Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Nchi za magharibi zalaani uchaguzi wa Urusi, India na China zikiunga mkono ushindi wa Putin
Hakuna mgombea anayeaminika wa upinzani aliyeruhusiwa kushiriki katika uchaguzi huo utakaomwezesha Putin kuwa madarakani hadi 2030.
Moja kwa moja
Abdalla Seif Dzungu and Ambia Hirsi
WHO 'ina wasiwasi mkubwa' kuhusu hali ya al-Shifa
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema "lina wasiwasi mkubwa" kuhusu kile kinachoendelea katika hospitali ya al-Shifa.
Katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii, mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus anasema hali katika hospitali hiyo "inahatarisha maisha ya wafanyikazi wa afya, wagonjwa na raia".
Anasema al-Shifa ilikuwa imerejesha hivi karibuni tu "huduma ndogo za afya", na kwamba uhasama wowote au uvamizi wa kijeshi wa hospitali "unahatarisha huduma za afya, upatikanaji wa ambulensi, na utoaji wa vifaa vya kuokoa maisha".
"Hospitali hazipaswi kamwe kuwa viwanja vya vita," anasema, akimalizia wadhifa huo kwa: "Hospitali lazima zilindwe. Kusitisha mapigano!"
Kenya: Facebook kuanza kuwalipa waandaji maudhui katika mitandao kijamii
Waandaji wa maudhui nchini Kenya wanatazamiwa kuanza kuchuma mapato kutokana na kazi zao katika muda wa miezi mitatu ijayo baada ya kampuni kubwa ya mitandao ya kijamii, Facebook, kupitia kampuni mama ya Meta kutangaza mpango wa kujumisha matangazo ya biashara ya moja kwa moja.
Ikitangaza mpango huo katika Ikulu mbele ya Rais Willia m Ruto, kampuni hiyo ilisema kuwa itazindua njia zingine za mapato kwenye Facebook na Instagram.
Watajumuisha Facebook stories, Instagram subs na zawadi za IGpia.
"Tuna furaha sana kutangaza kwamba tutakuwa na matangazo ya kibiashara kwenye Facebook kuanzia kiwango cha juu cha msimu wa joto," alisema Moon Baz ambaye anaongoza ushirikiano wa kimataifa kwa Afrika, Mashariki ya Kati na Uturuki.
Ili kupata mapato, ni lazima watayarishi maudhui wawe na angalau Wafuatiliaji 5,000, wawe na umri wa zaidi ya miaka 18, wawe na angalau video 5 amilifu kwenye kurasa zao za Facebook, na wawe wamekusanya dakika 60,000 za kutazamwa kwa video katika siku 60 zilizopita, ikiwa ni pamoja na video za moja kwa moja.
Wanafunzi wa kigeni wavamiwa India kisa sala ya Ramadhan (Taraweeh)
Polisi nchini India wamewakamata watu watano baada ya baadhi ya wanafunzi wa kimataifa kuvamiwa katika makazi yao ya chuo kikuu walipokuwa wakisali.
Maafisa wanasema mabishano makali kuhusu eneo la maombi yalisababisha shambulio hilo katika Chuo Kikuu cha Gujarat magharibi mwa India siku ya Jumamosi.
Duru za polisi zilisema wanafunzi watano walijeruhiwa.
Wizara ya mambo ya nje ya India ilisema kuwa mamlaka ya Gujarat ilikuwa inachukua "hatua kali" dhidi ya wahusika.
GS Malik, kamishna wa polisi wa jiji la Ahmedabad, aliwaambia waandishi wa habari kwamba karibu watu 22 waliingia katika makazi ya wanafunzi Jumamosi usiku na kuwapinga wanafunzi wanaosali, wakiwataka kufanya hivyo msikitini.
"Walizozana kuhusu suala hilo, wakiwashambulia na kuwarushia mawe.Pia waliharibu vyumba vyao," alisema na kuongeza kuwa jopo limeundwa kuchunguza kisa hicho.
Polisi hawajathibitisha iwapo watu hao wana uhusiano na mashirika yoyote ya kisiasa au kidini.
