Uchunguzi dhidi ya Trump: Ikulu ya White House yatoa taarifa inayothibitisha baadhi ya madai dhidi ya raisi

Pelosi and Trump

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Spika wa bunge la congress kutoka chama cha Democrat Nancy Pelosi (kushoto)amesema kuwa rais Trump "lazima awajibike
Muda wa kusoma: Dakika 5

Ikulu ya White House imetoa taarifa ya kina juu ya mazungumzo ya simu baina ya rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Ukraine.

Mazungumzo hayo ya simu yamewafanya wabunge kutoka chama cha upinzani cha Democrats kuanzisha uchunguzi rasmi wenye lengo la kumng'oa madarakani bw Trump.

Wabunge wa Democrats wanamshutumu Trump kwa kutaka usaidizi kutoka kwa taifa la kigeni ili kumuangamiza hasimu wake wa kisiasa.

Taarifa ya White House inathibitisha kuwa, mnamo Julai 25, Trump alimuomba rais Volodymyr Zelenski kumchunguza makamo wa rais wa zamani wa Marekani Joe Biden ambaye anasaka tiketi ya urais kupitia chama cha Democrats, ambaye mtoto wake alikuwa akifanya kazi na shirika la gesi la Ukraine.

Bw Trump anakanusha kuwa alizuia msaada wa kijeshi kwa Ukraine kama njia ya kuishinikiza nchi hiyo kumsaidia kumchafua adui wake wa kisiasa, bw Biden.

Taarifa juu ya mazungumzo hayo ya simu yametolewa na mtoa taarifa wa siri.

Trump aliahidi jana Jumanne kutoa ushirikiano wa kikamilifu juu ya suala hilo kwa kuchapisha mazungumzo yote bila kuondosha hata kipande.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Ikulu ya White House leo Jumatano si mnakala ya mzungumzo, bali mukhtasari wa mazungumzo hayo ambao uliandaliwa na maafisa wa Ikulu hiyo ambao walikuwepo wakati wa mazungumzo yakifanyika.

Hii leo Trump amesema uchunguzi huo ni "kisa kikubwa zaidi cha kusaka mchawi katika historia ya Marekani."

Mazungumzo hayo ya simu baina ya maraisi hao wawili yalifanyika siku chache baada ya Trump kuiagiza serikali yake kuzuia msaada wa kijeshi wa dola milioni 391 kwenda Ukraine.

Katika mukhtasari wa White Houe suala hilo la msaada wa kijeshi halijagusiwa.

Kwa mujibu wa mukhtasari, Trump alimwambia Zelensky juu ya namna ambavyo Joe Biden akiwa makamu wa rais alishawishi Ukraine kumtimua kazi mwendesha mashtaka wake mkuu, Viktor Shokin mwaka 2016.

Trump

Chanzo cha picha, The Washington Post/Getty

Ofisi ya Shokin ilifungua jalada la uchunguzi dhidi ya Burisma, kampuni ya gesi asili ambayo mwana wa Joe Biden, Hunter alikuwa ni mjumbe wa bodi yake.

Nchi kadhaa za magharibi pia zilikuwa zikishinikiza Bw Shokin atimuliwe kazi kwa madai alikuwa akivumilia vitendo vya rushwa.

"Nimesikia mlikuwa na mwendesha mashtaka ambaye alikuwa ni mzuri kweli na alifutwa kazi kwa njia ya uonevu. Watu wengi wanalizungumzia jambo hilo," Trump ananukuliwa akisem kwenye mazungumzo hayo na kuongeza: "Kitu kingine, kuna mjadala mkubwa kumhusu mtoto wa Biden, kuwa baba yake alizuia waendesha mashtaka na watu wengi wanataka kujua undani wa hilo, so chochote unachoweza kufanya na Mwanasheria Mkuu (wa Marekani) litakuwa jambo jema.

"Biden alikuwa akijitamba kuwa amezuia uchunguzi angalia utakachokifanya hapo...ni jambo baya sana kwangu."

Zelensky anaripotiwa kujibu: "Tutalishughulikia hilo na tutafanyia kazi uchunguzi wa kesi hiyo.

"Juu ya hilo, pia ningeomba kama una taarifa zozote za ziada pia tupatie, zitatusaidia sana."

Akimshukuru Trump, bw Zelensky alisema kuwa alikaa kwenye jumba lake la jijini New York, Trump Tower, mara ya mwisho alipozuru nchini humo.

Spika wa bunge la wawakilishi atangaza kuanza uchunguzi

Speaker of the House Nancy Pelosi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Awali Spika Nancy Pelosi alikataa kuanzishwa kwa uchunguzi dhidi ya rais

Spika wa bunge la wawakilishi la congress kutoka chama cha Democrats Nancy Pelosi amesema kuwa rais "lazima awajibike ".

