Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Jeff Bezos ampiku Elon Musk na kuwa mtu tajiri zaidi duniani

Ni mara ya kwanza kwa Bezos, 60, mwanzilishi wa kampuni ya Amazon kushika nafasi ya kwanza ya Bloomberg ya watu tajiri zaidi tangu 2021.

Moja kwa moja

Dinah Gahamanyi and Lizzy Masinga

  1. Tunakomea hapo kwa leo. Kwaheri.

  2. Vita vya Ukraine: Kyiv yasema watu saba wamefariki baada ya shambulio dhidi ya meli ya Urusi

    Idara ya ujasusi ya Ukraine inasema watu saba wameuawa na wengine sita kujeruhiwa baada ya meli ya Urusi kuzama katika shambulio la ndege zisizo na rubani baharini.

    Meli hiyo aina ya Sergei Kotov inadaiwa kushambuliwa mapema Jumanne asubuhi.

    BBC haijaweza kuthibitisha kiwango cha uharibifu kwenye meli hiyo.

    Katika chapisho la Telegram Kurugenzi Kuu ya Ujasusi ya Ukraine (HUR) ilisema wafanyakazi 52 walihamishwa.

    Sergei Kotov ni mojawapo ya meli nne za doria zilizokamilishwa kwa Project 22160 ya Jeshi la Wanamaji la Urusi.

    Meli hiyo iliwahi kushambuliwa na Ukraine mnamo Septemba mwaka jana.

    "Kwa sasa meli hii iko chini ya bahari," msemaji wa Jeshi la Wanamaji la Ukraine Dmytro Pletenchuk alisema, akiongeza kuwa helikopta inaweza kuwa ndani yake.

    Kulingana na Ukraine, meli hiyo ilishiriki katika shambulio la Kisiwa cha Nyoka katika siku ya kwanza ya uvamizi kamili wa Ukraine mnamo Februari 2022, pamoja na meli ya Moskva.

    Moskva ilizamishwa na Ukraine mnamo 2022. Urusi iliteka rasi ya Crimea kutoka Ukraine kwa njia isiyo halali karibu miaka 10 iliyopita.

    Katika miezi ya hivi karibuni Ukraine imeshambulia mara kwa mara meli za Bahari Nyeusi za Urusi zilizoko kwenye peninsula.

    Ukraine ilisema gharama ya meli iliyozama ya Sergei Kotov ilikuwa $65m (£51.2m), na kuongeza kuwa ilishambuliwa karibu na Kerch Strait, ambayo inatenganisha Crimea na Urusi.

    Video iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii inaonekana kuonyesha wakati meli hiyo iliposhambuliwa.

  3. Nyaya muhimu za mawasiliano katika Bahari ya Shamu zakatwa

    Nyaya kadhaa za mawasiliano chini ya bahari katika Bahari ya Shamu zimekatwa, na kuathiri 25% ya trafiki ya data kati ya Asia na Ulaya, kampuni ya mawasiliano ya simu na afisa wa Marekani wanasema.

    Kampuni ya HGC Global Communications yenye makao yake Hong Kong ilisema kuwa imechukua hatua za kubadilisha trafiki baada ya kebo nne kati ya 15 kukatwa hivi majuzi.

    Sababu bado haijawekwa wazi. Afisa huyo wa Marekani alisema ilikuwa ikijaribu kubaini iwapo nyaya hizo zilikatwa kimakusudi au kung'olewa na nanga.

    Mwezi uliopita, serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa ilionya kwamba waasi wa kihouthi wanaoungwa mkono na Iran huenda wakaharibu nyaya za chini ya bahari pamoja na kushambulia meli baharini.

    Wahouthi - ambao wanadhibiti sehemu kubwa ya pwani ya Bahari ya Shamu magharibi mwa Yemen - wiki iliyopita walikanusha kuhusika na uharibifu wa nyaya hizo na kuelekeza kidole cha lawama kwa mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na Uingereza.

    Vikosi vya Marekani na Uingereza vimelenga silaha na miundombinu ya Houthi katika kukabiliana na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora dhidi ya meli za wafanyabiashara zinazopitia Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden.