Wanahabari kutoka BBC Gujarati waliotembelea eneo hilo siku ya Jumamosi walisema waliona mawe na magari yaliyoharibiwa katika eneo la tukio.
Video zinazosambaa mtandaoni zilionyesha umati wa watu wakiinua mabango yaliyo na ishara ya kidini za Kihindu huku wakiwavamia wanafunzi hao, kuharibu magari na kuwarushia mawe.
Putin amtaja Navalny na kudai alikubali awe sehemu ya mpango wa kubadilishana wafungwa
Vladimir Putin amekuwa akiepuka kumtaja mpinzani wake mkuu nchini Urusi kwa jina, lakini baada ya Alexei Navalny kufariki, amebadili mbinu.
Baada ya kudshinda uchaguzi wa urais utakaomwezesha kuwa madarakani kwa muhula wake wa tano, aliwaambia waandishi wa habari: "Kuhusu Navalny, ndiyo aliaga dunia, hili huwa ni tukio la kusikitisha."
Pia aligusia kwamba alikuwa amekubali Navalny kuwa sehemu ya kubadilishana wafungwa.
Washirika wa Navalny wanasema aliuawa katika jela ya Arctic na mamlaka ya Urusi.
Rais wa Marekani Joe Biden wakati huo alisema "kifo hicho ni uthibitisho zaidi wa ukatili wa Putin".
Bw Putin alisema Jumapili usiku kwamba siku chache kabla ya kifo cha Navalny, aliambiwa na watu ambao hawakuwa sehemu ya utawala wake kuhusu mpango wa kubadilishana "kwa baadhi ya watu" uliofanyika Magharibi.
Alisema alikubali mara moja kwa sharti kwamba Navalny asirudi tena: "Lakini, kwa bahati mbaya, kilichotokea, kilitokea."
Baadhi wanahisi matamshi ya kiongozi huyo wa Urusi ni jaribio la kujiepusha na tuhuma za kifo cha Navalny.
Mwandishi wa habari wa Kirusi aliyefukuzwa Roman Dobrokhotov alisema lilikuwa jaribio la kuonyesha "haikuwa na faida kwangu".
Lakini mkuu wa wafanyikazi wa Navalny, Leonid Volkov, alisema matamshi ya kiongozi wa Urusi yalionyesha kuwa "sasa ameamua kuwa hahitaji kujifanya tena".
Wachambuzi wanaamini kuwa Bw Putin amewahi kutumia jina la Navalny hapo awali mara moja tu, mwaka wa 2013, alipoulizwa kwa nini alilikwepa.
Hitilafu ya mifumo yawawezesha wateja wa benki ya Ethiopia kutoa mamilioni
Benki kubwa zaidi ya kibiashara nchini Ethiopia inajaribu kurejesha mamilioni ya dola zilizochukuliwa na wateja wake kufuatia kile ilichotaja kama hitilafu ya mifumo.
Zaidi ya dola milioni 40 ziliripotiwa kuotolewa kwenye Benki ya Biashara ya Ethiopia inayomilikiwa na serikali, au kuhamishiwa kwa benki nyingine, wateja walipogundua wanaweza kuchukua pesa taslimu zaidi ya walizokuwa nazo kwenye akaunti zao.
Ilichukua saa kadhaa kabla ya taasisi hiyo kusimamisha shughuli zake zote.
Shambulio la kimtandao halijahusishwa na hitilafu hiyo.
Walioshuhudia waliambia BBC baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu, ambapo pesa nyingi zilidaiwa kutolewa wamezuiliwa.
Nzi Chuma: Mdudu anayebadilisha uchafu kuwa thamani
Angela Mauto maarufu kama mama wadudu amejikita katika ufugaji wa asili wa nzi chuma ambao hutumika kama chakula cha wanyama na hata mbolea katika kilimo.
Angela anasema alianza safari yake hii ya ufugaji akiwa na nzi mmoja tu kwa lengo la kupata mbolea ya asili kwa ajili ya bustani ya mboga mboga nyumbani.
