Taurini: Mbona asidi hii jamii ya amino ni muhimu sana maishani mwako?

Chanzo cha picha, Getty Images
Hivi karibuni wanasayansi wamegundua asidi ya taurini, inayowekwa katika vinywaji vya kuongeza nguvu, na inaonekana kuwa na nguvu ya kuongeza umri wa kuishi na kuboresha afya kwa baadhi ya wanyama.
Matokeo bado hayajatangazwa kwa binaadamu, lakini yanatarajiwa siku za usoni.
Kwanini virutubisho hivyo vinaongezwa katika vinywaji vya kuongeza nguvu? Je, kunywa taurini kunaweza kuwa na faida?
Taurini ni asidi ya jamii ya amino, ambayo kikawaida inapatikana katika vyakula vingi kama nyama, samaki na mayai na pia huongezwa kwenye vinywaji vya kuongeza nguvu.
Ni adimu katika miti, lakini inapatikana kwa kiwango kidogo sana katika mwani, bakteria na uyoga.
Pia, huuzwa kama virutubisho, ni maarufu kwa wajenga miili na wanamichezo ambao wanaamini inawasaidia kudhibiti hali joto ya miili yao na kupunguza uchovu wa misuli wakati wa mazoezi.
Ingawa taurini haitumiwi kutengeneza protini kama asidi nyingine za jamii ya amino, ina kazi nyingine, hasa katika eneo la kati la mfumo wa neva. Ikiratibu kiwango cha kalisi (calcium) katika seli za neva, na kudhibiti maambukizi, miongoni mwa mambo mengine.
Taurini inawakilisha asilimia 0.1 ya uzito wa mwili wa mnyama. Utafiti wa karibuni zaidi wa watafiti wa kimataifa, walichunguza athari za dozi ya kila siku kwa panya wa umri wa kati na kima (walikuwa ni wa umri kati ya miezi 14 na miaka 15 wakati wa utafiti huo).
Kiwango cha taurini katika damu ya panya, kima na binaadamu kikawaida hupungua kutokana na umri, timu hiyo ilikuwa na shauku ikiwa kuongeza dozi ya asidi ya amino kunaweza kuwa na faida.
Matokeo yalishangaza. Wanyama waliopewa taurini walionekana kuwa vijana zaidi na wenye afya, misuli yao na ubongo, mifumo ya ulinzi na viungo vingine vilionekana kufanya kazi vizuri, kuliko wale ambao hawakupokea virutubisho hivyo.
Kuongezeka kwa uhai wa panya kulikuwa kwa asilimia 10-12, na kwa kima hali ilikuwa vivo hivyo. Ikiwa kuongeza taurini kwa binadamu nako kunaweza kuwa na faida, itakuwa ni sawa na ongezeko la umri wa miaka kumi.
“Nilidhani hili sio kweli,” Henning Wackerhage, Profesa wa molekule katika chuo kikuu cha Technical huko Munich, na mmoja kati ya waandishi hamsini wa utafiti huo, aliiambia BBC.
Kwa kima wa umri wa kati, kutumia taurini kila siku kunawapa maisha marefu zaidi na ya ujana.

Chanzo cha picha, Getty Images
Historia yake
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kinywaji cha kwanza cha kuongeza nguvu kilizinduliwa Marekani 1949, kwa jina la Dr. Enuf. Kilivumbuliwa kama mbadala wenye afya wa vinywaji baridi, na ladha ya limau, vitamini B na kafeni.
Lakini miaka 35 baadaye ndipo taurini ikawa maarufu, pale timu ya maafisa masoko kutoka Australia ilipokutana na kinywaji cha Kithailand, Krating Daeng wakati timu hiyo ikiwa katika safari ya kibishara.
Kinywaji hiki kisicho na kabonati kilikuwa na taurini na vitamini vya inositoli, aina ya sukari inayopatikana katika ubongo. Iliuzwa kama tiba ya uchovu.
Wanaume waliboresha fomula yake ya asili na kuongeza gesi kutengeneza Red Bull. Hivyo ndivyo kinywaji hicho kilivyozaliwa.
Kanuni za awali za kuongeza taurini hazijulikani. Kampuni nyingi hazina maelezo pia, zaidi ya kueleza kuwa ina faida kwa moyo, ubongo na misuli.
Ingawa, zipo tafiti zilizofanywa kuhusu faida zake. Kwa mfano, utafiti mmoja uligundua mchanganyiko wa viungo vya Red Bull, ikijumuisha taurini, huboresha uwezo wa kufanya mazoezi na uwezo wa kiakili.

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, inaweza kukusaidia uishi maisha marefu?
Utafiti wa karibu juu ya taurini, faida za kiafya na kurefusha maisha zilipatikana kwa wanyama waliopokea kiwango cha miligramu 1,000 kwa siku kwa mwili wa uzito wa kilo moja.
Kwa kutumia njia hiyo kubadili dozi ya mnyama kuwa ya binaadamu, kwa kutumia uzito wa mwili, matokeo yatakuwa gramu sita kwa siku kwa mtu mzima. Sawa na kiwango kinachopatikana katika chupa sita za Red. Ama vinywaji vingine kama hicho. Ila hili sio pendekezo.
Mwandishi mkuu wa utafiti wa taurini hakutaka kufichua kwa BBC, ikiwa anatumia taurini ili asihamasishe watu wengine. Ikiwa taurini inaweza kuwa na faida pia kwa binaadamu, hilo bado hawajalieleza.
Red Bull imekuwepo kwa muda mrefu ikitangazwa kwa wana michezo na michezo ya hatari. Pia, tunapaswa kueleza uwezekano wa athari wa vinywaji kama hivyo hasa vile vyenye ujazo wa lita moja na nusu au lita tatu ikiwa utatumia kila siku.
Kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA), watu wazima hawapaswi kunywa zaidi ya asilimia 10 ya sukari kutoka vyakula vilivyoongezwa sukari, hiyo ni sawa na vijiko 12 vya chai kwa siku.
Kwa mantiki hiyo, sio jambo jema kutumia vinywaji vya kuongeza nguvu kupita kiasi. Inawezekana ni kweli taurini inaboresha afya ya binaadamu, lakini tafiti zaidi zinapaswa kufanywa.

Chanzo cha picha, Getty Images












