Tetemeko la Ardhi Uturuki: Matumaini ya kupata manusura yanafifia vifo vikifikia 23,000
Waokoaji bado wanatafuta manusura kwenye vifusi, lakini matumaini yanafifia ikiwa ni karibu saa 100 tangu kutokea kwa tetemeko hilo.
Moja kwa moja
Somalia yafungua tena ubalozi Uingereza baada ya miaka 32

Chanzo cha picha, Twitter
Somalia imefungua tena ubalozi wake nchini Uingereza baada ya miaka 32, katika hafla iliyohudhuriwa na balozi Abdulkadir Ahmed Kheyr, bingwa wa Olimpiki Mo Farah na mwanamitindo wa Somalia-Canada Sabrina Dhowre na wengineo.
Ubalozi wa Uingereza unatarajiwa kutoa huduma za kibalozi kwa Wasomali wapatao 500,000 wanaoishi nchini Uingereza ambao wanastahili uraia wa Somalia, na huduma zingine zikiwemo hati za kusafiria na vyeti vya ndoa.
Pia ubalozi utashughulikia masuala ya utamaduni na matukio mengine watakayotaarifiwa.
Balozi Kheyr alisema kuwa kufungua tena ubalozi huo ni hatua nzuri katika kuimarisha uhusiano wa Uingereza na Somalia.
Ubalozi wa Somalia mjini London ulifungwa rasmi mwaka 1991 kufuatia kusambaratika kwa serikali kuu.
Ingawa, uhusiano wa kidiplomasia umeimarishwa katika miaka ya hivi karibuni.
Uingereza ilifungua tena ubalozi wake mjini Mogadishu mwaka 2013 baada ya kutokuwepo kwa miaka 22.
Soma zaidi:
- Mji mmoja nchini Somalia ambapo kikombe cha chai kilinunuliwa kwa dhahabu
- Sir Mo Farah afichua kuwa alisafirishwa kinyume cha sheria kufanyishwa kazi Uingereza akiwa mtoto
Idadi ya vifo nchini Uturuki na Syria yakaribia 23,000
Idadi ya vifo nchini Uturuki kufuatia tetemeko la ardhi la Jumatatu imeongezeka hadi 19,388, kwa mujibu wa Rais wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdogan.
Idadi ya vifo vilivyoripotiwa katika nchi jirani ya Syria inafikia 3,377, ikimaanisha kuwa jumla ya walioaga dunia imefikia karibu 23,000.
Erdogan ameongeza kuwa zaidi ya watu 77,700 wamejeruhiwa nchini Uturuki na kusema kuwa serikali itatoa msaada wa kodi kwa manusura wa tetemeko hilo.
Awali, alisema mwitikio wa serikali kuhusu tetemeko hilo la ardhi haujakuwa wa haraka kama alivyotarajia.
'Nimepoteza zaidi ya watu 120 wa familia yangu'

Mtu mmoja raia wa Uturuki mwenye makazi yake mjini Edinburgh huko Scotland anasema amepoteza zaidi ya watu 120 wa familia yake katika tetemeko kubwa la ardhi lililokumba Uturuki na Syria siku ya Jumatatu.
Sahin Firat, rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Kituruki- wanaoishi Scotland na mratibu wa michango kwa ajili ya waathirika wa tetemeko hilo alisema: "Katika familia yangu pekee nimepoteza zaidi ya watu 120 - binamu zangu, shangazi, wajomba, wapwa... na pia wengine kutoka kijijini kwangu, majirani.
"Walikuwa Adiyaman, katikati ya jiji. Hali kote nchini Uturuki ni mbaya sana,’’ aliambia kipindi cha BBC cha Good Morning Scotland.
“Watu wanakaa kwenye gari au barabarani, wakipata petroli wanaingia ndani ya gari ili kupata joto, wakati mwingine mvua ikishanyesha wanatafuta kuni au karatasi ili kuwasha moto.
"Kadiri siku zinavyosonga hali inaendela kuwa mbaya zaidi, ni hali ya dharura, kama vita, hadi leo tumekuwa tukikusanya nguo, chakula, kusafisha vitu, lakini sasa wanahitaji pesa za kuwasaidia kwa sababu hawana nyumba tena."
Maelezo zaidi:
- Tetemeko la ardhi la Uturuki: lilipiga wapi na kwa nini lilikuwa baya sana?
- Tetemeko la ardhi la Syria-Uturuki:Kamera ya CCTV yanasa picha za tetemeko lilipotokea Uturuki na Syria
Ugonjwa usiojulikana waua watu Equatorial Guinea