Kwa sasa ana eneo lake ambalo hufuga wadudu hao na kuuza kama chakula cha kuku, mbegu kwa wanaotaka kuanza ufugaji wa Nzi hawa na mbolea,
Mwandishi wa BBC Veronica Mapunda alikutana na Angela na kuandaa taarifa hii.
Video: Bosha Nyanje
Jeshi la Israel lawaamuru wakazi wa Gaza kuondoka katika hospitali ya al-Shifa
Jeshi la Israel limewaambia watu wa Gaza kuondoka katika eneo karibu na hospitali ya al-Shifa.
Maelfu ya watu tayari wamekimbilia mji wa Gaza kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, tangu Israel ilipoanza operesheni yake mwezi Oktoba.
Hospitali hiyo ndiyo kubwa zaidi katika eneo hilo na inatumika kama makazi ya watu waliokimbia makazi yao, pamoja na wagonjwa.
Msemaji wa lugha ya Kiarabu wa IDF Avichay Adraee alisema kwenye mtandao wa kijamii:
"Wito kwa wale wote waliopo na waliokimbia makazi yao katika kitongoji cha al-Rimal na katika Hospitali ya al-Shifa na mazingira yake: Ili kudumisha usalama wako, lazima uhame eneo hilo mara moja na kwenda magharibi na kisha kuvuka Mtaa wa al-Rashid (al-Bahr) kuelekea kusini hadi eneo salam huko al-Mawasi.
Msako baada ya mikutano ya rais wa Kenya kutatizwa
Mamlaka nchini Kenya imeanzisha msako mkali dhidi ya watu waliotatiza mikutano ya kisiasa ya Rais William Ruto magharibi mwa nchi hiyo mwishoni mwa juma.
Ilifuatia visa viwili ambapo wavamizi walikatiza mikutano ya Rais Ruto katika kaunti za Bomet na Kericho.
Rais alikuwa katika eneo la Bonde la Ufa, ngome yake ya kisiasa, kuzindua miradi kadhaa mikutano yake ilipotatizwa huku mizozo ya kisiasa inayowakabili viongozi wa eneo hilo ikipamba moto.
Rais huyo aliyekasirishwa sana alisema viongozi wanaoshabikia machafuko kama hayo wanaathiri miradi ya maendeleo katika eneo hilo, akitaja usumbufu huo kuwa "upumbavu".
Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki Jumatatu aliagiza polisi kuwakamata mara moja watu waliohusika na matukio hayo.
Waziri huyo alikutana na wakuu wa usalama wa eneo hilo na kuwapa jukumu la "kuhitimisha uchunguzi na kuwakamata waandaaji, wafadhili na wahusika wa uhuni".
Viongozi wa ulimwengu waendelea kutoa maoni kuhusu uchaguzi wa Urusi
Viongozi wa mataifa tofauti duniani wamekuwa wakitoa maoni yao kuhusu uchaguzi wa Urusi huku ulimwengu ukiamkia taarifa za ushindi wa Vladimir Putin kwa muhula mpya wa miaka sita.
Wengi wametaja kura hiyo kama "uchaguzi wa bandia" - huku wengine wakiipongeza.
Haya ni baadhi ya maoni ya hivi punde:
Waziri wa Mambo ya Nje wa Lithuania Gabrielius Landsbergis anasema ushindi wa Putin katika uchaguzi hauna uhalali kwani watu hawakuwa na uhuru wa kuchagua.
Rais wa Iran Ebrahim Raisi amempongeza mwenzake wa Urusi kwa ushindi wake "maalum" katika uchaguzi wa rais, vyombo vya habari vya serikali vimeripoti.
Rais wa Venezuela Nicolas Maduro anasema: "Ndugu yetu mkubwa ameshinda, ishara ambayo ni nzuri kwa ulimwengu"
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Jan Lipavsky ametaja uchaguzi huo kuwa "ujanja na kichekesho"
Maelezo zaidi:
Pakistan yashutumiwa kwa mauaji ya Waafghanistan katika mashambulizi ya anga
Kundi la Taliban imeishutumu Pakistan kwa kuwauwa wanawake wanane na watoto katika mashambulizi mawili ya anga ya usiku nchini Afghanistan.
