'Nimeshuhudia hukumu 500 za kifo lakini sijawahi kuona kama ya Christa Pike'

Chanzo cha picha, AP
Mwandishi mkongwe wa habari Michael Graczyk, ambaye alifuatilia na kuripoti kuhusu takriban hukumu 500 za kifo katika jimbo la Texas, amesema hakushangazwa na tukio la hivi karibuni la Christa Pike, mfungwa ambaye aliendelea kuonyesha dalili za uhai baada ya kupewa dawa ya utekelezaji wa hukumu ya kifo.
Graczyk, ambaye aliendelea kuripoti kuhusu utekelezaji wa hukumu za kifo hata baada ya kustaafu kutoka Associated Press mwaka 2018, anasema ameshuhudia visa vya kipekee wakati wa kazi yake. Anakumbuka angalau matukio mawili ambapo sindano zililazimika kutolewa na kuingizwa tena kabla ya utekelezaji kukamilika, lakini hajawahi kushuhudia mfungwa akinusurika baada ya mchakato huo kuanza.
Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti wiki hii nchini Tennessee, ambako Christa Pike, mwenye umri wa miaka 50, aliendelea kupumua na kukoroma kwa sauti kubwa hata baada ya kupewa dozi mbili za pentobarbital, dawa inayotumiwa katika utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa njia ya sindano yenye sumu.
Akizungumza na BBC News, Graczyk alisema tukio hilo lisilo la kawaida halikumshangaza sana.
"Kwangu mimi, ilionekana kuwa ni suala la muda tu," alisema.
Kauli yake inaashiria mjadala mpana unaoendelea Marekani kuhusu matumizi ya dawa za utekelezaji wa hukumu ya kifo na uwezekano wa kutokea kwa matatizo wakati wa mchakato huo.

Chanzo cha picha, Reuters
Itifaki ya utekelezaji wa hukumu ya kifo katika jimbo la Tennessee inaruhusu mfungwa kupewa raundi ya pili ya sindano ya dawa ya pentobarbital iwapo hatafariki baada ya dozi ya kwanza. Hata hivyo, kwa mujibu wa Associated Press, utaratibu huo hauelezi hatua zinazopaswa kuchukuliwa ikiwa mfungwa ataendelea kuwa hai hata baada ya dozi ya pili.
Baada ya tukio hilo lisilo la kawaida lililomhusu Christa Pike, Gavana wa Tennessee, Bill Lee, alisitisha utekelezaji wa hukumu za kifo katika jimbo hilo na kuagiza uchunguzi huru kuhusu taratibu zinazotumika.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tukio hilo limeibua mjadala kuhusu matumizi ya sindano ya kifo nchini Marekani, ambapo utekelezaji wa hukumu hizo umekuwa ukikabiliwa na changamoto kwa karibu muongo mmoja. Upungufu wa kemikali zinazotumiwa katika sindano za kifo umeyalazimu baadhi ya majimbo kubadili aina ya dawa zinazotumika au kuzipata kutoka kwa wasambazaji wenye utata.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya majimbo ya Marekani yameanza kurejea mbinu nyingine za utekelezaji wa hukumu ya kifo, ikiwemo matumizi ya kikosi cha kufyatua risasi kama njia mbadala.
Wakati uchunguzi ukiendelea, Pike amelazwa hospitalini na anaendelea kupatiwa matibabu ya kuokoa maisha, kwa mujibu wa wakili wake. Tukio hilo limeibua maswali mapya kuhusu ufanisi na usalama wa taratibu za utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa kutumia sindano yenye sumu nchini Marekani.
Kwa mujibu wa wakili wake, Pike amelazwa hospitalini ambako anapatiwa matibabu ya kuokoa maisha.
Licha ya kuwa sindano ya sumu ndiyo mbinu inayotumika zaidi kutekeleza adhabu ya kifo katika majimbo 27 ya Marekani, mchakato huo haujawahi kukosa changamoto. Kituo cha Taarifa kuhusu Adhabu ya Kifo (Death Penalty Information Center) kinafafanua utekelezaji ulioshindikana au kutibuka kuwa ule unaokumbwa na matatizo au ucheleweshaji usiotarajiwa unaosababisha mateso yasiyo ya lazima kwa mfungwa au kuonyesha uzembe mkubwa katika utekelezaji wake.