    Waasi wa Houthi wanasema mashambulizi yao ni ishara ya kuwaunga mkono Wapalestina katika vita kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Magenge ya Haiti yajaribu kuuteka uwanja wa ndege wa Port-au-Prince

    Wanajeshi wamepelekwa kulinda uwanja wa ndege wa mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, dhidi ya mashambuliwa na magenge yenye silaha.

    Mashahidi waliripoti kusikia milio ya risasi ikisikika karibu na Uwanja wa Ndege wa Toussaint Louverture huku vikosi vya usalama vikikabiliana na watu waliokuwa na silaha.

    Lengo la magenge hayo ni kumzuia kurejea Haiti Waziri Mkuu Ariel Henry, ambaye anaaminika kuwa nje ya nchi.

    Ghasia zimeongezeka bila kuwepo kwake huku magenge ya watu wakimtaka ajiuzulu.

    Bw Henry aliondoka Haiti wiki iliyopita ili kuhudhuria mkutano wa kilele wa kikanda huko Guyana.

    Baada ya hapo, alisafiri hadi Kenya kutia saini mkataba wa kutumwa kwa jeshi la polisi wa kimataifa nchini Haiti.

    Waziri Mkuu kwa sasa hajulikani aliko lakini msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani alisema: "Tunafahamu kwamba waziri mkuu anarejea nchini [Haiti]".

    Akiwa nchini Kenya, muungano wa magenge ukiongozwa na afisa wa zamani wa polisi, Jimmy "Barbecue" Chérizier, ulishambulia shambulia vya polisi na kuvamia magereza makubwa mawili ya Haiti.

    Makumi ya watu waliuawa katika shambulio hilo la magereza.

    Maelfu ya wafungwa walitoroka na kubaki huru. Mamlaka nchini Haiti imetangaza hali ya dharura ya saa 72.

    Soma:

  5. Jeff Bezos ampiku Elon Musk na kuwa mtu tajiri zaidi duniani

    Kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miezi tisa, Elon Musk amevuliwa taji la kuwa mtu tajiri zaidi duniani.

    Musk amepoteza nafasi yake katika kipimo cha Mabilionea cha Bloomberg kwa Jeff Bezos baada ya hisa katika kampuni ya Tesla kushuka kwa 7.2% Jumatatu.

    Musk sasa ana utajiri wa dola bilioni 197.7 huku utajiri wa Bezos ukiwa dola bilioni 200.3.

    Ni mara ya kwanza kwa Bezos, 60, mwanzilishi wa kampuni ya Amazon kushika nafasi ya kwanza ya Bloomberg ya watu tajiri zaidi tangu 2021.

    Pengo la utajiri kati ya Musk, 52, na Bezos, ambalo wakati mmoja lilikuwa kubwa kama dola bilioni 142, limekuwa likipungua huku hisa za Amazon na Tesla zikienda pande tofauti.

    Ingawa kampuni zote mbili ni kati ya zenye hisa zinazojulikana sana ambazo zimekuza masoko ya hisa ya Marekani, hisa za Amazon zimeongezeka zaidi ya mara mbili tangu mwishoni mwa 2022 na ziko katika rekodi ya juu.

    Kampuni ya Tesla iko chini karibu 50% kutoka kilele chake cha 2021.

    Hisa za kampuni ya Tesla zilishuka Jumatatu baada ya data ya awali kuonyesha usafirishaji kutoka kwa kiwanda chake huko Shanghai ulipungua hadi chini zaidi katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja.

    Wakati huo huo, kampuni ya Amazon, imekuwa na ukuaji bora wa mauzo mtandaoni tangu mwanzoni mwa janga la corona.

    Soma zaidi:

  6. Mzozo wa Ukraine: Meli ya Urusi 'yaharibiwa katika shambulio la ndege isiyo na rubani'

    Meli ya doria ya Urusi imeharibiwa baada ya kushambuliwa na ndege zisizo na rubani katika Bahari Nyeusi, kulingana na ujasusi wa Ukraine.

    Sergei Kotov, ambayo ilizinduliwa mnamo 2021, inadaiwa kushambuliwa mapema asubuhi ya Jumanne.

