2021, mashirika yaliyohusishwa na Bw Navalny yalipigwa marufuku wakielezwa kuwa "wasimamizi wenye msimamo mkali", kumaanisha wale wanaowaunga mkono wanakabiliwa na kifungo jela.

    Mwandishi wa habari wa Forbes Russia, Sergei Mingazov, pia alikamatwa wiki hii.Anashutumiwa kwa kukosoa jeshi la Urusi.

    Mnamo 2022 Urusi ilipitisha sheria inayoweka kifungo cha hadi miaka 15 jela kwa kueneza habari "ghushi" kuhusu jeshi.

    Unaweza kusoma;

  2. Waaustralia watoa wito kwa sheria kali zaidi kuhusu unyanyasaji dhidi ya wanawake

    Maandamano yamefanyika kote Australia baada ya kuibuka wimbi la unyanyasaji wa hivi karibuni dhidi ya wanawake.

    Waandamanaji wanataka unyanyasaji wa kijinsia kutangazwa kuwa dharura ya kitaifa na sheria kali zaidi ziwekwe kukomesha.

    Waziri Mkuu Anthony Albanese alisema suala hilo ni mzozo wa kitaifa.

    Nchini Australia, mwanamke mmoja huuawa kwa wastani kila baada ya siku nne kufikia sasa.

    Mratibu Martina Ferrara alisema: "Tunataka chaguzi mbadala za kuripoti kwa waathiriwa ili kuwaruhusu kumiliki safari yao ya uponyaji na kuripoti.

    "Na tunaitaka serikali ikiri kuwa hii ni hatua ya dharura na ichukue hatua mara moja."

    Akizungumza katika maandamano katika mji mkuu Canberra yaliyohudhuriwa na maelfu ya waandamanaji, Bw Albanese alikiri serikali katika ngazi zote zinahitajika kufanya vyema zaidi.

    "Tunahitaji kubadili utamaduni, mitazamo, mfumo wa sheria na mbinu za serikali zote," alisema. "Tunapaswa kuhakikisha kuwa hii sio juu ya wanawake, ni juu ya wanaume kubadili tabia pia," aliongeza.

  3. Hamas waonesha video ya mateka wa Marekani na Israel wakiwa hai huko Gaza

    Hamas imechapisha video inayoonesha uthibitisho wa kwanza wa uhai wa mateka wengine wawili wanaoshikiliwa huko Gaza.

    Katika picha zisizo na tarehe zilizorekodiwa kwa kulazimishwa, Omri Miran anasema ameshikiliwa kwa siku 202 na Keith Siegel anataja likizo ya Pasaka ya wiki hii, akionesha vipande hivyo vya video vilivyorekodiwa hivi karibuni.

    Wote wawili walikamatwa wakati Hamas ilipoanzisha mashambulizi yake tarehe 7 Oktoba.

    Wakijibu kuhusu video hiyo, familia zao zilisema zitaendelea kupigania kurudi kwa wanaume hao. Pia waliitaka serikali ya Israel kupata mkataba mpya wa kuwaachilia mateka.

    Bw Siegel, raia wa Marekani, alitekwa nyara akiwa na mkewe Aviva, ingawa aliachiliwa mnamo Novemba wakati wa mapatano mafupi.

    Katika taarifa ya video mke wa Keith Aviva alisema: "Keith, nakupenda, tutapigana hadi utakaporudi."

    Mapema mwezi huu, aliiambia BBC jinsi wenzi hao wakati fulani walivyoachwa kwenye handaki na watekaji wao walipokuwa wakihamishwa kutoka sehemu moja hadi nyingine. Wakati wa mahojiano, alisema hakujua kama Keith bado alikuwa hai.

  4. Maelfu ya watu wajitokeza kumshawishi Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez asijiuzulu

    Maelfu ya wafuasi wa Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sánchez, wamekusanyika katika mitaa ya Madrid katika juhudi za kumshawishi asijiuzulu.

    Kiongozi huyo wa Kisoshalisti aliishangaza nchi siku ya Jumatano kwa kutangaza kuwa anaghairi shughuli zote rasmi ili kutafakari mustakabali wake.

    Alichukua uamuzi huo baada ya mahakama kufungua uchunguzi wa awali kuhusu mkewe kuhusu madai ya ufisadi. Bw Sanchez atatangaza uamuzi kuhusu mustakabali wake siku ya Jumatatu.

    Wafuasi wa kisoshalisti walisafiri kwa basi kutoka kote nchini kuhudhuria maandamano ya kumuunga mkono Bw.Sánchez nje ya makao makuu ya chama chake mjini Madrid, wakiimba "Pedro, usikate tamaa" na "Hauko peke yako".Mmoja wa wafuasi hao, Sara Dominguez, mshauri katika miaka yake ya 30, alisema anatumai serikali ya Sanchez "imechukua hatua nzuri kwa wanawake, jumuiya ya LGBT na wachache".

    Jose María Diez, afisa wa serikali mwenye umri wa miaka 44 kutoka Valladolid kaskazini mwa Uhispania, alisema kuna uwezekano wa kwamba wale wa mrengo wa kulia wanaweza kuchukua madaraka ikiwa Sanchez atang'atuka.

    "Hii itamaanisha kurudi nyuma kwa haki na uhuru wetu," alisema. Ujumbe wa serikali kuu huko Madrid ulisema kuwa watu 12,500 walishiriki katika maandamano.

  5. Vikosi vya Uingereza huenda vikatumwa Gaza kusaidia kutoa misaada

    Wanajeshi wa Uingereza wanaweza kutumwa huko Gaza kusaidia kutoa msaada kupitia njia mpya ya baharini, BBC imefahamishwa.

    Marekani imesema hakuna majeshi ya Marekani yatakayokwenda ufukweni na "mtu wa tatu" ambaye jina lake halijatajwa ataendesha malori kwenye barabara inayoelea kwenye ufuo.

    Uingereza inazingatia kuwapa wanajeshi wa Uingereza jukumu hili wakati njia za kupitisha misaada zitakapofunguliwa mwezi ujao.

    Vyanzo vya Whitehall vilisema hakuna uamuzi uliotolewa na suala hilo bado halijaifikia meza ya waziri mkuu.

    Wizara ya Ulinzi (MoD) na jeshi la Israeli walikataa kutoa maoni.

    Uingereza imekuwa ikishiriki kwa karibu katika kupanga operesheni ya usaidizi wa baharini na Waziri wa Ulinzi Grant Shapps alisema Uingereza iliendelea kuchukua "jukumu kuu katika utoaji wa msaada kwa uratibu na Marekani na washirika wengine wa kimataifa".

    Ingawa juhudi kubwa itafanywa kulinda vikosi vya washirika mbali na nchi kavu, wanajeshi wa Uingereza watakabiliwa na hatari kubwa ya kushambuliwa na Hamas na vikundi vingine vyenye silaha.

    Unaweza kusoma;