Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kenya: Mwizi wa watoto wachanga afungwa miaka 25 jela baada ya ufichuzi wa BBC
Mfanyakazi wa hospitali ya Kenya ambaye alifichuliwa na BBC akiuza mtoto kwenye masoko ya siri amehukumiwa kifungo cha miaka 25 jela.
Moja kwa moja
Rais Ruto afanya mabadiliko ya wizara katika Baraza lake la mawaziri
Rais William Ruto Jumatano usiku amefanya mabadiliko mapya ya Baraza lake la Mawaziri, huku wizara mbalimbali zikiunganishwa na kubadilishwa jina.
Katika hatua hiyo, Rais Ruto amepanua Ofisi ya Waziri Mkuu na kujumuisha Wizara ya Mambo ya Nje na Masuala ya Diaspora, inayoongozwa na Musalia Mudavadi.
Moses Kuria amehamishwa kutoka wizara ya Biashara hadi Wizara ya Utumishi wa Umma, Utendaji na Usimamizi wa Huduma za Umma.
Alfred Mutua, kwa upande mwingine, anaondoka katika wizara ya Mashauri ya Kigeni kuongoza wizara ya Utalii na Wanyamapori.
Mwenzake wa Masuala ya Kigeni na Diaspora Alfred Mutua, kwa upande wake, anaelekea katika Wizara ya Utalii na Wanyamapori.
Rais ameanzisha wizara mpya ya Wizara ya Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi, itakayoongozwa na Aisha Jumwa.
Ruto zaidi alibuni upya na kuipa jina la Wizara ya Masuala ya Vijana, Sanaa na Michezo, kuwa Wizara ya Masuala ya Vijana na Michezo, na atasalia chini ya Ababu Namwamba ambaye hakuathiriwa na mabadiliko hayo.
Rebecca Miano sasa anachukua nafasi ya Kuria katika Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda, huku Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ASAL na Maendeleo ya Kikanda ikiendelea kuongozwa na Peninah Malonza.
Alice Wahome anakwenda Wizara ya Ardhi, Kazi za Umma, Nyumba na Maendeleo ya Miji, akibadilishana na Zachariah Njeru ambaye sasa anachukua Wizara ya Maji, Usafi wa Mazingira na Umwagiliaji.
Rais Ruto pia amewateua upya Makatibu Wakuu, huku Harsama Kello akichukua Wizara husika na Maendeleo ya Kikanda.
Julius Korir amepelekwa katika Idara ya Jimbo la Maji na Usafi wa Mazingira, na Geoffrey Kaituko Idara ya Jimbo la Masuala ya Meli na Meli.
Mabadiliko mengine yaliyojitokeza ni katika Makatibu Wakuu ni pamoja na: Shadrack Mwadime (Maendeleo ya Kazi na Ujuzi), Paul Ronoh (Maendeleo ya Mazao), Idris Salim Dokota (Masuala ya Baraza la Mawaziri), Anne Wang'ombe (Jinsia ), na Veronic Nduva (Utendaji na Usimamizi wa Huduma za Umma)
Habari za hivi punde, Kombe la Dunia la 2030: Mashindano yatafanyika katika nchi sita katika mabara matatu
Kombe la Dunia la 2030 litafanyika katika nchi sita katika mabara matatu, FIFA imethibitisha.
Uhispania, Ureno na Morocco zimetajwa kuwa wenyeji, huku mechi tatu za ufunguzi zikifanyika Uruguay, Argentina na Paraguay.
Mechi za ufunguzi huko Amerika Kusini ni za kuadhimisha miaka 100 kwa Kombe la Dunia kwani itakuwa ni miaka 100 tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo huko Montevideo.
Uamuzi huo umepangwa kupitishwa kwenye kongamano la Fifa mwaka ujao.
"Katika ulimwengu uliogawanyika, Fifa na soka vinaungana," alisema rais wa Fifa Gianni Infantino.
“Baraza la Fifa, linalowakilisha ulimwengu mzima wa kandanda, lilikubali kwa kauli moja kusherehekea miaka 100 ya Kombe la Dunia la Fifa, ambalo toleo lake la kwanza lilichezwa Uruguay mnamo 1930, kwa njia inayofaa zaidi.
"Mnamo 2030, tutakuwa na historia ya kipekee duniani, mabara matatu - Afrika, Ulaya na Amerika Kusini - nchi sita - Argentina, Morocco, Paraguay, Ureno, Hispania na Uruguay - kukaribisha na kuunganisha dunia wakati wa kusherehekea pamoja mchezo mzuri, miaka mia moja na Kombe la Dunia la Fifa."