Zabihullah Mujahid, msemaji wa serikali ya Taliban, alisema mashambulizi hayo "ya kizembe" yameathiri nyumba karibu na mpaka na Pakistani yapata saa 03:00 kwa saa za huko (22:30 GMT).
Pakistan bado haijatoa kauli yoyote. Lakini inajiri baada ya Rais Asif Ali Zardari kuapa "kujibu vikali" vifo vya wanajeshi saba waliouawa na wanamgambo wasiojulikana siku ya Jumamosi.
Akizungumza katika mazishi ya wanajeshi wawili siku ya Jumapili, Rais Zardari aliongeza kuwa kulipiza kisasi kutafanywa "bila kujali ni nani au kutoka nchi gani" kundi hilo lilitoka.
Shambulio la Jumamosi dhidi ya kituo cha kijeshi lilifanyika karibu na mpaka wa Afghanistan kaskazini mwa Waziristan.
Pakistan inasema yalifanywa kutoka Afghanistan - moja ya idadi inayoongezeka ya mashambulizi katika miezi ya hivi karibuni, kulingana na serikali yake.
Afisa wa serikali ya mtaa - ambaye hakutaka jina lake litajwe - aliambia shirika la habari la AFP kwamba mashambulizi ya Jumatatu asubuhi katika majimbo ya Khost na Paktika yalikuwa ya kulipiza kisasi vifo vya Jumamosi.
Rais wa Somalia afanya mazungumzo ya usalama na kiongozi wa Eritrea
Rais wa Eritrea Isaias Afwerki na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud wamefanya mazungumzo ya pande mbili katika mji mkuu wa Eritrea, Asmara.
Wakati wa mkutano "wa kina" siku ya Jumapili, viongozi hao wawili walijadili masuala ya kikanda, ikiwa ni pamoja na mapambano ya Somalia dhidi ya wanamgambo, Waziri wa Habari wa Eritrea Yemane Meskel alichapisha kwenye X.
Mazungumzo kuhusu "mada muhimu ya kikanda na kimataifa" pia yaliangaziwa katika mkutano wao, Shirika la Habari la Kitaifa la Somalia lilisema, bila kutoa maelezo zaidi.
Hii ilikuwa ni ziara ya pili ya Rais Mohamud nchini Eritrea mwaka huu na ya sita tangu aingie madarakani Mei 2022, akiangazia uhusiano mkubwa kati ya nchi hizo mbili.
Rais Mohamud alitembelea Asmara mara ya mwisho mwezi Januari huku kukiwa na mvutano na nchi jirani ya Ethiopia kuhusu makubaliano kati ya Addis Ababa na jamhuri iliyojitangaza ya Somaliland.
Mpango huo unapingwa na serikali ya Somalia. Video iliiochapishwa kwenye X inamuonyesha Rais Isaias na mgeni wake Mohamud wakitembea-tembea katika mitaa ya Asmara, huku wakazi wakishangilia na kupiga picha.
Eritrea imekuwa ikitoa mafunzo kwa maelfu ya wanajeshi wa Somalia ili kuongeza nguvu katika jeshi la Somalia huku wanajeshi wa Umoja wa Afrika wakitarajiwa kuondoka katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika mwishoni mwa mwaka huu.
Rais Putin kutoa kipau mbele kwa vita vya Ukraine katika hotuba yake ya ushindi
Vladimir Putin alitoa hotuba ya ushindi baada ya kudai ushindi katika uchaguzi wa rais wa Urusi mwishoni mwa juma, katika mchakato ambao umeelezwa kuwa sio huru na wa haki na mamlaka kadhaa za kimataifa.
Haya ni maneno aliyosema :
Putin amewashukuru wananchi kwa kujitokeza kupiga kura, akisema ushindi wake utaiwezesha nchi hiyo kustawi.
Ameapa kuimarisha jeshi la Urusi na kutanguliza kile alichokiita "operesheni maalum ya kijeshi" ya Urusi nchini Ukraine.
