Watu wanne wauawa kwenye ghasia mjini Nairobi, Kenya

Pikipiki ikiteketea eneo la Ruaraka wakatia wa ghasia Nairobi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Pikipiki ikiteketea eneo la Ruaraka wakati wa ghasia Nairobi

Takriban watu wanne wamethibitishwa kuuawa wakati wa mashambulizi kwenye mtaa wa Mathare mjini Nairobi nchini Kenya

Wakaazi wa mtaa huo wa mabanda wanadai kuwa makundi yaliyokuwa yamejihami kwa panga na silaha zingine yalivamia mtaa huo na kuwaua watu hao ambapo pia waliharibu mali.

Wafuasi wa Raila Odinga mtaa wa River Nairobi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wafuasi wa Raila Odinga mtaa wa River Nairobi

Polisi wanasema kuwa wanachunguza kisa hicho na nia yake.

Wakaazi wanasema waliamka kwa mshangao asubuhi walipopata miili ya watu wanne iliyokuwa na majeraha.

Kuuliwa kwa watu hao kumesababisha ghasia kusambaa hadi mitaa iliyo karibu huku polisi wakikabiliana na wale waliokuwa wakilalamikia mauaji hayo.

Kamanda wa polisi mjini Nairobi Japheth Koome alithibitisha mauaji hayo na kusema kuwa uchunguzi unafanywa, lakini akatupilia mbali madai kuwa yamesababishwa na ghasia za kikabila kufuatia hali ya kisiasa iliyopo sasa.

Kinara wa Nasa Raila Odinga akiwahutubia wafuasi mtaa wa Ruaraka Nairobi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kinara wa Nasa Raila Odinga akiwahutubia wafuasi mtaa wa Ruaraka Nairobi

Mauaji hayo yanatokea siku moja baada ya watu wengine watano kuuwa wakati wa shughuli ya kumkaribisha kinara wa upinzani ambaye amekuwa ziarani Ulaya na Marekani.

Polisi wanasema kuwa wale waliouawa walikuwa ni wezi waliopigwa na watu waliokuwa na hasira.