    Idara ya ujasusi ya kijeshi ya Ukraine imesema meli ya Bahari Nyeusi ilipata uharibifu kwenye meli hiyo pamoja na upande wa kulia na kushoto.

    Kremlin bado haijatoa maoni. Baadhi ya wanablogu wa Urusi wanaounga mkono vita walithibitisha shambulio hilo.

    Afisa wa ujasusi wa Ukraine Andrii Yusov aliambia wanamaji wa shirika la utangazaji la RFERL waliokuwa ndani ya ndege hiyo wameuawa na kujeruhiwa.

    Sergei Kotov ni mojawapo ya meli nne za doria zilizokamilishwa kwa Mradi wa 22160 wa Jeshi la Wanamaji la Urusi.

    Kulingana na Ukraine, meli hiyo ilishiriki katika shambulio la Kisiwa cha Nyoka katika siku ya kwanza ya uvamizi kamili wa Ukraine mnamo Februari 2022, pamoja na meli ya Moskva.

    Moskva ilizamishwa na Ukraine mnamo 2022.

    Urusi iliteka rasi ya Crimea kutoka Ukraine kwa njia isiyo halali karibu miaka 10 iliyopita.

    Katika miezi ya hivi karibuni Ukraine imeshambulia mara kwa mara meli za Urusi katika Bahari Nyeusi zazilizoko kwenye peninsula.

    Ukraine ilisema thamani ya meli iliyozama ya Sergei Kotov ilikuwa $65, na kuongeza kuwa iligongwa karibu na Kerch Strait inayotenganisha Crimea na Urusi.

  7. Wawili wafariki baada ya ndege mbili kugongana angani Kenya

    Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Kenya imethibitisha tukio la kugongana kwa ndege ya abiria ya kampuni ya Safarilink na ndege ya mazoezi.

    Uchunguzi umeanza kubaini chanzo cha ajili hiyo.

    ‘’Uchunguzi umeanza kupitia mashirika mbalimbali ukiongozwa na Idara ya Uchunguzi wa Ajali za Anga na Huduma ya Taifa ya Polisi kubaini chanzo cha ajali,’’ Mamlaka ya Usafiri wa Anga Kenya imesema.

    Abiria wawili waliokuwa kwenye ndege ya mazoezi wote wameaga dunia huku abiria 39 na wafanyakazi 5 katika ndege ya Safarilink wakiokolewa hadi eneo salama.

    Shirika la ndege la Safarilink imesema kupitia mtandao waX kwamba muda mfupi baada ya kupaa mwendo wa saa tatu na dakika 45 asubuhi saa za eneo hilo, kishindo kikubwa kimesikika.

  8. DRC: Raia wa 5 wameuawa katika katika mashambulio ya mabomu wakati mapigano makali kati ya M23 na wanajeshi wa DRC

    Raia wa 5 wameuawa katika eneo la Nyanzale katika katika mashambulio ya mabomu wakati wa mapigano makali kati ya M23 na wanajeshi wa DRC wilayani Rutchuru.

    Haya yanajiri siku chache tuu baada ya Majeshi ya Tanzania, Malawi, Afrika Kusini na SADC,wakishirikiana na Majeshi ya Congo FARDC pamoja na hayo ya BurundiI kusema kuwa yanaweka mikakati muhimu ya kuimarisha operesheni zao za pamoja kwa lengo la kuleta amani na Usalama mashariki mwa Congo.

    Tangu Juma mosi juma lililo pita hadi sasa ni raia 7 ndio wamepoteza maisha baada ya mabomu kurushwa na wale wanaoaminika kuwa waasi wa M23, ambao wamekuwa wakikalia karibu vilima vyote vinavyoutazama mji wa Sake katika eneo la Kivu Kaskazini ,lakini piya Eneo la Nyanzale Wilayani Rutchuru.

    Haya yalitokea muda mfupi kabla ya kuwasili kwa wakuu wa vikosi vya ulinzi vya Tanzania, Malawi, Afrika Kusini na Burundi katika eneo la Mubambiro lakini piya Eneo la Nyanzale hapo jana baada ya Majeshi hayo kuondoka jijini Goma.