Marufuku ya kutotoka nje ya siku mbili yamewekwa katika jimbo la kaskazini mwa Guinea ya Ikweta, linaloitwa Kié-Ntem, baada ya watu 20 kufariki kutokana na ugonjwa ambao bado haujajulikana.
Vifo hivyo vilithibitishwa na mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Olamze, ambayo iko umbali mfupi kuvuka mpaka nchini Cameroon.
Kwa mujibu wa mamlaka ya afya ya Cameroon, waathiriwa walipata aina fulani ya homa na kutokwa na damu puani, kuwa dhaifu, kutapika na kuhara.
Visa vya maambukizi na vifo vinatoka katika maeneo matatu kaskazini mwa Equatorial Guinea. Wanne kati ya wahasiriwa walitoka kwa familia moja.
Maambukizi hutokea kwa kuwasiliana moja kwa moja na mtu aliyeambukizwa, kulingana na mamlaka ya afya ya Cameroon.
Ndio maana wanawanawaambia watu wa Cameroon wawe makini.
Mamlaka ya Equatorial imesema kuwa mgonjwa atawekwa karantini hadi hali ya ugonjwa huo na chanzo cha mlipuko huo kuthibitishwa.
Soma zaidi:
- Watu watatu wafariki kutokana na ugonjwa usiojulikana Tanzania
China yashauriwa ''kubuni njia'' ya kuongeza idadi ya watoto

Chanzo cha picha, FUTURE PUBLISHING
Afisa mkuu wa afya mjini Beijing amewataka viongozi wa eneo hilo nchini China kutafuta njia za kuongeza kiwango cha kuzaliwa nchini humo.
Yang Wenzhuang amesema maafisa lazima wachukue hatua madhubuti ili kukabiliana na athari mbaya za sera ya muda mrefu ya China dhidi ya ongezeko la watu.
Pia aliwataka maafisa "kuwa na udhubutu" katika hatua ya kukabiliana na gharama ya malezi na elimu ya watoto.
Mnamo mwezi Januari China iliripoti kwamba idadi ya watu ilipungua kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 60.
Sera kali ya nchi ya mtoto mmoja - ambayo ilitekelezwa kutoka 1980 hadi 2015 ili kukabiliana na ongezeko la watu waliokimbia - imelaumiwa kwa kupungua. Familia zilizovunja sheria zilitozwa faini na, katika visa fulani, hata kupoteza kazi.
Kiwango hicho kiliongezwa kitaifa kwa wanandoa hadi wawili mwaka 2016, na kuongezeka zaidi hadi watatu mwaka wa 2021.
Maelezo ya video, Je sera ya mtoto mmoja inaweza kukoma katika zama za kizazi kipya China? Tamasha la Sauti za Busara laanza Zanzibar

Tamasha la Sauti za Busara limeanza rasmi hii leo katika mji mkongwe wa kisiwa cha karafuu.
Wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wamejawa na shauku ya kutaka kuona tamasha la mwaka huu litakuwa na mvuto kiasi gani, huku wasanii kutoka zaidi ya nchi 12 wamejipanga kutumbuiza mashabiki wenye hamu ya kupata burudani.
Shamra shamza hizi zitarindima kisiwani hapa kwa muda wa siku tatu mfululizo.


Leo hii kinachoanza ni wasanii kuwa jukwaani na kuonyesha umahiri wao, huku kilele cha shughuli hiyo kitakuwa siku ya Jumapili ambapo kiwatakutanisha wasanii, wafadhili, na wadau wengine kwa ajili ya kubadilishana uzoefu.
Tangu kumalizika kwa janga la korona, hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa mashabiki wa tamasha la Sauti za Busara kujiachia bila hofu ya maambukizi.
Yusuf Mahmoud ambae ndio mwanzilishi wa tamasha hilo, anasema miaka 20 ya kuwepo kwa tamasha hilo, licha ya kuwa na mchango mkubwa katika mzunguko wa fedha kwa wakazi, lakini changamoto vile vile vimekuwa nyingi kiasi cha kuhatarisha kuendelea kuwepo kwa tamasha.
“Kutokana na uhaba wa fedha, mwaka huu kuna baadhi ya vitu tumeshindwa kuviweka katika tamasha, jukwaa la nje, mafunzo kwa wasanii lakini pia matembezi ya mwanzo kabla ya tamasha,” ameiambia BBC.