Putin amesema ushindi wake unaonyesha Warusi wameungana na hatatishika
Alichukua fursa hiyo kukosoa maandamano ya 'Mchana dhidi ya Putin', yaliyoandaliwa na mjane wa marehemu Alexei Navalny - Yulia Navalnaya - ambayo yalifanyika katika miji kadhaa ya Urusi na vituo vya kupigia kura vya kigeni.
Putin amewaambia waandishi wa habari kwamba alikubali makubaliano ya kubadilishana ili kumwachilia huru Navalny kabla ya kiongozi huyo wa upinzani kufariki katika gereza la Arctic.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa Kremlin kutamka jina la Navalny hadharani kwa miaka mingi
Wakenya wamuomboleza mwanahabari mashuhuri wa runinga Rita Tinina
Wakenya wanamuomboleza mwanahabari mkongwe wa TV Rita Tinina ambaye alipatikana akiwa amefariki nyumbani kwake katika mji mkuu, Nairobi, Jumapili.
Wenzake katika kituo cha NTV walisema alitarajiwa kuwa zamu siku ya Jumapili lakini alishindwa kufika, jambo lililosababisha ukaguzi wa afya katika nyumba yake ambapo alipatikana amepoteza fahamu.
Ripoti ya polisi ilisema hakuna majeraha ya mwili yaliyopatikana kwenye mwili wake.
Dadake Tinina aliwaambia polisi kwamba mwanahabari huyo alikuwa na kifafa na alikuwa akiugua homa kali katika wiki iliyopita.
Mwanahabari huyo wa muda mrefu wa televisheni alijulikana kwa taarifa za kuvutia za habari
Rais William Ruto alichapisha risala za rambi rambi katika mtandao wa X:
Wakenya kwenye mitandao ya kijamii wanasema watakosa ustadi wa uandishi na uchezaji wake wa maneno, huku wenzake wakimuomboleza kama mwanahabari mchapakazi na anayetegemewa.
"Kufariki kwake kunaacha pengo katika tasnia, lakini urithi wake wa kusimulia hadithi na uadilifu utadumu," kiongozi wa upinzani Raila Odinga alichapisha kwenye X.
Waziri wa Habari Eliud Owalo alielezea michango ya Tinina katika uandishi wa habari kuwa "ya thamani kubwa".
Sudan Kusini yafunga shule kutokana na joto kali,
Serikali ya Sudan Kusini imeamuru kufungwa kwa shule zote kwa muda usiojulikana kwa sababu ya wimbi la joto ambalo linaweza kusababisha joto kuongezeka hadi 45C (113F).
Mamlaka ya afya na elimu pia iliwataka wazazi kuwazuia watoto wao kucheza nje kwa muda mrefu, wakisema joto hilo linaweza kudumu kwa wiki mbili.
"Tayari kuna visa vya vifo vinavyohusiana na joto kupita kiasi vinavyoripotiwa," mamlaka ilisema katika taarifa Jumamosi.
Walisema kuwa nchi ilikuwa ikipitia "vipindi vilivyoongezwa vya halijoto ya mchana na usiku ambayo inaleta mkazo mwingi wa kisaikolojia kwenye mwili wa mwanadamu".
Shule yoyote itakayopatikana imefunguliwa kuanzia Jumatatu itaondolewa usajili wake, mamlaka ilionya.
Wiki iliyopita, takriban watoto 15 waliripotiwa kufariki kutokana na homa ya uti wa mgongo na magonjwa mengine yanayohusiana na joto, kulingana na wizara ya afya.
Mbappe afunga Hat-trick huku PSG ikiicharaza Montpellier
Kylian Mbappe alifunga hat-trick wakati Paris St-Germain ilipoilaza Montpellier na kupanda juu kwa pointi 12 kwenye Ligue 1.
Vitinha alifunga bao la kwanza kabla ya Mbappe kufunga bao lake la kwanza kutoka kwa kona.
Arnaud Nordin aliwafungia wenyeji naye Teji Savanier akawasawazishia.
Bao lake mshambuliaji wa Ufaransa dakika ya 50 lilipaa juu ya lango na kuingia wavuni kutokana na shambulkio kali huku Lee Kang-in na Nuno Mendes pia wakicheka na lango la PSG.