Fifa pia ilithibitisha pia kuwa zabuni kutoka kwa nchi za Shirikisho la Soka la Asia pekee na Shirikisho la Soka la Oceania ndio zitazingatiwa kwa fainali za 2034.
Saudia Arabia inatarajiwa kuwasilisha ombi la kuandaa michuano hiyo mwaka 2034 kwa mara ya kwanza.
Tazama: Wabeba mizigo walivyoponea chupu chupu ajali ya moto katika hosteli ya Sydney
Wabeba mizigo wawili waliponea chupuchupu wakati betri ya Lithium-ion ilipolipuka katika hosteli ya Sydney.
Moto huo unaaminiwa kusababishwa na betri ya e-bike ambayo ilikuwa inachaji, idara ya zimamoto ya New South Wales ilisema.
Ilituma magari sita ya zima moto na wazima moto 22 kwenye eneo la tukio.
Mmoja wa wapakiaji alihitaji matibabu kwa majeraha madogo kwenye mguu wake.
Mwizi wa watoto wachanga Kenya afungwa miaka 25 jela baada ya ufichuzi wa BBC
Mfanyakazi wa hospitali ya Kenya ambaye alifichuliwa na BBC akiuza mtoto kwenye masoko ya siri amehukumiwa kifungo cha miaka 25 jela.
Fred Leparan, ambaye alifanya kazi katika hospitali ya Mama Lucy Kibaki ya Nairobi, alirekodiwa akipokea $2,500 (£2,000) ili kumuuza mtoto wa kiume chini ya uangalizi wa hospitali hiyo.
Alikamatwa mwaka wa 2020 kufuatia uchunguzi wa BBC AFRICA EYE na kupatikana na hatia mwezi uliopita kwa ulanguzi wa watoto, kutelekeza watoto na kula njama ya kutenda uhalifu.
Mwandishi wa Africa Eye hapo awali alimjia Leparan akijifanya mnunuzi, baada ya kusikia kutoka kwa chanzo kwamba mfanyakazi mkuu wa kliniki ya kijamii alihusika katika ulanguzi haramu wa watoto kutoka hospitali inayosimamiwa na serikali.
Leparan alimuuliza mwandishi wa siri, ambaye alisema yeye na mumewe walikuwa na shida ya kupata mimba, maswali ya harakaharaka tu kuhusu hali yao kabla ya kukubali kumuuza mtoto wa kiume.
Siku ambayo mtoto huyo wa kiume na watoto wengine wawili walitakiwa kuhamishwa kutoka hospitali hadi kwenye makazi ya watoto ya serikali, Leparan alirekodiwa akidanganya hati za uhamisho ili makao hayo yatarajie watoto wawili, badala ya watatu.
Timu ya BBC ilihakikisha kwamba watoto wote watatu wamefikishwa moja kwa moja kwenye nyumba ya watoto, lakini walimrekodi Leparan akirekebisha makaratasi na kuwafahamisha kuwa mtoto huyo ni wao wa kumchukua.
Mahakama ya Kenya siku ya Jumatano ilisema Leparan atatumikia kifungo cha miaka 25 gerezani, kisha atatumia miaka 10 ya kipindi cha kuchunguzwa mienendo yake.
Soma zaidi:
- BBC Africa Eye: Kenya yaukamata mtandao wa wezi wa watoto
Uganda: Polisi wanaonya wafuasi wa Bobi wine kabla ya hafla ya kumkaribisha
Polisi katika mji mkuu wa Kampala Uganda wamewaonya wafuasi wa mwanasiasa wa upinzani nchini humo na mwanamuziki Bobi Wine, kufuata sheria wanapomkaribisha mwanasiasa huyo
Hii ni baada ya viongozi wa chama cha Bobi Wine, NUP wakiongozwa na sehemu ya wabunge wa chama hususan wale wanaowakilisha maeneo ya bunge la Kampala mjinikuwahamasisha watu kujitokeza kwa wingi kote nchini na kukusanyika katika wanja wa ndege wawa kimataifa wa Entebbe na barabara za Entebbena barabara nyingine zinazoelekea kwenyemakazi ya Bobi Wineya Wakiso kumpokea.
