Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Urusi huenda ndio waliohusika na kuvuja kwa nyaraka za siri kwenye mitandao ya kijamii
Urusi au wahusika wanaoiunga mkono Urusi huenda ndio waliohusika na kuvuja kwenye mitandao ya kijamii kwa nyaraka kadhaa za siri za kijeshi za Marekani
Moja kwa moja
Urusi huenda ndio waliohusika na kuvuja kwa nyaraka za siri kwenye mitandao ya kijamii
Urusi au wahusika wanaoiunga mkono Urusi huenda ndio waliohusika na kuvuja kwenye mitandao ya kijamii kwa nyaraka kadhaa za siri za kijeshi za Marekani kuhusu maandalizi ya mashambulizi ya Ukraine, ambayo kwa kiasi fulani yanafichua picha ya vita vya Ukraine mwezi mmoja uliopita, Reuters iliripoti Ijumaa, ikiwanukuu maafisa watatu wa Marekani.
Nyaraka hizo zilionekana kubadilishwa ili kupunguza idadi ya waliojeruhiwa na vikosi vya Urusi, maafisa wa Marekani waliambia shirika hilo, na kuongeza kuwa makadirio yao sio rasmi na hayakushughulikia uchunguzi wa uvujaji wenyewe.
Wizara ya Ulinzi ya Ukraine pia ilisema kwamba nyaraka kuhusu mipango ya mashambulizi ya Kiukreni "ilighushiwa na Urusi."
Pentagon ilikataa kutoa maoni juu ya uhalisi wa hati zinazozunguka kwenye tovuti, ikiwa ni pamoja na Twitter na Telegram, za tarehe 1 Machi na zilizoandikwa "Siri" na "Siri kubwa." Hata hivyo, awali msemaji wa Pentagon alithibitisha kwa CNN kwamba ofisi yake ilikuwa ikichunguza nyaraka zilizovuja.
Mbakaji wa Afrika Kusini aliyepatikana na hatia kutumia mitandao ya kijamii kuwarubuni watu akamatwa Tanzania
Mbakaji aliyepatikana na hatia ambaye alitumia mitandao ya kijamii kuwarubuni waathiriwa wake amekamatwa nchini Tanzania baada ya kutoroka gerezani kwa kudanganya kifo chake.
Thabo Bester, anayejulikana kama "mbakaji wa Facebook" alikuwa amejificha kwa karibu mwaka mmoja.
Jeshi la Polisi nchini Tanzania limethibitisha kukamatwa kwake katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa Instagram.
Ni mtu anayesakwa zaidi nchini Afrika Kusini na kutoroka kwake kumelishika taifa hilo. Kumekuwa na taarifa nyingi za kuonekana kwa Thabo Bester katika mwaka uliopita, ikiwa ni pamoja na madai kwamba alionekana akinunua mboga katika kitongoji cha watu matajiri cha Johannesburg.
Lakini wakati huu polisi wa Afrika Kusini wanasema hatimaye wamempata. Katika mkutano na wanahabari, maafisa waliviambia vyombo vya habari Bw Bester alikamatwa siku ya Ijumaa, akiwa na mpenzi wake na mshukiwa wa tatu.
Sasa atarejeshwa Afrika Kusini. Mamlaka ya magereza yamekosolewa vikali, kutokana na kutoroka kwa Bw Bester mnamo Mei mwaka jana. Wafanyakazi wa kampuni ya ulinzi inayomilikiwa na Uingereza ya G4S, waliokuwa wakiendesha gereza alimokuwa kizuizini, wanatuhumiwa kumsaidia kutoroka.
Thabo Bester alikuwa akitumikia kifungo cha maisha jela kwa mauaji ya mwanamitindo, alipotoroka kwa kuuchoma moto mwili wa mtu mwingine na kuuacha kwenye selo yake.
Hapo awali alipatikana na hatia ya kubaka na kuwaibia wanamitindo wawili waliokuwa wamewavutia kwenye mtandao wa Facebook.
Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi zenye viwango vya juu zaidi vya ubakaji duniani, ikiwa na wastani wa matukio 72 kwa kila watu 100,000.
Urusi yakataa ubadilishaji wa wafungwa uliopendekezwa na Kiev wakati huu wa Ramadhani
Urusi imekataa pendekezo la Kyiv la kubadilishana wafungwa wote wa kivita Waislamu katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, mamlaka ya Ukraine imesema.
"Tulikuja na pendekezo la kubadilishana Waislamu kutoka pande zote mbili kama ishara ya kuheshimu utamaduni na mila zao. Kwa bahati mbaya, upande wa Urusi ulikubali wazo hili bila shauku ,” alisema Mshauri wa Mawasiliano kwa Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Ukraine Daria Zarivna.
Kulingana naye, mpango huu ulikuwa mmoja wa wengi uliopendekezwa na upande wa Ukraine kwa ajili ya kubadilishana wafungwa.
Urusi haikutoa maoni yoyote juu ya taarifa hizi. Kwa jumla, Makao Makuu ya Uratibu wa Kiukreni kwa Matibabu ya Wafungwa wa Vita imefanya mabadilishano kadhaa tangu Machi 11, 2022, wakati ambao, kulingana na mamlaka ya Kiukreni, watu 2,005, wanajeshi na raia, walibadilishana.
