Licha ya Rais Rajapaksa kutangaza kujiuzulu, waandamanaji Sri Lanka hawatondoka kwenye makazi yake

Chanzo cha picha, Google
Waandamanaji wamesema hawataondoka na wataendelea kushikilia makaazi ya rais na waziri mkuu wa Sri Lanka hadi viongozi wote wawili watakapojiuzulu rasmi.
Rais Gotabaya Rajapaksa alisema atajiuzulu tarehe 13 Julai, kulingana na tangazo lililotolewa na spika wa bunge siku ya Jumamosi. Lakini rais mwenyewe hajaonekana au kutoa taarifa kwa umma.
Maelfu walifika Colombo Jumamosi wakimtaka ajiuzulu baada ya miezi kadhaa ya maandamano. Rais amelaumiwa kwa usimamizi mbaya wa uchumi wa nchi, ambao umesababisha uhaba wa chakula, mafuta na dawa kwa miezi kadhaa.
Waziri Mkuu Ranil Wickremesinghe pia alisema atajiuzulu kufuatia maandamano ya Jumamosi, ambapo makazi yake ya binafsi yalichomwa moto. Pamoja na kutangazwa kuachia ngazi, lakini waandamanaji wanasalia na mashaka kuhusu nia ya viongozi hao.