Kwa mujibu wa Yusuf, mwaka 2020 fedha zilizotumika kufanya tamasha hilo ilikuwa ni dola laki nne, lakini fedha zilizoingia katika mzunguko ni dola milioni 18.3.
Na ni sababu hii ndio inayowafanya wafanyabiashara wadogo wadogo na hata wakubwa kufurahia uwepo wa tamasha.
Hata, kila jema halikosi kasoro, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wakazi wa Unguja kwamba tamasha la Sauti za Busara kwa kiasi fulani linachangia mmomonyoko wa maadili hasa ikizingatiwa, asilimia kubwa ya jamii ya wazanzibari ni waislamu. Hata hivyo, Yusuf anasema, wamekuwa wakizingitia maadili ya wakazi ili kuepusha mikwaruzano.
Soma zaidi:
- Sauti za Busara zilivyochangamsha Zanzibar
- Tamasha la filamu lakamilika Zanzibar
Hofu yatanda baada ya Samaki waliokufa kukutwa katika fukwe ya Maputo

Chanzo cha picha, Radio Msumbiji
Tukio la samaki waliokufa kukutwa kwenye fukwe ya Maputo, kusini mwa Msumbiji mwishoni mwa wiki iliyopita imeleta wasiwasi kwa mamlaka, ambayo inachunguza pamoja na taasisi za kitaaluma, mashirika ya kiraia na wavuvi.
Ingawa kuna uwezekano kwamba samaki hao walikufa kutokana na kiwango kidogo cha oksijeni, kilichosababishwa na viwango vya juu vya miundombinu ya ndani ya maji, kutokana na kuchimba na kuweka nyaya.
Mamlaka inadhani pia kuwa maji safi kutoka kwenye mito inayotiririka kwenye fukwe hiyo inaweza kupunguza viwango vya chumvi.
Hii si mara ya kwanza kwa visa kama hivyo kutokea kwenye fukwe ya Maputo, huku matukio madogo yanayohusishwa na umwagikaji wa maji safi kwenye ghuba hiyo yakirekodiwa hapo awali.
Mamlaka hiyo imewataka wakazi hasa wavuvi kuwa waangalifu na kushirikiana na wataalamu waliopo ambao kuchunguza tukio hilo.
Pia wamewataka watu kutokula samaki waliokufa ambao wanaopatikana ufukweni na baharini.
Soma zaidi:
- Uganda yachunguza idadi kubwa ya vifo vya samaki ziwa victoria
Ethiopia yaweka zuio la mtandao wa kijamii kufuatia mvutano na kanisa la Orthodox

Chanzo cha picha, Getty Images
Ethiopia imeweka zuio la upatikanaji wa mitandao ya kijamii na majukwaa ya ujumbe mfupi huku kukiwa na mvutano unaoongezeka kati ya mamlaka na kanisa la Orthodox.
Netblocks, shirika linalofuatilia uhuru wa upatikanaji wa mtandao, lilisema vikwazo hivyo viliathiri Facebook, Messenger, Telegram na TikTok.
Haya yanajiri baada ya baraza kuu la kanisa hilo, kukataa marufuku ya mamlaka na kutangaza kuwa litaendelea na maandamano yaliyopangwa.
Shule zilifungwa Ijumaa kufuatia agizo la mamlaka.
Kanisa la Orthodox, dhehebu kubwa zaidi nchini Ethiopia, linashutumu serikali kwa kuunga mkono kundi lililojitenga katika eneo la Oromia.
Kanisa hilo linashutumiwa kwa kuendeleza mfumo wa lugha na utamaduni ambapo watu wenye asili ya Oromia hawatumii lugha hiyo.
Kanisa linakanusha shitaka hilo.
Hata hivyo mamlaka ya Ethiopia hapo awali ilishutumiwa na makundi ya haki za binadamu kwa kuzuia upatikanaji wa mtandao.
Soma zaidi:
- Ethiopia :Lifahamu taifa ambalo mwaka una miezi 13
- Haya ni mataifa yanayosherekea Krismasi leo Januari 7
Cheche za maneno zatanda kati ya DRC na Rwanda