Waukraine 11 walirudi nyumbani kama matokeo ya mabadilishano ya mwisho, ambayo yalifanyika.
Mo Farah amaliza wa saba katika mbio za Port-Gentil kilomita 10
Mo Farah alimaliza wa saba katika dakika 30 na sekunde 41 katika mbio za Port-Gentil 10km nchini Gabon, siku 15 kabla ya London Marathon.
Bingwa mara nne wa Olimpiki Farah, 40, amekuwa akifanya mazoezi nchini Ethiopia kujiandaa na mbio za marathon tarehe 23 Aprili.
Alitangaza mnamo Januari kwamba anatarajia 2023 kuwa mwaka wake wa mwisho wa mbio kabla ya kustaafu.
Mkenya Vincent Kipkemoi alishinda nchini Gabon kwa dakika 28 na sekunde 11.
Farah alikosa mbio za London Marathon za 2022 kutokana na jeraha la nyonga na mashindano ya mwaka huu yatakuwa ni marathon yake ya kwanza kamili tangu 2019.
Inatarajiwa London Marathon zitakuwa mbio za mwisho kwa Muingereza huyo na atachuana na wanariadha wanne kati ya watano wenye kasi zaidi katika historia, akiwemo Muethiopia Kenenisa Bekele. London Marathon ya 2023 itaoneshwa moja kwa moja kwenye BBC TV, iPlayer na mtandaoni.
Luca Attanasio: Wahukumiwa maisha gerezani DRC kwa mauaji ya balozi wa Italia,
Mahakama ya kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imewahukumu wanaume sita kifungo cha maisha jela kwa kumuua balozi wa Italia Februari 2021.
Luca Attanasio alikuwa miongoni mwa watu watatu waliopigwa risasi na kuuawa baada ya msafara wa Umoja wa Mataifa aliokuwa akisafiri nao kuvamiwa.
Dereva wake aliuawa kwanza kisha yeye na mlinzi wake kutekwa nyara, wakifa baada ya shughuli ya uokoaji kwenda vibaya.
Tukio hilo lilifanyika mashariki mwa nchi hiyo, ambapo vikundi vingi vyenye silaha hufanya kazi. Walikuwa wakisafiri kwenye barabara kupitia Mbuga ya Kitaifa ya Virunga, eneo la Urithi wa Dunia wa UNESCO kusini mwa mji wa Goma, kutembelea mpango wa kulisha chakula wa Umoja wa Mataifa wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wakati shambulio hilo lilipotokea.
Wanaume watano kati ya sita wanaotuhumiwa kuwaua walikamatwa Januari 2022 na wamekuwa kizuizini katika gereza la kijeshi la N'Dolo katika mji mkuu, Kinshasa.
Mtu wa sita alikimbia. Upande wa mashtaka ulisema washtakiwa walikuwa sehemu ya "genge la uhalifu" ambao baada ya kumuua dereva Mustapha Milambo walikuwa na nia ya kuwashikilia Bw Attanasio na mlinzi wake wa Italia Vittorio Iacovacci ili wapate kikombozi.
Mwendesha mashtaka Godé Bamusamba Kabambaa alikuwa ametoa wito wa hukumu ya kifo. Wakati wa kesi hiyo iliyoanza Oktoba mosi, washtakiwa walisema kukiri kwao makosa ya awali kulikuwa kwa mateso.
Wakili wao, Joseph Amzati, aliiambia BBC kwamba watakata rufaa dhidi ya kifungo hicho cha maisha.
Alisema kesi hiyo haikuwa ya haki na akataja ukweli kwamba hakuna hata mmoja wa manusura wanne wa shambulio hilo aliyetoa ushahidi mbele ya mahakama hiyo.
Washtakiwa, ambao kwa mujibu wa wakili wao wote walikuwa wameajiriwa awali kama madereva wa pikipiki, waliamriwa kulipa $2m (£1.6m) kama fidia kwa familia za waathiriwa.
Unaweza kusoma;
Jeshi China lafanya zoezi la kuizingira Taiwan
Jeshi nchini China linafanya mazoezi ya kuizingira Taiwan katika mazoezi ya siku tatu ya kijeshi. Beijing – inayoitazama Taiwan kama jimbo lake lililojitenga – imeitaja operesheni hiyo kama "onyo kali" kwa utawala wa kisiwa hicho.
Mazoezi hayo yalianza saa kadhaa baad ya rais Tsai Ing-wen kurudi kutoka ziara ta Marekani. Wizara ya ulinzi ya Taiwan inasema ndege 42 za kijeshi za China na meli nane zilivuka mpaka wa Taiwan baharini. Mpaka huo unazigawanya China na Taiwan.
Vyombo vya Habari China vinasema mazoezi hayo "yataanda doria na kusogea katika maeneo yanayokizunguka kisiwa cha Taiwan, na kutoa taswira ya kuizingira na kuitishia Taiwan".
Vimeongeza kwamba makombora ya roketi ya masafa marefu, mifumo ya kuharibu makombora ya baharini, boti za makombora, ndege za kivita miongoni mwa mengine imetumwa na jeshi la China.
Taiwan inajitazama kama taifa huru, yenye katiba na viongozi wake. Lakini China inatazama kama sehemu ya eneo lake lililojitenga ambalo hatimaye litarudishwa chini ya udhibiti wa Beijing – kwa nguvu ikibidi.
Unaweza kusoma;