Kenya yapinga usajili wa raia wake katika jeshi la Urusi

Chanzo cha picha, Ukraine Defence Intelligence
- Author, Peter Mwangangi
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
- Muda wa kusoma: Dakika 2
Kenya inasema kuwa itazungumza na Urusi kuhusu ripoti zinazoongezeka kuwa raia wake wanasajiliwa kupigana vita nchini Ukraine, ikielezea kitendo hicho kama kisichokubalika.
Shinikizo kubwa limeongezeka kwa serikali ya Kenya kuchukua hatua baada ya kugunduliwa kwa miili zaidi ya raia waliosajiliwa kupigana Pamoja na vikosi vya jeshi la Urusi dhidi ya Ukraine.
Mamlaka zinasema raia wanane waliosafiri hadi Urusi wamefariki au hawajulikani waliko, lakini watu zaidi bado wanajiunga na kampeni hiyo ya usajili kuelekea huko.
Waziri wa mambo ya nje wa Kenya Musalia Mudavadi, amesema ushirikiano na Moscow utazingatia kupunguza vitendo vya kusajili watu kinyume cha sheria, ikiwa ni pamoja na majadiliano kuhusu utoaji wa visa na makubaliano ya ajira ya pande zote mbili.
Alisema makubaliano sahihi ya ajira kati ya Kenya na Urusi 'yatafafanua maeneo yanayofaa ya kuajiri watu' ili kuhakikisha kwamba kuna uwazi, akiongeza kuwa 'wakenya hawawezi kuingizwa ama kusajiliwa jeshini nchini Urusi'.
"Kwetu sisi kama taifa la Kenya, tunataka kuweka wazi kwamba hatutaki Wakenya kusajiliwa kwa kazi hizo (za kijeshi)," alisema Musalia katika mahojiano na BBC.
Mamlaka imesema mpaka sasa wakenya 27 waliokuwa wakipigana nchini Urusi wamerudishwa nyumbani.
Siku ya Ijumaa, miili ya raia wawili wa Kenya walioasajiliwa kupigania vikosi vya jeshi la Urusi ilipatikana mashariki mwa Ukraine.
Idara ya ujasusi ya ulinzi ya Ukraine ilisema miili hiyo iligunduliwa karibu na jiji la Lyman katika eneo la Donetsk.

Chanzo cha picha, Kuloba family
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ugunduzi huo unakuja wiki moja baada ya Mkenya mwingine, kwa jina Clinton Nyapara Mogesa, 29, kuuawa, huku mwili wake ukipatikana katika eneo linaloshikiliwa na Urusi huko Donetsk kufuatia shambulio lililotibuliwa.
Katika kisa cha Mogesa, maafisa wa Ukraine walisema mwili huo ulipatikana ukiwa na pasipoti za raia wengine wawili wa Kenya, ambao wanaamini wanaweza kuwa wenzao wanaoandaliwa kwa ajili ya kupelekwa katika jeshi hivi karibuni.
Musalia amesema serikali imefunga zaidi ya mashirika 600 ya kusajili watu yanayoshukiwa kuwadanganya Wakenya kwa ahadi za kupata ajira nje ya nchi, na kukanusha ripoti kwamba serikali imeshindwa kusaidia familia za waathiriwa.
"Usajili huo unafanyika kisiri. Baadhi ya familia hizi hata wanapotulaumu, baadhi yao hawakuarifiwa na watu wao kwamba wanaondoka. Baadhi ya vijana hawa wameondoka majumbani mwao bila hata kuwaambia wazazi au ndugu zao.
Huwezi kulaumu serikali kwa hilo. Pale ambapo kuna usajili haramu, tumeyaondoa mashirika hayo na tutaendelea kuyaondoa," alisema Musalia.

Chanzo cha picha, Musalia Facebook
Serikali ya Kenya inakadiria kuwa Wakenya wapatao 200 wameajiriwa kupigana vita vya Urusi, lakini idadi kamili bado haijulikani, huku serikali ikisisitiza kwamba hakuna hata mmoja aliyesafiri kupitia njia rasmi na halali.
Kumekuwa na wasiwasi kwamba ukosefu wa fursa za kazi nchini kunawasukuma vijana kutafuta kazi hatari nje ya nchi licha ya athari zinazojitokeza.
"Ni kweli kuna changamoto ya ukosefu wa ajira, na lazima tutoe fursa za ndani na pia tuwaunge mkono Wakenya wanaotaka kupata fursa nje ya nchi.
Lakini tofautisha kati ya fursa halali na za kweli na fursa za kihalifu," alisema, akiongeza kuwa badala ya kurushiana lawama, lengo sasa linafaa kuwa ni kuwasaidia Wakenya wasijipate katika kazi hatari.












