Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Erdoğan: Uturuki ni nchi ambayo inasimama kidete nyuma ya Hamas

Rais Recep Tayyip Erdoğan amesema, "Hakuna mtu anayeweza kutufanya tuiite Hamas shirika la kigaidi. "Türkiye ni nchi ambayo inasimama kidete nyuma ya Hamas," alisema.

Moja kwa moja

Dinah Gahamanyi

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo, tukutane tena hapo kesho panapo majaaliwa.

  2. Vita vya Gaza vyazidisha hofu Jerusalem huku mwezi wa Ramadhan ukitarajiwa kuanza,

    Kuna hofu inayoendelea kujitokeza kutokana na ghasia zinazo kusambaa , hasa katika mji wa Jerusalem wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, huku ikiwa haijulikani mapigano yatasitishwa lini Gaza.

    Kundi la Hamas limesisitiza kwamba lingewataka Wapalestina kuongeza ibada zao katika msikiti mtakatifu wa Al Aqsa.

    Israel imeilaumu Hamas kwa kile imetaja kuwa, ‘ mbinu ya kuchochea ghasia katika eneo hilo, wakati wa ibada takatifu ya mfungo katika mwezi wa Ramadhan,’ ambao unatarajiwa kuanza wakati wowote katika wiki hii.

    Eneo la tatu lenye umuhimu katika ibada za Waislam lipo hapa na hutumika na wakazi wa hapa ambao ni waumini wa dini hiyo.

    Lakini eneo hili – ambalo pia ni takatifu katika dini ya Kiyahudi- linalofahamika kama hekalu la mlimani au TEMPLE MOUNT, hushuhudia makabiliano ya mara kwa mara katiak mzozo kati ya Israel na Palestina.

    Mwezi wa mfungo wa Ramdhan unatarajiwa kuanza Machi 10 au 11, kulingana na kuonekana kwa mwezi mpya.

    Wiki iliyopita eneo la nje la msikiti wa Al Aqsa lilikuwa tulivu wakati mwandishi wa BBC Yolande Knell alipozuru eneo hilo, ila waumini wa Kipalestina waliwazia sana vita vinavyoendelea ndani ya Gaza.

    ‘Wengi hawahisi kwamba kuna mengi ya kufurahia sherehe na tamaduni zinazoandaliwa katika mwezi wa mfungo wa Ramadhan,’ alisema mwanamke mmoja anayeitwa Ayat. Aliongeza kusema, ‘'Kwa huzuni, mwaka huu, sherehe na tamaduni hizo hazitafanyika kwa sababu ya yanayoendelea kutokea Gaza.’'

  3. Burundi yaondolewa kwenye shindano la mpira wa kikapu kwasababu ya fulana yenye chapa ya Rwanda

    Timu ya Dynamo kutoka Burundi imefungiwa kushiriki michuano ya Ligi ya Mpira wa Kikapu Afrika (BAL4) inayoendelea mjini Pretoria, Afrika Kusini.

    Hatua hiyo Imejumuishwa katika taarifa iliyowekwa kwenye tovuti na waandaaji wa shindano hilo.

    Mechi kati ya Dynamo na FUS Rabat ya Morocco leo ilifutwa kwa sababu Dynamo walipoteza mechi hiyo.

    Kwa mujibu wa barua ya mkuu wa BAL, Amadou Gallo Fall, Dynamo ilikataa kuvaa sare ya shindano hilo lenye maandishi ya "Visit Rwanda", mdhamini mkuu wa shindano hilo.

    Taarifa hizo zimethibitishwa na walioandamana na timu ya Dynamo mjini Pretoria.

    Kwa maneno machache, mmoja wao alituambia: "Hatukutoka, tulitaka kucheza lakini timu ya taifa ilitushambulia, inasikitisha sana kwetu.

    "Inasikitisha kwamba tulikuwa tayari kucheza kwa sababu ya siasa wakati michezo haihusishi na siasa. Ni hasara kwa Burundi na Warundi."

    Katika Wizara ya Michezo nchini Burundi, tuliwauliza wakatuambia kwamba watakuwa na jambo la kusema kuhusu hilo baadaye.

    Katika mchezo wa kwanza wa jana, Jumamosi, Dynamo ilishinda pointi 86 kati ya 73 za Cape Town Tigers ya Afrika Kusini, ingawa ilicheza ikiwa imevaa fulana yenye chapa ya "Visit Rwanda".

