Mwathirika wa Mrusi aliyerekodi video za faragha za wanawake azungumza na BBC

Mmoja wa wanawake wanaodaiwa kurekodiwa kwa siri na Mrusi, Vladislav Liulkov, alipokuwa ametembelea Ghana, amezungumza kuhusu mawasiliano yake na mtayarishaji huyo wa maudhui.
Mwanamke huyo, ambaye utambulisho wake umefichwa, aliiambia BBC Pidgin kwamba alimkataa mwanaume huyo, ambaye mamlaka za Ghana zimethibitisha kuwa ni raia wa Urusi, tarehe 22 Januari 2026.
Mitandao ya kijamii imejaa picha zilizosambaa kwa kasi za wanawake wengi wanaodaiwa kuwasiliana na kurekodiwa kwa siri na mwanaume huyo Mrusi nchini Ghana na Kenya.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mawasiliano wa nchi hiyo, Samuel George, uchunguzi uliofanywa na mamlaka ya usalama wa mtandao umeonesha kuwa Vladislav Liulkov "alirekodi matukio ya faragha na baadhi ya wanawake hawa na kujipatia kipato kutokana na maudhui hayo kwenye majukwaa ya kidijitali."
Jitihada zinaendelea za "kufuatilia ushahidi wa kidijitali na kifedha" wa maudhui hayo ya faragha kwenye majukwaa ya kulipia.
Mamlaka za Ghana zimeiambia BBC kuwa baadhi ya waathiriwa tayari wamewasilisha malalamiko rasmi kwa mamlaka ya usalama wa mtandao na idara ya upelelezi wa makosa ya jinai ya polisi (CID).
Waziri wa masuala ya jinsia, watoto na ulinzi wa jamii, Agnes Naa Momo Lartey, amesema ofisi yake inatoa msaada wa kisaikolojia kwa waathiriwa waliojitokeza.
Alieleza kusikitishwa na ukweli kwamba ingawa si wanawake wote ambao picha zao zimesambazwa mtandaoni walikuwa na mahusiano ya faragha na mshukiwa, wote wamekumbwa na dhihaka kutoka kwa umma.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Vyanzo mbalimbali vimethibitisha kuwa si wanawake wote waliandamana na mshukiwa hadi kwenye hoteli aliyokuwa akiishi.
Pia kuna wengine waliokataa kabisa majaribio yake ya kuwashawishi, kama vile Juliet (si jina lake halisi), ambaye amezungumza na BBC Pidgin.
"Alinifuatilia hata baada ya kumkataa; nilipaza sauti mbele ya watoto wangu wadogo siku hiyo," alisema.
Juliet aliiambia BBC Pidgin kuwa alizuiwa nje ya maduka makubwa katika mji mkuu, alipokuwa amewapeleka watoto wake wadogo matembezini.
"Alinisimamisha na kuniambia mimi ni mrembo; mwanzoni nilidhani ni sifa tu, hasa kwa sababu watoto wangu pia ni wazuri. Lakini alirudia tena na kuongeza kuwa alitaka tufahamiane, jambo ambalo lingeweza kuishia kwenye ndoa ikiwa mambo yangeenda vizuri," alisema.
Juliet alisema mwanaume huyo Mrusi alimfuata hadi alipofika kituo cha teksi ili kuwapeleka watoto wake sehemu nyingine.
"Aliniomba nimfuate ili nijue anakoishi; sikupendezwa na hilo, na wakati huo sauti yangu ilikuwa tayari imeanza kuwa kubwa kidogo," alisema.
Katika video nyingi fupi alizochapisha mtandaoni, maneno yake ya kuanzisha mazungumzo yalikuwa: "jina lako nani, wewe ni mrembo, nifuate."
Baada ya maneno hayo kuisha na Juliet kuendelea kukataa, inadaiwa kuwa alianza kumgusa bila ridhaa yake.
"Nilikuwa na hasira na kuchoshwa na ukweli kwamba aliweza kuniomba nimfuate hadi hotelini kwake wakati nilikuwa na watoto wangu na hapo hapo alikuwa ananigusa begani na karibu kunivuta, huku nikisimamisha teksi tayari kuingia," alisema.

