Zitto Kabwe aeleza kwanini anataka Benki ya Dunia isiikopeshe Tanzania kwa sasa

Maelezo ya video, Zitto Kabwe aeleza kwanini anataka Benki ya Dunia isiikopeshe Tanzania kwa sasa

Kiongozi wa chama upinzani cha ACT-Wazalendo nchini Tanzania Zitto Kabwe amesema kuwa Benki ya Dunia haitakiwi kuikopesha Tanzania dola milioni 500 za elimu kabla ya mabadiliko ya kisera kufanyika.

Vyama vya upinzani nchini Tanzania na wanaharakati wa haki za binadamu nchini humo na wa kimataifa wamekuwa wakitishia shinikizo la kutotolewa kwa mkopo huo mpaka pale Tanzania itakaporuhusu wanafunzi wanaopata ujauzito waruhusiwe kuendelea na mfumo rasmi wa elimu.

Kwa mujibu wa nyaraka za Benki ya Dunia, pamoja na mambo mengine, mkopo huu ulikusudiwa kwenda kusaidia upatikanaji wa elimu bora na kwa urahisi kwa wanafunzi waliokuwa wanarudi shule baada ya kuwa wamepata ujauzito. Lakini mradi huu wa elimu ulikuwa ni kupitia elimu mbadala na si katika mfumo rasmi.

Katika mahojiano na BBC jijini London, Zitto ameeleza kuwa jambo hilo halikubaliki.

"Ni dhahiri kuwa mkopo wa Benki ya Dunia kwa ajili ya elimu Tanzania utanufaisha watu wengi sana, lakini ukitekelezwa kwa namna ulivyopangwa hivi sasa utabagua pia watoto wengi sana. Na hoja yetu ya msingi ni kuboresha, hoja yetu si kuzuia mkopo.

"Kwa namna ambavyo mkopo umetengenezwa maana yake ni kwamba watoto wa kike wa Tanzania ambao watapata ujauzito njia yao mbadala ya kupita itakuwa ni kwenda kuwa wapishi, wasafishaji, wafumaji, washonaji na hatuwezi kwenda kutengeneza taifa la kuwafanya watoto wa kike kwa sababu tu ya kupata ujauzito asiweze kuwa na chaguo katika elimu."

Kwa upande wake Waziri wa elimu nchini Tanzania profesa Joyce Ndalichako amesema kwamba serikali ya Tanzania bado ina lengo la kuwapa fursa za kielimu watoto wa kike ambao wamekatiza masomo yao baada ya kupata mimba kwa kuwapa elimu mbadala.

Prof Ndalichako ameyasema hayo pindi alipoitembelea Shule wa Sekondari ya Msalato ambayo ni ya wasichana na ni moja ya shule za wanafunzi wenye vipaji maalumu nchini humo.

Waziri huyo amesema mkopo Tanzania uliyouomba Benki ya Dunia utasaidia kuendeleza miradi mbalimbali ya elimu nchini humo.

Serikali imesemaje?

Msemaji wa serikali ya Tanzania Dkt Hassan Abbas pia ameongelea suala hilo na kukanusha madai kuwa fedha za mkopo huo zitatumika katika uchaguzi mkuu mkuu wa nchi hiyo baadae mwaka huu.

Kwa mujibu wa Abbas Tanzania ina sheria nzuri katika matumizi ya fedha za uchaguzi.

Akuzungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma hii leo, Dkt Abbas amewaambia waandishi wa habari jijini Dodoma hii leo kuwa mkopo huo haujasitishwa bali majadiliano yanaendelea.