Huku kukiwa na uungaji mkono mkubwa kutoka kwa wafuasia wa Democrats juu ya uchunguzi huo unaoweza kumuondoa mamlakani , ikiwa utaendelea huenda usipitishwe na baraza la seneti - linalodhibitiwa na wabunge wa chama cha Trump cha Republican.

Katika tangazo lake Bi Pelosi alisema kuwa kamati nyingine sita zinazofanya uchunguziwa masuala mengine dhidi ya Trump nzitaendelea na uchunguzi wao chini ya uchunguzi wa sasa.

Ikiwa uchunguzi huu utaendelea, Bunge la wawakilishi litapigia kura mashtaka yoyote yatakayobainika na kwasababu Democrats ndio wengi katika bunge la congress wanaweza kupitisha umuzi wa kumshtaki.

Hata hivyo maamuzi hayo yanaweza kupelekwa katika bunge la Seneti ambako theluthi tatu ya wabunge inahitajika kupitisha maamuzi - na huko Republicans wataweza kuzuwia mashtaka.

Bwana Trump amekiri kuwa alimzungumzia Joe Biden na Bwana Zelensky lakini akasema alikuwa tu akijaribu kuitaka Ulaya iingilie kati kutoa msaada kwa kuitishia kusitisha msaada wa kijeshi.

Bi Pelosi alisema kuwa Bwana Trump amefanya kosa la "ukiukaji wa sheria ", na kuyataja matendo yake kama "uvunjaji wa wajibu wake wa kikatiba''.

Unaweza pia kusoma:

"Wiki hii rais Trump alikiri kumuomba rais wa Ukraine kuchukua hatua ambazo zitamnufaisha kisiasa ," alisema, na kuongeza kuwa : "Rais lazima awajibishwe."

Kama Spika wa bunge, Bi Pelosi ni afisa wa ngazi ya juu zaidi wa Democrat. Bi Pelosi awali amekuwa akipinga miito ya kutaka amuondoe madarakani rais wa Republican akidai juhudi za aina hiyo zinaweza kuimarisha uungaji mkono kwa Trump.

Trump anashutumiwa kuwashinikiza viongozi wa Ukraine kumchunguza hasimu wake kisiasa Joe Biden(kulia)

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Trump anashutumiwa kuwashinikiza viongozi wa Ukraine kumchunguza hasimu wake kisiasa Joe Biden(kulia)

Bwana Biden amekanusha kufanya kosa lolote na pia anaunga mkono juhudi za kumfanyia upelelezi rais iwapo hataonyesha ushirikiano katika sakata hiyo dhidi yake.

Uchunguzi dhidi ya Bwana Trump "unaweza kuwa janga ", alisema Bwana Biden . "Lakini janga alilojitengenezea mwenyewe ." Kwa sasa ndiye mtu aliyemstari wa mbele katika kukabiliana na Bwana Trump katika uchaguzi wa 2020.

Bwana Trump amejibu vipi ?

Akiwa katika kikao cha Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York hii leo, Trump amesema uchunguzi huo ni "kisa kikubwa zaidi cha kusaka mchawi katika historia ya Marekani."

"Jinsi ilivyoelezwa hapo mwanzo, ni kana kwamba ni simu kutoka jehanamu... lakini ilikuwa ni simu ya kawaida tu."

Katika msururu wa jumbe zake za twita hapo jana Trump alisema Democrats wana lengo la "makusudi la kuharibu " ziara yake katika Umoja wa Mataifa " kwa taarifa zaidi za hivi punde za hila chafu za takataka ".

"Hata hawajaona ujumbe ulioandikwa wa simu wanazodai nilipiga . Hila tupu !" aliongeza

Aliahidi kutoa ujumbe wa mazungumzo baina yake na mwenzake wa Ukraine kwa maandisi siku ya Jumatano ili kuonyesha kuwa "ulikuwa unafaa kabisa".

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

Katika jibu lake , Kiongozi wa Republican bungeni Kevin McCarthy amesema : " ilitokea Pelosi akawa Spika wa bunge hili , lakini hazungumzi kwa niaba ya Wamarekani inapokuja katika suala hili ."

"Hawezi kuamua peke yake kuwa tutakuwa katika upelelezi ," alisema.

Wakati huo huo , kaimu mkurugenzi wa shirika la taifa la ujasusi nchini Marekani , Joseph Maguire, amekataa kushirikisha bunge la Congress ripoti ya mtu aliyefichua taarifa za shutuma dhidi ya Trump . Anatarajiwa kutoa ushahidi mbele ya kamati ya umma ya ujasusi siku ya Alhamisi.

Kura ya maoni iliyoendeshwa na shirika la A YouGov ilisema kuwa 55% ya Wamarekani wangeunga mkono kushtakiwa kwa Trump ika ingethibitishwa kwamba Trump alisitisha msaada wa kijeshi kwa ukraine ili kuwashinikiza maafisa wa nchi hiyo kumchunguza Joe Biden.