Tangu mwaka 1982, shirika hilo limerekodi matukio 64 ya utekelezaji wa adhabu ya kifo yaliyoharibika nchini Marekani, huku 51 kati ya hayo yakihusisha sindano ya sumu. Katika visa saba, mchakato huo ulisitishwa baada ya maafisa kushindwa kupata mshipa wa kuingiza dawa hizo.
Hata hivyo, kisa cha Christa Pike kimezua maswali mapya kwa sababu kilitofautiana na matukio mengi yaliyowahi kushuhudiwa hapo awali. Michael Graczyk, mwandishi mkongwe ambaye amefuatilia karibu utekelezaji 500 wa hukumu za kifo katika jimbo la Texas, alisema hajawahi kuona hali ambayo utekelezaji unashindwa baada ya dawa tayari kuingizwa mwilini mwa mfungwa.
"Hili halijawahi kutokea hapa," alisema, akirejelea uzoefu wake wa miongo kadhaa ya kuripoti utekelezaji wa hukumu za kifo Texas.
Katika kipindi cha miaka 46 alichofanya kazi katika shirika la habari la Associated Press (AP), Graczyk aliripoti masuala mbalimbali. Hata hivyo, anasema jukumu la kushuhudia utekelezaji wa hukumu za kifo lilikuwa miongoni mwa majukumu muhimu zaidi ya taaluma yake.
"Hakuna mamlaka makubwa zaidi ambayo serikali inayo juu ya raia wake kuliko uwezo wa kuondoa uhai wake," alisema.
Takwimu za Death Penalty Information Center zinaonyesha kuwa watu 1,683 wameuawa kupitia adhabu ya kifo nchini Marekani tangu Mahakama ya Juu irejeshe adhabu hiyo mwaka 1976. Texas ndiyo jimbo lililotekeleza hukumu nyingi zaidi, likiwa limeua watu 602 waliohukumiwa kifo. Mwaka 1982, Texas pia liliandika historia kwa kuwa jimbo la kwanza nchini humo kutumia sindano ya sumu kama njia ya utekelezaji.
Kwa Graczyk, uwepo wa waandishi wa habari wakati wa utekelezaji wa hukumu hizo ni muhimu kwa uwajibikaji wa umma na uwazi wa serikali.
"Siku zote nimeamini kuwa ni muhimu mtu asiye na maslahi yoyote katika matokeo ya kesi kuwepo kushuhudia kile kinachotokea na kuwaambia wengine: Hiki ndicho nilichokiona, na hivi ndivyo ilivyotokea."

Chanzo cha picha, Through the steel bars of the observation area of the Texas State Prison in Huntsville, a stretcher with sheets, a pillow and straps can be seen in an execution chamber with green walls and door.Photo credit,Jenevieve Robbins/Texas Dept of Criminal Justice/Handout via Reuters
Ingawa amestaafu rasmi, Michael Graczyk bado huchangia kama mwandishi huru wa Associated Press (AP), akiendelea kufuatilia na kuripoti utekelezaji wa hukumu za kifo katika jimbo lake la Texas. Kwa miaka mingi ya kushuhudia matukio hayo, amesema amejifunza kuwa nyuma ya kila utekelezaji kuna familia ya mwathiriwa inayobeba maumivu makubwa, hata pale ambapo macho yote ya umma yanaelekezwa kwa mfungwa.
Graczyk anaamini waathiriwa mara nyingi husahaulika katika mijadala inayozunguka adhabu ya kifo, jambo ambalo humgusa sana, hasa wakati kesi fulani zinapopata uangalizi mdogo wa vyombo vya habari.
"Ninawasikitikia wahanga katika kesi hii. Wao ndio waliosahaulika. Daima wamekuwa hivyo," alisema.
Akiizungumzia kisa ya Christa Pike, alisema mijadala mingi imejikita kwa mfungwa huyo huku maumivu ya familia ya mwathiriwa yakipewa nafasi ndogo.
"Leo hii macho yote yameelekezwa kwa mfungwa wa Tennessee. Hakuna anayeangazia jamaa zake, isipokuwa familia ya karibu ya mwathiriwa. Ninaelewa kuwa hiyo ndiyo kazi yetu, lakini hilo halihalalishi mtazamo huu hata kidogo," alisema.
