Rais Vladmir Putin amesema nchi za magharibi zinailaghai mataifa ya Afrika

Vladmir Putin ana mipango kabambe kwa Afrika?

Raisi wa Urusi, Vladmir Putin amesema kuwa nchi yake inaweza kuisaidia Afrika bila masharti ambayo huambatanishwa kwenye misaada ya mataifa ya magharibi.

''Tunaona jinsi mataifa ya magharibi yanavyotoa mashinikizo na vitisho dhidi ya serikali huru za kiafrika,'' Putin ameeleza katika mahojiano na shirika la habari la Urusi TASS, kabla ya mkutano na viongozi wa Afrika.

''Wanatumia njia hizo ili kurejesha nguvu ya ushawishi na utawala kwenye makoloni yao ya zamani na kulinyonya bara la Afrika,'' aliongeza.

Urusi inatarajia kuwa mwenyeji wa viongozi 47 wa Afrika katika mkutano wa tarehe 23 -24 mwezi Oktoba mjini Sochi.

Bwana Putin amesema mahusiano na Afrika yemeimarika, akiainisha makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya silaha, ambapo Urusi imefanikiwa kushawishi mataifa zaidi ya 30 kuwasambazia silaha.

Rwanda ni moja ya nchi ambazo zimekuwa na mahusiano mazuri sana na Urusi

Baraza la mawaziri la Rwanda hivi karibuni liliridhia makubaliano na urusi katika masuala ya matumizi ya nishati ya nyukilia kwa ''matumizi ya amani'',Gazeti la The East Africa limeripoti.

Teknolojia hii itatumika katika uzalishaji wa nishati na utunzaji wa mazingira, ripoti imeeleza.

Donald Trump amekuwa kwenye mipango kabambe kurejesha mahusiano mazuri na Afrika

Chanzo cha picha, Getty Images

Nchi za Magharibi zina mpango wa kurejesha ushawishi barani Afrika?

Marekani imekuwa ikipoteza ushawishi barani Afrika- lakini mwanadiplomasia wa juu wa nchi hiyo barani Afrika anataka kubadili hali hiyo.

Trump alishawahi kuripotiwa kuyataja mataifa ya kiafrika kuwa ni ''nchi chafu'' na kuongelea Afrika kama sehemu ambayo marafiki zake wanakwenda kujaribu kutajirika.

''Kwa muda mrefu wakati wawekezaji walipokuwa wakibisha milango na waafrika wakifungua, mtu pekee aliyekuwa hapo ni mchina,'' Tibor Nagy, mjumbe wa maswala ya Afrika wa Marekani aliiambia BBC.

Biashara ya China na bara la Afrika imeifunika Amerika katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, na mwaka 2018 ilikuwa kubwa mara tatu zaidi.

Marekani imekuwa chanzo kikubwa cha uwekezaji wa moja kwa moja barani Afrika, lakini mchango wake umekuwa ukipungua.

Mwaka 2018, China ilitangaza uwekezaji wa thamani ya dola za kimarekani bilioni 60 kwa ajili ya miradi ya miundombinu.

Bi Benabdallah amesema kuwa biashara kati ya Marekani na mataifa ya Afrika imeshuka kwa sababu ya ongezeko la uhitaji si tu China,lakini nchi nyingine kama vile Urusi na Uturuki.

''Nafikiri ni kwa sababu ushindani kutoka kwa nchi nyingine umeongezeka katika kipindi cha muongo mmoja uliopita,'' amesema bi Benabdallah.

Ukuaji wa uchumi wa China umeonyesha dalili za kushuka hivi karibuni, hali ambayo itaathiri biashara na uwekezaji katika Afrika siku za usoni.

Lakini kutokana na ushindani kutoka duniani kote kwa kufanya biashara na nchi za kiafrika, Marekani inapambana kurejesha mahusiano na bara la Afrika kwa kujihusisha na nchi za uchumi unaochipukia.