Mbappe sasa ana mabao 24 ya ligi kwa msimu huu baada ya kufunga hat-trick yake ya tatu kwenye kampeni.
Putin aongoza kura ya Urais kwa asilimia 87
Dalili za ushindi wa Vladimir Putin wa upande mmoja kama Rais wa Urusi ni dhahiri.
Wasimamizi wa uchaguzi wametangaza kuwa alipata zaidi ya asilimia 87 ya kura katika matokeo yaliyotolewa kufikia sasa.
Putin amekuwa akisema kila mara kuwa ana uhakika wa kuchukua kiti cha urais kwa muhula wa tano.
Kufuatia tangazo la maafisa wa uchaguzi, Putin alitoa maoni kwamba demokrasia ya Urusi iko wazi zaidi kuliko katika nchi nyingi za Magharibi.
Hata hivyo, hakuna kiongozi mwenye nguvu wa upinzani aliyeweza kugombea uchaguzi huo dhidi ya Putin.
Nchi za Magharibi zilishutumu uchaguzi nchini Urusi kwa kutokuwa huru na wa haki.
Man United kukutana na Coventry baada ya kuindoa Liverpool FA
Manchester United waliweka hai matumaini yao ya kutwaa taji kwa msimu huu na kuhitimisha harakati za Liverpool kusaka mataji manne kwa ushindi mnono wa muda wa ziada katika mechi ya robo fainali ya Kombe la FA kwenye uwanja wa Old Trafford.
Hii ina maana kwamba Coventry City itamenyana na Manchester United katika nusu fainali ya Kombe la FA, huku mabingwa Manchester City wakicheza na Chelsea. Coventry City iliishinda Wolves katika robo fainali kwa bao la Haji Wright dakika ya 100.
Lakini katika pambano lililojaa matukio mengi, alikuwa mchezaji wa akiba Amad Diallo ambaye alipeleka kikosi cha Erik ten Hag Wembley kwa goli ndani ya sekunde chache za kipindi cha nyongeza. Baa ya bao hilo la ushindi mchezaji huyo alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kupata ya pili wakati akisherehekea bao lake.
Meneja wa United Ten Hag alifurahia huku shuti la Diallo likimpita kipa wa Liverpool Caoimhin Kelleher.
Hamu ya United ya kutinga hatua ya nne bora uwanjani Wembley ilionyeshwa katika mchezo wa mwanzo wa kasi ambao uliwafanya wapate bao la mapema, Scott McTominay akifunga bao la kufutia machozi katika dakika ya 10 baada ya Kelleher kusukuma nje shuti la Alejandro Garnacho.
Kelleher alimnyima McTominay tena kutoka karibu na goli kabla ya sare hiyo kugeuzwa kwa kichwa huku Liverpool wakifunga mabao mawili ndani ya dakika tatu kwa muda wa mapumziko na na kuwashangaza United.
Alexis Mac Allister alisawazisha wakati kombora lake lilipomgonga Kobbie Mainoo, United wakilazimika kulipa hatua ya kumruhusu Jarell Quansah kukimbilia mbele bila kupingwa na kumpatia pasi murua Darwin Nunez.
Naye Mohamed Salah, ambaye amezoa kuifunga United , alifunga tena kwa kasi kwa bao lake la 13 katika mechi 14 dhidi yao, baada ya Andre Onana kuokoa kutoka kwa Nunez.
Liverpool walipata nafasi nzuri zaidi baada ya kipindi cha mapumziko lakini Antony aliyetokea benchi aliisawazishia United dakika tatu kutoka mwisho wa muda wa kawaida kwa shuti hafifu lililopanguliwa na Marcus Rashford kisha akafunga bao rahisi na lake la ushindi la mchezo.
Mchezaji aliyetokea benchi Harvey Elliott aliiweka Liverpool mbele baada ya dakika 105, shuti lake la umbali wa yadi 20 lililomgusa Christian Eriksen aliyetokea benchi na kuingia wavuni .
Ilionekana kana kwamba mechi ilikuwa tayari kwa United lakini Rashford alirekebisha kosa lake la awali kwa bao lingine la kusawazisha na kumaliza mchezo baada ya Diallo kufunga .
Israel yafanya uvamizi mwengine wa usiku katika hospitali ya al-Shifa Gaza
Majeshi ya Israel yamefanya msako wa usiku kucha katika hospitali ya al-Shifa huko Gaza, huku kukiwa na ripoti za milipuko na milio ya risasi katika kituo hicho.
Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israeli alisema IDF ilikuwa ikifanya "operesheni ya usahihi wa hali ya juu katika maeneo machache" ya hospitali.
IDF ilisema "magaidi wakuu wa Hamas wamejipanga upya" ndani ya hospitali hiyo na wanaitumia kufanya mashambulizi.
Watu walioshuhudia tukio hilo walielezea hali ya hofu ndani ya jumba hilo la Gaza.
Katika simu iliyorekodiwa na kaka yake iliyotumwa kwenye kikundi cha WhatsApp, mwanamume mmoja alisema: "Milipuko imetuzunguka. Tumejificha ndani ya hema. Tunasikia mashambulizi ya vifaru karibu na boma."
Milio mikali ya risasi ilisikika karibu na hospitali hiyo katika picha ambazo hazijathibitishwa zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii.
Katika ujumbe wa sauti uliotumwa kwa waandishi wa habari kutoka ndani ya hospitali hiyo, Muhammad Al-Sayyid alisema: "Wanajeshi hapa ndani ya jengo hilo wamekufa na kujeruhiwa, na askari waliwakamata baadhi ya vijana. Hali hapa ni mbaya."
IDF haikuwa imeashiria hadharani mapema kwamba ilikuwa inapanga kuanzisha operesheni mpya katika al-Shifa.
Katika ujumbe wa video uliotumwa saa za mapema, msemaji mkuu wa IDF Rear Adm Daniel Hagari alisema jeshi la Israeli lilikuwa likijibu "intelijensia halisi ambayo ilitaka hatua za haraka".
Alisema hospitali hiyo itaweza kuendelea kufanya kazi wakati wa uvamizi huo na aliwaambia wagonjwa na wafanyakazi hawakulazimika kuhama.
Uchaguzi wa Urusi: Putin adai ushindi mkubwa huku akikejeli demokrasia ya Marekani
Rais Vladimir Putin bila shaka alitaraji kupata ushindi katika uchaguzi wake atakaohudumu kwa muhula wa tano kama rais wakati alipokuwa akikabiliana na wagombea wengine watatu wote wakiwa wamesimamishwa na serikali.
Lakini maafisa wa uchaguzi waliposema matokeo yalimpa zaidi ya 87% ya kura, alisema demokrasia ya Urusi ilikuwa ya uwazi zaidi kuliko nyingi katika nchi za Magharibi.Kwa kweli hakuna mgombea wa upinzani aliyekubalika kuruhusiwa kusimama.
Wafuasi wa mkosoaji aliyekufa wa Putin Alexei Navalny walifanya maandamanoMpango wao wa "Mchana dhidi ya Putin" ulimaanisha kuwa misururu mirefu ya wapiga kura ilijitokeza katika miji ya Urusi ikiwa ni pamoja na Moscow na St Petersburg na nje ya balozi nyingi nje ya nchi, lakini kamwe haikuweza kuwa na athari yoyote kwenye matokeo.
Kundi la ufuatiliaji la OVD-Info lilisema Warusi wasiopungua 80 walikamatwa. Hakukuwa na marudio ya mashambulizi ya hapa na pale kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura yaliyotokea siku ya Ijumaa.Nchi za Magharibi zilijitokeza kulaani upigaji kura huo kuwa haukuwa huru na wa haki.
Ujerumani iliuita "uchaguzi wa bandia" chini ya mtawala wa kimabavu anayeegemea kwenye udhibiti, ukandamizaji na vurugu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Bwana Cameron alilaani "kufanyika kinyume cha sheria kwa uchaguzi katika eneo la Ukraine".