Bw David Sserukenya, mbunge wa Makindye Ssabagabo, alibainisha kuwa wafuasi wa Bw Kyagulanyi wameamua kuandaa sherehe kubwa ya kumkaribisha kama njia ya kumpongeza kwa ziara zake za uhamasishaji ambazo amezifanya nchini Uganda na nje ya nchi kwa muda wa mwezi mmoja uliopita.
‘’Ninaomba wafuasi wa Bw Kyagulanyi waheshimu sheria za barabarani na miongozo ya usalama , wakati wa hafla hii. Hili litakua jaribio kwa vyombo vyetu vya usalama, lakini tunatarajia wataheshimu sheria na kuimarisha utulivu huku Waganda wakitekeleza haki zao siku huu,’’alisema .
Lakini Naibu Msemaji wa polis iwa jiji la Kampala , Bw Luke Owoyesigyire alinukuliwa na gazeti la Daily Monitor nchini humo akisema’’ Sijui hili [karamu ya kumkaribisha Bobi Wine], lakini maandamano yoyote yasiyo halali yatashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.’’
Polisi wanatarajia pia kutoa taarifa rasmi kuhusu suala hilo Jumatano, kulingana na Bw Owoyesigyire.
Kupitia ukurasa wake rasmi wa X (zamani ikiitwa Twitter ), Bw Kyagulanyi alithibitisha Jumanne kuwa atawasili ‘’Oktoba 5, 10.00AM’’
Habari za hivi punde, Jurgen Klopp anataka mechi ya marudio kati ya Tottenham na Liverpool baada ya makosa ya VAR
Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp anataka mchezo wa Ligi Kuu ya Uingereza dhidi ya Tottenham urudiwe baada ya bao la Luis Diaz kukataliwa kimakosa na mwamuzi msaidizi wa video.
VAR Darren England na msaidizi wake Dan Cook hawakughairi wakati Diaz alipodaiwa kuotea wakati mechi ilipokuwa 0-0 siku ya Jumamosi.
Liverpool ilipoteza kwa mabao 2-1 kwa bao la kujifunga dakika ya 96 kutoka kwa Joel Matip.
"Kitu kama hiki hakijawahi kutokea, ndiyo maana nadhani mchezo wa marudiano ni jambo sahihi," alisema Klopp.
Bodi ya waamuzi PGMOL ilitoa sauti ya majadiliano kati ya wasimamizi wa mechi kuhusu kuotea siku ya Jumanne.
Katika sauti hiyo, England anasikika akisema kwamba uchunguyzi wake ulikuwa "kamili" kabla ya kukiri baada ya kugundua kwamba kosa limefanywa.
Klopp alisema: "Sauti haikuibadilisha hata kidogo. Ni kosa dhahiri. Lazima kuwe na suluhu kwa hilo. Matokeo yanapaswa kuwa marudio. Lakini labda haitatokea.
"Hoja dhidi ya hilo itakuwa inafungua milango. Haijawahi kutokea. Nimezoea kufanya maamuzi mabaya na magumu, lakini jambo kama hili halijawahi kutokea."
Baada ya kutoa sauti, PGMOL ilisema kosa hilo lilitokana na "kukosa umakini na kupoteza umakini".
Mzozo huo umeibua mjadala kuhusu matumizi na ufanisi wa VAR.
Ingawa Klopp alisema kosa hilo halikufanywa "kwa makusudi", aliongeza: "Mambo haya hayapaswi kutokea. Makosa mengine yasitokee. Tafuta suluhu ya kukabiliana nayo.
Maandamano dhidi ya nia ya urais nchini Misri 'yalisababisha kukamatwa kwa watu 400'
Takriban watu 400 nchini Misri wamekamatwa kutokana na matukio ya ghasia baada ya Rais Abdul Fattah al-Sisi kutangaza kuwa atawania muhula wa tatu, kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo.
Matamshi ya Rais Sisi siku ya Jumanne yalizua ghadhabu ya nadra miongoni mwa umma - video za mitandao ya kijamii zilionyesha maandamano katika mji wa kaskazini-magharibi wa Marsa Matrouh.
Katika picha hizo, watu wanasikika wakiimba "Sisi nje" na kutaka utawala wake wa muongo mmoja uondolewe. Video zingine zilionyesha mapigano kati ya waandamanaji na polisi.
Al -Manassa tovuti kibinafsi ya habari ilimnukuu Saleh Abou-Attiya, katibu mkuu wa Chama cha Wanasheria wa Marsa Matrouh, akisema kuwa watu 400, wengi wao wakiwa "vijana", wamezuiliwa.