    ‘’Hali hii imewaathiri raia wengi ambao wamelazimika kuhama makwao na sasa wanaishi kambini…’’, anasema muwakilishi wa Gavana wa Nyanzale.

    ‘’Viongozi wa jeshi waliotembelea eneo hili wamesema kuwa wanaweka mikakati tofauti ili kurejesha usalama katika eneo hili.’’, mmoja wa raia waliathiriwa na mapigano ambaye yuko kambini

    Huku hayo yakijiri, raia wengi wanasema kuna haja ya juhudi za haraka za kuleta amani ya kudumu katika eneo hili.

  9. Korea Kaskazini yadukua watengenezaji wa vifaa vya Korea Kusini, Seoul yasema

    Wadukuzi wa Korea Kaskazini wamevamia watengenezaji wa vifaa vya saketi (chip) vya Korea Kusini, kulingana na shirika la kijasusi la Korea Kusini.

    Pyongyang inajaribu kutengeneza semiconductors kwa ajili ya programu zake za silaha, Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) inasema.

    Htua hiyo inakuja mwezi mmoja baada ya Rais Yoon Suk Yeol kuionya Korea Kaskazini kuwa inaweza kufanya uchochezi kama vile mashambulizi ya mtandao ili kuingilia uchaguzi ujao.

    Mwaka jana, Korea Kaskazini ilidukua barua pepe za msaidizi wa Rais Yoon. "Tunaamini kuwa Korea Kaskazini inaweza kuwa inajiandaa kuzalisha semiconductors yake yenyewe NIS ilisema katika taarifa.

    Imeongeza kuwa juhudi za Pyongyang zinaweza kuchochewa na hitaji la kuwa na 'chip' kwa ajili ya programu zake za silaha, zikiwemo satelaiti na makombora.

    NIS inaamini kwamba Korea Kaskazini ilipenya kwenye seva za kampuni mbili za vifaa hivyo mnamo Desemba na Februari, na kuiba miundo ya bidhaa na picha za vifaa vyao.

    Pia ilionya makampuni mengine katika tasnia ya kutengeneza 'chip' kuchukua tahadhari dhidi ya mashambulizi ya mtandao.

    Hata hivyo, shirika hilo la kijasusi halikutaja makampuni au kusema kama Korea Kaskazini iliweza kupata chochote cha thamani.

    NIS ilisema kampuni za Korea Kusini zimekuwa shabaha kuu ya wadukuzi wa Korea Kaskazini tangu mwishoni mwa mwaka jana.

  10. Mahakama Kuu Kenya yaamua kusitishwa kwa ajira za maafisa huduma ya mapato kwa madai ya ukabila

    Mahakama kuu ya Busia nchini Kenya imebainisha kuwa ajira kwa wasaidizi 1,406 wa huduma ya mapato na Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA) ni kinyume na katiba yan chi hiyo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni makabila mawili pekee yaliyonufaika zaidi na ajira hizoo.

    Ombi la kusitishwa kwa ajira hizo lililowasilishwa na Peter Kabinga mnamo Oktoba 12, 2023, lilisema kuwa kati ya wale walioajiriwa, 785 walitoka katika jamii mbili nchini Kenya huku 621 wakitoka katika jamii nyingine za Kenya.

    Jaji William Musyoka ameizuia KRA kuwajiri wafanyikazi wa ngazi zote hadi sera ya utofauti wa kikabila na usawa wa kikanda itakapotekelezwa kama ilivyoelezwa katika katiba.

  11. Luteni kanali mstaafu wa Jeshi la Marekani ashtakiwa kwa kusambaza taarifa za siri kupitia tovuti ya uchumba

    Luteni kanali mstaafu na mfanyakazi wa makao makuu ya vikosi vya nyuklia vya Marekani ameshtakiwa kwa kutoa taarifa za siri kwa "mwanamke fulani kutoka Ukraine" ambaye aliwasiliana naye kupitia tovuti ya uchumba.