Matamshi ya rais Paul Kagame dhidi ya rais wa DR Congo Felix Tshisekedi kuhusu hali ya usalama ya taifa lake hayakumfurahisha Waziri wa mawasiliano katika taifa hilo Muyaya Katembwe.
Akizungumza na vyombo vya habarisiku ya Alhamisi, Patrick Muyaya alisema kwamba matamshi ya kiongozi huyo wa Rwanda hayana ukweli wowote na kwamba anataka kuonesha kwamba kile kinachofanywa na wanajeshi wake ni haki.
“Tamko la Luanda lilitumiwa na jumuiya ya kimataifa kama sauti ambayo itaturuhusu kutatua tatizo hilo kwa muda mrefu…Hakuna mahali popote katika hati ya Bujumbura, ambapo taarifa ya Luanda ilitajwa….”,
Ni juu yake kuendelea “Leo, kuna ramani ya barabara ya kutatua tatizo la usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo… Maneno ya Kagame ni ya kawaida. Maneno anayotoa ni kujaribu kuhalalisha ajenda yake iliyofichwa ambayo inalenga kuweka mashariki mwa DRC katika hali ya kutokuwa na utulivu”.
Kulingana na Muyaya, Kagame lazima aelewe kwamba mpango wa vurugu umekwisha, lazima sasa tuimarishe amani.
“Haya ni matamshi yanayomruhusu kuendelea kusababisha madhara. Haki itapatikana hivi karibuni”, alimalizia Waziri huyo.
Kagame alisema Alhamisi hii wakati wa chakula cha jioni cha kila mwaka na mabalozi wa kidiplomasia huko Kigali "Tshisekedi amevunja makubaliano kadhaa aliyoafikia.
Melezo zaidi:
- Mzozo wa DRC na Rwanda : M23, majirani na bahati mbaya ya DRC
- Jumuiya ya Afrika Mashariki, majeshi na mustakabali wa amani DRC
- Ipi nafasi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutatua mvutano wa Congo na Rwanda?
- Kwa nini jeshi la Kenya linajiunga na mzozo wa DRC
Kiongozi wa zamani wa Kenya ahimiza wanajeshi zaidi wa kikanda kupelekwa nchini DR Congo

Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Mratibu wa mazungumzo ya amani na rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta ameelezea wasiwasi wake kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama nchini DR Congo. Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamehimizwa kuharakisha uwekaji wa wanajeshi wa ziada katika kikosi cha kikanda kinachotumwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta, mpatanishi wa jumuiya ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) anasema wanajeshi zaidi wanatakiwa kuchukua nyadhifa katika maeneo ambayo makundi yenye silaha yamejiondoa, kwa mujibu wa makubaliano ya kusitisha mapigano ya Luanda.
Bw Kenyatta alionyesha wasiwasi wake kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama katika jimbo la Kivu Kaskazini ambako waasi wa M23 wamepambana na vikosi vya usalama katika wiki za hivi karibuni.
Uganda na Sudan Kusini zinapanga kutuma wanajeshi baada ya wanajeshi kutoka Burundi na Kenya kuwasili mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwaka jana kusaidia kumaliza miongo kadhaa ya ukosefu wa utulivu.
Bw Kenyatta alikaribisha wito wa hivi majuzi wa kusitishwa kwa uhasama na pande zote katika mzozo huo na viongozi wa Afrika Mashariki.
Katika taarifa yake, mratibu huyo wa mazungumzo ya amani alisema ataimarisha mipango ya duru ya nne ya mazungumzo jijini Nairobi kwa kuhamasisha uungwaji mkono wa kikanda na kimataifa kwa mkutano huo.
Amezitaka pande zote zinazohusika kuharakisha utekelezaji wa maazimio ya mazungumzo ya tatu ya mashauriano jijini Nairobi.
Pia ameomba msaada wa haraka wa kibinadamu kwa zaidi ya watu nusu milioni waliokimbia makazi yao kutokana na mzozo katika jimbo la Kivu Kaskazini.
Mzozo huo umezorotesha uhusiano na DR Congo, ambayo inaituhumu nchi jirani ya Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23.
Rwanda inakanusha tuhuma hizo.
Melezo zaidi:
Zana za mawe za zaidi ya miaka milioni mbili iliyopita zafukuliwa nchini Kenya

Chanzo cha picha, Reuters
Wanaikiolojia nchini Kenya wamechimba baadhi ya zana kongwe zaidi za mawe zilizowahi kutumiwa na wanadamu wa kale, za nyuma karibu miaka milioni 2.9.
Wanasema ugunduzi huo ni ushahidi kwamba zana zilitumiwa na matawi mengine ya wanadamu wa mapema, sio tu mababu wa Homo Sapiens kama wanasayansi walivyofikiria hapo awali.
Watafiti wanasema meno mawili makubwa ya kisukuku yaliyopatikana kwenye eneo nchini Kenya ni ya binamu wa binadamu aliyetoweka, anayejulikana kama Paranthropus.
Timu ilipata ushahidi wa kupendekeza zana hizo zilitumika kuwachinja viboko na kusaga vifaa vya mimea kama vile mizizi na matunda.
Soma pia:

Chanzo cha picha, Reuters
Auawa na bastola yake iliyojifyatua kiunoni baada ya kuingia nayo kwa kificho kwenye chumba cha MRI

Chanzo cha picha, Jam Press via Independent
Mwanasheria mmoja wa Brazil amefariki kwa risasi baada ya bastola yake kufyatuka kwa bahati mbaya kwenye chumba cha uchunguzi cha MRI hospitalini.
Leandro Mathias de Novaes alimpeleka mama yake kwa uchunguzi kwenye maabara ya Laboratorio Cura huko São Paulo, Brazili, tarehe 16 Januari.
Inaeezwa mwanasheria huyo mwenye umri wa miaka 40 hakuwaambia wahudumu wa hospitali kuwa alikuwa na silaha licha ya kuambiwa yeye na mama yake kutoa vitu vyote vya chuma kabla ya kuingia kwenye chumba hicho cha uchunguzi au kuskani.
Kawaida MRI inatumia sumaku kusafirisha picha kwenda kwenye kompyuta. Baada ya kuingia kwenye chumba hicho chenye MRI maafa yalitokea kufuatia mzutano wa sumaku ya mashine hiyo na silaha ambayo ni chuma. Mvutano huo ulisababisha kuchomoka kwa silaha yake kabla ya kujifyatua na kumpiga wakili huyo tumboni.
Baadaye alikimbizwa katika Hospitali ya São Luiz Morumbi, ambako aliweza kutibiwa kwa wiki kadhaa, kabla ya kufariki dunia Februari 6.
Aliaga dunia tarehe 6 Februari baada ya kupigania maisha yake katika Hospitali ya São Luiz Morumbi.
Habari za hivi punde, Ubalozi wa Marekani Nairobi waonya kuhusu shambulio la kigaidi

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Kundi la wapiganaji wa Al -shabab Marekani imetoa tahadhari ya usalama kwa raia wake nchini Kenya kuhusu mashambulizi ya kigaidi yanayoweza kutokea nchini humo.
Ujumbe huo unaonya kuwa hoteli, balozi, mikahawa na maduka makubwa yanayotembelewa na wageni na watalii yanaweza kushambuliwa .
Haya yanajiri saa chache baada ya mamlaka nchini Kenya kutangaza majina ya wanaume watano wanaosakwa kwa ajili ya kuwa na uhusiano na kundi la Al Shabab.
Watano hao wameorodheshwa miongoni mwa watu wanaosakwa zaidi nchini Kenya kwa madai ya mashambulizi yaliyotekelezwa katika mji wa pwani wa Lamu.
Kundi hilo la kijihadi limelaumiwa kwa kufanya mashambulizi Kaskazini na pwani ya Kenya likilenga raia, maafisa wa usalama na vituo vya serikali.
Kundi tanzu la Al Qaeda limepata hasara kubwa katika siku za hivi karibuni, likiwapoteza makamanda wakuu, mamia ya wapiganaji na maeneo makubwa ya maeneo ya kati na Kusini mwa Somalia ambako wamekuwa wakidhibiti kwa miongo kadhaa.
Vurugu zaibuka bungeni Afrika Kusini wapinzani wakitaka kumzuia rais kuhutubia

Chanzo cha picha, Getty Images
Hotuba ya Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa kuhusu hali ya taifa hilo kwa mwaka 2023 ilikatizwa na dhihaka kutoka kwa chama kimoja cha upinzani na kusababisha ghasia bungeni mjini Cape Town.
Aliposimama kuanza hotuba kundi la wabunge lilijaribu kuzima hotuba yake, kabla ya kutakiwa kuondoka ndani ya bunge.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kundi la wabunge wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) wakiongozwa kingozi wao Julius Malema walijaribu kuvamia jukwaa, huku baadhi yao wakiwa wamebeba mabango, na kulazimika kuondolewa nje na walinzi katika moja ya matukio ya kutatanisha.
Utulivu ulivyopatikana, hotuba iliendelea.