Mkuu huyo wa zamani wa jeshi amekuwa madarakani tangu aliposaidia kumuondoa madarakani Mohammed Morsi, kiongozi wa Muslim Brotherhood mwaka 2013 huku kukiwa na maandamano makubwa ya kupinga utawala wake.
Wanaharakati wanasema kuwa muhula wa Bw Sisi madarakani umegubikwa na ukandamizaji wa kikatili wa upinzani na kuporomoka kwa uchumi wa Misri.
Uchaguzi wa rais nchini Misri umepangwa kufanyika mwezi Disemba.
Kieran Trippier: Natumai nitamnyamazisha Kylian Mbappe
Winga wa upande wa kulia wa klabu ya Newcastle Kieran Trippier ana matumaini ya kumnyamazisha mshambuliaji wa PSG Kylian Mbappe wakati timu zao zitakapkutana siku ya Jumatano hata iwapo hatua hiyo itamkasirisha mwanawe mdogo.
PSG inazuru uwanja wa James Park katika mechi ya kimakundi ya ligi ya mabingwa Ulaya, lakini mwanawe Trippier anampenda sana Kylian Mbappe.
‘’Anampenda sana kila mara anatazama vídeo zake katika mtandao wa You Tube’’ , alisema Trippier mwenye umri wa miaka 33.
Beki huyo alitoa mzaha kwamba mwanawe angependelea kutembea na Mbappe badala yake. ‘’ Sikufurahishwa na hilo’’ , Tripper aliongeza. ‘’Nilimwambia , iwapo utatembea na Mbape usiniangalie’’.
Newcastle inacheza mechi hiyo katika kundi F ikiwa bado haijafungwa katika mechi tano , ikishinda nne ikiwemo ushindi wa magoli 8-0 dhidi ya Sheffield United.
Kenya: Shule ya upili ya wasichana yafungwa baada ya 'ugonjwa wa ajabu'
Wizara ya Elimu imefunga shule ya upili ya wasichana ya St Theresa's Eregi baada ya wanafunzi kadhaa kulazwa hospitalini kutokana na ‘’ugonjwa wa ajabu’’.
Hatua hii inachukuliwa huku Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu akitarajiwa kutembelea taasisi hiyo baadaye leo.
Maafisa wa elimu katika Kaunti ya Kakamega waliamua kufunga kwa muda shule hiyo Jumatano baada ya wanafunzi kuibua ghasia.
Walikuwa wanataka kuruhusiwa kurudi nyumbani baada ya wanafunzi 90 kulazwa katika hospitali mbalimbali kufuatia mlipuko wa 'ugonjwa wa ajabu.'
Taarifa ya Serikali ya Kaunti ilisema kuwa Bodi ya Usimamizi, Maafisa wa Wizara ya Elimu na Tume ya Utumishi wa Walimu walifanya mashauriano kabla ya uamuzi kutolewa.
Hatahivyo wanafunzi wa kidato cha 4 wanaotarajiwa kuanza mitihani yao watasalia shuleni.
Mnamo Jumatano, maafisa wakuu wa kaunti wakiongozwa na Mwanachama wa Kamati Tendaji ya Kaunti ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bonface Okoth na mwenzake wa Huduma za Afya Benard Wesonga walitembelea shule hiyo.
Bw Okoth amesema sampuli za damu kutoka kwa wanafunzi walioathiriwa zimetumwa katika Taasisi ya Utafiti wa Matibabu ya Kenya (Kemri) jijini Nairobi na Kisumu kwa uchunguzi zaidi.
Vita vya Ukraine: Wizara ya Ulinzi ya Urusi yatangaza kuzuia makumi ya ndege zisizo na rubani kwenye maeneo ya mpaka
Wizara ya Ulinzi ya Urusi inadai kuwa usiku wa kuamkia leo, ndege 31 zisizo na rubani za Ukraine zilidunguliwa katika mikoa mitatu inayopakana na Ukraine - Belgorod, Bryansk na Kursk. Hii ni idadi kubwa isivyo kawaida ikilinganishwa na iliyopita.
"Mifumo ya ulinzi wa anga katika eneo la Belgorod, Bryansk na Kursk ilinasa na kuharibu ndege 31 za angani zisizokuwa na rubani," jeshi la Urusi lilisema katika taarifa.
Usiku na asubuhi, magavana wa mikoa ya Belgorod na Bryansk waliripoti mara mbili mashambulizi ya ulinzi wa anga dhidi ya droni.