    Taarifaya wizara ya sheria ya Marekani kwa vyombo vya habarivya Marekaniilisema David Franklin Slater mwenye umri wa miaka 63 alihudumu kama raia, lakini akiwa na kibali cha usalama, katika makao makuu ya USSTRATCOM katika Kambi ya Jeshi la anga la Offutt baada ya kustaafu. Vikosi vya nyuklia vya Marekaniviko chini ya Stratcom.

    Slater alikamatwa Jumamosi na atafikishwa mahakamani leo Jumanne.

    Siku ya Jumatatu, waendesha mashitaka walitoa mashtaka katika kesi ya Slater, ambayo yanaonyesha kuwa kuanzia takriban Februari hadi Aprili 2022, alisambaza taarifa za siri kutoka kwa ripoti za Stratcom kuhusu shambulio la Urusi dhidi ya Ukraine kupitia tovuti ya uchumba kwa mtu aliyejitambulisha kuwa mwanamke kutoka Ukraine.

    Taarifaya Wizara ya sheria kwa vyombo vya habari ilidokeza kwamba Slater alijua anachokifanya na mtu ambaye alikuwa akizungumza naye.

  12. Ghasia za Haiti: Magenge ya Haiti yamtaka Waziri Mkuu ajiuzulu baada ya kuvamiwa kwa gereza

    Serikali ya Haiti imetangaza hali ya hatari ya saa 72 siku ya Jumapili baada ya magenge yenye silaha kuvamia gereza kuu.

    Takribani watu 12 waliuawa na wafungwa wapatao 3,700 walitoroka katika ajali hiyo ya jela.

    Viongozi wa magenge wamemtaka Waziri Mkuu Ariel Henry kujiuzulu, ambaye hajulikani aliko tangu aliposafiri hadi Kenya.

    Magenge yanadhibiti karibu 80% ya mji mkuu, Port-au-Prince. Ghasia za magenge zimeikumba Haiti kwa miaka mingi. Taarifa ya serikali ilisema magereza mawili, moja huko Port-au-Prince na nyingine katika Croix des Bouquets iliyo karibu, yalivamiwa mwishoni mwa wiki.

    Ilisema vitendo vya "kutotii" ni tishio kwa usalama wa taifa na kusema kuwa inaanzisha amri ya kutotoka nje usiku, ambayo ilianza saa 20:00 kwa saa za ndani (01:00 GMT siku ya Jumatatu).

    Vyombo vya habari vya Haiti viliripoti kwamba vituo vya polisi vilishambuliwa, na kuvuruga mamlaka kabla ya shambulio lililoratibiwa kwenye jela.

    Akizungumza na BBC kutoka Haiti, Serge Dalexis kutoka Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji alisema kuwa vituo vingi vya polisi vilikuwa chini ya udhibiti wa magenge siku ya Ijumaa, huku "polisi wengi wakiuawa mwishoni mwa juma".

    Miongoni mwa waliozuiliwa huko Port-au-Prince walikuwa washukiwa walioshtakiwa kuhusiana na mauaji ya 2021 ya Rais Jovenel Moïse.

    Ghasia za magenge zimeongezeka zaidi tangu kuuawa kwake mwaka wa 2021. Bw Moïse hajabadilishwa na uchaguzi wa urais haujafanyika tangu 2016.

    Jinsi magenge yalivyokuja kutawala Haiti Katika mji mkuu, magenge yameweka vizuizi kuzuia vikosi vya usalama kuvamia eneo lao, wakati ngome zao katika mitaa ya mabanda ya Port-au-Prince bado kwa kiasi kikubwa zimefungwa.

    Shule na biashara nyingi zimefungwa, na kuna ripoti za uporaji katika baadhi ya vitongoji. Watu wanaogopa na barabara hazina watu, Boby Sander kutoka shirika la misaada ya kibinadamu la Food for the Hungry aliambia BBC. Tangu Ijumaa, watu 15,000 wamekimbia makazi yao na wengi sasa wanakaa katika jengo la shule katikati mwa Port-au-Prince, Bw Sander alisema.

