Rebecca Kadaga ,Spika wa bunge la Uganda ataka waliomtesa Bobi Wine kukamatwa

Bobi Wine (katikati) baada ya kuachiliwa kwa dhamana Jumatatu
Maelezo ya picha, Bobi Wine (katikati) baada ya kuachiliwa kwa dhamana Jumatatu

Spika wa bunge la Uganda Rebecca Kadaga ametaka kukamatwa mara moja kwa polisi waliohusika kumpiga na kumjeruhi vibaya mbunge na mwanamuziki Bobi Wine pamoja na wabunge wenzake.

Kadaga ameandika barua hiyo kwenda kwa Rais wa Uganda Yoweri Museveni.

Bobi Wine ambaye jina lake kamili ni Robert Kyagulanyi, aliachiliwa kwa dhamana siku ya Jumatatu lakini akiwa katika afya dhoofu pamoja na makovu ya kipigo.

Rebecca Kadaga amekua spika wa bunge la Uganda tokea Mei 2011
Maelezo ya picha, Rebecca Kadaga amekua spika wa bunge la Uganda tokea Mei 2011

Mwanasiasa mwingine ambaye aliwekwa kizuizini pamoja naye Kassiano Wadri ameiambia BBC kuwa Bobi Wine alipigwa mara kwa mara na walinzi wa Rais ambao wengine walikua wamefisha nyuso zao.

Serikali imekanusha tuhuma hizo na kuziita za uongo.

Zaidi ya watu 30 walikamatwa wakihusishwa na uvamizi wa msafara wa Rais Museveni wiki mbili zilizopita na wote wameachiliwa kwa dhamana.