Wanawake wa jamii ya Alawite nchini Syria waelezea walivyotekwa na kubakwa

Picha ya mwanamke akiwa amevalia niqab nyeusi, uso wake hauonekani vizuri. Nyuma yake kuna kivuli cha mwanaume akiwa amevalia barakoa.
    • Author, By BBC News Arabic
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Onyo:Ripoti hii ina maelezo ya unyanyasaji wa kingono na vurugu ambayo huenda yakawaathiri baadhi ya wasomaji.

Ramia alikuwa akijiandaa kujumuika na familia yake, katika kijiji chake wilaya ya Latakia magharibi mwa Syria, kabla ya gari jeupe kuendeshwa hadi alikokuwa, anasema.

Wanaume watatu waliokuwa wamejihami, waliosema wanafanya kazi na serikali, walimlazimisha kuingia kwenye gari lao kwa nguvu, msichana huyo ambaye tumezuia utambulisho wake aliaambia BBC.

Wanaume hao walimpiga,alisema, walimpiga kwa nguvu hadi akaanza kulia na kupiga kelele.

"Mmoja wao aliniuliza kama mimi ni MSunii au Alawite, na wakaanza kunitusi," aliongezea

Ramia ni mmoja wa makumi ya wanawake walioripotiwa kutekwanyara baada ya kuondolewa kwa Bashar al Assad madarakani.

Kundi la kutetea wanawake la Syrian Feminist Lobby (SFL) linasema lilirekodi ripoti kutoka kwa familia, vyombo vya habari na vyanzo vingine, kuwa zaidi ya wanawake 80 hawajulikani walipo. Kundi hilo linasema lilithibitisha matukio 26 ya utekaji nyara.

Karibu wanawake wote waliopotea ni kutoka jamii ya Alawite, ambao ni waislamu wa Shia, na wanajumuisha 10% ya idadi ya watu nchini Syria, na ni jamii anakotokea rais aliyeondolewa madarakani.

Wanawake wawili wakiwa wamebeba mabango wakati wa maandamano ya tarehe 28 mwezi Disemba 2025 wakipinga mauaji ya jamii ya Alawite.

Chanzo cha picha, Kenana Hendawi/Anadolu via Getty Image

Vurugu

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wanawake wawili kutoka jamii ya Alawite na familia za wanawake wengine watatu, wote wameelezea BBC jinsi walivyotekwa na kushambuliwa. Tumebadilisha majina yao kwa usalama wao.

Wote walisema kikosi cha polisi cha serikali ya mpito kilishindwa kuchunguza kilichokuwa kikiendelea. Mmoja wao alituambia polisi walimkejeli aliporipoti kisa chake.

Msemaji wa Wizara ya usalama wa Ndani alisema mwezi Novemba kwamba walikuwa wamechunguza madai 42 ya utekaji nyara, na kugundua kuwa yote isipokuwa moja yalikuwa ya "uongo".

Walipoulizwa na BBC, wizara hiyo ilisema haikuwa na maoni zaidi.

Hata hivyo, chanzo kimoja cha usalama kiliiambia BBC kwamba utekaji nyara ulikuwa umetokea, ikiwemo baadhi iliyohusisha watu kutoka idara ya usalama, ambao alisema walikuwa wamefutwa kazi.

Utekaji nyara na watu kutoweka uliorekodiwa na kundi la SFL, unaanzia mwezi Februari 2025 hadi mwanzoni mwa Desemba. Hiki ni kipindi cha kabla na baada ya mwezi Machi, ambapo zaidi ya watu 1,400, wengi wao wakiwa kutoka jamii ya Kialawite, waliuawa katika ghasia za kidini katika maeneo ya pwani ya magharibi.

Vikosi vilivyoaminika kuwa vinaegemea upande wa serikali inayoongozwa na Waislamu wa Kisunni vilituhumiwa kwa wimbi la mauaji ya kulipiza kisasi kufuatia shambulizi baya lililofanywa na wafuasi wa Assad.

Watu wengi waliokuwa wanahudumu katika utawala wa Assad walikuwa Waalawite, lakini raia kutoka mirengo mingine walikumbana na ukandamizaji kwa kumpinga rais huyo wa zamani.