  13. Tazama: Afisa wa polisi anamburuza na kumkanyaga mtu asiye na makazi kwenye mfuko wa kulalia Uingereza

    Video iliyotumwa kwa BBC inaonyesha afisa wa polisi mjini Manchester akimburuza chini sakafuni mwanamume asiye na makazi ambaye alikuwa amejilaza ndani ya mfuko wa kulalia, kabla ya kumkanyaga kwenye tumbo lake.

    Polisi wa Greater Manchester walisema afisa huyo alikuwa na tabia "isiyokubalika".

  14. Ufaransa yafanya uavyaji mimba kuwa haki ya kikatiba

    Ufaransa imekuwa nchi ya kwanza duniani kujumuisha kwa uwazi haki ya utoaji mimba katika katiba yake.

    Wabunge walipiga kura kurekebisha katiba ya nchi ya 1958 ili kuweka "uhuru uliohakikishwa" wa wanawake wa kutoa mimba.

    Kura nyingi za 780-72 zilishuhudia shangwe kubwa katika bunge la Versailles wakati matokeo yalipotangazwa.

    Rais Emmanuel Macron alielezea hatua hiyo kama "fahari ya Ufaransa" ambayo ilituma "ujumbe wa ulimwengu wote".

    Hata hivyo makundi yanayopinga uavyaji mimba yamekosoa vikali mabadiliko hayo, kama ilivyofanya Vatican.

    Uavyaji mimba umekuwa halali nchini Ufaransa tangu 1975, lakini kura za maoni zinaonesha karibu 85% ya umma waliunga mkono marekebisho ya katiba ili kulinda haki ya kumaliza ujauzito.

    Na wakati nchi nyingine kadhaa zinajumuisha haki za uzazi katika katiba zao, Ufaransa ndiyo ya kwanza kusema kwa uwazi kwamba utoaji mimba utahakikishwa.

    Kufuatia kura hiyo, Mnara wa Eiffel mjini Paris uliangaziwa katika sherehe, ukiwa na ujumbe: "My Body My Choice".

    Kabla ya kura hiyo, Waziri Mkuu Gabriel Attal aliliambia bunge kwamba haki ya kutoa mimba inasalia "katika hatari" na "kwa huruma ya watoa maamuzi".

    "Tunatuma ujumbe kwa wanawake wote: mwili wako ni wako na hakuna anayeweza kukuamulia," aliongeza.

  15. Timu ya Umoja wa Mataifa inasema Hamas huenda ilitekeleza ukatili wa kingono Israel tarehe 7 Oktoba

    Timu ya Umoja wa Mataifa imehitimisha kuwa kuna "sababu nzuri za kuamini" unyanyasaji wa kingono, ikiwa ni pamoja na ubakaji na ubakaji wa genge, ulifanyika wakati wa mashambulizi ya Hamas nchini Israel tarehe 7 Oktoba.

    Pia walisema kuna "taarifa za kushawishi" kwamba mateka wamefanyiwa ukatili wa kijinsia.

    Safari hiyo iliongozwa na Pramila Patten, Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Unyanyasaji wa Kijinsia katika Migogoro.

    Hamas imekanusha watu wake wenye silaha kuwanyanyasa kingono wanawake wakati wa mashambulizi hayo.

    "Timu ya misheni iligundua kuwa kuna sababu za kuridhisha za kuamini kwamba unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro ulitokea katika maeneo mengi wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7," ripoti ya Umoja wa Mataifa ilisema.

    Haya yalifanyika katika takribani maeneo matatu, eneo tamasha la muziki la Nova na mazingira yake, Road 232, na Kibbutz Re'im, iliongeza.

    Watu wenye silaha wa Hamas walijipenyeza kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba na kuua takribani watu 1,200 na kuwachukua wengine 253 mateka.

    Israel ilijibu kwa kuanzisha kampeni ya kijeshi huko Gaza, ambapo watu 30,500 wameuawa, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas.

    Ripoti za unyanyasaji wa kijinsia unaofanywa na Hamas, ambayo imeelezwa kama shirika la kigaidi na Israel, Uingereza na wengine, ilianza kuibuka mara baada ya 7 Oktoba na imeongezeka kwa kasi tangu wakati huo.

