Atletico Madrid yapata bao la ugenini dhidi ya Arsenal

Chanzo cha picha, Getty Images
Antoine Griezmann aliiadhibu safu ya ulinzi ya Arsenal katika dakika za lala salama huku timu ya Atletico iliokuwa na wachezaji 10 kupata sare katika nusu fainali ya kombe la bara Yuropa iliofanyika katika uwanja wa Emirates.
Wageni hao wa Uhispania walilazimika kurudi nyuma na kulinda lango lao katika kipindi kirefu cha mchezo baada ya beki Sime Vrsajko kupewa kadi nyekundu kwa kucheza visivyo katika dakika 10 za kwanza.

Chanzo cha picha, Reuters
Huku kocha wao pia naye akiondolewa katika eneo la kocha na kulazimishwa kuketi na mashabiki baada ya kumkaripia refa kwa hatua yake.
Uhispania ilinusurika mashambulizi makali kutoka kwa mshambuliaji wa Arsenal Alexandre Lacazette akigonga mwamba wa goli katika fursa ya wazi ya Arsenal.

Chanzo cha picha, Reuters
Lacazette alifunga krosi ya Jack Wilshere baada ya saa moja na kuipatia Arsenal fursa ya kufuzu katika fainali ya kombe hilo .
Lakini ikiwa zimesalia dakika nane pekee, Griezman alivamia lango la Arsenal baada ya beki Laurent Kolscieny kufanya masikhara na kuwapatia Atltico Madrid fursa ya kufuzu nyumbani siku ya Alhamisi ijayo.

Chanzo cha picha, Reuters
Mashabiki wa Arsenal waliwachwa wakilalama kuhusu timu hiyo kushindwa kukamilisha fursa za wazi katika mechi ya mwisho ya nyumbani ya yuropa ya Arsene Wenger.
Arsenal sasa italazimika kuvunja safu ya ulinzi ya Atletico ambayo imefungwa mara nne pekee katika ligi ya La Liga msimu huu ili kuweza kuwa na matumaini ya kuongeza ufanisi wa Wenger katika uongozi wake wa miaka 22 wakati watakapofuzu kwa fainali Mei 16.