Mwathiriwa katika kesi hiyo alikuwa Colleen Slemmer, kijana mwenye umri wa miaka 19 kutoka Florida ambaye, kwa mujibu wa familia na marafiki zake, alipenda kuteleza kwa viatu vya magurudumu (rollerblading), kuwasaidia wengine na alikuwa na tabasamu la kuvutia. Slemmer aliuawa baada ya kuteswa na Christa Pike pamoja na mpenzi wake wa wakati huo, Tadaryl Shipp, baada ya kukutana naye katika kituo cha mafunzo ya ufundi.
Mama wa Slemmer, May Martinez, alikuwepo Tennessee wakati wa jaribio la kutekeleza hukumu ya kifo dhidi ya Pike Jumatano. Baadaye aliliambia NBC News kwamba tukio hilo lilikuwa "vurugu tupu", akielezea hali ya mshtuko iliyotokana na kushindwa kwa utekelezaji huo kukamilika kama ilivyotarajiwa.
Akizungumzia utaratibu wa utekelezaji wa hukumu za kifo Texas, Graczyk alisema mashahidi huwa hawaruhusiwi kuingia katika chumba cha utekelezaji wakati maafisa wanapoweka dripu ya mishipani kwa mfungwa.
"Tunapoingia ndani ya chumba hicho, mfungwa huwa tayari ameunganishwa na mashine," alisema.
Kwa mujibu wake, bomba la dripu kwa kawaida huwekwa katika eneo la kiwiko cha mkono. Hata hivyo, ikiwa hilo haliwezekani, linaweza kuingizwa kwenye sehemu nyingine za mwili kama vile nyuma ya kiganja, mguuni, shingoni au maeneo mengine yenye mshipa unaoweza kufikiwa.
Graczyk amesema katika utekelezaji unaokwenda kama ulivyopangwa, wafungwa wengi hupoteza fahamu ndani ya sekunde chache baada ya dawa kuingizwa mwilini.
"Walipoteza fahamu waziwazi ndani ya sekunde chache," alisema.
Aliongeza kuwa mara nyingi kifo huthibitishwa kati ya dakika 20 na 40 baada ya sindano ya sumu kutolewa, jambo ambalo ndilo limefanya tukio la Christa Pike lionekane la kipekee na lisilo la kawaida hata kwa watu waliobobea katika kufuatilia utekelezaji wa hukumu za kifo.

Chanzo cha picha, The Tennessean/Reuters
Licha ya kushuhudia mamia ya utekelezaji wa hukumu za kifo katika kipindi chake cha uandishi wa habari Michael Graczyk anasema kuna tukio ambalo hatawahi kulisahau.
Anakumbuka hukumu ya kifo ya Jonathan Nobles mwaka 1998 huko Texas. Nobles alikuwa amehukumiwa baada ya kupatikana na hatia ya kuwaua wanawake wawili wa Austin, Kelley Fraquhar na Mitzi Johnson-Nalley, mwaka 1986.
Dakika zake za mwisho zilibaki zimejikita katika kumbukumbu za Graczyk kwa sababu ya jambo alilosema kabla ya kufariki. Nobles alianza kuimba wimbo maarufu wa Krismasi, Silent Night, huku akiwa amelala kwenye kitanda cha utekelezaji wa hukumu.
"Alipofika kwenye mstari unaosema 'Round yon virgin' ghafla akaacha kuimba," Graczyk aliiambia BBC News. "Ndiyo ilikuwa momenti ambayo dawa ilianza kufanya kazi na akapoteza fahamu."
Karibu miongo mitatu baadaye, kumbukumbu hiyo bado haijafutika akilini mwake.
"Hata leo, ninapokuwa kanisani wakati wa Krismasi na kusikia kwaya ikiimba Silent Night, huwa ninakumbuka tukio hilo. Mara nyingi nahisi huenda mimi ndiye pekee miongoni mwa waumini waliopo anayelibeba kumbukumbu hiyo."
Licha ya uzoefu huo wa kipekee, Graczyk hataki taaluma yake itambulike kwa kuripoti utekelezaji wa hukumu za kifo pekee. Anasema mara nyingi watu wanaposikia kuhusu kazi yake, jambo la kwanza hutaka kujua ni jinsi ilivyokuwa kushuhudia watu wakifariki.
"Watu wengi hawapati nafasi ya kushuhudia kifo cha mtu," alisema.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa hiyo ilikuwa sehemu ndogo tu ya kazi yake ndefu ya uandishi wa habari.
"Hilo si jambo pekee nililofanya, au nitakalofanya," alisema.

