Gavana wa Bryansk Alexander Bogomaz aliandika katika chaneli yake ya telegramu kwamba "ndege isiyokuwa na rubani iliharibiwa katika eneo la Bryansk."
Asubuhi, gavana wa mkoa wa Belgorod, Vyacheslav Gladkov, alisema kuwa katika mkoa wake mfumo wa ulinzi wa anga ulidungua ndege 19 zisizo na rubani. "Leo, kati ya saa saba na saa nane mfumo wetu wa ulinzi wa anga ulifanya kazi juu ya Belgorod, wilaya ya Belgorod na wilaya ya Korochansky.
Kulingana na taarifa za awali, kulikuwa na shambulio la ndege isiyo na rubani. Pia kulingana na data ya awali, karibu vitu 19 vilipigwa risasi, "Gladkov alisema kwenye video iliyowekwa kwenye mtandao wa VKontakte.
Taarifa nyingine kutoka kwa Wizara ya Ulinzi ya Urusi zinasema kuwa "jaribio la kupenya katika eneo la Crimea lililofanywa na kundi la anga la Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine lilizuiwa."
Urusi yaishambulia Ukraine: Mengi zaidi:
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
Mwanasiasa wa Uganda 'awapokonya' wananchi gari la wagonjwa baada kushindwa Uchaguzi
Mwanasiasa mmoja wa kike wa Uganda ameibua hisia tofauti mtandaoni baada ya kukiri kwa ujasiri kuwa ameamua kujirejeshea gari la wagonjwa alilotoa kama msaada kwa wapiga kura wake kwa matumaini kwamba wangempigia kura.
Anite Evelyn, Waziri wa sasa wa Fedha wa Uwekezaji na Ubinafsishaji nchini Uganda, aliwashangaza wengi baada ya kukiri kuwa kweli amejirudishia gari la kubebea wagonjwa alilolitoa kabla ya uchaguzi, akisisitiza kuwa wananchi aliokuwa amewapatia msaada huo ni watu wasio na shukrani.
Ufichuzi wote ulianza baada ya akaunti ya X (zamani kiitwa Twitter) kwa jina @AfricaFactsZone kuchapisha habari za maoni yake baada ya uchaguzi.
"Mwanasiasa wa Uganda, Evelyn Anite alichukua tena gari la wagonjwa alilotoa kwa wilaya yake, baada ya kushindwa katika uchaguzi wa 2021," waliandika kwenye Twitter.
Anite Evelyn hakuwa na aibu yoyote wa kujutia kitendo hicho, ambacho baadhi wanakiona kama cha aibu.
Akijibu kuhusu uamuzi wake huo Bi Anite alisema: "@AfricaFactsZone, asante kwa kuleta hili. Kwanza, ni kweli nilirudisha gari langu la wagonjwa na sina pole kwa hilo. Kwa nini nilifanya hivyo? Ni kwa sababu hawakunipigia kura. Kwa hivyo ulitarajia niende zangu bila kitu? Wagalatia 6:7 Mtu huvuna alichopanda! aliandika kwenye ujumbe wake wa X.
TikTok yasimamisha huduma ya ununuzi wa mtandaoni Indonesia
Programu ya mitandao ya kijamii TikTok inasitisha huduma yake ya ununuzi mtandaoni nchini Indonesia ili kutii sheria mpya katika nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi Kusini Mashariki mwa Asia.
Hatua hiyo itaanza kutekelezwa saa 17:00 saa za Jakarta (10:00 GMT).
Serikali ya nchi hiyo inasema kanuni hizo zinalenga kusaidia kuwalinda wauzaji bidhaa wa ndani na wa mtandaoni.
Indonesia ilikuwa nchi ya kwanza kufanya majaribio ya huduma ya e-commerce mnamo 2021 na TikTok ikawa moja ya soko kubwa la ununuzi.
Wiki iliyopita, Indonesia ilitangaza kanuni ambazo zingelazimisha TikTok kugawa kipengele chake cha ununuzi kutoka kwa huduma maarufu ya kushirikisha video nchini humo.
Akitangaza hatua hizo, waziri wa biashara wa Indonesia Zulkifli Hasan alisema: "Sasa, biashara ya mtandaoni haiwezi kuwa mitandao ya kijamii. Imetenganishwa."