Juliet aliiambia BBC Pidgin kwamba Vladislav Liulkov hakukata tamaa "mpaka alipoongeza sauti yake zaidi, akamsaidia mmoja wa watoto wake kuingia kwenye teksi huku dereva akiondoka."
"Watoto walikuwa wakitazama huku akiendelea kushika bega langu, hata simu yangu ilianguka chini wakati huo, mbele ya watoto wangu," alisema.
Alipoulizwa anahisije kuhusu picha na video za wanawake wengine zilizosambazwa mtandaoni, Juliet alisema anahuzunika sana.
Waziri wa mawasiliano wa Ghana ameonya dhidi ya kusambaza picha na video hizo za waathiriwa, akisema kitendo hicho ni kosa la jinai chini ya sheria ya usalama wa mtandao ya nchi hiyo.
Juliet amesema anasumbuka kutokana na tukio hilo.
"Ninahisi vibaya ninapoona picha hizo; zinanirudishia kumbukumbu za tukio lile; ingeweza kuwa mimi kama ningemfuata siku ile," alisema, huku akiutaka umma kuacha kuwadhihaki na kuwaaibisha waathiriwa.
Inadaiwa kuwa Vladislav Liulkov alihariri rekodi hizo za siri ili ziendane na mahitaji ya maudhui yake kwa ajili ya kujipatia mapato.
Juliet anaamini hilo ni kosa la jinai.
"Video nilizoona zimehaririwa, hazioneshi kwa ukamilifu mikutano yake na wanawake hao wote. Nyingi zimekatwa ili kuunda taswira kwamba waathiriwa wote walimfuata mara tu baada ya kukutana naye."
Anataka waathiriwa wahurumiwe.
"Kila mtu hufanya makosa, sisi ni binadamu. Huu si wakati wa kuwadhihaki dada zetu, ningeweza kuvumilia aibu kama ningekuwa kwenye video hizo, lakini mtu mwingine anaweza asivumilie; kwa kweli baadhi ya waathiriwa wana mawazo ya kujiua."
"Natamani serikali yetu iweze kufanikiwa kumfikisha mahakamani."
Aidha, Urusi haitoi raia wake kwa nchi nyingine kwa ajili ya kushtakiwa (hairuhusu uhamishaji wa watuhumiwa wake kwenda nchi za nje).
Waziri wa Mawasiliano wa Ghana, Samuel George, alithibitisha hilo baada ya mkutano wao na balozi wa Urusi nchini Ghana, Sergei Berdnikov.
Samuel George alisema katika mkutano wa hivi karibuni na waandishi wa habari kwamba "polisi kwa kushirikiana na mamlaka ya usalama wa mtandao watawasilisha suala hilo kwa Interpol ili kutoa hati ya kimataifa ya kukamatwa, ili aweze kukamatwa popote nje ya Urusi atakapopatikana."
Alidokeza pia kwamba Vladislav Liulkov anaweza kushtakiwa hata bila kuwepo mahakamani, huku serikali ikilichukulia suala hilo kwa uzito mkubwa.
"Mwanaume huyu alikuwa na mawasiliano na wanawake hawa na akawarekodi bila ridhaa yao; hilo ni suala ovu. Serikali inapaswa kuchukua hatua kuhusu hili."
Juliet anataka waathiriwa wapewe kipaumbele kupata tiba na ushauri wa kisaikolojia.
"Wanawake hawa wanahitaji uangalizi na tiba kwa wakati huu; watu watawahukumu na kuwadhihaki, lakini wanapaswa kuangalia kwa upana zaidi, hili pia litapita."
Sheria ya usalama wa mtandao ya Ghana ya mwaka 2020 (Cybersecurity Act, 2020 – Act 1038) inapiga marufuku kurekodi na kusambaza picha za faragha bila ridhaa ya mhusika.
Watu watakaopatikana na hatia wanaweza kukabiliwa na kifungo cha hadi miaka 25 jela, kulingana na uzito wa kosa chini ya sheria hiyo ya usalama wa mtandao.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na Kuhaririwa na Ambia Hirsi












