Kimbunga Hermine chakumba pwani ya Florida

Picha ya NOAA iliyopigwa Septemba 1, 2016

Chanzo cha picha, NOAA

Maelezo ya picha, Hermine ndicho kimbunga cha kwanza kukumba Florida katika karibu siku 4,000

Kimbunga Hermine kimefika maeneo ya kaskazini mwa Florida, Marekani na kuwa kimbunga cha kwanza kukumba jimbo hilo tangu mwaka 2005.

Kimbunga hicho kilifika katika ghuba ya Florida mapema Ijumaa kikiwa katika kitengo nambari moja, na kusababisha mvua kubwa na upepo.

Gavana Rick Scott ametangaza hali ya tahadhari katika kaunti 51 za jimbo hilo huku wakazi wakijiandaa kwa athari za kimbunga hicho.

Upepo ulioandamana na kimbunga hicho ulifikia kasi ya 80mph (130km/h) Alhamisi, kwa mujibu wa taasisi ya taifa ya Marekani inayofuatilia vimbunga.

Maafisa katika mji mkuu wa jimbo hilo Tallahassee, ambao utakumbwa na kimbunga hicho, wamesema karibu nyumba 70,000 kwa sasa hazina umeme.

Kimbunga cha mwisho kukumba Florida kilikuwa Wilma Oktoba 2005, na kilitokea mwaka ambao kimbunga cha Katrina kilitokea.

Kimbunga hicho kilisababisha vifo vya watu watano na uharibifu wa karibu $23bn (£17bn).

Miti iliangushwa na upepo mkali Carabelle

Chanzo cha picha, AP

Maelezo ya picha, Miti iliangushwa na upepo mkali Carabelle
Mji wa Tarpon Springs unajiandaa kukumbwa na mafuriko

Chanzo cha picha, AP

Maelezo ya picha, Mji wa Tarpon Springs unajiandaa kukumbwa na mafuriko

"Hili linatishia maisha. Hatujashuhudia kimbunga katika miaka mingi," Gavana Scott amesema.

Ameongeza kwamba maafisa 8,000 wa usalama na uokoaji wamewekwa tayari kusaidia raia.