Pia aliambia majukwaa ya mitandao ya kijamii kuwa walikuwa na wiki moja ya kufuata sheria hizo mpya la sivyo watapoteza leseni yao ya kufanya kazi nchini.
Tangazo hilo linawadia baada ya Rais wa Indonesia Joko Widodo kusema mwezi uliopita: "Tunahitaji kuwa makini na biashara ya mtandaoni. Inaweza kuwa nzuri sana ikiwa kuna kanuni lakini inaweza kuwa mbaya ikiwa hakuna kanuni zozote."
"Kipaumbele chetu ni kubaki kuzingatia sheria na kanuni za eneo," TikTok ilisema katika taarifa Jumanne .
"Kwa hivyo, hatutawezesha tena shughuli za biashara ya mtandaoni katika Duka la TikTok Indonesia," iliongeza.
Soma zaidi:
- Kwa nini TikTok inaweza kukushawishi kununua vitu
Netflix yamaliza mpango wake wa usajili bila malipo nchini Kenya
Kampuni ya kutoa huduma za upeperushaji wa filamu Netflix imetangaza kuwa itasitisha huduma yake ya bure nchini Kenya mwezi ujao huku ikitafuta njia za kuongeza mapato yake huku kukiwa na ushindani wa soko.
Mnamo 2021, Netflix iliruhusu watumiaji katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki kufikia baadhi ya filamu zake bila kulipia usajili.Hili lilikuwa jaribio la kuingia katika soko la Kenya linalokua.
Katika taarifa, Netflix inasema mpango huo wa bure hautapatikana tena kuanzia tarehe 1 Novemba.
"Hakuna hatua itakayohitajika, uanachama wako utaghairiwa moja kwa moja mpango wa bila malipo utakapokamilika," kampuni hiyo ilisema.
Iliwahimiza waliojisajili kuboresha hadi mipango mbalimbali ya malipo inayotolewa.
Hatua hiyo inajiri miezi kadhaa baada ya Netflix kupunguza bei ya usajili kwa wateja wake wa Kenya.
Pakistani yaawaamuru wanaotafuta hifadhi kutoka Afghanistan kuondoka nchini ifikapo Novemba
Serikali ya Pakistani imewaamuru watu wote wanaotafuta hifadhi bila idhini kutoka Afghanistan - takriban watu milioni 1.7 - kuondoka nchini humo kufikia Novemba.
Kuongezeka kwa mashambulizi ya wanamgambo kwenye mpaka wa nchi hizo mbili mwaka huu kumeongeza hali ya wasiwasi.
Pakistan imelaumu mashambulizi ya mpakani inayodai yanatekelezwa na makundi yaliyo na makao ndani ya Afghanistan - mashtaka yaliyokanushwa na utawala wa Taliban.
Lakini imechochea chuki katika mji wa Islamabad, ambao siku ya Jumanne ulitangaza msako dhidi ya wahamiaji "haramu".
Wiki iliyopita,mlipuko katika msikiti mmoja katika mji wa Mastung, karibu na mpaka na Afghanistan, uliua takriban watu 50 wakati wa sherehe za kidini.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan Sarfraz Bugti hakuonekana kurejelea moja kwa moja hilo na shambulio lingine katika jimbo la Balochistan alipotangaza amri ya kuwafurusha Waafghan "haramu" siku ya Jumanne.
Haki ya kutafuta hifadhi katika nchi ya kigeni imewekwa katika sheria za kimataifa.Pakistan imechukua mamia ya maelfu ya wakimbizi wa Afghanistan - haswa tangu Taliban iliporejea madarakani nchini Afghanistan mnamo 2021.
Takriban Waafghanistan milioni 1.3 wamesajiliwa kama wakimbizi huku wengine 880,000 wakipata hadhi ya kisheria ya kusalia Pakistan kulingana na Umoja wa Mataifa.
Lakini watu wengine milioni 1.7 wako nchini "kinyume cha sheria", alidai Waziri Bugti siku ya Jumanne .
Mwanamuziki Naira Marley azuiliwa kwa kifo cha MohBad
Polisi wa Nigeria wamemshikilia mwimbaji na mtunzi wa nyimbo Naira Marley kuhusiana na kifo cha nyota wa Afrobeats MohBad.
Msemaji wa polisi wa Lagos Benjamin Hundeyin alisema kuwa Marley anazuiliwa "kwa mahojiano na shughuli zingine za uchunguzi".
