Baada ya kukosolewa vikali waandaji wa Tuzo za Nobel waziondoa Urusi, Belarus na Iran
Taasisi ya tuzo za Nobel imebatilisha uamuzi wake wa awali uliokosolewa sana wa kuzialika Urusi, Belarus na Iran kwenye sherehe za tuzo za mwaka huu huko Stockholm.
"Tunatambua maoni na muitikio mkubwa nchini Sweden," Taasisi hiyo ilisema. Urusi na mshirika wake Belarus hawakualikwa mwaka jana kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, huku Iran ikiachwa nje kutokana na rekodi yake ya haki za binadamu. Ukraine ilikosoa uamuzi wa mwaka huu na kupongeza uamuzi mpya wa Jumamosi wa kuziondoa nchi hizo ikisema ni "ushindi kwa masuala ya binadamu".
Sherehe ya tuzo hizo zinafanyika mjini Stockholm tarehe 10 Desemba - siku ya kumbukumbu ya kifo cha Alfred Nobel, mtu aliyeanzisha Taasisi hiyo.