    BBC pia imeona na kupata ushahidi wa ubakaji, unyanyasaji wa kijinsia na ukeketaji wa wanawake.

  16. Watoto wanakufa kwa njaa kaskazini mwa Gaza – WHO

    Watoto wanakufa kwa njaa kaskazini mwa Gaza, mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) anasema.

    Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema ziara za shirika hilo mwishoni mwa juma katika hospitali za Al-Awda na Kamal Adwan zilikuwa za kwanza tangu mapema Oktoba.

    Katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii, alizungumza juu ya "matokeo ya kutisha".

    Ukosefu wa chakula ulisababisha vifo vya watoto 10 na "kiwango kikubwa cha utapiamlo", wakati majengo ya hospitali yameharibiwa, aliandika.

    Wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas huko Gaza iliripoti siku ya Jumapili kwamba watoto wasiopungua 15 walikufa kutokana na utapiamlo na upungufu wa maji mwilini katika hospitali ya Kamal Adwan.

    Mtoto wa 16 alifariki siku ya Jumapili katika hospitali moja katika mji wa kusini wa Rafah, shirika rasmi la habari la Palestina Wafa liliripoti Jumatatu.

    Dkt. Tedros aliripoti "kiwango kikubwa cha utapiamlo, watoto kufa kwa njaa, uhaba mkubwa wa mafuta, chakula na vifaa vya matibabu, majengo ya hospitali kuharibiwa" kaskazini mwa Gaza, ambako takribani watu 300,000 wanaishi na chakula kidogo au maji safi.

    "Ukosefu wa chakula ulisababisha vifo vya watoto 10," aliandika kwenye X, ambayo zamani ilijulikana kama Twitter.

    Ziara hizo zilikuwa za kwanza kwa WHO katika miezi "licha ya juhudi zetu za kupata ufikiaji wa mara kwa mara kaskazini mwa Gaza", aliandika.

    Unaweza kusoma;

  17. Marekani yamuwekea vikwazo rais wa Zimbabwe kwa ufisadi

    Serikali ya Marekani imemuwekea vikwazo Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa pamoja na maafisa wengine wakuu kwa ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu.

    Siku ya Jumatatu serikali ya Marekani ilisema viongozi nchini Zimbabwe wamekuwa wakipora rasilimali za umma kwa manufaa yao kibinafsi.

    Hatua hii inafutilia mbali agizo la zamani la vikwazo vya serikali vilivyoanzishwa mwaka 2003 na kuwaweka watu 11 na mashirika matatu kwenye orodha ya kimataifa - mpango wa vikwazo wa Global Magnitsky.

    "Shughuli hizi haramu zinasaidia na kuchangia mtandao wa uhalifu wa kimataifa wa hongo, magendo, na utakatishaji fedha unaosababisha umaskini kwa jamii nchini Zimbabwe, kusini mwa Afrika, na sehemu nyingine za dunia," ilisema taarifa.

    Marekani pia ilikosoa kulengwa kwa mashirika ya kiraia na vikwazo vikali kwa shughuli za kisiasa.

    Vilevile Rais Mnangagwa, Makamu wa Rais Constantino Chiwenga na mfanyabiashara Kudakwashe Tagwirei pia wamewekewa vikwazo.

    Mkewe Bw Mnangaga, Auxillia Mnangagwa, pia amewekewa vikwazo kwa sababu "anarahisisha shughuli za mume wake za ufisadi".

    Serikali ya Marekani ilisema tabia chafu ya baadhi ya watu na makampuni yenye nguvu zaidi nchini Zimbabwe inalingana na vitendo vya wakiukaji wakubwa zaidi wa haki za binadamu na watendaji wafisadi duniani.

    Marekani ilihakikisha kwamba "vikwazo hivi vya watu binafsi na mashirika haviiathiri Zimbabwe au umma wake".

    Serikali ya Zimbabwe haijazungumzia kuhusu madai hayo ya hivi punde lakini ilitupilia mbali vikwazo vya hapo awali kama sehemu ya njama za nchi za Magharibi kuleta mabadiliko ya kisiasa.

  18. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya mubashara leo ikiwa ni tarehe 05.03.2024