Marley alishiriki kwenye mtandao wa X kwamba alikuwa akisaidia mamlaka katika uchunguzi wa kifo cha MohBad na alikuwa "akikutana na polisi akiwa na matumaini ya ukweli kufichuliwa na haki kutendeka".
MohBad alikufa kwa njia isiyoeleweka katika hospitali ya Lagos mnamo Septemba 12 na akazikwa haraka na familia yake.
Kifo cha nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 kilizua maandamano na kutaka uchunguzi kutoka kwa mashabiki wake, jambo ambalo lilipelekea polisi kuufukua mwili wake kwa uchunguzi.
Mashabiki walielekeza hasira zao kwa Marley, ambaye alikuwa amesaini MohBad chini ya lebo yake ya muziki ya Marlian Records.
MohBad aliondoka kwenye lebo hiyo mwaka jana, baada ya kutofautiana na Marley.
Kufuatia kifo chake, video kadhaa za MohBad akilalamika kuhusu uhusiano wake na Marlian Records ziliibuka tena.
Mwanajeshi wa kike aliyefariki alipitia unyanyasaji - Ripoti ya Jeshi
Mwanajeshi wa kike wa jeshi la kifalme anaaminika kujiua baada ya kunyanyaswa kingono na mmoja wa wakubwa wake kazini, uchunguzi wa Jeshi umegundua.
Jaysley Beck, 19, alipatikana amefariki katika Kambi ya Larkhill huko Wiltshire mnamo Desemba 2021.
Ripoti ya uchunguzi iliyoonekana na BBC inaelezea "kipindi kigumu cha tabia zisizokubalika".
"Inaaminika kabisa kwamba hii ilikuwa sababu ya kifo chake," ripoti iligundua.
Tabia hiyo kutoka kwa bosi wake wa karibu, iliendelea kwa muda wa miezi miwili kabla ya kifo chake, inasema ripoti hiyo, ambayo inatarajiwa kuchapishwa saa sita mchana Jumatano.
"Ingawa tabia hii iliisha wiki moja kabla ya kifo chake, inaonekana kwamba iliendelea kumuathiri na kwa kiasi kikubwa uwezo wake wa kiakili na ustawi," ripoti hiyo inaendelea.
Maelfu ya ujumbe
Akiongea na BBC pekee, mamake Beck alisema binti yake alikuwa "amekuwa mnyonge" baada ya miezi kadhaa ya kunyanyaswa.
Tarehe ya uchunguzi kubainisha rasmi jinsi Beck alivyofariki bado haijawekwa.
Uchunguzi wa Jeshi ulimbaini bosi wake, ambaye kama kila mtu kwenye ripoti hiyo, hakutajwa, alitaka uhusiano naye lakini alikuwa na mpenzi na hakujibu hisia zake.
Inaeleza jinsi mnamo Oktoba 2021 bosi wake alimtumia zaidi ya jumbe za sauti 1,000 na WhatsApp. Mwezi uliofuata hii iliongezeka hadi zaidi ya 3,500.
Ujumbe ulihusisha kudhibiti tabia. Mara kwa mara alitafuta uhakikisho kwamba alikuwa peke yake na aliweka wazi kuwa hawezi kustahimili wazo la kuwa na mtu mwingine.
Pia unaweza kusoma:
- 'Nilibakwa na afisa wa polisi'
Mamlaka Kenya zachunguza ugonjwa usiojulikana uliowakumba watoto 95 wa shule
Mamlaka ya afya nchini Kenya inachunguza ugonjwa usiojulikana baada ya zaidi ya wanafunzi 90 wa shule za upili kulazwa katika hospitali mbalimbali za Kakamega, Magharibi mwa Kenya.
Wanafunzi hao kutoka Shule ya Upili ya Wasichana ya Eregi walikuwa na dalili za maumivu ya goti na walikuwa na ugumu wa kutembea.
Afisa mkuu wa Wizara ya Elimu ambaye alitembelea shule hiyo Jumanne aliwaambia wazazi waliokuwa na wasiwasi kwamba hali imedhibitiwa.
Alisema wanafunzi wengine watasalia shuleni.
"Idara ya elimu, serikali ya kaunti na idara ya afya ya umma wanatoa ahadi kwamba watoto watatibiwa," alisema Jared Obiero, mkurugenzi wa elimu katika eneo hilo.
Sampuli za damu, mkojo na kinyesi zilitumwa kwa maabara katika jiji jirani la Kisumu na mji mkuu, Nairobi.
