Charles Ndereyehe: Mshukiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda atiwa nguvuni na kuachiliwa Uholanzi

Chanzo cha picha, SOCIAL MEDIA
Mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 Charles Ntahontuye Ndereyehe amekamatwa kutoka nyumbani kwake mjini Amsterdam nchini Uholanzi, kabla ya kuachiliwa kimesema chama chake.
"Alikamatwa kutoka nyumbani kwake ambako anaishi na mke wake ." Alisema rais wa chama cha chake cha FDU , Justin Bahunga akizunguma na BBC.
Kulingana na Bahunga mshukiwa huyo hatahivyo aliachiliwa na kurudi nyumbani baada ya kulala kizuizini wakati wakili wake alipoingilia kati
Bwana Ndereyehe ,70, ni mjumbe maarufu wa FDU na mkosoaji wa serikali ya Rwanda. Wakati wa mauaji ya kimbari alikuwa ni Mkuu wa taasisi ya utafiti wa kilimo ya serikali iliyopo kusini mwa Rwanda.
"Alipokuwa akikamatwa polisi walimwambia kuwa aliombwa na serikali ya Rwanda. Hicho ndicho tunachokifahamu ", Bwana Bahunga amesema.
Polisi bado hawajatoa kauli yoyote juu ya kukamatwa kwa Bwana Ndereyehe, ambaye amekuwa akiishi nchini Uholanzi kwa miaka zaidi ya 15.
Ndereyehe anashukiwa kuwa mmoja wa watu waliopanga mauaji ya mwaka 1994 na kesi yake ilisikilizwa bila mtuhumiwa huyo kuwepo katika mahakama ya kijadi maarufu Gacaca mwaka 2008.
Mnamo mwaka 2010, Rwanda ilitoa kibali cha kimataifa cha kumkamata na alikuwa katika orodha ya watu waliokuwa wakisakwa na polisi wa kimataifa Interpol.
Wakati huo huo Ofisi ya upelelezi wa uhalifu nchini (RIB) imekamilisha uchunguzi wake dhidi ya Paul Rusesabagina na itawasilisha faili za uchunguzi wake kwa waendesha mashitaka nchini humo Jumatano , umeandika wavuti wa gazeti la New Times.
Kiongozi huyo wa vuguvugu la upinzani la Rwanda -Rwanda Movement for Democratic Change (MRCD) anatuhumiwa kufanya makosa ya ugaidi, kuharibu mali kwa kuziteketeza kwa moto , utekaji nyara na mauaji. Bwana Rusesabagina amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais Paul Kagame .
Mnamo mwezi Julai mwaka 2018, kundi lenye silaha la vuguvugu lake la MRCD lilidai kuwa ndilo lililohusika na mashambulio katika mkoa wa kusini mwa Rwanda.

Rusesabagina alikamatwa tarehe 31 Agosti katika mji mkuu wa Muungano wa nchi za kiarabu Dubai.
Familia yake imezishutumu mamlaka za Rwanda kwa kumteka nyara na kuwakataa mawakili wake wawili wanaomuwakilisha katika kesi dhidi yake.
Akizungumza kuhusu kukamatwa kwake, Rais wa Rwanda Paul Kagame Jumapili alisema kwamba Paul Rusesabagina hakutekwa, alidanganywa akajileta mwenyewe nchini Rwanda.
Rais Kagame alisema kwamba lazima Rusesabagina awajibishwe kuhusu mauaji dhidi ya raia wa Rwanda kufuatia mashambulio ya makundi ya waasi anayoongoza yaliyofanywa dhidi ya maeneo ya Rwanda miaka miwili iliyopita.
Rusesabagina alifahamika kufuatia filamu ya Hotel Rwanda ikielezea jinsi alivyookoa maisha ya Watutsi waliokuwa wamekimbilia katika hoteli moja mjini Kigali aliyokuwa meneja wake mwaka 1994.
Hata hivyo manusura wa mauaji ya kimbari ya Rwanda walisema katika filamu hiyo alitia chumvi juu ya hali halisi ya mauaji ya kimbari na kupotosha ukweli juu ya mauaji ya kimbari.

Chanzo cha picha, RIB
Rais Paul Kagame alisema kikubwa sio ushujaa wa Bwana Rusesabagina au vitendo vyake wakati wa mauaji ya kimbari akisema kinachoangaliwa kwa sasa ni yeye.
kuwajibishwa kuhusu vitendo alivyotaja kuwa vya mauaji dhidi ya raia wa Rwanda.
Ripoti ya baraza la haki za binadamu lilisemaje ?
Baraza la kimataifa kuhusu msaada wa kibinadamu nchini Rwanda limekana madai kwamba kuna wakili aliyechaguliwa kumwakilisha mpinzani wa rais wa Rwanda Paul Rusesabagina.
''Kwa siku kadhaa , wakili anayemwakilisha Rusesabagina nchini Rwanda amezuiwa kumuona mteja wake'', ilisema ripoti hiyo.
Ripoti ya baraza hili lilisema sema mtu asiyejulikana kwa familia ya Rusesabagina alifanya kikao na vyombo vya habari akisema kwamba ndie anayemwakilisha mshukiwa huyo.
Hatahivyo baraza hilo lilikataa katakata kuhusu uwakilishi huo likisema kwamba hiyo ni njia moja ya ukiukaji wa haki ambao jamii ya kimataifa haifai kuvumilia.