Ramani inayoonyesha eneo la Latakia,pwani magharibi mwa Syria.

'Jaribio la kujitoa uhai'

Ramia alizungumza kwa sauti ya chini alipokuwa akielezea jinsi alivyolazimishwa kuvaa vazi la kufunika mwili mzima la niqab na ushungi unaoacha sehemu ya macho pekee wazi.

Alisema alifungiwa katika chumba cha chini ya ardhi kilichokuwa na kitanda na kabati la nguo, juu yake kukiwa na vifaa vya kujisafisha pamoja na kondomu.

Alizuiliwa kwa siku mbili, alijaribu kutoroka mara moja na kujaribu kujiua mara mbili.

Aliyekuwa amemteka nyara hakuwa akizungumza Kiarabu kwa ufasaha na alikuwa na "sura ya watu kutoka bara Asia", aliongeza kwamba alimvua niqab yake na kumpiga picha.

Ramia alisema kuwa mwanamke aliyekuwa akiishi katika jengo hilo, ambaye alidai kuwa mke wa aliyekuwa amemteka nyara, alimweleza kwamba picha hiyo "ilikuwa ya kuamua bei yake ya kuuzwa."

Alisema mwanamke huyo alimweleza kwamba "wengi" wengine walikuwa wametekwa kabla yake, na kwamba baadhi yao walikuwa wamebakwa na kuachiwa huru, wengine "waliuzwa."

BBC haikuweza kuthibitisha kesi zozote za kubadilishana fedha kwa ajili ya wanawake waliotekwa, lakini wanaharakati wameripoti matukio ambapo waathiriwa walisema walitishiwa kuuzwa au kulazimishwa kuolewa.

Walibakwa mara kadhaa

Nesma, mama mwenye umri wa miaka 30, aliiambia BBC kwamba alichukuliwa kutoka kijijini kwake, mkoa wa Latakia, na kulazimishwa kuingia kwa gari la kubebea mizigo lililokuwa na pazia kwenye madirisha.

Sauti yake ilikuwa ikitetemeka akituelezea kwa njia ya simu, jinsi alizuiliwa kwa siku saba katika chumba chenye madirisha ya juu kilichoonekana kuwa kiwanda, na kuhojiwa na wanaume watatu kuhusu wakazi wa kijiji chake na uhusiano wowote na utawala wa zamani.

Kundi la wanajeshi wanane wakiwa juu ya gari wakiwa wamejihami kwa bunduki.

Chanzo cha picha, Abdulvacit Haci Isteyfi/Anadolu via Getty Images

Maelezo ya picha, Vurugu iliyotokea mwezi Machi nchini Syria iliwauwa zaidi ya watu 1,400

Alituelezea kuwa watekaji wake wote walikuwa wamevaa barakoa na walizungumza kwa lahaja ya Kiarabu ya Syria. Anasema walimwambia kwamba "wanawake wa Kialawite waliumbwa kuwa sabaya" neno la Kiarabu linalomaanisha "wanawake mateka," na linalotumiwa na baadhi ya watu wenye misimamo mikali ya Kiislamu, ambao huwaona wanawake kama watumwa wa ngono.

Watekaji wake walimbaka mara kadhaa, alisema, "Kitu pekee nilichokuwa nikifikiria ni kifo kwamba ningekufa na kumuacha mtoto wangu bila mama."

Leen, ni msichana mwingine, aliyevumilia kupigwa, kutishiwa kwa bunduki na kunyanyaswa kingono kila siku, mama yake Hasna aliambia BBC.

Hasna anasema aliyemteka nyara alikuwa akifunika uso wake, alizungumza Kiarabu kibovu, na alijigamba kuhusu kushiriki katika mauaji ya Waalawite wakati wa ghasia za mwezi Machi.

"Alikuwa akiwaita wasichana wetu sabaya, kwa sababu 'hawaamini Mungu,'" Hasna anasema

baadhi ya Wasunni wenye misimamo mikali huwaona Waalawite kama watu wazushi.

BBC pia ilizungumza na Ali, ambaye alisema mke wake Noor alitekwa nyara na kuzuiliwa kwa wiki kadhaa, na mama mmoja kwa jina Somaya, ambaye alisema binti yake alinyanyaswa kingono "kwa siku 10 mfululizo."