    Siku ya Jumamosi, timu ya Dynamo iliamriwa na shirika la mpira wa kikapu nchini Burundi, FEBABU, na serikali ya Burundi, kutovaa shati yenye maandishi "Visit Rwanda", ambayo huitangaza Rwanda kiutalii.

    Sababu ni kwamba Burundi inailaumu Rwanda kwa kuvuruga usalama wa Burundi, jambo ambalo Rwanda inalikanusha.

  4. Habari za hivi punde, Waumini wa Kiislamu nchini Saudi Arabia kuanza Mwezi Mtukufu wa Ramadhan Jumatatu tarehe 11 Machi,

    Waumuni wa dini ya Kiislamu nchini Saudi Arabia wataanza kuadhimisha mwezi mtukufu wa Ramadhan kuanzia jumatatu tarehe 11, Machi

    Haya yamethibitishwa na wasimamizi wa Msikiti mkuu wa Al Haramain ambao dakika chache zilizopita wametangaza kuonekana kwa mwezi nchini humo.

    Kuonekana kwa mwezi huo kunaashirika kukamilika kwa mwezi wa Shaaban na manzo wa ibada ya mfungo ambayo hufanyika kwa muda wa kati ya siku 29 au 30 kulingana na kuonekana kwa mwezi.

    Katika nchi za Afrika mashariki kadhi mkuu wa Kenya Athman AbdulHalim aliwataka Waislamu kuanza kutazama mwezi wa Ramadhan kuanzia magharibi ya Jumatatu tarehe 11 Machi.

    Ibada ya saumu au kufunga ni mojawapo ya nguzo tano za Uislamu kama vile kuswali mara tano kwa siku, kutoa zaka, na kutoa shahada.

  5. Tazama: Ndege ya United Airlines ilipopoteza gurudumu lake wakati wa kupaa

    Ndege hiyo aina ya Boeing-777 iliyokuwa ikienda Tokyo ilielekezwa Los Angeles, ambako ilitua kwa dharura kwa usalama. Hakuna aliyejeruhiwa.

    Video inaonyesha moja ya magurudumu yake kutoka kwa kifaa kikuu cha kutua cha ndege ikianguka sekunde chache baada ya ndege hiyo kupaa kutoka uwanja wa ndege wa San Francisco siku ya Alhamisi.

    Vifusi vilitua katika eneo la kuegesha magari ya wafanyikazi wa uwanja wa ndege, ambapo angalau gari moja lilionekana kuharibiwa.

  6. Papa Francis aitaka Ukraine kuwa na 'ujasiri wa bendera nyeupe' na kufanya mazungumzo ya kumaliza vita na Urusi

    Papa Francis anasema Ukraine inapaswa kuwa na kile alichokiita "ujasiri wa bendera nyeupe" na kujadiliana kusitisha vita na Urusi vilivyofuatia uvamizi kamili wa Moscow miaka miwili iliyopita.

    Francis alitoa maoni yake katika mahojiano yaliyorekodiwa mwezi uliopita na shirika la utangazaji la Uswizi RSI, kabla ya Ijumaa ya hivi punde kutolewa na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdoğan kuandaa mkutano wa kilele kati ya Ukraine na Urusi kumaliza vita.

    Bw Erdoğan alitoa fursa hiyo mpya baada ya mkutano mjini Istanbul na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy. Bw Zelenskyy amesema ingawa anataka amani, hataacha eneo lolote.

    Mpango wa amani wa kiongozi huyo wa Ukraine mwenyewe unatoa wito wa kuondolewa kwa wanajeshi wa Urusi kutoka Ukraine yote na kurejeshwa kwa mipaka yake ya majimbo. Ikulu ya Kremlin imekataa kushiriki katika mazungumzo ya amani kwa masharti yaliyowekwa na Kyiv.

    Msemaji wa Bw Zelenskyy hakujibu mara moja ombi la maoni yake kuhusu matamshi ya papa.

    Katika mahojiano hayo, Francis aliulizwa msimamo wake kuhusu mdahalo kati ya wale wanaosema Ukraine inapaswa kukata tamaa kwa vile haijaweza kuwafukuza wanajeshi wa Urusi, na wale wanaosema kufanya hivyo kungehalalisha vitendo vya chama chenye nguvu zaidi.

    Mhojiwa alitumia neno "bendera nyeupe" katika swali.

    "Ni tafsiri moja, hiyo ni kweli," Francis alisema, kulingana na nakala ya mapema ya mahojiano na sehemu ya video iliyotolewa kwa Reuters siku ya Jumamosi.

    Inatarajiwa kutangazwa Machi 20 kama sehemu ya programu mpya ya kitamaduni.

    "Lakini nadhani aliye na nguvu zaidi ni yule anayeangalia hali, anafikiria watu na ana ujasiri wa bendera nyeupe, na kufanya mazungumzo," Francis alisema.

    "Jadili kwa wakati, tafuta aina fulani ya nchi mpatanishi. Leo, kwa mfano, katika vita vya Ukraine kuna wengi ambao wanataka kufanya kama wapatanishi. Uturuki ilijitolea kwa hili. Na wengine.Usione aibu kujadiliana kabla mambo hayajawa mabaya zaidi,” Francis aliongeza.

    Hatahivyo wanaoiunga mkono Ukraine katika vita vyake na Urusi wamekosoa hatua hiyo ya Papa kwenye mitandao ya kijamii wakisema kuwa kwa Ukraine kuzungumza na Urusi ni kuhalalisha uvamizi wa Urusi.

    Ukraine imeapa kutozungumza na Urusi hadi itakapositisha vita na kurejesha maeneo iliyoyateka.

  7. Vita vya Ukraine: Ndege isiyo na rubani ya kamikaze ya Urusi ilivyogonga kituo cha viwanda Odessa.

    Usiku wa kuamkia leo, ndege isiyo na rubani ya kamikaze iligonga kituo cha viwanda katika eneo la Odessa, na kuharibu jengo muhimu ambalo ni kituo cha viwanda

    Moto huo umezimwa na hakukuwa na majeruhi, mamlaka ya jiji inaripoti.

    Mamlaka ya mkoa wa Nikolaev iliripoti uharibifu wa nyaya za umeme na kwamba kazi imekuwa ikiendelea kuzikarabati nyaya za umeme ili kuurejesha.

    Wakati haya yakijiri jeshi la Ukraine limesema kuwa ndege hizo 35 kati ya 39 wzililipuliwa risasi usiku kucha.

    Kufikia saa 7 asubuhi, mashambulio 35 ya droni za Urusi aina ya UAVs Shahed-136/131 zililipuliwa kwa risasi mjini Kyiv, kulingana na kituo cha amri za kijeshi cha Kikosi cha Wanga cha Ukraine.

    Jumla ya ndege zisizo na rubani 39 za aina hii za Urusi zilifanya mashambulizi kote nchini Ukraine kwa mpigo, ripoti hiyo inasema.

  8. Mwanafunzi wa Urusi afungwa jela kwa kutumia jina la Wi-fi ambalo linaashiria uungaji mkono wa Ukraine

    Mwanafunzi wa Chuo kikuu nchini Urusi amehukumiwa kifungo cha siku kumi gerezani, jijini Moscow baada ya kuipa anwani yake ya Wi-fi jina ambalo linaashiria uungaji mkono wa taifa la Ukraine.

    Mwanafunzi huyo anayesoma katika chou kikuu cha Moscow State alikuwa ameliupa anwani ya mtandao wake wa Wi-fi, jina la kirusi la ‘Slava Ukrani!’ ambalo lina maana ya , ‘Ushindi kwa Ukraine!’.

    Mahakama moja jijini Moscow ilimpata na hatia ya kuchapisha ‘ishara au nembo za makundi yenye itikadi kali, alipofikishwa mbele yake siku ya alhamisi wiki jana.

    Tangu kuanza kwa vita vya Urusi dhidi ya Ukraine, maelfu wamehukumiwa kifungo cha muda tofauti gerezani au kutozwa faini kwa kuikashifu serikali ya Urusi katika uvamizi wake wa Ukraine au kuonekana kuiunga mkono Ukraine.

    Mwanafunzi huyo alikamatwa Jumatano wiki iliyopita mjini Moscow, baada ya afisa wa polisi kuiripoti mtandao wake wa Wi-Fi kwa mamlaka.

    Kuklingana na stakabadhi za mahakama, mwanafunzi huyo alikamatwa kwenye chumba chake katika bweni la chuo hicho alipokamatwa na vifaa vya mtandao na kusambaza huduma ya wifi.

    Mahakama hiyo imesema kwamba alitumia mtanadao kusambaza maneno ya kuunga mkono ‘ushindi kwa Ukraine’ au ‘Slava Ukrani’ kwa idadi isiyojulikana ya watu wanaotumia WiFi hiyo.

    Tamko hilo la ‘Slava Ukrani’ limekuwa wito ambao Ukraine umeitumia kuwashawishi wafuasi wake kuishinikiza Urusi katika vita hivyo vya miaka miwili. Na limekuwa likitumika katika maandamano yaliyoandaliwa ndani ya Urusi hasa baada ya kiongozi wa taifa hilo kuamrisha majeshi ya Urusi kulivamia taifa Jirani la Ukraine.

    Vita vya Ukraine : Mengi zaidi

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  9. Erdoğan: Uturuki ni nchi ambayo inasimama kidete nyuma ya Hamas

    Rais Recep Tayyip Erdoğan amesema, "Hakuna mtu anayeweza kutufanya tuiite Hamas shirika la kigaidi. "Türkiye ni nchi ambayo inasimama kidete nyuma ya Hamas," alisema.

    Akizungumzia mkutano wake na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas mjini Ankara wiki hii, Erdoğan alisema, "Israel, taifa la kigaidi, linatekeleza sera ya mauaji ya kimbari dhidi ya ndugu zetu wa Palestina."

    Erdoğan alizungumza katika Mkutano Mkuu wa Wakfu wa Usambazaji wa Sayansi uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo Kikuu cha Haliç mjini Istanbul.

    "Uturuki ndio nchi pekee inayoiunga mkono Palestina kwa kiwango cha juu. "Yeyote anayekosoa 'Hawezi kufanya chochote' amingia bila ruhusa," alisema Erdogan, na akarudia shutuma ya "Nazi" aliyotumia Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

    Rais alisema, "Netanyahu na utawala wake dhalimu, kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu waliofanya huko Gaza, ameongeza jina lake kwa Hitler, Mussolini, Stalin, Franco na wauaji wengine wa kisasa kama Wanazi wa leo."

    Erdogan pia alikuwa alimuelezea Netanyahu kama Mnazi katika hotuba zake za awali.

  10. Jeshi la Israel lakamilisha ujenzi wa barabara inayopita katikati ya ukanda wa Gaza, picha za Satilaiti zaonyesha

    Jeshi la Israel limekamilisha ujenzi wa barabara mpya inayopita katitaki ya eneo la kaskazini mwa Gaza kutoka mashariki hadi magharibi mwa eneo hilo. Haya ni kwa mujibu wa picha za satelaiti zilizodhibitishwa na kitengo cha uchunguzi cha BBC verify.

    Jeshi hilo limeiambia BBC kuwa linajaribu kuhakikisha kwamba linapata udhibiti wa eneo husika na kuwawezesha wanajeshi wake kusafiri kwa magari na silaha zao katika eneo hilo kwa usalama na bila changamoto.

    Lakini baadhi ya wataalamu wanahofu kwamba huenda barabara hiyo ikatumika kama kizingiti cha kuwazuia wapalestina kutorejea katika makazi yao kaskazini mwa Gaza.

    Wengine wanasema kwamba inaonekana kuwa nisehemu ya mipango ya Israel ya kuendelea kuwa ndani ya Gaza, hata baada ya vita vinavyoendelea kukamilika.

    Mnamo Februari mwaka huu, Waziri mkuu Benjamin Netanyahu alizindua ruwaza ya baada ya vita ambayo inaonyesha jinsi Israel inanavyoweza kuchukua jukumu la kusimamia ukanda wa Gaza kwa muda usiojulikana.

    Viongozi wa kimataifa wameionya Israel dhidi ya kufanya mipango ya kikamilifu itakayo wapotezea makao Wapalestina au kupunguza eneo la ardhi ya Ukanda huo wa Gaza.

    Ni kipi tunachokifahamu kuhusu barabara hii?

    • Inapita katikati kati ya eneo la kaskazini la Gaza, na kuwa kati kati ya eneo la kaskazini lililoko juu yake na la kusini lililoko chini yake.
    • Inaanzia kwenye mpaka wa Gaza na Israel karibu na mji wa Nahal oz Kibbutz na kumalizikia karibu na bahari.
    • Inaungana na barabara za salah al din na ile ya nahal oz Kibbutz, ambazo ni barabara mbiili kubwa zinazotumika katika eneo hilo kuu.

    Picha za Satelaiti ambazo zimefanyiwa uchunguzi na utafiti wa kina na BBC, zimeonyesha kwamba jeshi la Israel limejenga barabara mpya yenye umbali wa kilomita zaidi ya tano ya maeneo mapya ya barabara ili kuuunganisha barabara zingine ambazo hazikuwa zimeshikana.

  11. Shughuli ya uokoaji inaendelea baada ya moto kuibuka katika soko muhimu la Somalia

    Wazima moto nchini Somalia wamekuwa wakishirikiana na polisi na raia katika juhudi za kuuzima moto mkubwa ambao umezuka mapema Jumapili katika soko la Bakara mjini Mogadishu.

    Moto huo mkubwa unaoripotiwa kuanza mapema asubuhi, umeteketeza maduka kwenye soko hilo kubwa kabisa mjini Mogadishu ambalo ni mashuhuri kwa wafanyibiashara wa bidhaa mbali mbali na wanunuzi.

    Wengi waliofika kuanza shughuli zao za mwanzo wa wiki baada ya mapumziko ya wikendi, walipatwa na mshtuko kuuona moto ukisambaa kwa haraka.

    Polisi nchini humo wamesema kwamba pindi tu, moto utakapo dhibitiwa, uchunguzi kujuwa chanzo cha moto huo utaanzishwa mara moja.

  12. 'Nataka wa kunitua mzigo nilioubeba' - Kagame baada ya kuidhinishwa kuwa mgombea wa RPF

    Rais Kagame alisema kuwa "upekee wa nchi yetu, wa historia yetu" ulimfanya afanye kampeni tena

    Mkutano wa chama tawala cha RPF-Inkotanyi nchini Rwanda jana usiku ulimthibitisha Rais Paul Kagame kuwa mgombea wake katika uchaguzi wa urais wa Julai (7) mwaka huu.

    Miongoni mwa waliopiga kura katika mkutano huo uliohudhuriwa zaidi ya ule wa mwaka 2000, Kagame alichaguliwa kwa asilimia 99.1 ya kura, kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari vya Rwanda.

    Septemba (9) mwaka jana, Kagame aliliambia gazeti la Ufaransa la Jeune Afrique kuwa yeye ni mgombea urais kwa awamu ya nne. Inabakia chama tawala cha RPF kumuidhinisha kuwa mgombea.

    Hadi sasa baadhi ya watu waliojitokeza kutaka kugombea nafasi ya kiti cha rais wa Jamhuri wakiwemo kiongozi wa upinzani Victoire Ingabire wa chama cha DALFA-Umurinzi na Bernard Ntaganda wa chama cha PS-Imberakuri , vyama vyao vyote viwili havitambuliwi na sheria nchini Rwanda.

    'Nataka wa kunitua mzigo'

    Katika hotuba yake baada ya kuidhinishwa kuwa mgombea, Kagame aliwashukuru wanachama kwa kumuamini, lakini akawataka waanze kufikiria juu ya nani atakayekuwa mbadala wake.

    Akasema: "Mzigo mlionipa niubebe, nimekubali kuubeba. Lakini... nataka wa kunitua mzigo nilioubeba. Na watakaoubeba wako miongoni mwenu."aliwambia wajumbe wa mkutano wa RPF.

    Akizungumzia kuhusu kukubali kufanya kampeni tena, Kagame alisema kuwa "upekee wa nchi yetu, historia yetu, na ulimwengu mgumu tunaoishi, ndio maana naangalia pande zote na kukubali’’

    "Vinginevyo tunafaa kuwatafuta wengine miongoni mwetu... na kuendelea na safari ipasavyo", anasema kwamba kuna haja ya "bima ya kile tunachokijenga".

    Akasema, "Hata kama nilikubali - na sina pa kukimbilia ... sitaki kuwashtukiza ... na msisubiri nitakaowapatia, mujitafutie wenyewe miongoni mwenu." Alisema.

    Lakini Kagame alisema wakimchagua mtu ambaye hafai kuchukua nafasi yake haimzuii kuwaambia kuwa “hili ni kosa”. Alisema angependa nafasi yake kuchukuliwa na mtu wa kati ya miaka 30 na 49.

    Katika mkutano huo, RPF ilipitisha orodha ya watu 70 watakaoiwakilisha kuwa naibu wagombea katika uchaguzi wa urais utakaofanyika wakati huo huo wa ubunge, Julai 15 (7) mwaka huu.

  13. Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika alaani utekaji nyara kaskazini mwa Nigeria

    Mwenyekiti wa baraza la umoja wa Afrika Moussa Faki Mahammat amelaani mashambulizi yanayozidi kuripotiwa kaskazini mwa Nigeria ambapo Watoto wadogo na kina mama wamelengwa na wapiganaji wa kundi la Boko Haramu kwa kutekwa nyara.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X, Faki amewataka ,‘''waliotekeleza uhalifu huo kuwarejesha Watoto waliotekwa mara moja kwa familia zao''.

    Ameendelea kusema kwamba, ‘ kitendo hicho ni ishara kwamba tishio la ugaidi na wizi wa mifugo ni masuala yanayotishia sio tu usalama wa eneo la kaskazini mwa Nigeria bali eneo zima na hata mataifa Jirani na jambo ambalo linasikitisha wote barani Afrika.’

    Haya yanajiri wakati ambapo wanafunzi 15 walitekwa Jumamosi, katika eneo la Gada, katika jimbo la Sokoto, kaskazini mwa Nigeria.

    Mbunge wa eneo hilo aliiambia idhaa ya Hausa ya BBC kwamba shambulizi hilo lilitokea alfajiri, ambapo wapiganaji pia waliwateka wanawake wanne.

    Siku ya Alhamisi wiki iiyopita , wanafunzi takriban 300 walitekwa na wapiganaji waliojihami kwa silaha ambao walitumia pikipiki kushambulia shule ya umma katika jimbo la Kaduna.

    Aidha, awali makumi ya wanawake waliokuwa kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani katika jimbo la Borno, walitekwa huku mamlaka nchini humo ikihofia kwamba huenda wakawa watumwa wa wapiganaji wa kundi hilo wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

    Jeshi la Nigeria linaongoza vikosi vya usalama katika operesheni ya kusawaka mateka hao waliosemekana kufichwa katika misitu iliyopo kaskazini mwa taifa hilo, huku vifaa kama ndege zisizo na rubani zikitumwa kufanya uchunguzi zaidi katika maeneo yanayojulikana kuwa maficho ya kundi hilo ili kujaribu kuwarejesha Watoto.

    Hadi ijumaa, ni Watoto chini ya 70 waliokuwa wameokolewa.

  14. Meli ya kijeshi ya Marekani yaelekea Gaza kujenga bandari

    Meli ya kijeshi ya Marekani inasafiri kuelekea Mashariki ya Kati, ikiwa na vifaa vya kujenga bandari yya muda kwenye pwani ya Gaza, jeshi linasema.

    Meli hiyo ya msaada, Jenerali Frank S Besson, ilisafiri kutoka kambi ya kijeshi katika jimbo la Virginia siku ya Jumamosi.

    Inakuja baada ya Rais Joe Biden kusema kuwa Marekani itajenga bandari inayoelea ili kusaidia upatikanaji wa msaada Gaza kwa njia ya bahari.

    Umoja wa Mataifa umeonya kuwa njaa katika Ukanda wa Gaza ni "karibu isiyoepukika" na watoto wanakufa kwa njaa.

    Uwasilishaji wa misaada kwa njia ya ardhi na anga umeonekana kuwa mgumu na hatari.

    Shirika la mpango wa chakula duniani lililazimika kusitisha usafirishaji wa barabarabaada ya misafara yake kushambuliwa kwa risasi na uporaji.

    Na mnamo Ijumaa kulikuwa na ripoti kuwa watu watano waliuliwa na kifurushi cha misaada kilianguka, wakati parashuti yake iliposhindwa kufunguka vizuri.

    Meli ya Marekani iliondoka "chini ya saa 36" baada ya Bw Biden kutoa tangazo lake, Kamanda Mkuu wa Marekani aliandika kwenye X.

    "Inabeba vifaa vya kwanza vya kuanzisha bandari ya muda ya kupeleka vifaa muhimu vya kibinadamu" huko Gaza, taarifa hiyo iliendelea.

    Pentagon imesema inaweza kuchukua hadi siku 60 kujenga bandari hiyo kwa usaidizi wa wanajeshi 1,000 - hakuna hata mmoja ambaye angeenda ufukwenii

  15. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya mubashara leo ikiwa ni Jumapili tarehe 10.03.2024