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelfu wataka kumuasili mtoto mchanga aliyezaliwa chini ya vifusi vya tetemeko la ardhi Uturuki,

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelfu ya watu wamejitokeza kutaka kumuasili mtoto wa kike aliyezaliwa chini ya vifusi vya jengo lililoporomoka kaskazini-magharibi mwa Syria, kufuatia tetemeko la ardhi la Jumatatu.
Alipookolewa, mtoto huyo aliyepewa jina la Aya - maana yake muujiza kwa Kiarabu - alikuwa bado kitovu chake kilikuwa kimeungana na mamake aliyejifungua kwenye kifusi. Mama yake, baba yake na ndugu zake wote wanne walifariki baada ya tetemeko hilo kupiga mji wa Jindayris.
Aya sasa yuko hospitali. "Alifika Jumatatu akiwa katika hali mbaya sana, alikuwa na michubuko, alishikwa na baridi na alikuwa anapumua kwa shida," alisema Hani Marouf, daktari wa watoto anayemuhudumia.
Sasa yuko katika hali thabiti. Video za uokoaji wa Aya zilienea kwenye mitandao ya kijamii. Picha zilionyesha mwanamume mmoja akikimbia kutoka kwa kifusi cha jengo lililoporomoka, akiwa amemshikilia mtoto mchanga aliyekuwa ameenea vumbi.
Khalil al-Suwadi, jamaa wa mbali, ambaye alikuwepo wakati alipookolewa, alimleta mtoto mchanga huyo kwa Dk Marouf katika jiji la Syria la Afrin.

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelfu ya watu kwenye mitandao ya kijamii sasa wamekuwa wakiomba maelezo ya namna ya kumuasili. "Ningependa kumchukua na kumpa maisha ya heshima," alisema mtu mmoja.
Mtangazaji wa televisheni ya Kuwait alisema, "Niko tayari kumtunza na kumlea mtoto huyu... ikiwa taratibu za kisheria zitaniruhusu."
Meneja wa hospitali anakohudumiwa mtoto huyo, Khalid Attiah, anasema amepokea simu nyingi kutoka kwa watu kote ulimwenguni wakitaka kumuasili mtoto Aya.
Dk Attiah anayemuhudumia na ambaye ana binti mchanga wa tofauti ya minne zaidi, alisema, "Sitaruhusu mtu yeyote kumlea kwa sasa hadi itakapopatikana familia yake, ninamchukulia kama mmoja wa watoto wangu."
Kwa sasa, mkewe na Dk Attiah ndiye anayemnyonyesha pamoja na binti yao wenyewe.
Katika mji wa nyumbani kwa Aya wa Jindayris, watu wamekuwa wakitafuta wapendwa wao katika majengo yaliyoporomoka.
Tetemeko la ardhi Uturuki: Matumaini ya kupata manusura yanafifia vifo vikifikia 21,000

Chanzo cha picha, Getty Images
Idadi ya vifo kutokana na tetemeko la ardhi la Jumatatu sasa imezidi 22,300.
Maafisa wa Uturuki na madaktari wanasema kuwa watu 18,991 wamekufa kutokana na tetemeko hilo, huku vifo 3,377 vikiripotiwa Syria, kulingana na shirika la habari la AFP, na kufanya jumla ya vifo kuwa 22,368 kufikia sasa.
Umoja wa Mataifa unaonya kwamba kiwango kamili cha maafa hayo bado hakijafahamika.
Waokoaji bado wanatafuta manusura kwenye vifusi, lakini matumaini yanafifia ikiwa ni karibu saa 100 tangu kutokea kwa tetemeko hilo.
Hali ya baridi kali inatishia maisha ya maelfu ya walionusurika ambao sasa hawana makazi, maji na chakula.
Rais wa Uturuki aliita tetemeko hilo "janga la karne".Juhudi kubwa za kimataifa za kutoa misaada zinaongezeka kwa kasi.
Siku ya Alhamisi Benki ya Dunia iliahidi msaada wa dola $1.78bn kwa Uturuki ikiwa ni pamoja na fedha za haraka kwa ajili ya kujenga upya miundombinu ya msingi na kusaidia wale walioathiriwa na tetemeko la ardhi.
Hapo jana maafisa walisema kuwa watu 17,600 wamekufa nchini Uturuki na idadi ya vifo ilikuwa angalau 3,377 nchini Syria.
Idadi hiyo inazidi ile ya zaidi ya 17,000 waliouawa wakati tetemeko kama hilo lilipotokea kaskazini-magharibi mwa Uturuki mwaka 1999.
Makumi ya maelfu ya watu kote Uturuki na Syria wanalala kwa usiku wa nne wakijikinga na halijoto kali katika makazi ya muda baada ya kukosa makazi kutokana na tetemeko hilo.