'Vitisho kwa njia ya simu'

Nesma aliambia BBC kwamba maafisa wa usalama walimkejeli kwa kicheko alipokwenda kuripoti kwamba alitekwa nyara, "walisema labda nilikuwa nimeenda kujivinjari"

Ramia alisema maafisa hao awali walionekana kuzingatia kesi yake, lakini waliacha kushika simu zake baada ya kumtambua aliyekuwa amemteka. Familia yake ilipokea vitisho kwa njia ya simu kwamba "tungelipa dhamana iwapo tungezungumza" Alisema. Waliaumua kukimbilia nje ya nchi

Ali aliiambia BBC kuwa "Walimkamata mtekaji, lakini hatujui kilichotokea baadaye." Alisema alikuwa na hofu kwamba mtekaji huyo anaweza kuachiliwa na kuwakujia baadaye.

Mama yake Leen alisema binti yake alihojiwa mara kadhaa na maafisa wa usalama, lakini hakuna matokeo ya uchunguzi waliyoyapata, hata baada ya miezi kadhaa. Somaya anasema aliripoti kilichotokea, lakini hakupokea taarifa zozote kuhusu ripoti yake.

Mwezi Novemba, wizara ya usalama ya ndani nchini Syria, inayosimamia utoaji huduma ya usalama, ilifanya mkutano na waandishi wa habari kuhusu matokeo yake kuhusu visa 42 vilivyoripotiwa vya utekaji nyara.

Msemaji Nour al-Din al-Baba alisema ni kesi moja tu ilikuwa "utekaji halisi". Alisema zingine ziligunduliwa kama "kutoroka kwa hiari," "kukaa na jamaa au marafiki," "kukimbia vurugu za nyumbani," "madai ya uongo mitandaoni" au "kushiriki katika ukahaba na kudhulumiwa," huku kesi nne zikiwa "makosa ya jinai ambayo yalisababisha kukamatwa."

Msemaji huyo alisema wizara husika ilishughulikia ripoti hizo kwa "umakini mkubwa na uwajibikaji."

Baadaye mwezi wa Novemba, BBC iliwasiliana na wizara hiyo ili kupata majibu yake kuhusu taarifa tulizokusanya. Walisema hawana maoni zaidi.

Picha ya juu ya angani ikionyesha majengo ya ghorofa na barabara kuu eneo la Latakia.

Chanzo cha picha, OMAR HAJ KADOUR/AFP via Getty Images

Chanzo kimoja cha usalama kutoka eneo la pwani, akizungumza na BBC bila kutaka kutambuliwa alidai kuwa "Kuna vitendo vya utekaji nyara ambavyo watu wanafanya kujinufaisha kifedha, na kwa kupuuza sheria au kutokana na sababu za kibinafsi zinazohusiana na utawala uliopita."

Alisema hili linajumuisha "Baadhi ya maafisa wa polisi wanaochukua utekaji kama njia ya kulipiza kisasi," alisema. "Baadhi ya visa vya maafisa wa polisi vimegunduliwa, na maafisa waliohusika walifutwa kazi mara moja."

Wanawake wanne na familia zilizozungumza na BBC walisema hawajui watekaji hao ni kina nani.Mmoja alisema alimjua, na alisema hakuwa mtu kutoka kwa vyombo vya usalama. Wawili walisema waliachiliwa baada ya shinikizo la umma, wengine walisema hawakujuwa kwanini waliachiliwa huru.

'Kutokujali'

Mwezi Julai,shirika la Amnesty International lilisema kuwa limepokea ripoti za utekaji nyara wa wanawake 36 wa Kialawite wenye umri kati ya miaka mitatu hadi 40.

Kwa familia ambazo BBC ilizungumza nao, bado wanaishi kwa hofu, na wanakumbana na unyanyapaa na aibu inayotokana na unyanyasaji wa kingono.

Mama yake Leen anatuelezea kuwa binti yake anaishi kwa wasiwasi akihofia mlango wake unaweza kubishwa wakati wowote. Ndoa ya Nesma ilivunjika. "Ningeamka usingizini na kupiga nduru" anasema Ramia. Alisema anazungumza na mtaalam wa afya ya akili ila bado anapata changamoto ya kupata utulivu.

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula