Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Waasi wa Houthi waapa kulipiza mashambulizi ya Marekani na Uingereza nchini Yemen

Marekani na Uingereza zilianzisha mashambulizi kulenga vituo vya kijeshi kujibu mashambulizi ya Wahouthi dhidi ya meli katika Bahari ya Shamu.

Moja kwa moja

Yusuf Jumah, Ambia Hirsi and Dinah Gahamanyi

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Hadi kesho kwaheri.

  2. Utawala wa kijeshi nchini Mali junta kufanya uchaguzi 'haraka iwezekanavyo'- waziri

    Waziri katika serikali ya kijeshi ya Mali amesema serikali yake inataka kufanya uchaguzi wa mpito "haraka iwezekanavyo", kulingana na tovuti ya habari inayomilikiwa na serikali L'Essor.

    Kanali Abdoulaye Maiga alisema changamoto ya hivi punde katika mchakato wa uchaguzi ni kuanza tena kwa uhasama na makundi ya zamani ya watu wanaotaka kujitenga kaskazini mwa nchi, lakini aliwahakikishia umma kuwa serikali inajitahidi kuhakikisha utulivu unadumishwa.

    Pia alihutubia kuahirishwa kwa uchaguzi wa Septemba mwaka jana.

    “Tupende tusipende, iwe tunaunga mkono hoja hizo au la, leo hii Kidal [ngome kuu ilikombolewa na jeshi mwaka jana] kama hatua ya kurefushautawala huu.

    " Hii ni hali halisi isiyopingika na lazima izingatiwe,” Kanali Maiga alisema.

    Serikali ya kijeshi, inayoongozwa na Kanali Assimi Goïta, ilichukua mamlaka mnamo Mei 2021.

    Viongozi wa mapinduzi wamekuwa chini ya shinikizo la kutangaza tarehe za uchaguzi mpya wa mpito baada ya uchaguzi wa awali uliokuwa umepangwa kufanyika Februari 2024 "kuahirishwa".

    Utawala wa kijeshi ulitaja sababu za "kiufundi" zinazohusiana na kupitishwa kwa katiba mpya na marekebisho ya sajili ya wapigakura na wakala wa uchaguzi.

  3. Afrika Kusini: Sanamu ya Desmond Tutu iliyofunikwa kilemba cha Wapalestina yazinduliwa

    Sanamu ya marehemu Askofu Mkuu wa Afrika Kusini Desmond Tutu iliyofunikwa kilemba cha Wapalestina imezinduliwa mjini Cape Town kuashiria uungaji mkono wake kwa Palestina.

    Wakfu wa Desmond na Leah Tutu Legacy ulisema kuwa sanamu hiyo itaonyeshwa kwa muda hadi shambulio la bomu mjini Gaza litakapositishwa.

    Israel inasema inajaribu kuiondoa Hamas, ambayo ilianzisha mashambulizi dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba, na kuua watu 1,300 na kuwashikilia wengine 240 huko Gaza kama mateka.

    Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas mjini Gaza inasema zaidi ya watu 23,350 - wengi wao wakiwa wanawake na watoto - wameuawa na Israel katika vita hivyo.

    Askofu Mkuu Tutu alikuwa mkosoaji mkubwa wa sera za Israel dhidi ya Wapalestina ambazo alizifananisha na vitendo vya mamlaka ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

    Chama tawala cha ANC pia kwa muda mrefu kimekuwa kikiunga mkono hoja ya Palestina.

    Israel leo(Ijumaa) imekuwa ikijitetea katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki mjini The Hague dhidi ya shutuma za Afrika Kusini kwamba inatekeleza mauaji ya kimbari huko Gaza

    Ilisema Afrika Kusini imepotosha ukweli na kwamba ilikuwa imewasilisha "maelezo yanayopingana na ukweli" kuhusu mzozo wa Israel na Palestina.

  4. AFCON: Tazama shauku ya mashabiki wa soka nchini Ivory Coast

    Michuano ya soka barani Afrika AFCON kwa mwaka 2024 iko mbioni kupuliza kipenga.

    Tanzania ikiwa ni mmoja wa wawakilishi katika ukanda wa Afrika Mashariki ambapo imepangwa katika kundi F ambalo lipo Taifa la Morocco, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo na nchi jirani na Tanzania ya Zambia.

    Mwandishi wetu aliyeko nchini Ivory Coast Frank Mavura amezungumza na baadhi ya mashabiki wa soka nchini humo.

  5. Israel inasema Afrika Kusini inapotosha ukweli katika kesi ya mauaji ya kimbari ya ICJ

    Israel imesema Afrika Kusini imepotosha ukweli katika kesi yake iliyowasilisha kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ, ambapo inaishutumu Israel kwa mauaji ya halaiki.

    Afrika Kusini ilikuwa imewasilisha "maelezo yanayopingana na ukweli" ya mzozo wa Israel na Palestina, wakili wa Israel Tal Becker aliiambia ICJ.

    Afrika Kusini inasema Israel inafanya mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina katika vita vyake huko Gaza.

    Pia inaomba mahakama iamuru Israel kusitisha shughuli zake za kijeshi. ICJ ndiyo mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa.

    Maamuzi yake kinadharia yanawabana kisheria pande zinazohusika na ICJ - ambazo ni pamoja na Israel na Afrika Kusini - lakini hazitekelezeki. Israel inatoa utetezi wake mbele ya mahakama siku moja baada ya Afrika Kusini kuwasilisha kesi yake.

    Nje ya uwanja wa vita vya kisheria wa ICJ, polisi wameunda kamba kuhakikisha vikundi vinavyopingana vinawekwa mbali.

    Afrika Kusini inadai kuwa Israel inakiuka Mkataba wa Mauaji ya Kimbari ya mwaka 1949, ambapo mataifa yote mawili yametia saini, na ambayo inajihusisha na kuzuia mauaji ya kimbari kutokea.

    Israel imekuwa ikiendesha vita dhidi ya Hamas, kundi tawala la Gaza, tangu tarehe 7 Oktoba, wakati mamia ya watu wenye silaha wa Hamas walipoivamia Israel, na kuua takriban watu 1,300 na kuwarudisha karibu watu 240 huko Gaza kama mateka.

    Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas huko Gaza inasema zaidi ya watu 23,350 - wengi wao wakiwa wanawake na watoto - wameuawa na Israel katika vita hivyo.

  6. Viongozi wa kikatoliki wa Afrika wapinga agizo la Papa la kuwabariki wapenzi wa jinsi moja

    Maaskofu wa Kanisa Katoliki barani Afrika wamepinga tamko la Papa Francis la kuwabariki wapenzi wa jinsi moja wakidai kuwa ni kinyume na mapenzi ya Mungu.

    Kongamano la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar(Secam) - Muungano wa Maaskofu wa Kikatoliki kote Afrika - ulisema katika taarifa kwamba hatua ya Vatican kubariki wapenzi wa jinsi moja "haifai".

    "Mafundisho ya mara kwa mara ya Kanisa yanaelezea vitendo vya wapenzi wa aina hiyo kuwa 'vya kuchukiza' na kinyume na sheria ya asili.''

    Rais wa Secam, Kardinali Fridolin Ambongo, alisema ujumbe huo umeidhinishwa na Papa Francis na wataendelea na ushirika wao na mkuu wa Kanisa Katoliki.

    Mwezi uliopita, Papa Francis alitangaza kwamba makasisi wanapaswa kuruhusiwa kuwabariki wapenzi wa jinsi moja.

    Hili limezua hisia tofauti kutoka kwa Kanisa Katoliki na jumuiya ya LGBT.

    Lakini Vatican ilisema baraka hazipaswi kuwa sehemu ya taratibu za kawaida za Kanisa au zinazohusiana na miungano ya kiraia au harusi.

    Iliongeza kuwa msimamo wa kanisi ni kwamba ndoa ni ya kati ya mwanamume na mwanamke.

    Kuna nchi 64 ulimwenguni ambazo zinaharamisha mapenzi ya jinsi moja na karibu nusu ya hizi ziko barani Afrika.

  7. Urusi yasema mashambulio ya marekani na Uingereza nchini Yemen 'sio halali'

    Tumesikia hivi punde kutoka kwa msemaji wa Kremlin akilaani mashambulizi ya Marekani na Uingereza nchini Yemen.

    "Kwa mtazamo wa sheria za kimataifa, sio halali," anasema Dmitry Peskov.

    Peskov pia anasema kwamba Kremlin imewahimiza mara kwa mara Wahouthi kusitisha mashambulio dhidi ya meli.

    Urusi, ambayo imekosolewa kwa kile nchi za Magharibi zinasema kuwa ni vita haramu nchini Ukraine, inasema shambulio hilo dhidi ya Yemen lilifanyika bila ya idhini yoyote kutoka kwa Umoja wa Mataifa na lilikuwa ni "udiriki " usio halali wa Marekani na washirika wake.

    Urusi pia inataka mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa.

    Urusi ni mshirika wa karibu wa Iran, ambayo huwapa silaha, kuwafunza na kuwaunga mkono Wahouthi.

    Urusi na Uchina hazikupifa kura juu ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano lililowataka Wahouthi kusitisha mara moja mashambulizi yao dhidi ya meli na kubainisha haki ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa "kulinda meli zao dhidi ya mashambulizi".

  8. Mawakili wa Kenya waandamana kupinga vitisho vya Rais Ruto dhidi ya majaji

    Makumi ya mawakili wanaandamana katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, kujibu vitisho vya kukaidi amri ya mahakama yvilivyotolewa na Rais William Ruto.

    Mawakili hao wanaandamana kutoka Mahakama ya Juu hadi afisi ya rais katika maandamano yaliyopangwa na Chama cha Wanasheria nchini (LSK).

    Rais Ruto alikosolewa wiki iliyopita baada ya kutishia kutotii maagizo ya mahakama, akidai kuwa baadhi ya majaji ambao hawakutaja waliungana na wanasiasa wa upinzani kuzuia miradi ya utawala wake.

    "Rais wa nchi hii hayuko juu ya sheria. Kwa hivyo, hatutarajii azungumze kana kwamba kutii amri za mahakama ni upendeleo anaofanyia nchi. Ni hitaji la kikatiba," rais wa LSK Eric Theuri alisema.katika mkutano na wanahabari siku ya Alhamisi.

    Bw Theuri aliongeza kuwa LSK itafikiria kuanzisha mchakato wa kumuondoa madarakani Rais Ruto kwa "kukiuka katiba" ikiwa ataendelea na mashambulizi yake dhidi ya mahakama.

    LSK imekusanya timu ya wanasheria kuwasilisha ombi katika Mahakama ya Juu dhdi ya Bw Ruto kwa kukiuka katiba, Bw Theuri aliambia gazeti la Standard.

    Mawakili kadhaa maarufu nchini Kenya wamejiunga na maandamano hayo, akiwemo Makamu wa Rais wa zamani Kalonzo Musyoka na waziri wa zamani Eugene Wamalwa, ambao kwa sasa ni wanasiasa wa upinzani.

    Jaji Mkuu Martha Koome na kinara wa upinzani Raila Odinga wiki jana walimuonya Bw Ruto kwamba kukaidi mahakama kutaanzisha hali ya machafuko nchini.

  9. Raia wauawa katika shambulio la makombora dhidi ya mji mkuu wa Sudan

    Raia 10 wameuawa baada ya jeshi la Sudan na kundi hasimu la Rapid Support Forces (RSF) kushambuliana kwa mizinga kusini mwa mji mkuu Khartoum.

    Mwanaharakati Muhammad Kindasha aliiambia tovuti ya habari ya Sudan Tribune kwamba baadhi ya wahasiriwa walikufa wakati kombora la risasi lilipopiga "nyumba ambayo tukio la kijamii lilikuwa likifanywa" siku ya Alhamisi.

    Aliongeza kuwa kulikuwa na "makabiliano makali" kati ya jeshi na RSF katika maeneo ya makazi, akielezea hali kama "janga".

    Shells pia zimeripotiwa kugonga soko la ndani. Raia wengi wameuawa kwa kushambuliwa kwa makombora kiholela mjini Khartoum tangu vita kati ya jeshi na RSF kuanza Aprili 2023.

    Mapigano kati ya pande hizo mbili yameongezeka zaidi ya wiki iliyopita katika mji mkuu na miji ya karibu ya Omdurman na Bahri, huku jeshi likidai kusonga mbele.

    Mzozo huo umesababisha vifo vya takriban watu 12,000 na wengine zaidi ya milioni saba kuyahama makazi yao, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

  10. Mahakama DR Congo yawafunga 15 kwa 'kufadhili ugaidi'

    Mahakama ya kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imewahukumu watu 15 jela baada ya kuwapata na hatia ya kufadhili ugaidi kupitia biashara haramu ya dhahabu.

    Mahakama hiyo mnamo Alhamisi iliwafunga washukiwa 10 kwa vifungo vya kati ya miaka mitano na minane na kuwapa wengine watano kifungo cha miaka 10.

    Mahakama pia iliwaachia huru washtakiwa tisa.

    Washtakiwa walisimama wakituhumiwa kuwezesha uhamishaji wa pesa zilizopatikana kutokana na uuzaji haramu wa dhahabu na vito vya thamani kwenda kwa vikundi vya wapiganaji.

    Msemaji wa timu ya wanasheria wa washtakiwa alikanusha mashtaka na kuliambia shirika la habari la AFP kwamba watakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

  11. Katika picha: Mtazamo wa shughuli za kijeshi za Marekani dhidi wa Wahouthi

    Tumepokea hivi punde picha hizi zilizotolewa na Kamandi Kuu ya Marekani na wizara ya ulinzi ya Uingereza, zikionyesha sehemu ya operesheni dhidi ya Wahouthi

  12. Iran, Hezbollah walaani mashambulizi ya anga ya Marekani na Uingereza

    Wizara ya mambo ya nje ya Iran imelaani mashambulizi dhidi ya Yemen na kusema ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka na uadilifu wa ardhi ya Yemen na ukiukaji wa sheria za kimataifa.

    Mashambulizi hayo "hayatakuwa na matokeo yoyote zaidi ya kuchochea ukosefu wa usalama na ukosefu wa utulivu katika eneo hilo," msemaji wa wizara hiyo Nasser Kanani alisema katika chapisho kwenye kikundi cha Telegram cha wizara hiyo.

    Wakati huo huo kundi la Hezbollah la Lebanon linaloungwa mkono na Iran pia limelaani mashambulizi dhidi ya Yemen.

    "Uchokozi wa Marekani unathibitisha kwa mara nyingine tena kwamba Marekani ni mshirika kamili katika majanga na mauaji yaliyofanywa na adui Mzayuni huko Gaza na eneo hilo", lilisema kundi hilo linaloungwa mkono na Iran, kwa mujibu wa ripoti ya Reuters.

    Urusi yaomba mkutano wa dharura wa Umoja wa Mataifa

    Urusi imeomba mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa kuhusiana na mashambulizi ya Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen, Ujumbe wa Kudumu wa Urusi katika Umoja wa Mataifa umesema.

    Ujumbe huo uliambia shirika la habari la Tass la Urusi kwamba mkutano huo ulipangwa kufanyika saa 10:00 mjini New York (saa 15:00 GMT).

    Siku ya Jumatano azimio la Baraza la Usalama liliwataka Wahouthi wa Yemen wakomeshe mara moja mashambulizi yao dhidi ya meli katika Bahari Nyekundu.

    Urusi na Uchina - wanachama wa kudumu wa Baraza - hawakupiga kura ya azimio hilo, pamoja na Algeria na Msumbiji, huku mataifa 11 yakilipigia kura.

  13. Zambia yaweka kikomo muda wa ibada hadi saa mbili ili kukabiliana na kipindupindu

    Makanisa nchini Zambia yameagizwa kupunguza muda wa ibada hadi saa mbili kama sehemu ya hatua za kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu.

    Hakuna uuzaji wa vyakula vinavyoharibika na vilivyo tayari kuliwa katika makanisa yote, Ndiwa Mutelo, afisa mkuu anayehusika na masuala ya kidini, alisema.

    Waumini pia wametakiwa kuepuka kusalimiana kwa mikono na kukumbatiana ili kupunguza hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo.

    Bw Mutelo katika taarifa pia aliagiza vituo vya ibada kuwapa washiriki wao maji salama ya kunywa, sehemu za kunawia mikono pamoja na dawa za kujisafisha mikono.

    Zaidi ya visa 7,800 vya kipindupindu vimeripotiwa nchini kote tangu Oktoba mwaka jana.

    Katika saa 24 zilizopita, kulikuwa na visa vipya zaidi ya 400 na vifo 18, wizara ya afya ilisema.

  14. Waziri Msaidizi wa zamani wa Kenya azuiliwa nchini Uganda kwa tuhuma za ulaghai wa dhahabu

    Mamlaka ya Uganda inamshikilia aliyekuwa Waziri Msaidizi wa Usalama wa Ndani wa Kenya Stephen Tarus kwa tuhuma za kuingiza dhahabu nchini humo kwa kutumia nyaraka ghushi.

    Bw Tarus alikamatwa wiki jana na kufikishwa mbele ya mahakama ya Uganda ya kukabiliana na ufisadi siku ya Jumatano kwa kughushi nyaraka za mauzo ya nje, Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA) ilisema.

    Nyaraka za biashara haramu zilisababisha hasara kubwa ya kifedha kwa serikali ya Uganda, URA iliongeza.

    Alishtakiwa kwa kughushi nyaraka za mauzo ya nje kwa kilo 13 za dhahabu yenye thamani ya $30,000 (£24,000).

    Dhahabu hiyo ilitumwa Dubai katika eneo linaloshukiwa kuwa la magendo, kulingana na URA.

    Bw Tarus anazuiliwa katika gereza la Luzira hadi Januari 18, akisubiri uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo.

    Tarus mwenye umri wa miaka 57 aliwahi kuwa waziri msaidizi chini ya hayati Rais Mwai Kibaki na kama balozi wa Kenya nchini Australia kati ya 2009 na 2012.

    Pia aliwahi kuwa mbunge kati ya 2003 na 2007.

  15. Mzozo wa Somalia: Helikopta ya UN ilipigwa na 'kitu' - chanzo

    Helikopta ya Umoja wa Mataifa ilitua ghafla katika eneo linalodhibitiwa wanamgambo wenye silaha nchini Somalia baada ya kugongwa na kitu, chanzo cha Umoja wa Mataifa kimesema.

    Wapiganaji wa Al-Shabab walikamata helikopta hiyo, huku ripoti ambazo hazijathibitishwa zikidokeza kwamba abiria mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi, chanzo kiliiambia BBC.

    Watu wengine sita waliokuwa ndani ya ndege hiyo wanazuiliwa na wanamgambo hao, huku wawili wakiripotiwa kutoroka, chanzo kiliongeza.

    Helikopta hiyo ilikuwa katika shughuli ya matibabu ilipotua karibu na kijiji.

    Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia ulithibitisha "tukio la anga" siku ya Jumatano lililohusisha helikopta ya Umoja wa Mataifa iliyokuwa imepewa kandarasi za huduma zake ktika sehemu hiyo.

    Haikutaja al-Shabab, lakini ilisema "juhudi za kukabiliana na tukio hilo zinaendelea".

    Chanzo hicho cha Umoja wa Mataifa kiliiambia BBC kuwa mmoja wa watu waliokuwemo ndani ya ndege hiyo ni Msomali, huku wengine wanane wakitoka kwingineko barani Afrika na Ulaya.

    Raia hao wa kigeni ni pamoja na mtu aliyeripotiwa kuuawa na wawili waliofanikiwa kutoroka.Hatima yao haijulikani.

    Wote tisa, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wanne, walikuwa wakandarasi na si wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.Baadhi yao walikuwa madaktari, chanzo cha UN kilisema.

    Helikopta hiyo ilikuwa ikielekea katika mji wa Wisil karibu na mstari wa mbele wa mashambulizi ya serikali dhidi ya al-Shabab ilipoanguka baada ya kupigwa na kitu kisichojulikana, chanzo kiliongeza.

    Afisa wa jeshi la Somalia Meja Hassan Ali aliliambia shirika la habari la Reuters Jumatano kwamba ndege hiyo "ilikuwa ikibeba vifaa vya matibabu na ilipaswa kuwasafirisha wanajeshi waliojeruhiwa kutoka eneo la Galgudud".

    Al-Shabab inadhibiti maeneo makubwa ya kusini na katikati mwa Somalia.

    Kundi hilo lina mfungamano na al-Qaeda na limeendesha uasi wa kikatili kwa karibu miaka 20.

    Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilichapisha kwenye mitandao ya kijamii Jumatano usiku kwamba ndege hiyo "siyo ya WFP au ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Huduma ya Kibinadamu ya Anga na hakuna wafanyakazi wa WFP waliokuwa ndani".

    WFP iliongeza kuwa kama tahadhari, safari zake za ndege katika eneo hilo zimesitishwa kwa muda.

    Serikali ya Somalia katika miezi ya hivi karibuni imezidisha mapambano yake dhidi ya kundi lenye uhusiano na al-Qaeda.

  16. Mji mkubwa wa zamani wapatikana katika Amazon

    Jiji kubwa la kale limepatikana katika Amazon, lililofichwa kwa maelfu ya miaka na mimea yenye majani.

    Ugunduzi huo unabadilisha kile tunachojua kuhusu historia ya watu wanaoishi Amazon.

    Nyumba na plaza katika eneo la Upano mashariki mwa Ekuado ziliunganishwa na mtandao wa ajabu wa barabara na mifereji.

    Eneo hilo liko katika kivuli cha volkano ambayo iliunda udongo wenye rutuba wa eneo hilo lakini pia inaweza kuwa imesababisha uharibifu wa jamii.

    Ingawa tulijua kuhusu majiji katika nyanda za juu za Amerika Kusini, kama Machu Picchu huko Peru, iliaminika kuwa watu waliishi tu kwa kuhamahama au katika makazi madogo katika Amazon.

    "Hii ni ya zamani kuliko sehemu nyingine yoyote tunayojua katika Amazon.Hii inaonyesha kwamba tunapaswa kubadilisha mawazo yetu kuhusu utamaduni na ustaarabuwa Amazon," anasema Prof Stephen Rostain, mkurugenzi wa uchunguzi katika Kituo cha Utafiti wa Kisayansi nchini Ufaransa, ambaye aliongoza utafiti.

    "Inabadilisha jinsi tunavyoona tamaduni za Amazoni. Watu wengi hupiga picha ya vikundi vidogo vidogo, pengine wakiwa uchi, wanaoishi katika vibanda na kusafisha ardhi - hii inaonyesha watu wa kale waliishi katika jamii ngumu za mijini," anasema mwandishi mwenza Antoine Dorison.

    Jiji lilijengwa karibu miaka 2,500 iliyopita, na watu waliishi huko kwa hadi miaka 1,000, kulingana na wanaakiolojia.

    Ni vigumu kukadiria kwa usahihi ni watu wangapi waliishi huko kwa wakati mmoja, lakini wanasayansi wanasema hakika ni katika miaka ya 10,000 ikiwa sio 100,000.

    Waakiolojia walichanganya uchimbaji wa ardhini na uchunguzi wa eneo la kilomita za mraba 300 (maili za mraba 116) kwa kutumia vihisi leza vilivyorushwa kwenye ndege ambayo ingeweza kutambua mabaki ya jiji chini ya mimea na miti minene.

  17. Kwa Muhtasari:Marekani na Uingereza zashambuliwa Wahouthi

    Ikiwa unajiunga nasi tu ...

    Huu hapa ni muhtasari wa haraka wa mashambulizi ya anga ya Marekani na Uingereza yaliyoanzishwa dhidi ya waasi wa Houthi nchini Yemen mapema Ijumaa.

    Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak walithibitisha mashambulizi hayo, wakisema ni jibu la mashambulizi ya mara kwa mara ya Wahouthi dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari Nyekundu.

    • Makombora ya kivita ya Marekani ya Tomahawk na ndege za Marekani yalishambulia zaidi ya maeneo 12, ikiwa ni pamoja na katika mji mkuu, Sanaa, na Hudaydah, ngome ya bandari ya Houthi Red Sea, maafisa wa Marekani wanasema.
    • Ndege nne RAF Typhoon zilishambulia maeneo mawili ya Wahouthi, zikiruka kutoka kambi ya Akrotiri huko Cyprus.
    • Rais Biden alionya juu ya hatua zaidi zinazowezekana kuhakikisha mtiririko huru wa biashara
    • Msaada ulitolewa na Australia, Bahrain, Kanada na Uholanzi, viongozi hao walisema
    • Afisa wa Houthi alionya Marekani na Uingereza "zitalipa gharama kubwa" kwa "uchokozi huo wa wazi"

    Unaweza pia kusoma

  18. Saudi Arabia yaitaka Marekani 'kujizuia' baada ya mashambulizi dhidi ya Wahouthi

    Saudi Arabia imeitaka Marekani na washirika wake kujizuia na "kuepusha kuzidisha mzozo' katika mashariki ya kati baada ya mashambulizi yanayoongozwa na Marekani dhidi ya was wa Houthi nchini Yemen .

    Vyombo vya habari vinavyonukuu taarifa ya wizara yake ya mambo ya nje vilisema Riyadh inafuatilia kwa karibu hali hiyo kwa "wasiwasi mkubwa".

    Wahouthi bado hawajalipiza kisasi - afisa wa Marekani

    Katika mazungumzo na waandishi wa habari kwa njia ya simu, afisa mkuu wa Marekani alisema bado hakuna jibu lolote la kijeshi kutoka kwa makamanda wa Houthis.

    "Hadi sasa hivi, hatujaona hatua zozote za kulipiza kisasi moja kwa moja kwa Marekani au wanachama wengine wa muungano," afisa huyo alisema, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina.

    "Tunasalia kubwa tayari, bila shaka kujilinda, lakini hatujaona jibu kutoka kwa Houthis kwa wakati huu," afisa huyo aliendelea kusema

    Unaweza pia kusoma

  19. Marekani na Uingereza zaanzisha mashambulizi dhidi ya waasi wa Houthi nchini Yemen

    Vikosi vya Marekani na Uingereza vimeanza mashambulizi ya anga dhidi ya waasi wa Houthi nchini Yemen, maafisa wa Marekani wanasema.

    Rais Joe Biden amethibitisha kwamba mashambulizi yameanzishwa "kwa maelekezo yangu" dhidi ya "malengo kadhaa nchini Yemen yanayotumiwa na waasi wa Houthi kuhatarisha uhuru wasafari za baharini katika mojawapo ya njia muhimu zaidi za maji duniani".

    Alisema mashambulizi hayo yalifanywa na vikosi vya Marekani, "pamoja na Uingereza na kwa msaada kutoka Australia, Bahrain, Canada na Uholanzi".

    Maafisa wa Marekani walionukuliwa na Shirika la Habari la Associated Press walizungumzia mashabulizi makubwaya kulipiza kisasi kwa kutumia makombora ya kivita ya Tomahawk na ndege za kivita zilizopaa kutoka kwameli ya kivita.

    Malengo ya Houthi ni pamoja na vituo vya vifaa, mifumo ya ulinzi wa anga na ghala za silaha, walisema.

    Waandishi wa habari wa AP mjini Sanaa walisikia milipuko minne, lakini hawakuona dalili zozote za ndege za kivita. Wakaazi wawili wa Hudaydah walisema walisikia milipuko mitano mikali.

    Hilo ni shambulio la kwanza la kijeshi la Marekani dhidi ya Wahouthi nchini Yemen tangu kundi hilo linaloungwa mkono na Iran lianze kurusha ndege zisizo na rubani na makombora dhidi ya meli za mizigo katika Bahari Nyekundu mwezi Novemba.

    Afisa wa Houthi athibitisha 'uvamizi' wa nchi nzima

    Afisa wa Houthi amethibitisha kwenye X, ambayo zamani ilikuwa Twitter, kwamba mashambulizi yamefanywa kote Yemen.

    "Uchokozi wa Marekani-Wazayuni-Waingereza dhidi ya Yemen unaanzisha mashambulizi kadhaa kwenye mji mkuu, Sanaa, mkoa wa Hudaydah, Saada na Dhamar," afisa wa Houthi Abdul Qader al-Mortada aliandika.

    Unaweza pia kusoma

  20. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja leo Ijuma tarehe 12 Januari 2024