Matokeo ya mwisho ya kubaini chanzo cha ugonjwa huo yanatarajiwa baadaye Jumatano.
Ubalozi wa Ethiopia nchini Sudan waharibiwa kwa shambulio
Ubalozi wa Ethiopia katika mji mkuu wa Sudan Khartoum umeshambuliwa kwa silaha nzito Jumanne asubuhi, balozi wa Ethiopia huko amethibitisha.
Hakuna majeruhi walioripotiwa katika shambulio hilo lakini jengo la ubalozi huo liliharibiwa kiasi, balozi wa Ethiopia nchini Sudan Yibeltal Ayimiro Alemu ameiambia BBC.
Jeshi laRapid Support Forces (RSF), ambalo limekuwa likipigana tangu Aprili 15, limelaumu jeshi la serikali kwa shambulio hilo.
Jeshi la Sudan halijazungumza lolote kuhusu shambulio hilo.
Si mara ya kwanza kwa ubalozi wa Ethiopia mjini Khartoum kushambuliwa.
Mfanyakazi wa ubalozi wa Ethiopia nchini Sudan aliambia BBC kuwa ubalozi huo ulishambuliwa kwa mashambulizi ya anga wiki tatu zilizopita na kumjeruhi mlinzi. Pia ilivunja madirisha ya jengo la ubalozi huo.
Zaidi ya watu 5,000 wamefariki katika mzozo huo na wengine milioni tano kutoroka makazi yao, kulingana na UN.
Pia unaweza kusoma:
- Africa Eye: Ushahidi wa uwezekano wa uhalifu wa kivita Sudan wazuka
Marekani yaweka vikwazo kwa makampuni ya China kukabili utumizi mbaya wa fentanyl
Marekani imetangaza vikwazo kwa makampuni 25 ya China na watu binafsi wanaodaiwa kuhusika katika utengenezaji wa kemikali zinazotumika kutengeneza fentanyl.
Fentanyl, afyuni (opioidi) yenye nguvu inayotumiwa kama dawa ya kutuliza maumivu makali sana, ina jukumu kubwa katika mgogoro unaoendelea wa madawa ya kulevya nchini Marekani.
Mwanasheria Mkuu Merrick Garland amesema msururu wa usambazaji wa dawa "mara nyingi huanza na kampuni za kemikali nchini Uchina".
Ubalozi wa China mjini Washington haukujibu mara moja ombi la kutoa maoni kutoka kwa shirika la habari la Reuters.
Mnamo Aprili, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China alisema "hakuna kitu kama usafirishaji haramu wa fentanyl" kati ya Uchina na Mexico.
Hii ilikuja baada ya Rais wa Mexico Andrés Manuel López Obrador kuitaka serikali ya Uchina kusaidia kukomesha madai ya kuingia kwa wingi kwa fentanyl na dawa nyingine nchini mwake.
Mamlaka ya Marekani inalaumu magenge ya madawa ya kulevya ya Mexico kwa kusambaza fentanyl kwa watumiaji kote Marekani.
Fentanyl inaweza kuagizwa kisheria na madaktari, lakini ongezeko kubwa la uraibu wa opioidi nchini Marekani katika miongo ya hivi karibuni imesababisha kuongezeka kwa utengenezaji haramu na kutumia kiwango cha juu cha dawa kuliko dozi inayohitajika.
Mnamo 2022, dawa hiyo ilihusishwa na rekodi ya vifo 109,680.
Wizara ya Fedha Marekani ilitangaza vikwazo dhidi ya kile ilichokiita "mtandao wa China unaohusika na utengenezaji na usambazaji" wa vitangulizi vya fentanyl na idadi ya dawa zingine haramu.
Maafisa wanasema kampuni katika msururu wa usambazaji wa fentanyl hutumia mara kwa mara anwani za uwongo na kuweka lebo vibaya ili kuzuia bidhaa zao kutambuliwa na mkono wa sheria.
Wale walioathiriwa na vikwazo hivyo ni pamoja na mashirika 12 na watu 13 walioko Uchina, pamoja na mashirika mawili na mtu mmoja anayeishi Canada, wizara ya fedha ilisema.
Vikwazo hivyo vitazuia mali ya mashirika ya Marekani na kuwazuia Wamarekani kufanyakazi nayo.
Soma zaidi:
- Kwa nini dawa za kuondoa maumivu zinazosababisha uraibu zinatumika?
- Simulizi ya kusikitisha ya uraibu wa dawa za kutuliza maumivu